Maandiko Matakatifu
2 Nefi 30


Mlango wa 30

Wayunani walioongoka watahesabika kuwa watu wa maagano—Walamani wengi na Wayahudi wataliamini neno na kuwa wema—Israeli itarudishwa na walio waovu kuangamizwa. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Na sasa tazama, ndugu zangu wapendwa, nitawazungumzia; kwani mimi, Nefi, sitakubali kwamba ninyi mdhani kuwa ninyi ni watakatifu zaidi ya vile Wayunani watakavyokuwa. Kwani tazameni, msipotii amri za Mungu wote mtaangamia pia; na kwa sababu ya maneno ambayo yamezungumzwa msidhani kwamba Wayunani wameangamizwa kabisa.

2 Kwani tazama, nawaambia kwamba kadiri Wayunani watakavyotubu wao wanakuwa watu wa maagano wa Bwana; na kadiri wengi Wayahudi wasivyotubu watatengwa; kwani Bwana haagani na yeyote ila tu wale wanaotubu na kumwamini Mwana wake, ambaye ndiye Mtakatifu wa Israeli.

3 Na sasa, nitatoa unabii mchache zaidi kuhusu Wayahudi na Wayunani. Kwani baada ya kitabu kile nilichokizungumzia kutokea, na kuandikiwa Wayunani, na kutiwa muhuri tena katika Bwana, kutakuwa na wengi ambao wataamini maneno yaliyoandikwa; na wao watayapelekea baki la uzao wetu.

4 Na kisha baki la uzao wetu litajua kutuhusu, vile tulivyotoka Yerusalemu, na kwamba wao ni ukoo wa Wayahudi.

5 Na injili ya Yesu Kristo itatangazwa miongoni mwao; kwa hivyo, wao watarejeshwa tena kwa ufahamu wa baba zao, na pia kwa ufahamu wa Yesu Kristo, ambao ulikuwa miongoni mwa baba zao.

6 Na kisha watashangilia; kwani watajua kwamba ni baraka kwao kutoka mkono wa Mungu; na magamba yao ya giza yataanza kuanguka kutoka macho yao; na vizazi vingi havitapita miongoni mwao, ila tu watakuwa safi na watu wema.

7 Na itakuwa kwamba Wayahudi waliotawanyika wataanza kumwamini Kristo; na wataanza kukusanyika katika uso wa nchi; na kadiri wengi watakavyomwamini Kristo pia nao watakuwa watu wema.

8 Na itakuwa kwamba Bwana Mungu ataanza kazi yake miongoni mwa mataifa yote, makabila, lugha, na watu, kuleta marejesho ya watu wake katika dunia.

9 Na kwa haki Bwana Mungu atawahukumu maskini, na kuwakemea kwa kiasi kwa walio wapole duniani. Na ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake; na kwa pumzi ya midomo yake atawaua walio waovu.

10 Kwani wakati unafika upesi ambapo Bwana Mungu atasababisha mgawanyiko mkuu miongoni mwa watu, na ataangamiza waovu; na atawahurumia watu wake, ndiyo, hata kama lazima aangamize waovu kwa moto.

11 Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu utakuwa mshipi wa mafigo yake.

12 Na kisha mbwa mwitu ataishi na mwanakondoo; na chui atalala na mwanambuzi, na ndama, na mwana-simba, na kinono, pamoja; na mtoto mdogo atawaongoza.

13 Na ngʼombe na dubu watakula; na watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ngʼombe.

14 Na mtoto anayenyonya atachezea katika tundu la nyoka sumu, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake kwenye pango la fira.

15 Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na ufahamu wa Bwana kama vile maji yanavyofunika baharini.

16 Kwa hivyo, vitu vya mataifa yote vitajulikana; ndiyo, vitu vyote vitajulikana na watoto wa watu.

17 Hakuna jambo ambalo ni la siri ambalo halitafunuliwa; hakuna kazi ya giza ambayo haitafunuliwa katika nuru; na hakuna jambo lolote ambalo limetiwa muhuri duniani ambalo halitafunguliwa.

18 Kwa hivyo, vitu vyote ambavyo vimewahi kufunuliwa watoto wa watu katika siku ile vitafunuliwa; na Shetani hatakuwa na nguvu juu ya mioyo ya watoto wa watu tena, kwa muda mrefu. Na sasa, ndugu zangu wapendwa, namalizia maneno yangu hapo.