Maandiko Matakatifu
Alma 13


Mlango wa 13

Wanaume wanaitwa kama makuhani wakuu kwa sababu ya imani yao kuu na matendo mema—Watapaswa kufundisha amri—Kupitia haki wanatakaswa na kuingia katika pumziko la Bwana—Melkizedeki alikuwa mmoja wa hawa—Malaika wanatangaza habari njema kote nchini—Watatangaza ujio halisi wa Kristo. Karibia mwaka 82 K.K.

1 Na tena, ndugu zangu, ningetaka nikumbushe fikira zenu kuhusu ule wakati ambao Bwana Mungu aliwapatia watoto wake amri hizi; na ningetaka mkumbuke kwamba Bwana Mungu aliwatawaza makuhani, kulingana na mpango wake mtakatifu, ambao ni ule mpango wa Mwana wake, kufundisha watu vitu hivi.

2 Na makuhani hao walitawazwa kulingana na mpango wa Mwana wake, katika hali ambayo watu wangejua ni vipi watakavyomtumainia Mwana wake kwa ukombozi.

3 Na hivi ndivyo jinsi walivyotawazwa—wakiitwa na kutayarishwa tangu msingi wa ulimwengu kulingana na ufahamu wa mbeleni wa Mungu, kwa ajili ya imani yao kuu na vitendo vyao vyema; mwanzoni wakiruhusiwa kuchagua baina ya mema na maovu; kwa hivyo wao wakiwa wamechagua mema, na kufanya mazoezi ya imani kuu, wameitwa kwa mwito mtakatifu, ndiyo, kwa ule mwito mtakatifu ambao ulitayarishwa, na kulingana na, matayarisho ya ukombozi wao.

4 Na hivyo wameitwa kwa mwito huu mtakatifu kwa ajili ya imani yao, wakati wengine wangemkataa Roho wa Mungu kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao na upofu wa fikira zao, wakati, kama isingekuwa kwa sababu hii wangekuwa na mamlaka makuu kama ndugu zao.

5 Au kwa kifupi, hapo mwanzoni walikuwa katika hali sawa na ndugu zao; hivyo mwito huu mtakatifu ukiwa umetayarishwa tangu msingi wa ulimwengu kwa wale ambao hawangeshupaza mioyo yao, kupitia na katika upatanisho wa Mwana wa Pekee, ambaye alitayarishwa—

6 Na hivyo kuitwa na mwito huu mtakatifu, na kutawazwa ukuhani mkuu wa mpango mtakatifu wa Mungu, kufundisha watoto wa watu amri zake, ili nao pia waingie katika pumziko lake—

7 Ukuhani huu mkuu ukiwa kwa ule mpango wa Mwana wake, mpango ambao ulikuwa tangu msingi wa ulimwengu; au kwa maneno mengine, haukuwa na mwanzo wa siku au mwisho wa miaka, ukiwa ulitayarishwa tangu milele hadi milele, kulingana na ufahamu wake wa mbele wa vitu vyote—

8 Sasa walitawazwa kwa njia hii—wakiwa wameitwa kwa mwito mtakatifu, na kutawazwa kwa agizo takatifu, na kuchukua ukuhani mkuu juu yao wa mpango mtakatifu, ambao ni mwito, na agizo, na ukuhani mkuu, usio na mwanzo au mwisho—

9 Hivyo wakawa makuhani wakuu milele, kulingana na mpango mtakatifu wa Mwana wa Pekee wa Baba, ambaye hana mwanzo wa siku au mwisho wa miaka, ambaye amejaa neema, ukweli, na haki. Na hivyo ndivyo ilivyo. Amina.

10 Sasa, kama vile nilivyosema kuhusu mpango huu mtakatifu, au huu ukuhani mkuu, kulikuwa na wengi ambao walitawazwa na kuwa makuhani wakuu wa Mungu; na ilikuwa kwa ajili ya imani yao kuu na toba, na haki yao mbele ya Mungu, wao wakichagua kutubu na kutenda haki badala ya kuangamia;

11 Kwa hivyo waliitwa kulingana na mpango huu mtakatifu, na wakatakaswa, na mavazi yao yakaoshwa na kuwa meupe kupitia damu ya Mwanakondoo.

12 Na wao, baada ya kutakaswa na Roho Mtakatifu, na mavazi yao kufanywa meupe, yakiwa safi na bila doa mbele ya Mungu, hawangetazama dhambi bila kukerwa; na kulikuwa na wengi, wengi sana, ambao walifanywa safi na kuingia katika pumziko la Bwana Mungu wao.

13 Na sasa, ndugu zangu, ningetaka kwamba mjinyeyekeze mbele ya Mungu, na mzae matunda yanayostahili toba, ili ninyi pia muingie katika hilo pumziko.

14 Ndiyo, jinyenyekeeni hata kama wale watu waliokuwa katika siku za Melkizedeki, ambaye pia alikuwa kuhani mkuu kulingana na ule mpango ambao nimeuzungumzia, ambaye pia aliuchukua ukuhani mkuu milele.

15 Na ilikuwa ni kwa huyu Melkizedeki ambaye Ibrahimu alilipa zaka; ndiyo, hata baba yetu Ibrahimu alilipa zaka ya fungu la kumi ya mali yote aliyokuwa nayo.

16 Sasa haya maagizo yalitolewa kwa namna hii, ili watu wamtazamie Mwana wa Mungu, ambayo ikiwa ni mfano wa mpango wake, au ukiwa mpango wake, na ili wamtazamie mbele kwake kwa ondoleo la dhambi zao, ili waingie katika pumziko la Bwana.

17 Sasa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme katika nchi ya Salemu; na watu wake walikuwa wametumbukia katika uovu na machukizo; ndiyo, wote walikuwa wamepotea njia; walikuwa wamejaa kila aina ya uovu;

18 Lakini Melkizedeki akiwa na imani kuu, na kuipokea ofisi ya ukuhani mkuu kulingana na mpango mtakatifu wa Mungu, aliwahubiria watu wake toba. Na tazama, walitubu; na Melkizedeki aliimarisha amani nchini katika siku zake; kwa hivyo aliitwa mwana mfalme wa amani, kwani alikuwa mfalme wa Salemu; na alitawala chini ya baba yake.

19 Sasa, kulikuwa na wengi mbele yake, na pia kulikuwa na wengi baadaye, lakini hapakuwa na yeyote aliyekuwa mkuu zaidi; kwa hivyo, wamemtaja yeye zaidi.

20 Sasa hakuna haja ya kurudia jambo hili; yale ambayo nimesema yametosha. Tazama, maandiko yako mbele yenu; mkiyapinga itakuwa ni kwa maangamizo yenu.

21 Na sasa ikawa kwamba baada ya Alma kusema maneno haya kwao, alinyosha mkono wake kwao na kuongea kwa sauti kuu, akisema: Sasa ndiyo wakati wa kutubu, kwani siku ya wokovu inakaribia;

22 Ndiyo, na sauti ya Bwana, kwa mdomo wa malaika, inatangazia mataifa yote; ndiyo, inaitangaza, kwamba wawe na habari njema kuu ya shangwe kuu; ndiyo, anaitangaza habari hii njema miongoni mwa watu wake wote, ndiyo, hata kwa wale ambao wametawanyika kote usoni mwa dunia kwa hivyo wametujia.

23 Na wametufahamisha kwa misemo iliyo wazi, ili tufahamu, ili tusikose; na hii ni kwa sababu sisi ni wazururaji katika nchi ngeni; kwa hivyo, tumeheshimiwa zaidi, kwani tumeelezewa habari hii njema katika pande zote za shamba letu la mizabibu.

24 Kwani tazama, malaika wanawatangazia wengi sasa katika nchi yetu; na hii ni kwa lengo la kutayarisha mioyo ya watoto wa watu ili wapokee neno lake atakaporudi katika utukufu wake.

25 Na sasa tunasubiri tu kusikia habari njema tukihubiriwa kwa mdomo wa malaika, kuhusa kuja kwake; kwani wakati unakuja, na hatujui ni lini. Namwomba Mungu kwamba iwe katika siku zangu; lakini ikiwa sasa au baadaye, nitaifurahia.

26 Na itafahamishwa kwa watu wenye haki na watakatifu, kwa mdomo wa malaika, wakati wa kuja kwake, kwamba maneno ya babu zetu yatimizwe, kulingana na yale ambayo waliyozungumza kumhusu, ambayo yalikuwa ni kulingana na roho ya unabii iliyokuwa ndani yao.

27 Na sasa, ndugu zangu, natamani kutoka sehemu za ndani kabisa za moyo wangu, ndiyo, kwa wasiwasi mwingi na hata kwa uchungu, kwamba msikilize maneno yangu, na mtupe dhambi zenu, na kwamba msiahirishe siku ya toba yenu;

28 Lakini kwamba mtajinyenyekeza mbele ya Bwana, na mliite jina lake takatifu, na kukesha na kusali daima, kwamba msijaribiwe zaidi ya yale ambayo mnaweza kuvumilia, na hivyo mwongozwe na Roho Mtakatifu, katika kuwa wanyenyekevu, wapole, watiifu, wenye subira, wenye upendo na wenye uvumilivu;

29 Mkimwamini Bwana; mkitumaini kwamba mtapokea uzima wa milele; mkiwa na upendo wa Mungu daima katika mioyo yenu, kwamba muinuliwe katika siku ya mwisho na muingie katika pumziko lake.

30 Na ikiwezekana Bwana awape toba, kwamba msijiteremshie ghadhabu yake, kwamba msifungiwe na minyororo ya jehanamu, kwamba msipate mauti ya pili.

31 Na Alma aliwazungumzia watu maneno mengi, ambayo hayajaandikwa katika kitabu hiki.