Maandiko Matakatifu
Etheri 4


Mlango wa 4

Moroni anaamrishwa kuyafungia maandishi ya kaka wa Yaredi—Hayatafunuliwa mpaka watu wote watakapokuwa na imani kama ya kaka wa Yaredi—Kristo anaamuru watu wote waamini maneno Yake, na yale ya wanafunzi Wake—Watu wanaamriwa watubu, waamini injili, na waokolewe.

1 Na Bwana alimwamuru kaka wa Yaredi aende chini kutoka mlimani kutoka kwenye uwepo wa Bwana, na aviandike vitu alivyokuwa ameviona; na vilikatazwa kuonekana na watoto wa watu mpaka atakapoinuliwa juu ya msalaba; na kwa sababu hii mfalme Mosia alivificha, kwamba visijulikane duniani mpaka Kristo atakapojidhihirisha kwa watu wake.

2 Na baada ya Kristo kujidhihirisha kwa ukweli kwa watu wake aliamrisha kwamba vijulikane.

3 Na sasa, baada ya hayo, wote wamefifia katika kutoamini; na hakuna yeyote isipokuwa Walamani, na wamekataa injili ya Kristo; kwa hivyo nimeamriwa kwamba nivifiche tena ardhini.

4 Tazama, nimeandika juu ya mabamba haya vitu vivyo hivyo ambavyo kaka wa Yaredi aliviona; na hakujakuwa vitu vikubwa vilivyoonyeshwa kuliko hivyo ambavyo vilionyeshwa kwa kaka wa Yaredi.

5 Kwa hivyo Bwana ameniamuru niviandike; na nimeviandika. Na aliniamuru kwamba nivifunge; na pia ameniamuru kwamba nifungie tafsiri yake; kwa hivyo nimeifungia tafsiri, kulingana na amri ya Bwana.

6 Kwani Bwana aliniambia: Havitawaendea Wayunani mpaka siku watakapotubu uovu wao, na kuwa safi mbele ya Bwana.

7 Na katika siku hiyo watakapofanya imani kwangu, asema Bwana, hata kama kaka wa Yaredi alivyofanya, kwamba watakaswe kupitia kwangu, ndipo nitawaonyesha vitu ambavyo kaka wa Yaredi aliviona, hata kwa kuwakunjulia ufunuo wangu wote, anasema Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Baba wa mbingu na wa dunia, na vitu vyote vilivyomo.

8 Na yule ambaye atapingana na neno la Bwana, acha alaaniwe; na yule ambaye atakana vitu hivi, acha alaaniwe; kwani kwao, sitaonyesha vitu vikubwa zaidi, anasema Yesu Kristo; kwani ni mimi ninayezungumza.

9 Na kwa amri yangu mbingu hufunguliwa na kufungwa; na kwa neno langu dunia itatetemeka; na kwa amri yangu wakazi wake watakufa, kama waliochomwa na moto.

10 Na yule ambaye haamini maneno yangu, haamini wanafunzi wangu; na ikiwa hivyo kwamba sisemi, hukumu wewe; kwani utajua kwamba ni mimi ninayezungumza, katika siku ya mwisho.

11 Lakini yule aaminiye maneno haya ambayo nimesema, yeye nitamtembelea na ufunuo wa Roho yangu, na atajua na kushuhudia. Kwani kwa sababu ya Roho yangu atafahamu kwamba vitu hivi ni vya kweli; kwani huwashawishi watu kutenda mema.

12 Na kitu chochote ambacho hushawishi watu kutenda mema ni changu; kwani mema hayatoki kwa yeyote isipokuwa kwangu. Mimi ni yule yule ambaye huongoza watu kwa wema wote; yule ambaye hataamini maneno yangu hataniamini—kwamba ni mimi; na yule ambaye hataniamini hatamwamini Baba ambaye alinituma. Kwani tazama, mimi ni Baba, mimi ni mwangaza, na maisha, na ukweli wa dunia.

13 Njooni kwangu, Ee ninyi Wayunani, na nitawaonyesha vitu vikuu zaidi, ufahamu ambao umefichwa kwa sababu ya kutoamini.

14 Njooni kwangu, Ee ninyi nyumba ya Israeli, na itafanywa kujulikana kwenu jinsi Baba alivyoweka vitu kwenu, kutokea msingi wa dunia; na haijawafikia, kwa sababu ya kutoamini.

15 Tazama, wakati mtakapopasua lile pazia la kutoamini ambalo linawasababisha kubaki katika hali yenu ya kutisha ya uovu, na ugumu wa moyo, na upofu wa akili, ndipo vitu vikubwa na vya kustaajabisha ambavyo vilifichwa kutokea mwanzo wa dunia kutoka kwenu—ndiyo, wakati mtakapomlingana Baba katika jina langu, na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, ndipo mtajua kwamba Baba amekumbuka agano ambalo alifanya na babu zenu, Ee nyumba ya Israeli.

16 Na ndipo ufunuo wangu ambao nimesababisha kuandikwa na mtumishi wangu Yohana utakunjuliwa machoni mwa watu wote. Kumbuka, wakati mtakapoona vitu hivi, mtajua kwamba wakati uko karibu kwamba vitafanywa kuwa wazi kabisa.

17 Kwa hivyo, mtakapopokea maandishi haya mjue kwamba kazi ya Baba imeanza juu ya uso wa nchi.

18 Kwa hivyo, tubuni enyi miisho ya dunia, na mje kwangu, na mwamini katika injili yangu, na mbatizwe katika jina langu; kwani yule ambaye anaamini na kubatizwa atakombolewa; lakini yule ambaye haamini atalaaniwa; na ishara zitaonyeshwa kwa wale ambao wanaamini katika jina langu.

19 Na ana baraka yule atakayepatikana akiwa mwaminifu kwa jina langu katika siku ya mwisho, kwani atainuliwa kuishi katika ufalme uliotayarishwa kutokea mwanzo wa dunia. Na tazama ni mimi ambaye nimezungumza. Amina.