Maandiko Matakatifu
Maneno ya Mormoni 1


Maneno ya Mormoni

Mlango wa 1

Mormoni anafupisha mabamba makubwa ya Nefi—Anaweka mabamba yale madogo na mabamba yale mengine—Mfalme Benjamini anaimarisha amani nchini. Karibia mwaka 385 B.K.

1 Na sasa mimi, Mormoni, nikikaribia kuyakabidhi yale maandishi ambayo nimeandika mikononi mwa mwana wangu Moroni, tazama nimeshuhudia karibu maangamizo yote ya watu wangu, Wanefi.

2 Na ni baada ya miaka mia kadha baada ya kuja kwa Kristo ninapompatia mwana wangu maandishi haya; na ninadhani kwamba atashuhudia maangamizo yote ya watu wangu. Lakini na Mungu amjalie aweze kuishi, ili aandike juu yao, na kwa vyovyote kuhusu Kristo, ili pengine wafaidike katika nyakati zingine.

3 Na sasa, ninazungumza kuhusu yale ambayo nimeandika; kwani baada ya kufanya ufupisho kutoka yale mabamba ya Nefi, hadi utawala wa huyu mfalme Benjamini, ambaye alizungumziwa na Amaleki, nilipekua miongoni mwa maandishi haya niliyopewa, na nikapata mabamba haya, ambayo yalikuwa na historia hii ndogo ya manabii, kutoka Yakobo hadi utawala huu wa mfalme Benjamini, na pia maneno mengi ya Nefi.

4 Na vitu ambavyo vimo katika mabamba haya vinanifurahisha, kwa sababu ya unabii wa kuja kwa Kristo; na baba zangu wakijua kwamba vingi vimetimizwa; ndiyo, na pia najua kwamba vingi vilivyobashiriwa kutuhusu sisi hadi siku hii vimetimizwa, na vingi ambavyo vitazidi leo lazima kwa ukweli vitatokea—

5 Kwa hivyo, nachagua vitu hivi, ili nimalize maandishi yangu juu yao, maandishi ambayo nitatoa kutoka mabamba ya Nefi; na siwezi kuandika hata sehemu moja ya mia ya vitu vya watu wangu.

6 Lakini tazama, nitachukua mabamba haya, ambayo yana unabii na ufunuo, na kuyaweka pamoja na mabaki ya yale maandishi yangu, kwani ni bora kwangu; na ninajua kwamba yatakuwa bora kwa ndugu zangu.

7 Na ninatenda haya kwa madhumuni ya busara; kwani ninanongʼonezewa, kulingana na kazi za Roho wa Bwana aliye ndani yangu. Na sasa, sijui mambo yote; lakini Bwana anajua vitu vyote vitakavyokuja; kwa hivyo, anafanya kazi ndani yangu ili nitende kulingana na nia yake.

8 Na sala yangu kwa Mungu ni kuhusu ndugu zangu, kwamba wamfahamu Mungu tena, ndiyo, ukombozi wa Kristo; ili tena wawe watu wema.

9 Na sasa mimi, Mormoni, namalizia maandishi yangu, ambayo ninayatoa kutoka mabamba ya Nefi; na ninayaandika kulingana na maarifa na ufahamu ambao Mungu amenipatia.

10 Kwa hivyo, ikawa kwamba baada ya Amaleki kumpatia mfalme Benjamini mabamba haya, aliyachukua na kuyaweka pamoja na yale mabamba mengine, ambayo yalikuwa na maandishi ambayo yalitolewa na wafalme, kutoka kizazi hadi kizazi mpaka siku za Benjamini.

11 Na yalipitishwa kutoka mfalme Benjamini, kutoka kizazi hadi kizazi mpaka zikafika mikononi mwangu. Na mimi, Mormoni, naomba Mungu kwamba yahifadhiwe tangu sasa. Na ninajua kwamba yatahifadhiwa; kwani kuna mambo makuu ambayo yameandikwa juu yake, ambayo yatahukumu watu wangu na ndugu zao katika siku ile kuu ya mwisho, kulingana na neno la Mungu ambalo limeandikwa.

12 Na sasa, kuhusu huyu mfalme Benjamini—alikuwa na mabishano fulani miongoni mwa watu wake.

13 Na ikawa kwamba pia majeshi ya Walamani yaliondoka nchi ya Nefi, ili yapigane na watu wake. Lakini tazama, mfalme Benjamini alikusanya pamoja majeshi yake, na akawapinga; na alipigana kwa nguvu ya mkono wake mwenyewe, akitumia upanga wa Labani.

14 Na kwa nguvu za Bwana walipigana dhidi ya maadui wao, hadi wakawaua maelfu mengi ya Walamani. Na ikawa kwamba walipigana na Walamani hadi wakawaondoa kutoka nchi yao yote ya urithi wao.

15 Na ikawa kwamba baada ya kuwa na Kristo wengi bandia, na vinywa vyao vikafungwa, na wakaadhibiwa kulingana na makosa yao;

16 Na baada ya kuwepo na manabii wa bandia, na wahubiri bandia na walimu bandia miongoni mwa watu, na hawa wote wakiwa wameadhibiwa kulingana na makosa yao; na baada ya kuwepo na ubishi mwingi na ukengeufu mwingi kwa Walamani, tazama, ikawa kwamba mfalme Benjamini, kwa msaada wa manabii watakatifu waliokuwa miongoni mwa watu wake—

17 Kwani tazama, mfalme Benjamini alikuwa mtu mtakatifu, na alitawala watu wake kwa haki; na kulikwa na watu wengi watakatifu nchini ile, na walinena neno la Mungu kwa nguvu na mamlaka; na walitumia ukali mwingi kwa sababu ya utukutu wa wale watu—

18 Kwa hivyo, kwa msaada wa hawa, mfalme Benjamini, kwa kutumikia kwa nguvu zote za mwili wake na uwezo wa nafsi yake yote, na pia manabii, aliimarisha tena amani katika nchi ile.