Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 31


Sehemu ya 31

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Thomas B. Marsh, Septemba 1830. Tukio hili lilitokea muda mfupi baada ya mkutano wa Kanisa (ona kichwa cha habari cha sehemu ya 30). Thomas B. Marsh alikuwa amebatizwa mwanzoni mwa mwezi huo na kutawazwa kuwa mzee katika Kanisa kabla ya kutolewa kwa ufunuo huu.

1–6, Thomas B. Marsh ameitwa kuihubiri injili na anahakikishiwa ustawi wa familia yake; 7–13, Anashauriwa kuwa mvumilivu, kusali daima, na kumtii Mfariji.

1 Thomas, mwanangu, umebarikiwa kwa sababu ya imani yako katika kazi yangu.

2 Tazama, umepata mateso mengi kwa sababu ya familia yako; hata hivyo, nitakubariki wewe na familia yako, ndiyo, watoto wako; na siku yaja ambayo wataamini na kujua ukweli na kuwa pamoja na wewe katika kanisa langu.

3 Inua moyo wako na ufurahi, kwani saa ya huduma yako imewadia; na ulimi wako utalegezwa, nawe utatangaza habari njema ya shangwe kuu kwa kizazi hiki.

4 Utatangaza mambo yale ambayo yamefunuliwa kwa mtumishi wangu, Joseph Smith, Mdogo. Utaanza kuhubiri kutoka wakati huu, ndiyo, kuvuna katika shamba ambalo ni jeupe lililo tayari kuchomwa.

5 Kwa hiyo, ingiza mundu yako kwa moyo wako wote, na dhambi zako zitasamehewa, na wewe utachukua miganda mgongoni mwako, kwani mtenda kazi amestahili ujira wake. Kwa hivyo, familia yako itaishi.

6 Tazama, amini ninakuambia, enenda kutoka kwao japo kwa wakati mfupi, na utangaze neno langu, na Mimi nitawatayarishia mahali.

7 Ndiyo, nitaifungua mioyo ya watu, nao watakupokea. Nami nitalianzisha kanisa kwa mkono wako;

8 Nawe utawaimarisha na kuwatayarisha kwa ajili ya wakati watakapo kusanyika.

9 Uwe mvumilivu wakati wa mateso, usiwashutumu wenye kukushutumu. Itawale nyumba yako kwa unyenyekevu, na uwe thabiti.

10 Tazama, ninakuambia kwamba utakuwa tabibu kwa kanisa, bali siyo kwa walimwengu, kwani wao hawatakupokea.

11 Nenda zako kokote nitakakokutuma, na utapewa na Mfariji, lile la kufanya na mahali pa kwenda.

12 Omba daima, usije ukaanguka majaribuni na kupoteza thawabu yako.

13 Uwe mwaminifu hata mwisho, na lo, Mimi ni pamoja nawe. Maneno haya siyo ya mwanadamu wala ya wanadamu, bali yangu Mimi, Yesu Kristo, Mkombozi wako, kwa mapenzi ya Baba. Amina.