Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 41


Sehemu ya 41

Ufunuo uliotolewa kupitia kwa Joseph Smith Nabii kwa Kanisa, huko Kirtland, Ohio, 4 Februari 1832. Ufunuo huu unawaamuru Nabii na wazee wa Kanisa wasali ili kupokea “sheria” ya Bwana (ona sehemu ya 42). Joseph Smith alikuwa ndiyo amewasili tu huko Kirtland akitokea New York, na Leman Copley, muumini wa Kanisa katika jirani ya Thompson, Ohio, “aliomba Ndugu Joseph na Sidney [Rigdon] … waishi pamoja naye na kwamba yeye angewapa nyumba na mahitaji yao mengine.” Ufunuo ufuatao unaelezea mahali ambapo Joseph na Sidney wangepaswa kuishi na pia unamwita Edward Partridge kuwa askofu wa kwanza wa Kanisa.

1–3, Wazee wataliongoza Kanisa kwa roho wa ufunuo; 4–6, Wanafunzi wa kweli watapokea na kuzishika sheria za Bwana; 7–12, Edward Partridge atajwa kama askofu wa Kanisa.

1 Sikilizeni na mkasikie, Ee enyi watu wangu, asema Bwana na Mungu wenu, ninyi ambao nataka kuwabariki kwa baraka kubwa kuliko baraka zote, ninyi mnaonisikia; na nitawalaani ninyi ambao hamnisikii, ambao mmelikiri jina langu, kwa laana nzito kuliko zote.

2 Sikilizeni, Enyi wazee wa kanisa langu ambao nimewaita, tazameni ninawapa amri kwamba mtakusanyika pamoja ninyi wenyewe ili kukubaliana juu ya neno langu;

3 Na kwa sala ya imani yenu mtapokea sheria yangu, ili muweze kujua jinsi ya kulitawala kanisa langu na mambo yote yawe sawa mbele yangu.

4 Na Mimi nitakuwa mtawala wenu wakati nitakapokuja; na tazama, naja upesi, nanyi mtaangalia kwamba sheria yangu imeshikwa.

5 Yeye ambaye huipokea sheria yangu na kuitenda, huyo ndiye mwanafunzi wangu; na yule asemaye ameipokea na haitendi, huyo siyo mwanafunzi wangu, na ataondolewa kutoka miongoni mwenu;

6 Kwani si vyema kwamba vitu ambavyo ni vya watoto wa ufalme wakapewa wao ambao hawastahili, au kwa mbwa, au lulu kutupwa mbele ya nguruwe.

7 Na tena, ni vyema kwamba mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, ajengewe nyumba, ambamo ataishi na kutafsiri.

8 Na tena, ni vyema kwamba mtumishi wangu Sidney Rigdon aishi kama aonavyo yeye kuwa vyema, ili mradi ashike amri zangu.

9 Na tena, nimemwita mtumishi wangu Edward Partridge; ninatoa amri, kwamba anapaswa kuteuliwa kwa sauti ya kanisa, na kutawazwa kuwa askofu kwa kanisa, kuacha biashara zake na kutumia muda wake wote kwa kazi za kanisa;

10 Kuangalia mambo yote kama itakavyoteuliwa kwake katika sheria zangu katika siku ambayo nitazitoa.

11 Na hii ni kwa sababu moyo wake ni safi mbele zangu, kwani yeye ni kama Nathanieli wa zamani, hamna hila ndani yake.

12 Maneno haya yametolewa kwenu, nayo ni safi mbele zangu; kwa hiyo, angalieni jinsi mnavyoyashika, kwani yatajibiwa juu ya nafsi zenu katika siku ya hukumu. Hivyo ndivyo. Amina.