Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 50


Sehemu ya 50

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 9 Mei 1831. Historia ya Joseph Smith inaeleza kwamba baadhi ya wazee walikuwa hawaelewi kujitokeza kwa roho tofauti zilizoenea katika nchi na kwamba ufunuo huu ulitolewa kama jibu kwa maulizo yake maalumu juu ya jambo hili. Yaliyokuwa yakiitwa matukio ya kiroho wala hayakuwa mageni miongoni mwa waumini, baadhi yao walikuwa wakidai kupokea maono na mafunuo.

1–5, Roho nyingi za uongo zimeenea katika nchi; 6–9, Ole wao wanafiki na wale waliotengwa na Kanisa; 10–14, Wazee watahubiri injili kwa Roho; 15–22, Wote mhubiri na msikilizaji wanahitaji kuangaziwa na Roho; 23–25, Kile kisichojenga siyo cha Mungu; 26–28, Waaminifu ni wamiliki wa vitu vyote; 29–36, Sala za walio safi hujibiwa; 37–46, Kristo ndiye Mchungaji Mwema na Jiwe la Israeli.

1 Sikilizeni, Enyi wazee wa kanisa langu, na itegeeni sikio sauti ya Mungu aliye hai; na litilieni maanani neno la hekima ambalo litatolewa kwenu, kulingana na vile mlivyoomba na kukubaliwa juu ya kanisa, na roho ambazo zimeenea katika nchi.

2 Tazama, amini ninawaambia, kwamba kuna roho nyingi ambazo ni roho za uongo, ambazo zimeenea katika nchi, zikiudanganya ulimwengu.

3 Na pia Shetani ametafuta kuwadanganya ninyi, ili aweze kuwapindua.

4 Tazama, Mimi, Bwana, nimewaangalia, na nimeona machukizo katika kanisa ambalo hulikiri jina langu.

5 Lakini wamebarikiwa wale walio waaminifu na wenye subira, ikiwa katika kuishi au katika kifo, kwani wataurithi uzima wa milele.

6 Bali ole wao wadanganyifu na wanafiki, kwani, hivyo ndivyo asemavyo Bwana, nitawaleta kwenye hukumu.

7 Tazama, amini ninawaambia, kuna wanafiki miongoni mwenu, ambao wamewadanganya baadhi yenu, ambao wamempa nguvu adui; lakini wa aina hiyo wataokolewa;

8 Lakini wanafiki watatambulika na kukatiliwa mbali, iwe katika kuishi au katika kufa, kama vile mimi nitakavyo; na ole wao waliokatiliwa mbali kutoka kwenye kanisa langu, kwani wao ulimwengu umewashinda.

9 Kwa hiyo, acha kila mtu ajihadhari ili asije akafanya kile kisicho cha kweli na haki mbele zangu.

10 Na sasa njooni kwa njia ya Roho, asema Bwana, kwa wazee wa kanisa lake, na tusemezane, ili mpate kuelewa;

11 Na tusemezane kama vile watu wanavyosemezana mmoja kwa mwingine uso kwa uso.

12 Sasa, wakati watu wanaposemezana, huelewana, kwa sababu husemezana kama watu; hivyo ndivyo nitakavyo Mimi, Bwana, kusemezana nanyi ili kwamba muweze kunielewa.

13 Kwa hiyo, Mimi Bwana ninawauliza swali hili—mmetawazwa kwa lipi?

14 Kwa kuhubiri injili yangu kwa njia ya Roho, hata Mfariji aliyetumwa kufundisha ukweli.

15 Nanyi mkapokea roho nyingine ambazo hamkuweza kuzielewa, na mkazipokea kama ni za Mungu; na katika hili ninyi mnajiteteaje?

16 Tazama, mtajibu swali hili ninyi wenyewe; hata hivyo, nitakuwa mwenye huruma kwenu; yule aliye dhaifu miongoni mwenu atafanywa baadaye kuwa mwenye nguvu.

17 Amini ninawaambia, yule aliyetawazwa na mimi na kutumwa kwenda kulihubiri neno la kweli kwa njia ya Mfariji, katika Roho wa kweli, je, afundisha kwa Roho wa kweli au kwa njia nyingine?

18 Na kama itakuwa kwa njia nyingine hatokani na Mungu.

19 Na tena, yule apokeaye neno la kweli, je, hulipokea kwa Roho wa kweli au kwa njia nyingine?

20 Kama ni kwa njia nyingine hatokani na Mungu.

21 Kwa hiyo, kwa nini kwamba hamwezi kuelewa na kujua, kwamba yule ambaye hulipokea neno kwa njia ya Roho wa kweli hulipokea kama vile lifundishwavyo na Roho wa kweli?

22 Kwa sababu hiyo, yule ambaye huhubiri na yule apokeaye, huelewana, na wote hujengana na kufurahi kwa pamoja.

23 Na kile kisichojenga siyo cha Mungu, nacho ni giza.

24 Kile kilicho cha Mungu ni nuru; na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi; na nuru hiyo huzidi kungʼara hata mchana mkamilifu.

25 Na tena, amini ninawaambia, na ninalisema ili muweze kujua ukweli, ili muweze kuifukuza giza kutoka miongoni mwenu;

26 Yule aliyetawazwa na Mungu na kutumwa, huyo ndiye ameteuliwa kuwa mkuu, bila kujali kuwa yeye ni mdogo na mtumishi wa wote.

27 Kwa hiyo, yeye ni mmiliki wa vitu vyote; kwani vitu vyote viko chini yake, kote mbinguni na duniani, uzima na nuru, Roho na nguvu, ametumwa kwa mapenzi ya Baba kupitia Mwana wake, Yesu Kristo.

28 Lakini hakuna mwanadamu aliye mmiliki wa vitu vyote isipokuwa yule aliye takaswa na kuoshwa dhambi zote.

29 Na kama umetakaswa na kuoshwa kutokana na dhambi zote, utaomba kitu chochote utakacho katika jina la Yesu nalo litafanyika.

30 Lakini jueni hili, mtafunuliwa nini cha kuomba; na kama vile mlivyoteuliwa kuongoza, roho zitakuwa chini yenu.

31 Kwa hiyo, itakuja kutokea, kwamba kama utaona roho amejitokeza ambaye huwezi kumwelewa, na wewe humpokei roho huyo, utamwuliza Baba katika jina la Yesu; na kama haitoi roho hiyo kwako, ndipo waweza kujua kwamba haitokani na Mungu.

32 Na utatolewa kwako, uwezo juu ya pepo hao; nawe utatangaza dhidi ya pepo huyo kwa sauti kubwa kama hatokani na Mungu—

33 Siyo kwa mashtaka ya kumlaumu, ili asije akakushinda, wala siyo kwa kujisifu wala kufurahia, ili nawe usije ukakamatwa.

34 Yule ambaye hupokea vya Mungu, na avihesabu kuwa ni vya Mungu; na afurahi kwamba Mungu humhesabu kuwa mwenye kustahili kupokea.

35 Na kwa kutilia maanani na kuyatenda mambo haya ambayo mmeyapokea, na yale mtakayoyapokea—na ufalme mliopewa na Baba, na uwezo wa kuvishinda vitu vyote ambavyo yeye hakuvianzisha.

36 Na tazama, amini ninawaambia, mmebarikiwa ninyi ambao sasa mnayasikiliza maneno yangu kutoka kinywa cha mtumishi wangu, kwani ninyi mmesamehewa dhambi zenu.

37 Na mtumishi wangu Joseph Wakefield, ambaye napendezwa naye, na mtumishi wangu Parley P. Pratt waende miongoni mwa makanisa na kuyaimarisha kwa neno la kufaa;

38 Na pia mtumishi wangu John Corrill, au na watumishi wangu wengi wengineo kama walivyotawazwa kwenye ofisi hii, na acheni wafanye kazi katika shamba la mizabibu, na acheni mtu yeyote asiwazuie kufanya kile ambacho nimekiteua kwao—

39 Kwa hiyo, katika hili mtumishi wangu Edward Partridge hasamehewi; isipokuwa atubu na atasamehewa.

40 Tazama, ninyi ni watoto wadogo na hamuwezi kuyastahimili yote hivi sasa; na lazima mkue katika neema na katika ujuzi wa ukweli.

41 Msiogope, ninyi watoto wadogo, kwani ninyi ni wangu, na Mimi nimeushinda ulimwengu, nanyi ndiyo wale ambao Baba alinipa;

42 Na hakuna hata mmoja wao wale ambao baba amenipatia atakayepotea.

43 Na Baba na Mimi tu wamoja. Mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu; na kadiri ninyi mlivyonipokea Mimi, ninyi mu ndani yangu nami ni ndani yenu,

44 Kwa hivyo, Mimi nipo katikati yenu, na mimi ni mchungaji mwema, na jiwe la Israeli. Yule ajengaye juu ya mwamba huu hataanguka kamwe.

45 Na siku yaja ambayo mtaisikia sauti yangu na kuniona, na kujua kwamba Mimi ndimi.

46 Kesheni basi, ili muweze kuwa tayari. Hivyo ndivyo. Amina.