Simama katika Kichaka Kitakatifu

Mkutano wa Ibada wa MEC wa Vijana • Mei 6, 2012 • Sacramento California


 

Habari za jioni ndugu na kina dada. Nahisi shukrani nyingi, bali pia nimenyenyekezwa sana, kupatiwa hii nafasi ya ajabu na Urais wa Kwanza kunena leo. Kwanza, ningependa ninyi mjue kwamba wakati mmoja nilikuwa sina kunyanzi, kichwa cheusi, na ujalivu wa maisha kama ninyi---sehemu ya kile maandiko yanaita “kizazi kinachoinukia.” Sina hakika jina la kinyume au wajina wa kuinuka ni nini labda “kuzama” au “kudidimia” ni---lakini lolote lile, linaelezea kipindi cha maisha nilichoko ndani yake sasa, na hakionekani cha kupendeza sana!

Ingawaje ninaongea nanyi kutoka kanisani karibu na Hekalu la Sacramento Calfornia, ninaweza kuona katika jicho la akili zangu maefu yenu---mkiongea lugha 40 tofauti---ambao mmekusanyika kote ulimwenguni. Nimebarikiwa kutembelea nchi nyingi zenu, kuwasikia ninyi mkiongea na kutoa ushuhuda katika lugha zenu za mama, na kushuhudia imani yenu na uchaji Bwana. Nawapenda na kuwasifu kwa wema wenu. Najua maisha katika umri wenu yanaweza kuwa na changamoto, na mimi najua wakati mwingine tunakosea na tunahitaji kutubu. Lakini nawashukuru kwa kutaka kusimama imara katika imani yenu katika Kristo na injili Yake ya urejesho. Upendeleo wangu usiku wa leo ni kwamba niweze kubarikiwa niongee kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kwa hivyo kuchangia katika ongezeko la imani yenu.

Mahali Patakatifu

Kuna mahali katika ulimwengu ambako kumetakaswa kwa kile kilichofanyika hapo. Kulingana na Agano Jipya, mojawapo wa mahali huku ni Sinai, Horebu, or “mlima wa Mungu,” ((Kutoka 3:1; ona pia Kutoka 3:12; 34:2), ambapo Bwana alimtokea Musa katika kichaka kichokuwa kikichomeka. Musa alipokuwa akikaribia hicho kichaka, Bwana alisema: “Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.(Kutoka 3:5).

Familia yangu nami wakati mmoja tulibarikiwa kusihi katika mahali patakatifu. Katika mwaka wa 1993---miaka minne baada ya wito wangu kwa wale Sabini---tuliombwa kuhudumu miaka miwili katika Misheni ya New York Rochester ya Kanisa. Hio misheni ilijumuisha mji wa Palmyra (ambako Joseph Smith na familia yake wakikuwa wakiishi wakati mwingi wa miaka ya 1820), na Fayette (ambako Kanisa lilitengenezwa katika Aprili 1830). Karibu maili 110 kusini mwa Palmyra katika Jimbo la Pennsylvania, ni sehemu ya Harmony (ambako Joseph Smith alikutana na Emma Hale na ndipo waliishi kama maarusi wapya wakati sehemu kubwa ya Kitabu cha Mormoni ilitafsiriwa katika miaka ya mwisho ya 1820). Hili eneo linajulikana kama “Chanzo cha Urejesho,” na hapa ndipo Kanisa lilizaliwa. Ni nchi ya kupendeza mno iliyo na vilima vya miti ya mbao, maziwa na vijito visafi, na watu wachangamfu na wakupendeza. Pia ni mahali palipofanywa patakatifu kwa sababu ya yale yaliyotokea hapo.

Kichaka Kitakatifu

Katika kichaka cha mti kama mifune, mialoni, mimapoli, na mti mingine, karibu robo maili magharibi mwa boma la Joseph na Lucy Mack Smith karibu na Palmyra, Joseph Smith wa umri wa 14 aliona katika ono Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, katika majira ya kuchipua ya 1820. Maonyesho haya matakatifu, kama jibu la maombi ya Joseph ili kujua ukweli kuhusu dini na jinsi angeweza kupokea ondoleo la dhambi zake, lilianzisha urejesho wa injili katika kipindi hiki cha mwisho. Pia ilifanya hiki kichaka cha miti kuwa mahali pa kutukuzwa katika historia ya Kanisa letu---mahali tunapopaheshimu kwa jina; “Kichaka Kitakatifu.”

Nilipokuwa nikihudumu kama rais wa misheni, familia yangu nami tulikuja kukipenda hicho kichaka cha miti na kuhisi utakatifu wake. Tulienda huko kila mara. Kila mwezi wakati wamisionari wapya walipowasili na wale waliokuwa wanakamilisha misheni zao wakiondoka, tuliwapeleka mahali hapo. Desturi yetu ilikuwa ni kukusanyika katika lango la kichaka na baada ya kuimba wimbo wa kufungua wa usiku wa huu---“Joseph Smith’s First Prayer” ”1—tuliwaalika wazee na kina dada kutawanyika na kutafuta sehemu ya faragha katika kichaka ambapo kina mmoja anaweza kuwasiliana na Mungu kwa maombi na kufanya na kuripoti masharti ya kibinafsi Kwake. Haya matembezi kwenye Kichaka Kitakatifu yalikuwa na hubakia kuwa uzoefu wa thamani kwa wote ambao wamebarikiwa kuyafanya.

Natambua,hata hivyo, kwamba ni idadi ndogo kati yenu ambayo itaweza kutembelea Kichaka Kitakatifu kibinafsi. Kwa sababu hii, katika majira ya kuchipua ya 2012---miaka 192 baada ya Ono la Kwanza la Joseph Smith---Ningependa mje pamoja nami kwa fikra katika Kichaka Kitakatifu. Simameni nami hapo, wakati ninaposhiriki nanyi kati ya twasira fulani za kichaka, sababu za upendo wangu kwa hapo mahali patakatifu, na masomo ya maisha yenye thamani mtu anayoweza kujifunza hapo.

Ninamshukuru Ndugu Robert Parrott, bwana misitu na mwanaviumbe, aliyeajiriwa na Kanisa, ambaye anaishi Palmyra, kwa kunifahamisha kati ya umaizi kuhusu Kichaka Kitakatifu ambao nitashiriki. Ingawaje bado yeye si mshiriki wa imani yetu, Ndugu Parrott uheshimu Kichaka Kitakatifu na hulipalilia na kukitunza kwa umahiri sana.

Thamathali ya Kiroho Inajumuisha Miti

Jinsi nilivyotembea kwa staha katika Kichaka Kitakatifu au kukaa nikiwa katika tafakari kwenye benchi zilizopo hapo, Mara nyingi nimetafakari juu ya utele wa thamathali ya kiroho inayojumuisha miti, matawi, mizizi, mbegu, matunda, na misitu. Adamu na Hawa, wazazi wetu wa kwanza, bila shaka walipokea somo la kwanza katika ukulima wa miti. Nabii Yakobo, akimnukuu Zenusi katika Kitabu cha Mormoni, alishiriki istiari changamani au hadithi ya miti ya mizeituni shamba na mizeituni mwitu kama anavyofunza kuhusu kutawanyika na kukusanyika kwa Israeli (see Yakobo 5). Na ni nani miongoni mwenu ambaye hajasoma, kusoma tena, na kwa maombi kutafakari mbegu ya imani ambayo Alma anatualika kuipanda ambayo kwa utunzaji makini na lishe sahihi litakuwa “mti utakaokua hata maisha ya milele”?(Alma 32:41; ona vifungu vya 27–43).

Na hivyo ndivyo ilivyo na Kichaka Kitakatifu. Mtazamaji makini wa mambo ya asili---hasa wakati anaambatana na mwanaviumbe wa uhodari wa Ndugu Robert Parrott---anaweza kujifunza masomo muhimu kutoka kwa mfumo wa ikolojia ule uliopo hapo. Ningependa kwa kifupi kushiriki masomo manne ya haya masomo nanyi usiku wa leo:

Masomo ya Maisha kutoka kwa Kichaka Kitakatifu

Somo nambari 1: Miti kawaida ukua ikielekea mwanga.

Jambo moja la kupendenza la kuonekana katika Kichaka Kitakatifu ni miti inayokua kandoni mwa msitu wa asili, pamoja na ile inayopamba mapito mengi ya ndani. Inakua ikielekea nje---ile kuepuka kivuli cha miti iliyo juu yake---na kisha kwenda juu ile kupata mwangaza wa jua. Mashina na matawi yaliyopinda yanaonekana bayana kulinganisha na miti jirani inayokua karibu wima kabisa. Miti, kama vile viumbe vinavyoishi, inahitaji nuru ili kukua na kunawiri. Inafanya kila kitu katika uwezo wake kupata mwanga wa jua inavyowezekana ili kudumisha usanidinuru---mafanyiko wa kugeuza nishati nuru kuwa nishati kemikali au “fueli” inayotumika na karibu viumbe hai vyote.

Nina hakika akili zenu changa na angavu, tayari zinajua hii sitiari kutoka kwa Kichaka Kitakatifu inapotuelekeza sisi! “Nuru” hata ni kichocheo muhimu zaidi katika uwanda wa kiroho kuliko ilivyo katika halisi. Hivi ndiyo ilivyo, kwa sababu nuru ni muhimu kwa ukuaji wetu wa kiroho na utimizaji wa uwezo wetu kamili kama wana na babinti wa Mungu.

“Giza” kinyume cha nuru na uashiria nguvu katika ulimwengu ambazo zinataka kututenganisha sisi na Mungu na kupinga mpango Wake mtakatifu kwa maisha yetu. Kwa kawaida ni baada ya giza au katika maeneo ya giza ambapo nguvu za uovu zinatia ushawishi wake mkubwa. Katika wakati huu wa maisha yenu, uvunjaji wa sheria ya usafi wa maadili, vitendo vya wivi, kucheza kamare, ukeukaji wa Neno la Hekima, na tabia zingine zilizokatazwa na Baba yetu wa Mbinguni, kwa kawaida zinafanywa gizani. Hata wakati tunachagua kufanya makosa wakati nuru ya mchana--- kwa mfano, kuiba mtihani, tunapoiba mawazo ya wengine katika kuandika mtungo wa mtihani, usengenyaji ovu kuhusu mtu, kutumia lugha chafu, au kulaghai---hatuwezi kukosa kuwa na hisia za gizani.

Kwa bahati nzuri, Roho wa Kristo “hutoa nuru kwa kila mtu ajaye katika ulimwengu; na Roho humwangazia kila mtu kote ulimwenguni, yule aisikilizaye sauti ya Roho.

“Na kila mtu aisikilizaye sauti ya Roho huja kwa Mungu, hata Baba” (M&M 84:46–47).

Hili fungu kutoka kwa Mafundisho na Maagano kwa uzuri linaelezea mfikio wa juu wa mtu, dhamira ya kiroho iliyotolewa na Mungu kiasili ambayo tunayo---kama hatutaisonga---kuenda kwenye nuru na kwa kufanya hivyo, kwenda kwa Mungu na Mwanawe na kuwa zaidi kama Wao. Juu Yake mwenyewe, Kristo alisema, “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 8:12).

Katika kuelewa maandiko, unaweza kujua sana kuhusu neno kwa kiambatanishi chake. Katika kujifunza maandiko kwako, utaweza kuona jinsi maneno nuru, Roho, kweli na Yesu Kristo yanapatikana katika ukaribu sana. Yanakaribia sana, na yote yanatuelekeza sisi juu hata juu sana na zaidi kwa njia takatifu ya maisha.

Kwa moyo wangu wote nawahimiza ninyi kuepukana na giza la dhambi katika maumbo yake potovu yote na mjaze maisha yenu na Roho, kweli, na nuru ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Mnaweza kufanya hivi kwa kutafuta marafiki wema, muziki na sanaa ya kuinua, elimu kutoka kwa vitabu bora (hasa maandiko), nyakati za maombi ya uaminifu, nyakati tulivu katika mazingira halisi, shughuli nzuri na mazungumzo, na maisha yanayolenga Kristo na mafundisho yake ya upendo na huduma. Kumbukeni daima, na hasa katika kutafuta mwenzi wa milele, tamko la Bwana kwamba “kweli huikumbatia kweli; wema hupenda wema; nuru huambatana na nuru” (M&M 88:40). Hii kanuni ya uzuri hukivutiwa ni uzuri---ikipatiana matumaini ‎kwamba kama tutaishi maisha katika nuru ya injili, hatimaye tutapata mwenzi akitembea mapito sambamba ya wema. Najua zaidi tunavyojitahidi kujaza maisha yetu wenyewe na nuru, patakuwa na nafasi kidogo sana ya hili giza na ndivyo hatimaye tutakaribia kuwa kama Kristo, Nuru ya Ulimwengu.

Kwa sababu ya baraka maalum ambazo ni zangu usiku wa leo katika kuongea nanyi vijana Watakatifu wa Siku za Mwisho wa kipekee, ningependa kupaza sauti ya onyo lakini pia sauti ya kutia moyo na matumaini kuhusu giza ambalo bila shaka litavamia maisha yenu kama mtajihusisha na picha za ngono. Kutumia vifaa vya picha za ngono kwa njia yoyote ile kunamchukiza Mungu na kunavunja amri Yake kwamba tusizini “wala usifanye chochote kinachofanana na hayo (M&M 59:6). Utumiaji wa picha za ngono daima uelekeza kwenye uvunjaji zaidi wa amri za usafi wa maadili. Kurudilia matumizi ya vifaa vya picha ngono na kushiriki katika aina za uvunjaji wa maadili kujamiana ambayo kwa kawaida hufuata kunaweza kuleta uteja ambao lazima ushughulikiwe na kutibiwa na utunzaji ule ule unaopatiwa uteja wa pombe au madawa.

Kama picha za ngono tayari zimeshaathiri maisha yako, na ni shida ya kudumu na mara kwa mara, nakuomba utafute usaidizi wa kidini na utaalamu. Tafadhali jua kwamba uteja wa picha za ngono sio “shida ndogo tu” ambayo unaweza kuishinda kwa maombi ya kisiri, kujifunza maandiko, na kujithibiti sana.

Kwa sababu uteja wa picha za ngono unawezakufifisha uwezo wako wa kuchagua mema badala ya maovu, utahitaji upole na unyenyekevu wa kuukubali Upatanisho wa Yesu Kristo na kubarikiwa na nguvu za kuwezesha za Upatanisho. Hii inamaanisha nini katika hali halisi, ni kwamba kama tutafanya jitihada zetu bora wenyewe---zile zinazojumuisha kupitia mfanyiko wa toba kwa usaidizi wa askofu wako au rais wako wa tawi ili kupokea msamaha wa dhambi na kupitia mfanyiko wa kupona unahitaji ushauri wa kitaalamu na labda uhimili wa kikundi cha kushinda uteja wako---nguvu za kuwezesha za Upatanisho (ambavyo Kamusi ya Biblia inaelezea kama njia takatifu ya usaidizi au nguvu2), utakusaidia kushinda shuruti za uteja wa picha za ngono na baada ya muda kuponya kutokana na madhara ya kuozesha. Kupitia uwezo wa Upatanisho, yote msamaha wa dhambi na kupona kutokana uteja yanawezekana na yote ni ya ajabu.

Tafadhali, epukana na giza, na kama miti, daima tafuta kukua kuelekea nuru.

Somo nambari 2: Miti huhitaji upinzani ili kutimiza kipimo cha uumbaji wake.

Dhana aina nyingi kuhusu usimamizi wa msitu zmefuatiliwa katika miaka mingi katika utunzaji wa Kichaka Kitakatifu. Wakati mmoja ploti ya majaribio ilichaguliwa, na mtindo unaojulikana kama “punguza miche” ulitumika. Ilitendeka hivi: watunza misitu walichagua ile waliyohisi kuwa miti michanga mikubwa na yenye afya katika ploti ya majaribio na kisha wangekata na kupogoa ile miti iliyokuwa isiyo mizuri na inayokuwa chini ya hiyo mingine. Kwa kufikiria kwamba kwa kuondoa kushindania maji, jua, na rutuba ya mchanga, miti ilichaguliwa ingeachiliwa kukua na kunawiri katika njia za ajabu.

Baada ya miaka kadha ilikuwa bayana kuwa kinyume ndio kilichokuwa kinafanyika. Mara ilipokuwa huru kutokana na ushindani, miti iliyochaguliwa iliridhika mno. Badala ya kunyoroka kuelekea nuru, ilipunguza ukuaji wao wa kuwa wima, ikafanya miguu mingi ya chini ambayo itakuwa bure wakati mwavuli utafanyika, na kunono sana. Hali, miti ambayo iling’olewa ilichomoa upya kama vichaka vya mshina mengi ambayo haitakuwa miti ya kufaa, lakini inaendelea kutumia maji na rutuba. Vichaka hivi viliendelea kushindana na miti iliyochaguliwa, lakini sio kwa njia ambayo italeta ukuaji mwema katika hiyo yote. Kama matokeo, hamna miti katika ploti ya majaribio ingelinganishwa na ukubwa au uzima na ile iliyokuwa katika hali ya halisi sana na ambayo ilishindana na kushinda upinzani ili kudumu na kustawi.

Kama mnavyojua, mojawapo wa mafundisho muhimu ya Kitabu cha Mormoni ni kwamba kuna lazima ya upinzani katika mambo yote. Ulimwengu wa upinzani upatiana uchaguzi kati ya mema na maovu, ili kwamba wakala utendeke. Kilicho muhimu pia, haya hivyo, ni kanuni ya upinzani ambayo lazima iwepo ili ukuaji wa kiroho kufanyika---au kama baba Lehi alivyosema---ili “utakatifu” uweze kutendeka (2 Nephi 2:11). Ningependa kusisitiza kwamba ufahamu wa hii kanuni---kwamba ukuaji wa kiroho unahitaji upinzani na dhiki---na hata kukubali hii kanuni katika umri wenu ni kuhimu katika kukubali na kuwa wenye furaha kwa kawaida maishani. Pia ni muhimu ili kupata uzoefu wa ukuaji na maendeleo ya kibinafsi yanayohitajika.

Sasa au baadaye, sisi sote tutakabiliana na upinzani na dhiki. Nyingine zake ziatakuja kiurahisi kama matokeo ya kuwa hapa katika maisha ya muda katika ulimwengu uliyo na ukengeufu. Ni jambo la kawaida kwa wanadamu wote. Upinzani kama huu unaweza kuchukua maumbo mengi. Inaweza kuwa na nguvu za asili. Inaweza kujumuisha maradhi na ugonjwa (Inaonekana kuweza kuambukizwa homa hata kama imechanjwa dhidi yake!). Inaweza kuja katika maumbo ya majaribu. Kwa wengine inaweza kuwa matarajio yasiyofikiwa (Ningependa kuwa mrefu futi 6 inchi 5”, lakini nimejifunza kuwa mwenye furaha na futi 5 inchi 9 nilizopewa, na kulazimisha kushushwa kwa mimbari ninapokuja kutoa hotuba). Inaweza kuwa katika umbo la upweke, upungufu wa kimwili na kiakili na ulemavu---orodha ya nguvu za upinzani haina mwisho---na vivyo hivyo baraka za ukuaji na maendeleo ya kibinafsi kama tuna imani ya kuchukua mtazamo mkubwa na kuvumilia yote vyema. Ninapata ufariji mkubwa kutoka kwa maneno ya Bwana kwa Joseph Smith katika Gereza la Liberty wakati mizigo ya Joseph ilikuwa migumu sana: “Fahamu wewe, mwanangu,kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako. (M&M 122:7).‎

Wakati mwingine upinzani na ugumu huja kwa sababu ya chaguzi zetu wenyewe zizizo sawa. Afya mbaya au majeraha ambayo yanatokana na maisha yasiyo na hadhari, maumivu makali na huzuni ambao hutokana na uvunjaji wa sheria za Mungu, majuto tunayohisi baada ya sisi kukosa kutumia wakati vyema na talanta tuzipatiwa---haya yote ni ya kujitakiya wenyewe. Ni shukrani jinsi gani sote tunafaa kuhisi kwa Mwokozi wetu ambaye Upatanisho Wake unapatiana njia kwetu ya kurekebisha kila kitu kilichovunjwa.

Nimetambua kwamba wakati tunakabiliwa na upinzani kila mara tunauliza “kwa nini”---Kwa nini mimi? Kwa nini sasa? Kwa nini haya?---hali kuuliza “nini” itakuwa bora zaidi. Wakati mmoja nilituma barua ya faraja kwa wenzi waliokuwa katika dhiki kwa sababu mume alikuwa anakufa kutokana na ugonjwa usio na tiba. Jibu lao lilikuwa la kunyenyekeza: walioorodhesha baraka ambazo Mungu alikuwa amewapatia wao katika miaka mingi ya wao wakiwa pamoja, na kisha kwa imani kushangaa “nini” ndio kile Mungu alikuwa anajaribu kuwafundisha wao katika haya mafunzo ya hitimisho.

Kuna miti katika Kichaka Kitakatifu ambayo Ndugu Parrott anaiita “miti silika.” Hii ni miti ambayo inaonyesha kwamba upinzani unaweza kufanya kazi kwa manufaa yetu na kwamba katika upeo wa ugumu kuna mengi ya kunufaisha. Hii miti inajibu na kutohoa na wakati mwingine kupona kutokana na maumbo tofauti za upinzani au dhiki---mpigo wa radi, dhoruba kali ya upepo, mlimbilizi ya theluji au barafu, kujitwalia na dhuluma za wanadamu wazembe, na hata wakati mwingine uchokozi wa mti jirani! Kutoka kwa hizi hali za dhiki pametokea miti shupavu na ya kupendeza sana kwa twasira katika kichaka. Kile inachoweza kukosa katika urembo wa ulinganifu, inafanya hivyo kwa ushupavu na silika.

Kutoka kwa uzoefu wa maisha yetu wenyewe naweza kushuhudia kwamba upinzani, ugumu, na dhiki inayozalisha silika na ukuaji. Kati ya uzoefu ulio na changamoto na mgumu wa maisha yetu wenyewe---hisia za kutojitosheleza na kujitambua wakati wa ujana, misheni yangu huko Ujerumani kama kijana, na kujifunza lugha ya Kijerumani, kupata shahada ya sheria na kufuzu mtihani wa mawakili, juhudi zangu kuwa mume na baba anakubalika na kukidhi familia yetu za watoto wanane kiroho na kimwili, kupoteza wazazi wangu na wapendwa wangu, hata huduma yangu ya umma ambayo mara nyingi ina matatizo kama Kiongozi mwenye Mamlaka (ikijumuisha matayarisho na kutoa hii hotuba kwenu usiku wa leo)---haya yote na zaidi, hata kama kuna changamoto na vigumu, imenipatia mimi uzoefu na imekuwa vyema kwangu!

Najua si rahisi kuwashawishi ninyi vijana kwamba uchungu kidogo ni vizuri kwenu, bali hakika ndivyo. Kama tutapokea “yote ambayo Baba alivyonavyo,” (M&M 84:38), haitatokea bila kufanya yote tunayoweza kama jibu. Baba yetu wa Mbinguni anataka wana na mabinti wema na kama Lehi alifunza, utakatifu unaweza kuja kupitia dhiki na majaribu. Watu, kama miti, wanahitaji upinzani ili kutimiza kipimo cha uumbaji wetu.

Somo nambari 3: Miti ukuaji vyema katika misitu, sio katika upekee.

Kama ukifikiria juu ya haya, katika uhalisi sio kawaida kuona mti umesimama peke yake. Mara nyingi inakusanyika katika kichaka, na baada ya muda mrefu, vichaka vinaweza kuwa misitu. Kichaka Kitakatifu, hata hivyo, ni zaidi ya kundi la miti. Ni changamano la mfumo wa ikologia ambao unajumuisha viumbe tofauti vya maua mwitu, vichaka, vijisitu, miti, ukungu, vivumwani, ndege, wanyama wagugunaji, sungura, paa, na viumbe vingine. Hivi viumbe huchamgamana na utegemea mmoja na mwingine kwa chakula, hifadhi, na mazingira umoja na ujamaa ambapo wote wanaweza kupata uzoefu katika majira ya maisha.

Mpango wa Mungu kwa maisha yetu unazingatia mshikamo na ujamaa huo huo kwetu. Tunafaa kutekeleza wokovu wetu pamoja, na si pekee yetu. Kanisa hujenga majengo ya mikutano, sio makao ya watawa. Tunaulizwa kuhudhuria kata au tawi mahususi---sio teua na kuchagua kusanyiko kama katika imani fulani. Hii sera ya hekima inatuhitaji sisi kujifunza kuelewana mmoja na mwengine na kuwajibika kwa askofu wetu au rais wa tawi tabia mbaya, na sio kutoroka na kijificha wakati mambo yamekuwa magumu! Tumeamriwa kuwapenda majirani wetu (ambayo inajumuisha wanafamilia), na kujifunza kuwapenda wale waliokaribu nasi mara nyingi vigumu kushinda kimbali “ulimwengu wote.” Kutoka mwanzo wa Urejesho, amri imekuwa kwa Watakatifu “njooni Sayuni,”ma kukusanyika kama jamii ambapo sisi tunaweza kujifunza kuishi na upatanifu na uhimili wa upendano mmoja wa mwingine kwa kuheshimu agano letu la ubatizo la “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine ... kuomboleza na wale wanaoomboleza .... na kufariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa” (Mosia 18:8–9). Kama watoto wa Mungu, sisi ahatuwezi kustawi peke yetu kuliko mti mpweke. Miti yenye afya inahitaji mfumo ikolojia; watu wenye afya wanahitajiana.

Bahati nzuri, ndani yetu sote kuna hamu ya ujamaa, kwa uenzi, kwa marafiki waaminifu. Kama washiriki wa familia ya milele ya Mungu, sisi sote tunatamani kutoshelezwa na usalama ambao urafiki wa karibu na wa kudumu unaweza kupatiana. Mtajifunza kwamba uundaji wa uhusiano kama huu huchukua muda, juhudi, na utele wa hisani. Kama Mormoni alielezea hivi, “hisani .... haitafuti mambo yake” ” (Moroni 7:45)— sio ajenda yake; sio upendeleo wake; sio furaha yake. Ingawaje intaneti na maeneo ya mfumo wa kijamii, hamna mubadala wa uaminifu, mawasiliano uria, na ana kwa ana ambayo lazima yatokee kwa uhusiano wa halisi na wa kudumu kuanzishwa.

Hasa nyumbani ndio maabara ya mapema na bora ya kujifunza ya kuelewa na wengine. Ni nyumbani ambapo tunajifunza masomo ya huduma, ukarimu, msamaha, na subira ambayo ni muhimu kwa kuanzisha uhusiano wa kudumu na wengine. Nafikiria kwa hii sababu kwamba sehemu ya kuwa “mstahiki wa hekalu” ni hitaji kwamba tuishi kwa upendo na upatanifu na wanafamilia yetu.

Ya kufurahisha, kundi la maongozi la Kanisa pia linapatiana nafasi na fursa ambapo tunaweza kukua kijamii. Kutoka kwa miaka ya ujana sana na uzee sana sisi ni wa kata au tawi na tuko kwenye hali ambayo uhusiano na wengine na kijamii unaweza kustawi. Katika wito, mikutano, madarasa, jamii, mabaraza, shughuli, na nafasi zingine tofauti tofauti za uhusiano, tunaweza kuendeleza sifa na ujuzi wa kijamii ambao utatusaidia kujitayarisha kwa mipangilio ya kijamii ambayo itakuwepo huko mbinguni. Katika kuongea kuhusu huu mpangilio wa juu, Bwana kupitia Joseph Smith alisema: “Na kwamba uhusiano huu huu uliopo miongoni mwetu hapa utakuwepo miongoni mwetu kule, isipokuwa utazidishiwa utukufu wa milele, utukufu ambao sasa hatuufaidi. (M&M 130:2).

Kama tunatumainia kufurahia ujamii wa mbinguni na utukufu husika katika dunia ijayo, tunahitaji kuendelea kukomaa kijamii pamoja na kiroho wakati tuko hapa ulimwenguni. Watu, kama miti wanakua vyema katika jamii, na si katika upekee.

Somo nambari 4: Miti hupata nguvu kutoka kwa rutuba iliyotengenezwa na vizazi vilivyopita vya miti.

Kulikuwa na kipindi cha nyakati katika kupalilia Kichaka Kitakatifu wakati wale waliokuwa wanakisimamia waliamua kwamba kichaka kinafaa sura ya kuchanwa vyema. Mradi ya huduma kwa vijana na wamisionari ilipangwa mara kwa mara kuondosha miti iliyoanguka na mashina, magugu, na hata visiki na majani yaliyonyauka. Chini ya mpango huu, haukuchukua muda kabla ya uzima wa kichaka kuanza kufifia. Ukuaji wa miti ilienda pole, miti michache mipya ilichomoza, aina mpya ya maua mwitu na mimea ilianza kupotea, na idadi ya wanyama mwitu na ndege ikapungua.

Wakati Ndugu Parrott alipochukua usimamizi wa kichaka miaka fulani iliyopita, alipendekeza kwamba kichaka kiwachwe kiwe katika hali halisi iwezekanavyo. Miti iliyoanguka na mashina iliwachwa kuoza na kurutubisha mchana. Majani yawachwa pale yalianguka. Wageni waliombwa kutembea katika mapito yaliyowekwa alama ili kwamba kichaka kisiaribiwa na mchanga katika kichaka usishindiliwe. Katika miaka michache tu, kichaka kilianza kufufuka na kufanyika upya chenyewe kwa njia ya ajabu. Leo kinanawiri katika hali njema sana, kikiwa na mimea iliyostawi sana na utele wa wanyama mwitu.

Somo la kujifunza kutokana na uzoefu huu katika usimamizi wa misitu ni wakifu kwa moyoni mwangu. Kwa miaka saba sasa imekuwa nafasi yangu kuhudumu kama Mtaalum wa historia na Mwandishi wa Kumbukumbu wa Kanisa. Hii ni ofisi ambayo ilianzishwa na Nabii Joseph Smith kama kutenda amri ya Bwana kwake katika ile siku Kanisa lilitengenzwa: Tazama, pawepo na kumbukumbu itakayotunzwa miongoni mwenu” (M&M 21:1). Kutoka siku hiyo---kuanzia uteuzi wa Oliver Cowdery kama Mtaalum wa historia na Mwandishi wa Kumbukumbu wa Kanisa.---na kuendelea hadi wakati huu---kumbukumbu ya ajabu ya historia ya Kanisa yetu imewekwa. John Whitmer aliteuliwa badala ya Oliver Cowdery na aliambiwa na Bwana kuweka historia ya “mambo yote muhimu” …. mambo yote yatakayokuwa kwa faida ya kanisa, na kwa vizazi vinavyo chipukia vitakavyokua katika nchi ya Sayuni” (M&M 69:3, 8).

Kwa nini tunaweka kumbukumbu na kukusanya, kuhifadhi, na kushiriki historia kunakuwa na kipaumbele muhimu katika Kanisa la Yesu Kristo? Kwa nini ni muhimu ninyi kuwa sehemu ya “kizazi kinachochipuka” cha leo ili kushungulikia na kupata nguvu za kizazi kilichopita?

Kama jibu, nashauri kwamba haiwezekani kuishi kikamilifu sasa---sembuse kwa mpango wa kudura yako ya siku zijazo---bila msingi wa yaliyopita. Ukweli huu ililetwa kwa nguvu kwa usikilivu wangu miezi iliyopita katika kukutana na wenzi ambao wana uzoefu wa majaribio yasiyokuwa ya kawaida ambayo ninashiriki kwa idhini. Baada ya miaka fulani ya ndoa na kuzaliwa kwa watoto kadha, mke alihusika na ajali mbaya. Alibakia hospitali kwa majuma kadha katika hali ya kukosa fahamu. Alipopata fahamu, alikuwa ameathiriwa na kupoteza kumbukumbu kabisa! Kwa kweli hakuwa na historia. Bila kumbukumbu ya yaliyopita, hakuwa na kitu cha kurejelea. Hakumjua mmewe, watoto wake, wala wazazi wake! Mmewe alipokuwa akinihadithia hadithi hii, iliniambia kwa siri kwamba katika hizo miezi ya mapema baada ya ajali, alikuwa na hofu kwamba mke wake angepota kama angewachwa peke yake. Pia aliogopa kwamba mke wake angempenda tena. Wakati wa uchumba, alikuwa mwembamba, kijana mchangamfu aliyejaa nywele kichwani. Sasa, miaka ya katikati, yeye alikuwa kitumbo na upara!

Kwa yote bahati nzuri, angalau sehemu ya kumbukumbu ilikuwa imewekwa. Mmewe alikuwa amehifadhi barua za mkewe kabla na baada ya misheni yake. Hii inaonyesha ushahidi wa kwamba hawa wawili walikuwa kwa kweli wapenzi. Pia alikuwa ameweka shajara ambayo ilikuwa na mambo ya kusaidia sana. Pole pole, baada ya miaka, huyu mke alipata sehemu kubwa ya mambo yake yaliyopita kurejesha kwake kupitia kushiriki hiyo historia ya wapendwa wake.

Hii hali ya kipekee na hisia ororo inaonyesha vyema umuhimu wa uhusiano wa yaliyopita na ya sasa na siku zijazo. Inatusaidia sisi zaidi kutambua maelezo ya kweli ya Bwana kama ilivyofunuliwa kwa Joseph Smith: “Ukweli ni maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa” (M&M 93:24). Elimu ya vitu tiliyonayo ya yaliyopita kwa sababu ya kumbukumbu ambazo zimewekwa, na ya yatakayokuwa kwa sababu ya maandiko na mafundisho ya kinabii ya manabii hai, hutupatia sisi muktadha ambao unatuwezesha matumizi mema ya wakala wetu katika maisha yetu ya sasa. Matokeo yake, elimu hii inatupatia sisi mtazamo wa uungu kwa sababu inatuleta karibu na uwezo Wake kuwa na "vitu vyote …. mbele ya macho [Yake]” (M&M 38:2).

Kama washiriki wa Kanisa kutoka mataifa mengi, sote tunashiriki historia ya Kanisa kwa njia ya sawa. Ni muhimu kwetu sote kujifahamisha historia yetu ya Kanisa, hasa “hadithi zake za uanzilishi.” Hizi hadithi---Ono la Kwanza la Joseph Smith, kuja kwa Kitabu cha Mormoni, matembezi ya kimalaika ya Yohana Mbatizaji, Petero, Yakobo, na Yohana, Eliya, Elia, na wengine---zina kweli za kimsingi ambazo kwazo urejesho wa injili unatoa kiini.

Cha kuhuzunisha, katika nyakati hizi za tekinolojia ambapo habari zimetapakaa---kati ya matukio muhimu na watu katika historia ya Kanisa---Watakatifu wa Siku za Mwisho wanatingisika katika imani yao na kuanza kutilia shaka imani zilizoshikiliwa. Kwa watu wenye shaka kama hawa nawaenezea upendo wangu na ufahamu na hakikisho kwamba kama wanashikilia kanuni za injili na kwa maombi kushikilia kujifunza kwao kwa historia ya Kanisa---kujifunza vya kutosha ili kupokea elimu kamili kabisa badala ya vipande vipande au elimu isiyo kamili---Roho Mtakatifu atathibitisha imani yao katika matukio muhimu katika historia ya Kanisa kwa kusema imani katika akili zao. Kwa njia hii wazika nanga katika uthibitisho wao kuhusu historia ya Kanisa la urejesho na tena “kuchukuliwa na kila upepo wa elimu” (Waefeso 4:14). Nimekomelea njia ya maisha yangu yote kwenye hisia za amani kuhusu Ono la Kwanza la Joseph Smith na yale matukio mengine ya kimsingi ya historia ya Kanisa, kama vile wengi wenu mmefanya, na najua hamtaangushwa.

Historia katika hali ya kimsingi sana ni kumbukumbu ya watu na maisha yao na kutoka kwa maisha hayo hutokeza hadithi na masomo ambayo yanaimarisha kila tunachoamini, kila tunachotetea, na kile tunachofaa kufanya tunapokabiliwa na dhiki. Sio hadithi zote ambazo zilizo katika historia yetu ni za upeo kihalisi kama vile Ono la Kwanza la Joseph Smith au misheni ya Wilford Woodruff huko Uingereza. Kwa kweli, nyingine ni hadithi za ajabu kutoka kwa maisha ya Watakatifu wa Siku za Mwisho wa kawaida sana. Hizi hasa ni wakifu na zenye usaidizi kwetu zinapokuwa hadithi za kuhusika wa wahenga wetu wenyewe.

Kwa mfano, katika miaka ya 1920 babu na bibi Jensen---licha ya kazi ya sulubu ya masaa mengi---walilazimika kumrudishia muuja shamba walilokuwa wananunua na ambalo walikuwa wameishi ndani yake katika Jimbo la Idaho. Walikuwa wanataka kurudi katika mji wao katika Utah pamoja na watoto lakini hawangeweza kuondoka Idaho mpaka walipe deni la $350. Hii inaweza kuonekana kama kiwango kidogo leo, lakini wakati huo kilikuwa kikubwa mno. Babu yangu alijaribu kukopa pesa kutoka kwa watu ambao waliokuwa nazo, lakini hakufanikiwa. Kukopa kutoka kwa benki hakungewezekana kwa sababu ya hali yao ya ufukara. Yeye na bibi waliomba ili wapate usaidizi kila siku. Jumapili moja katika mkutano wa ukuhani, mtu ambaye babu hakumjua kabisa alikuja kwake na kumwambia alikuwa amesikia shida zake na atamkopesha babu $350 kwa matarajio kwamba wakati babu atarudi Utah, atamlipa mtu huyu upesi iwezekanavyo. Huu mkataba ulikamilishwa kwa kupenyana mikono na babu akaweka ahadi yake.

Hii hadithi rahisi iliyoandikwa na babu yangu Jensen ni hazina ya familia. Hunitia motisha kwa kuonyesha sifa za kuchapa kazi, uaminifu, kushinda dhiki, umoja wa familia, na muhimu sana, inaonyesha mkono wa Mungu katika maisha ya babu zetu waaminifu. Ninapata nguvu na motisha kutoka kwa mfano wao na kutoka kwa mfano wa wengine, wote wakuu na wa kawaida, wa vizazi vilivyopita.

Mnaweza kupata hadithi zilizofanana na hizi katika nchi yenu wenyewe na katika familia yenu wenyewe. Pale zinapopatikana, nawasihi mzikusanye hadithi hizi, msihifadhi, na mzishiriki. Muwe makini kizipitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Watoto wangu ( na hasa sasa wajukuu wangu) daima wanazipenda wakati ninapowasimulia hadithi juu ya “wakati nilipokuwa mvulana mdogo”! Nimepata kusikia kwamba watu hawawezi kuwa wakuu kushinda hadithi zao, na naamini hivyi ndivyo ilivyo kwa familia. Hadithi nzuri---kama ni kweli---ufanya historia nzuri. Kumbuka, watu kama vile miti hupata nguvu kutoka kwa rutuba iliyotengenezwa na vizazi vilivyopita.

Hitimisho

Sasa, nikihitimisha, nataka ninyi mrudi pamoja nami hata kwenye Kichaka Kitakatifu na kusimama pamoja nami hapo karibu na mmoja wa inayoitwa “miti shahidi.” Hii miti ambayo ilikuwa ikikua katika kichaka kwa miaka 192 iliyopita wakati wa Ono la Kwanza la Joseph Smith. Kuna mitatu kati yao ambayo bado hiko hai katika kichaka na mitatu ya miti shahidi iliyoyauka imesimama kwa sababu ya juhudi za uhifadhi wa umahiri wa Ndugu Parrott.

Wakati nilipokuwa nikihudumu misheni yangu Palmyra, wakati mwingine nilikuwa nikienda katika Kichaka Kitakatifu peke yangu na kusimama kwa staha karibu miti shahidi nilioupenda. Nilikuwa nikifikiria kwamba kama mti huu ingeweza kusema, ungeweza kuniambia kile ulichoshuhudia ile siku ya majira ya kuchipua ya mwaka wa 1820. Lakini kwa kweli sikuhitaji ule mti kuniambia---tayari nilikuwa nikijua. Kwa sababu ya uzoefu wa kiroho na hisia kuanzia ujana wangu na kuendelea mpaka saa hii sasa, nimekuja kujua, bila kutegemea mtu yeyote yule, kwamba Mungu, Baba yetu yu hai. Najua, pia kwamba Mwanawe Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa binadamu wote. Najua kwamba Viumbe wawili watukufu walimtokea Joseph Smith katika Kichaka Kitakatifu katika majira ya kuchipua ya mwaka wa 1820. Walimuinua Joseph Smith kama nabii wanzilishi wa hiki, kipindi cha mwisho cha injili. Akifanya kazi chini ya usimamizi Wao mtakatifu, Joseph Smith alitafsiri Kitabu cha Mormoni, alipokea funguo za ukuhani na mamlaka, na kutengeneza Kanisa la Kristo tena katika hizi siku za mwisho. Tumebarikiwa sana kuishi katika nyakati hizi na kuwa washiriki wa Kanisa la Kristo.

Hizi kweli tukufu, ambazo nimeshuhudia, zina mwanzo wake katika Kichaka Kitakatifu. Kama ulivyosimama kitamathali pamoja nami katika Kichaka Kitakatifu usiku wa leo, vivyo hivyo simameni daima akilini mwenu na katika mioyo yenu katika mahali patakatifu na kuishi halisi kwa kweli ambazo Mungu alianza kufunua hapo.

Kumbuka, pia, masomo ya maisha ambayo Kichaka Kitakatifu hufunza:

  1. Wakati nguvu za giza zinapojaribu kukuangamiza---kama zilivyofanya wakati mmoja kwa kijana Joseph Smith aliyekuwa akitafuta, simama katika Kichaka Kitakatifu na ukumbuke nguzo ya nuru, zaidi mng’aro wa jua (ona Historia ya Joseph Smith 1:15–17)

  2. Wakati upinzani na dhiki inaposongea katika njia yako na matumaini kudidimia, simama katika Kichaka Kitakatifu na ukumbuke kwamba “kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako” (M&M 122:7).

  3. Wakati upweke na upekee ni tatizo lako, na unasumbuka kutengeneza uhusiano wa kibinadamu wa kutosheleza, simama katika Kichaka Kitakatifu pamoja na jamii ya Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao wamefanya agano la kubeba mizigo yako na kukufariji wewe katika mahitaji yako.

  4. Na wakati uzoefu, au watu, au kweli zinazokanganya zinakupatia chamgamoto katika imani yako na kutia hofu kuhusu urejesho wa injili ya Yesu Kristo, simama katika Kichaka Kitakatifu na hupate nguvu na motisha kutoka kwa vizazi vya Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu ambao walisimama imara mbele yako.

Haya ndio maombi yangu kwenu, rafiki zangu vijana, na nayatoa kwa upendo na katika jina la Yesu Kristo, amina.

© 2012 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Kiingereza kiliidhinishwa: 5/12. Tafsiri iliidhinishwa: 5/12. Tafsiri ya Stand in the Sacred Grove.Language. PD50039048 743

Muhtasari

  1. Hymns, no. 26.

  2. Ona Bible Dictionary, “Atonement”; ona pia Guide to the Scriptures, “Atone, Atonement,” scriptures.lds.org.