Nitajitolea Kwake

Russell  T. Osguthorpe

Rais Mkuu wa Shule ya Jumapili

Ibada ya MEK kwa Vijana Watu Wazima • Novemba 3, 2013 • Brigham Young University

 

Ni fursa nzuri sana kuwa nanyi usiku wa leo, ndugu na dada zangu wapendwa vijana. Nataka mjue jinsi ilivyo baraka kwa mke wangu nami kuwa nanyi jioni hii. Tunapowatazama, tunaona uwezekano usiohesabika. Mmejawa na uwezo. Haijalishi matumaini yenu yako juu kiasi gani, niko hapa kuwaambia yanaweza kuwa hata juu zaidi. Mnaweza kutimiza zaidi katika maisha haya kuliko vile mnavyojua. Na Bwana akiwa upande wenu, mnaweza kuona miujiza. Mnaweza kufanya kitu kile ambacho kwa mara ya kwanza mlidhani hakiwezekani. Mnaweza kushinda tatizo lolote. Mnaweza kupanda juu ya chochote kile ambacho kingeweza kuwavuta chini. Mnaweza kukataa uovu na kukumbatia kila kitu ambacho ni kizuri. Mlikuja duniani kwa kusudi fulani, na kwa msaada wa Bwana mtafikia kusudi hilo.

Natumaini mnatambua ni wangapi wanawaombea. Kuna maombi mengi sana yanayotolewa katika Kanisa hili kila siku kwa ajili ya vijana wa Kanisa---kwa ajili ya vijana wazima. Wakati mwingine, mnapokuwa na muda mtulivu, ninawaalika mtafakari juu ya maombi yote yanayotolewa kila siku mahususi kwa ajili yenu----kizazi kinachoinukia. Sala katika mahekalu, sala za Viongozi Wakuu Wenye Mamlaka na maafisa wakuu wa Kanisa, sala za viongozi wa vigingi na kata, na sala za wazazi, wana familia wengine, na marafiki. Mimi husikia sala hizi nyingi. Huwa za dhati. Natumaini mtatafakari juu ya nguvu zinazovutwa kutoka mbinguni kwa niaba yenu.

Na natumaini mnahisi kupendwa, si tu na wale ambao wanawajua, lakini na wale wote ambao wanawajali na kuwajali hata kama kamwe hawajawahi kukutana nanyi.Najua kwamba kama Rais Monson angalikuwa hapa leo, angeelezea upendo wake kwenu. Tuna nabii aliye hai ambaye anawapenda vijana wa Kanisa hili.

Mke wangu nami tunaishukuru sana kwaya hii kwa kuimba wimbo “I Will Give Myself ti Him.”. Tuliuandika wimbo kwa ajili ya wamisionari wetu tulipokuwa tunahudumu katika Misheni ya South Dakota Rapid City, na tunashukuru kwa ajili ya Steve Shank, aliyeupangia kwaya.Lakini maneno yanatumika kwa kila moja wetu maishani mwetu wote. Mstari wa kwanza unasema:

Alijitolea kwa ajili yangu, Alikufa ili niweze kuishi.
Ninaweza kumfanyia nini? Ninaweza kutoa nini kweli?1

Haya ni maneno ya mtu anayetafakari juu ya baraka za Upatanisho, baraka za kuhisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo. Sote tuna nyakati kama hizi---nyakati ambapo tunajua Bwana anatujali.

Nawaalika hivi sasa mtafakari juu ya baraka mnazohisi kama washiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na kama kuna mtu katika mkusanyiko huu ambaye anafikiria kujiunga na Kanisa, ninakualika utafakari juu ya baraka unayotafuta. Kisha ningependa ushiriki baraka hiyo na mtu ambaye ameketi karibu nawe. Kama humjui mtu huyo---ni bora zaidi---mnaweza kujuana mnaposhiriki. Hivyo basi, shiriki baraka nyingi muwezavyo kwa dakika moja ama mbili zifuatazo.

Hivi karibuni nilialika kikundi cha wanafunzi nyumbani kwangu ili kujadili mada ya jioni hii. Acheni tuone walisema nini nilipowauliza washiriki hisia zao kuhusu baraka maishani mwao:

Mwanamume 1: Ufahamu nilio nao---ufahamu wa mpango wa wokovu, Baba yangu wa Mbinguni, na kile Yeye apendacho na kile Yeye atakacho kwangu, na kujua nini ninaweza kufanya ili niishi maisha yangu kwa upatanifu na kile anachotaka kutoka kwangu. Baraka zinazotokana na nguvu za kuunganishwa na kutoka mahekalu duniani---nikijua kwamba tunaweza kuwa na familia yangu milele, kama familia.

Mwanamke 1: Ufahamu wa Upatanisho, na kisha uwezo na nafasi ya kupata nguvu zitokanazo na Upatanisho. Wingi wake ni kupitia maagizo ya ukuhani na kuhisi kwangu uhusiano wa kweli na Baba yangu wa Mbinguni kupitia maagizo hayo na maagano ambayo ninafanya Naye. Kuwa na nguvu katika maisha yetu, kuwa na uwezo na mambo yote ambayo tunahitaji ili kurudi Kwake.

Mwanamke 2: Nafasi na fursa ya kuwa na karama ya Roho Mtakatifu pamoja nasi wakati wote, kuongoza maamuzi yetu katika kuwasilisha dhamira zetu na kutupatia faraja hiyo na nguvu ya kufaulu katika maisha haya na baadaye kuwa Naye milele.

Mwanamume 2: Nahisi kama zote hizi ni baraka za ukuhani ambazo zinapatikana kwa wanaume na wanawake. Ninashukuru kwa kweli kwa ajili ya ukuhani ambao ulirejeshwa ili kwamba tuweze kuwa na baraka hizi zote: hekalu, Roho Mtakatifu, nafasi ya kutumia Upatanisho.

Mwanamke 3: Ninashukuru jinsi gani kujua ninaweza kuendelea na kwamba maisha haya hayahusu kuwa na ubaridi ama kuwa bila msimamo---ama kukaa mahali popote. Yanahusu kusimama juu na kwenda mahali fulani. Na kwangu mimi, maendeleo ni muhimu, kujua kwamba hicho hutendeka na kwamba bado kinaweza kutendeka hata baada ya kifo.

Mwanamume 3: Kitabu cha Mormoni. Kama mwanafunzi mimi hutumia muda mwingi kusoma mambo ambayo mimi huwa na ulinzi wa juu---kama, Je, hii ni kweli? Wana mawazo gani? Je, ninawezaje kuchuja mambo yote ambayo wanayasema? Lakini nahisi kama naweza tu kuvivua viatu vyangu, kwa njia ya kusema, ninaposoma Kitabu cha Mormoni. Kwa sababu ni cha kweli tu---kilitafsiriwa kwa karama na nguvu za Mungu.

Hivyo basi, bila injili ya urejesho ya Yesu Kristo, hatungekuwa na baraka zozote ambazo rafiki zangu wamezitaja hivi punde. Kutafakari juu ya baraka zetu kunatupa nguvu ya kusonga mbele maishani, lakini sote tunajua kwamba kusonga mbele kuna changamoto. Haya ni maisha ya duniani, na maisha ya duniani si rahisi. Aya mbili za pili za wimbo kwaya iliimba zinasema:

Wakati wengine wanapogeuka, wakati hakuna anayeonekana kujali,
Nawezaje kuhisi upendo Wake? Nitajuaje Yeye yupo pale?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Uchungu na huzuni ujapo kwa wale wanaouliza swali kwa nini,
Nitawaleteaje amani? Nitawasaidiaje kujaribu?2

Wakati huu ninawaalika muandike---ama muweke kumbukumbu akilini---ya changamoto ambazo mnakumbana nazo hivi sasa katika maisha yenu, wasiwasi ambao wakati mwingine huwafanya muwe macho usiku.

Niliwauliza marafiki zangu ambao walikuja nyumbani kwangu changamoto zao zilikuwa nini na haya ndiyo waliyosema:

Mwanamke 2: Mawazo mengi moja kwa moja! Jambo moja nililokuwa ninalifikiria ni kwamba ni rahisi kuweka thamani yako na utambulisho wako pamoja na mafanikio: bado sijaoa, au sijapata shahada ya elimu ama shahada ya uzamili, au mambo hayo ambayo unafanya ama haukamilishi.

Mwanamume 2: Kudumisha kiwango cha kiroho tulichokuwa nacho tulipokuwa tunahudumu kwa muda kwa ajili ya Bwana. Hicho ni kitu ambacho lazima nichague kila siku, kama nitaweza kuendelea na tabia zile zile ambazo nilikuza misheni au la.

Mwanamume 1: Mojawapo ya mambo makubwa ambayo yalileta Roho katika maisha yetu wakati wa misheni ilikuwa nafasi yetu ya kutumikia na kushiriki ushuhuda ambao unaendelea kupitia mafundisho ya nyumbani na kupitia ushirika –pamoja na nafasi kubwa ya kufanya mambo mengi ya maana. Na Roho ile ile inaweza kuwa nasi tunapowahudumia wengine.

Mwanamume 3: Kupata uwiano sawa kati ya kuongozwa na Roho na msukumo katika maamuzi ambayo unafanya katika maisha yako na kuyafanya tu. Baadhi ya watu wanaonekana kama wana muongozo mwingi kutoka kwa Bwana. Na baadhi ya watu wanalazimika tu kufanya kazi na kwenda kabla ya kujua ni nini kilicho cha haki na nini kisicho cha haki.

Mwanamke 1: Mandhari makuu, kama vile baraka zilizochelewa na kuelewa kwamba zitakuja wakati fulani. Lakini kuwa tu na ile imani na uaminifu na kuwasilisha mapenzi yetu kwa Baba yetu wa Mbinguni.

Mwanamke 3: Kwa nini mambo mabaya hutokea kwa watu wema? Ama mambo magumu---hasamambo magumu kweli kweli---hutokea kwa watu wema ? Hiyo imekuwa kitu ambacho kimekuwa akilini mwangu. Kwa mfano, nimekuja kujua hivi karibuni kwamba baba yangu ana saratani. Na niliwaza, “Hiyo inawezaje kufanyika kwa mtu ambaye amehudumu sana?”

Bila kujali changamoto yenu ni gani, ninashuhudia kwamba mada tutayojadili jioni hii inaweza kukusaidia kuishinda.

Kwa kuanza, hebu tufikiri kwa muda juu ya ibada yetu ya mwisho ya MEK. Katika baraka ya kitume ambayo Mzee Russell  M.Nelson alitamka siku hiyo. Alisema, “Ninawabariki ... kwamba mapenzi [ya Mungu] yatimizwe na ninyi na kupitia ninyi.”3 Zingatia nguvu ya maneno haya. Kama mapenzi ya Mungu yanafaa yafanywe nasi na kutupitia sisi, basi mapenzi yetu yanahitaji kuwa sawa na ya Mungu. Tunahitaji kutaka kile anachotaka .

Mzee Neal  A. Maxwell aliwahi kusema: “Unapojiweka mapenzi yako kwa Mungu, unampatu kitu cha pekee ambacho unaweza kwa kweli kumpa ambacho ni kweli chako cha kutoa. Usingoje kwa muda mrefu mno kupata madhabahu au kuanza kuweka zawadi ya mapenzi yako juu yake!”4

Jioni hii ninawakaribisha mzingatie nami maswali matatu: (1) Ni nini maana ya neno mapenzi? (2) Tunawezaje kutoa mapenzi yetu kwa Mungu? Na (3) Tunawezaje kujua kwamba tunafanikiwa ?

Kwanza ,neno mapenzi linamaanisha nini? Mara nyingi huwa hatuzungumzii kuhusu mapenzi, angalau kwa kutumia neno hilo. Wakati mwingine sisi husema “utashi”. Kwa mfano, “Sina tu utashi wa kupinga keki ya jibini hiyo .”Hivyo basi mapenzi ni “mvutio wa kufanya kitu,”5  tamaa inayotufanya tutenda.

Ukiwauliza watu katika Marekani waseme ni vitu gani viwili vya umuhimu kwa afya yetu ya kimwili, karibu asilimia 95  wanasema “chakula bora na mazoezi”---kama vile tungedhania. Kisha, ukiwauliza watu hawa hawa, “Je, unakula vyema na kufanya mazoezi ya kutosha?” ---mnadhania watasema nini? Kati ya asilimia 5  na10  husema huwa wanafanya hivyo. Kuna pengo la wazi kati ya kujua kitu na kukifanya. Watu wengi wanajua kile wanachopaswa wafanye, lakini wachache wana mapenzi ya kukifanya.

Mfano kutoka misheni yetu unaonyesha kwamba tunapopata msaada tunaweza kuendeleza mapenzi ya kufanya kile tunapaswa kufanya.

Mmoja wa wasaidizi wetu katika misheni yetu siku moja alimwambia mwenzake, “Ona, nimeongeza ratili 30 tangu nije misheni. Siwezi kwenda nyumbani hivi. Je, unaweza kunisaidia kupoteza kiasi cha uzito?” (Alikuwa katika timu ya mpira wa kikapu, na hakuwa anataka kuridi akiwa vile.)

Mwenziwe alikubali.

Muda mfupi baada ya hayo nilikuwa nikiwafuata hawa wamisionari wawili katika mstari wa maamkuli. Mmisionari ambaye alitaka kupoteza uzito alienda kuchukua keki ya brownie. Mwenziwe alimnong'oneza masikioni mwake, “Huhitaji hiyo.”

Mmisionari aliyekuwa na njaa, akiwa ameudhika kidogo, alisema,“Ah, ndio, ninaitaka.”

“La, hakika huhitaji hiyo, kweli huhitaji,” alimshauri mwenzake.

Mmisionari hakuichukua ile keki ya brownie.

Hivyo basi, mmisionari huyu alitaka kupunguza uzito, lakini alihitaji msaada kukabiliana na tamaa yake ya keki ile ya brownie. Kumbuka laini ile katika wimbo iliyosema, “Nitawasaidiaje kujaribu?”Mwenziwe alikuwa anamsaidia mmisionari mwenzake kujaribu kufanya kile alichotaka kwa kweli kufanya lakini hangefanya bila msaada kidogo kutoka nje kutoka kwa mtu mwingine. Alikuwa anajaribu kumsaidia mmisionari huyu kuona kwamba nia yake ya kuwa na afya nzuri ingeweza kushinda tamaa yake ya keki ile ya brownie. Alikuwa anajaribu kumsaidia kuimarisha mapenzi yake.

Adui angetutaka tuamini kwamba hakuna kitu kama mapenzi- kwamba hatuna chaguo ila kufuata misukumo yetu alisi---kula keki za brownie nyingi tuwezavyo. Baadhi huamini kimakosa kwamba mapenzi yetu yameamuliwana jeni yetu, na kwamba hatuna udhibiti wakati wote juu yake.

Ili kuonyesha swali hili lina umuhimu, ninashiriki sehemu kutoka makala ya habari ya hivi karibuni. Mwandishi ni profesa aliyeheshimiwa wa biolojia. Hivi ndivyo anavyoanzisha insha yake yenye kichwa “Why You Don’t Really Have Free Will.”(Kwa Wewe Hauna Hasa Mapenzi Huru.”) Kichwa hiki kilinivutia kwa sababu, kama mshiriki wa Kanisa, najua kwamba tuna mapenzi.

Anaeleza kwamba maamuzi tunayofikiri tunayafanya, hatuyafanyi hasa kamwe. Akizungumzia uchaguzi tuliofanya wa kifungua kinywa asubuhi hii, anasema: “Unaweza kuhisi ni kama umefanya uchaguzi, lakini katika hali halisi ya uamuzi wako … kula mayai ama gole [asubuhi hii] kuliamuliwa muda mrefu kabla uwe na ufahamu juu yake----pengine hata kabla uamke leo. Na mapenzi yako hayakuwa na sehemu katika uamuzi huo.”6

Hivyo, anasema kwamba hatuna dhamira, hatuna udhibiti juu ya tamaa zetu. Tuko chini ya kile jeni yetu inachotulazimishatu. Niliposoma makala hii, nilitaka kumwambia kuhusu mmisionari wetu. Kwa kweli alifanyauamuzi. Alipoteza paundi zake 30. Dhamira yake ilishinda matamanio yake ya kimwili.

Tunajifunza kutoka kwa ufunuo, ya kale na ya kisasa, kwamba tuna wakala, kwamba tuna mapenzi, kwamba tuna hamu, na kwamba hamu hizo zinaweza kubadilika. Mzee Russell  M. Nelson, katika mkutano mkuu wa hivi karibuni, alisema:“Tunaweza kubadili tabia zetu. Hamu zetu zenyewe zinaweza kubadilika. Kwa jinsi gani? ... Mabadiliko ya kudumu ... yanaweza kuja tu kwa njia ya uponyaji, utakaso, na nguvu ya kuwezesha ya Upatanisho wa Yesu Kristo.”7

Wakati Mzee Maxwell aliposema kuwa mapenzi yetu ndio jambo la kipekee tunaloweza kweli kutoa kwa Mungu, alikuwa anafundisha kwamba chochote kingine tunachotoa ni kitu ambacho Mungu tayari alitupa. Tunapotoa zaka au sadaka , tunamrudishia tu Mungu kile alichotupa kwanza. Fedha yoyote tunayolipwa katika maisha haya, kwa mfano, huja kwetu kwa sababu ya viumbe vya Mungu. Tukitoa wakati wetu, tunatoa kile ambacho Mungu tayari alitupa---siku zetu duniani. Lakini tunapotoa mapenzi yetu kwake, tunajitolea kikamilifu, bila kuzuia chochote.

Haya ndiyo yale rafiki zangu walisema pale nilipowauliza watafute maandiko na kisha watoe mawazo yao kuhusu maana ya neno mapenzi:

Mwanamume 3: Kuwa " tayari kukubali vitu vyote [ambavyo] Bwana anaona vinafaa kuja juu [yao] hata kama vile mtoto kunyenyekea kwa baba yake.”8 Basi hiyo ni kuongea kuhusu kujiweka chini na kukubali kwako, kuwa tayari. Kisha tukajipata tukizungumza kuhusu suala hilo, na likatuelekeza kwa andiko hili lingine katika Helamani 3.

Mwanamume 1: Helamani 3:35—“Ndio, hata kwenye kusafishwa na utakaso wa mioyo yao, utakaso ambao huja kwa sababu ya wao kumtolea Mungu mioyo yao.”

Mwanamke 3: Hii huwa haifanyiki mara moja, sidhani , lakini ni dhahiri kwamba ni mchakato ambao huja kwa wakati na kazi.

Mwanamke 2: Nahisi karibu kama unapata kasi unapofanya uchaguzi sahihi. Ni rahisi kufanya uchaguzi sahihi wakati ujao. Maombi na kujifunza maandiko kila siku na kutafakari na kuandika katika jarida.

Mwanamke 2: katika Mosia 5:2, inazungumza kuhusu mabadiliko makuu ndani yetu na mioyoni mwetu kwamba hatuna “tamaa ya kutenda maovu, lakini kutenda mema daima.”

Mwanamke 1: Inafurahisha kwa sababu tulikuwa tunasoma maandiko haya haya, lakini tulikuwa tuna mazungumzo tofauti kabisa. Kweli nilidhani kwamba hilo lilikuwa kuu zaidi katika Helamani 3:35, kuhusu kujitolea mioyo yetu kwa Mungu na jinsi hiyo inatutakasa. Nadhani inahusisha uaminifu mwingi kujitolea Kwake na kusema, “La , nitaamini hivi sasa kwamba mpango wako ni kamilifu. Nitakupa mapenzi yangu na kukuruhusu kuniunda na kuwa yule ambaye unahitaji miwe.”

Mwanamume 2: Tulikuwa tunazungumza juu ya Vita Mbinguni---jinsi tulivyopigana kwa ajili ya wakala, jinsi tuliamua kumfuata Kristo na kufanya kile Yeye angetaka tufanya. Tulizungumzia jinsi katika maisha haya ni karibu vita vya wakala. Je, tutachagua kutaka kile Kristo angetaka, kuwa kama vile Yeye alivyo, badala ya kusema tu kwamba tutafanya vitu ambavyo anatutaka tufanye----je, tutataka kuvifanya?

Hivyo basi, kutoa mapenzi yetu kwa Bwana haina maana kwamba tunaachilia wakala wetu. Katika hali halisi, kinyume ni kweli. Zaidi tunavyotoa mapenzi yetu kwa Bwana, ndipo zaidi uwezo wetu wenyewe wa kutumia wakala wetu wa kimaadili unakua. Kujua kile ambacho Mungu anataka tujue, kusema kile anachotaka tuseme, kufanya kile anachotaka tufanye yote inatuelekeza kuwa kile anachotaka tuwe. Mungu alitupa wakala ili tuweze kijitolea wenyewe kwake, si ndio tuweze kukabiliwa na majaribu.

Unapoangalia ndani na kuchimba chini kwa kina, unaweza kupata hamu ambazo hukuelekeza kwa matendo yako ya maana sana kwako. Utagundua kwamba mimi sikusema “ambazo huelekeza kwa hatua yoyote” ---kwa sababu baadhi ya vitendo vyetu huwa havishawishiwi na hamu zetu za kina kabisa na za kudhaminiwa sana nasi. Baadhi ya vitendo hutendeka kwa mawazo kidogo. Baadhi ya vitendo hata huonekana kwenda kinyume kabisa na kile tunachotamani zaidi.

Mvulana siku moja alikuja kwangu kwa ajili ya kusaidiwa katika mchakato wa toba. Akieleza huzuni aliyoihisi kwa ajili ya kile alichokuwa amefanya, alisema, “Nikiangalia nyuma, siwezi kuamini kweli nilifanya hivyo. Ni kama mtu mwingine alikifanya na si mimi.” Moyoni mwake hakutaka kufanya alichokifanya , lakini kwa namna fulani mtu wa asili alimdhibiti , na alikubali ushawishi wa adui badala ya ushawishi wa Roho Mtakatifu , ambaye angemsaidia kupinga majaribio.9 Alikuwa anazungumzia mapenzi. Alitaka kuwa mzuri, lakini kulikuwa na sehemu ndani yake---kilele cha mapenzi yake---ambayo bado hakuwa ameyatoa. Alikuwa anazuia sehemu hiyo ndogo, na hiyo ndiyo iliyomwelekeza kufanya kitu alichojuta. Lakini alikuja kwa kiongozi wa ukuhani ili kufanya mambo yawe vyema - awe yule ambaye kweli alikuwa, mwana mwaminifu wa Baba yake wa Mbinguni. Alikuja ili aweze kujaribu kutoa mapenzi yake yote kwa Bwana, mara hii akiwa hazuii chochote.

Mvulana huyu alipata mabadiliko ya moyo. Alikuwa “hana[ tamaa ] ya kutenda maovu , lakini kutenda mema daima.”10 Hamu zake zilikuwa zimebadilika, na kwa sababu hamu zake zilikuwa zimebadilika, mwenendo wake pia ulibadilika. Alikuwa anamweka mbali yule mtu wa asili na kujitolea kwa ushawishi wa Roho Mtakatifu. Mabadiliko ya moyo ni mabadiliko ya nia , si tu mabadiliko ya vitendo. Tunahitaji kufanya mambo mema, lakini hata zaidi, tunahitaji kuyafanya kwa sababu ya haki.

(bofya ili kuona ukubwa)

Mchoro huu unanisadia kuelewa uhusiano kati ya nia yetu ama hamu na matendo yetu. Tunapokuwa kwenye njia ya agano la uanafunzi, nia zetu ni safi na matendo yetu ni ya haki. Sisi hufanya mambo mema kwa sababu tunampenda Bwana na watoto Wake. Lakini pia inawezekana kufanya jambo jema kwa nia isiyo adilifu. Basi tunatenda kama wanafiki---tunafanya mema kwa sababu tunataka kuonekana kuwa wema, ama kwa sababu tunataka kuonekana bora kuliko mtu mwingine.

Tukifanya tendo lisilo la haki na nia ovu, sisi ni , kama vile maandiko yasemavyo, “ [tunaasi] dhidi ya Mungu kwa kimakusudi.”11 Wale katika sura hii wanafurahia mambo mabaya ambayo wanafanya. Lakini tunapotaka kwa kweli kuwa wema lakini tunateleza na kuanguka, kujitoa kwa mtu wa asili au mwanamke aliye ndani yetu. Tunapojiona sisi weneyewe tupo popote isipokuwa katika njia ya ufuasi, tunahitaji kukaribia kwenye mamlaka ya Upatanisho kwa kutubu, na tutakuwa tena kwenye njia ya haki.

Mchakato huu wa toba hakika ni mchakato wa kubadilisha hamu. Ni utaratibu wa kuweka nafasi ya Roho. Na tunapoweka nafasi ya Roho, hakuna nafasi ya dhambi iliyobaki.

Hivyo basi, dhamira yetu ni nguvu ya pamoja ya hamu zetu au nia. Mapenzi yetu inaongoza vitendo vyetu. Hivyo basi, ni jinsi gani tunaendeleza kuimarisha mapenzi yetu? Tunawezaji kuyatoa mapenzi yetu kwa Bwana? Ninaialika kwaya iimbe tena kiitikio cha wimbo walioimba mwanzoni mwa ibada yetu jioni hii. Sikilizeni kwa makini wakati huu kwa maneno.

Nitasema kile anachotaka kisemwe, nitafanya kile anachotaka kifanywe.
Nitakuwa shahidi kwa ulimwengu wa Mwana Mpendwa wa Mungu
Nitajitoa Kwake, moyo wangu, mapenzi yangu, nafsi yangu.
Daima nitaimba upendo unaokomboa , wimbo unaonifanya niwe mzima.12

Sote tunaweza kusema kile anachotaka kisemwe.

Nilipokuwa nikihudumu kama rais wa kigingi, nilimuhoji dada ambaye alikuwa ameolewa hivi karibuni. Nilimuliza, "Je, ni ndoa yako inaendelea vipi?”

Alijibu,“Naam, ni sawa, nadhani. Hatupigani sana sana.”

Nilimuliza,“Unamaanisha nini, sana sana ?"

Alisema, “ Naam, unajua , wanandoa wote hupigana.”

Nilimjibu , “Si wanandoa wote. Mke wangu nami huwa hatupigani. Wazazi wangu hawakupigana.”

Kisha tulikuwa na mazungumzo mazuri kuhusu jinsi yeye na mume wake wanavyoweza kuzungumza kwa upendo kuliko kwa upinzani au kwa ukali.

Tunaweza kusema kile ambacho Bwana angetaka tuseme. Tunaweza kuondoa ukali kutoka kwenye maneno yetu na sauti yetu. Tunaweza kuinua na kujenga wengine badala ya kuwaleta chini.

Siku moja niliandamana na Mzee Jeffrey  R. Holland kupanga upya urais wa kigingi. Tulipoingia hotelini tulipokuwa tunakaa, alitambua karani wa hoteli na kumwuliza, “Je, yule mpenzi wako mzuri yuko vipi?”

Alisema, “Oh, tuliachana wiki chache tu zilizopita.”

Alisema,“Naam, utapata mwingine, na atakuwa mwema zaidi.”

Alitabasamu, na tukaondoka. Siku iliyofuata nilitazama Mzee Holland akiwapongeza washiriki na viongozi, mmoja baada ya mwingine. Aliifanya kwa urahisi kwa njia za asili sana ili kwamba kila mtu tuliyekutana naye alihisi vyema kuhusu wenyewe na kuhusu maisha---kwa sababu tu aliwainua juu.

Tunaweza kufanya hivi. Kama Mwokozi angekuwa hapa, angeinua kila mtu katika njia Yake, kama tu vile alivyofanya alipokuwa hapa duniani. Sote tunaweza kusema kile anachotaka kisemwe.

Mtu anaponiuliza ninahisi vipi kuhudumu na Viongozi Wakuu Wenye Mamlaka, jambo la kwanza ambalo huja akilini mwangu ni upendo ambao mimi huhisi ninapokuwa karibu nao. Mtu anaweza kufikiri kwamba kusimama kwenye jukwa katika Kituo cha Mkutano Mkuu inatisha mno kwa sababu Urais wa Kwanza na wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili wameketi nyuma yako unapozungumza. Lakini wao hukupa kwa njia fulani hisia kuwa unaweza kweli kufanya hivyo.

Mara tu unapomaliza kuzungumza, Wale Kumi na Wawili hunyosha mikono yao na kukushukuru kwa mchango wako kwenye mkutano unapotembea kurudi kitini mwako. Mara ya kwanza hii ilitendeka, nilishangazwa kidogo. Si​kutarajia waonyeshe hisia zao kwa kiwango hicho, lakini wao huwa hivyo. Wao hujenga kila mtu katika njia yao kama vile tu Mwokozi alivyofanya. Hii kwa kweli ni fadhila mahususi ya Rais Monson.

Rais Monson huonyesha upendo kwa kila mtu. Kufuatia kikao kimoja cha mkutano wa Oktoba, Rais Monson alimwona mvulana mdogo akimpungia mkono hewani. Aliinama kwenye reli na kumwashiria kijana aje karibu. Kisha akamshika mkono. Mvulana huyu kwa kueleweka alijawa na furaha sana.

Katika tukio lingine, kufuatia onyesho katika Kituo cha Mkutano, Rais Monson alibaki baada ya mkutano kusalimia kwa mikonoya vijana alivyoweza. Alitembea kwenye jukwaa na kuwakaribia kundi la vijana wenye ulemavu mkali. Hata ingawa vijana hawa hawangeweza kujibu kwa maneno kwa Rais Monson, tabasamu nyusoni mwao zilionyesha jinsi gani walifurahia salamu yake mkononi na mamkio ya upendo.

Kama tunawafikia wengine, basi uwezo wetu wa kufikia hata zaidi huongezeka. Hii ni moja ya viashiria wazi kwamba tunatoa mapenzi yetu kwa Mungu.

Hivyo basi, tunaweza kusema kile ambacho Bwana anataka tuseme. Tunaweza pia kufanya kile anachotaka tufanye. Wakati mwingine vitendo hujalisha zaidi kuliko maneno.

Tulipokuwa tunalea familia yetu, mke wangu alipata maambukizo makali na ilibidi alazwe hospitalini. Nilikuwa najaribu kukidhi familia na kuwatunza watoto wetu wadogo watano alipokuwa anapata nafuu. Lakini sikuhitajika kufanya kazi kwa nguvu kulisha familia. Chakula kililetwa mlangoni mwetu kimoja baada ya kingine---kingi sana, kwa kweli, hatungekila chote. Hivyo basi, nilianza kuweka vyakula hivi katika friza mapka ikajaa.

Vitendo hivi vinaweza kuonekana kuwa vidogo kwa kulinganisha na baadhi ya vitendo vya huduma ya huruma, lakini Mimi nitawaambia kwamba milo hii ilikuwa na maana sana. Iliniokoa. Mke wangu alikuwa dhaifu, nami nilikuwa nimekata tamaa. Lakini ningeenda kwenye friza na kuona nini kilikuwa chakula cha jioni hiyo. Na kila mlo wale washiriki wazuri wa kata walileta mlangoni mwetu, walikuwa wanatoa mapenzi yao kwa Mungu. Walikuwa wanafanya kile alichotaka kifanywe.

Washiriki hao wa kata walikuwa na nia safi ya kusaidia familia iliyo na haja, lakini inawezekana kufanya jambo jema kwa nia mbaya. Kisha, kama vile maandiko yanafundisha, kitu kizuri tunachofanya kwa kweli kinahesabiwa kama kiovu kwa sababu ya moyo wetu haukuwa ya haki.13 Tulilifanya jambo jema, lakini tulilifanya kwa kusitasita. Hivyo basi, nia huwa kila kitu. Tunahitaji kutaka kile ambacho Mungu anataka. Tunahitaji kusema kile anachotaka kisemwe kwa sababu ttunataka kusema kile anachotaka kisemwe. Tunahitaji kufanya kile anachotaka kifanyike kwa sababu tunataka kufanya kile anachotaka kifanyike. Na tunahitaji kuwa shahidi wa Mwana Mpendwa wa Mungu kwa sababu tunataka kuwa shahidi. Basi tunajua tunatoa nafsi yetu yote Kwake---hakuna kipande kidogo chetu kinachotaka kufanya kitu kinyume na mapenzi Yake.

Kusema na kufanya mambo ya haki huwa rahisi tunapofanya ahadi na Bwana.

Maagano huwa na jukumu kuu katika kukuza mapenzi. Tunapobatizwa, tunaahidi kuchukua jina la Bwana juu yetu--- kufanya kile angetaka tufanye. Kisha, kila siku ya Sabato tunalifanya upya agano hilo. Tunashuhudia upya kwa Baba yetu wa Mbinguni kwamba bado tuko tayari kuchukua jina la Bwana juu yetu na kumkumbuka na kushika amri Zake. Kila wakati tunapochukua kwa ustahiki kipande cha mkate cha sakramenti katika mikono yetu ama kukiweka kile kikombe cha maji kwenye midomo yetu ,tunatoa mapenzi yetu Kwake. Tunasema, “Nitakuwa shahidi kwa ulimwengu wa Mwana Mpendwa wa Mungu.”14

Tunapounganishwa katika hekalu kwa mpenzi wetu ya milele, sisi tena hufanya maagano ambayo yanaimarisha mapenzi yetu. Tunaweza kuhisi nguvu ya kuimarisha ya Upatanisho kila wakati tunapoingia nyumba takatifu ya Mungu. Ni pale ambapo tunaahidi kujiweka wakfu kwake Bwana. Hii ndiyo sababu Mzee Maxwell alisema, “Usisubiri muda mrefu mno kwenda kwa madhabahu [na] kuweka karama ya mapenzi yako juu yake.” 15 Huenda alikuwa akizungumza kwa njia ya mifano, lakini alikuwa, naamini, pia akizungumza wazi wazi kuhusu jinsi tunavyoweza kutoa mapenzi yetu kwa Mungu kwa kufanya na kuweka maagano Naye.

Hivyo basi, tunafanya tuwezavyo ili kujitoa Kwake--- moyo wetu, mapenzi yetu, nafsi zetu. Zaidi tunavyofuata njia hii, ndivyo zaidi Bwana atatubariki na upendo Wake. Na zaidi tunavyohisi upendo Wake, ndivyo zaidi tunavyojua tunafanikiwa katika kutoa mapenzi yetu Kwake.

Natumaini tunajifunza kitu jioni hii ambacho kitatusaidia kutimiza baraka za Mzee Nelson kwamba mapenzi ya Mungu yaweze kufanywa nasi na kupitia kwetu. Nilipowauliza marafiki zangu kile walichokuwa wamejifunza, hivi ndivyo walivyosema:

Mwanamume 2:: Nadhani mara nyingi nimeshirikisha wakala na kutoa mapenzi yangu kwake Mungu, na hii imenisaidia kuona kama mambo mawili tofauti. Ninahisi kama huwa nafanya mambo mengi mema, lakini sasa hiyo inanifanya nitake kwenda na kulisafisha lengo ili niweze kuwa kama vile atakavyo.

Mwanamke 2: Ninapenda kufanya miunganisho. Ninafikiria, sawa, hiki ndicho kinachotokea katika maisha yangu, na ala, hiki ni kile nilichokuwa ninajifunza, na oh, mtu huyu alisema hayo. Na, hivyo, nadhani nimekuwa tu nikifanya miunganisho mingi.

Mwanamume 1: Bila kujali changamoto zetu, tunahitaji tu kutoa zaidi wenyewe kwa Mungu. Ni kama vile Rais Eyring husema, “mambo yanavyoonekana kuwa magumu leo, yatakuwa bora katika siku ifuatayo kama [sisi] tutachagua kumtumikia [Mungu] siku hii.”16

Mwanamume 3: Kutoa moyo wako na mapenzi yako kwa Mungu ... jambo la kwanza Yeye hufanya nayo ni kuwa Yeye huyatakasa. Siyo kama sisi sote tunatoa mioyo yetu kwa Mungu Naye anaiweka katika kuba kubwa na kusema, “Ndiyo, moyo moja zaidi yangu kufurahia.” Yeye huuchukuwa na kuutakasa na kuuthibitisha na kuturudishia na kusema, “Sasa nenda uutumia huu na kufanya mambo makubwa.” Sikuwahi kuwaza kuhusu kile ambacho hutendeka baada ya kuupatiana Kwake. Nilidhani kwamba hiyo ilikuwa ndiyo mwisho, lakini hiyo ni mwanzo tu.

Mwanamke 3: Najua sijui kila kitu, na inaonekana kama zaidi ninavyojifunza, zaidi ninavyotambua kiasi gani sijui. Lakini najua kwamba Mungu yu hai. Na nadhani leo ilikuwa tu uthibitisho zaidi ya hayo---kwamba anafahamu na kweli anajali na kusubiri na anataka tubariki watoto Wake, na hao ndiyo sisi.

Mwanamke 1: Karibu siku tatu zilizopita nilipata baraka ya ukuhani kwa kitu kinachokuja katika maisha yangu. Na kitu kilichosemwa katika baraka kilikuwa jinsi ninahitaji kuwa na tumaini zaidi katika Mungu na kuwasilisha mapenzi yangu. Lakini kwa sababu fulani, wakati wa baraka hiyo nilihisi hasa kabisa kwamba nilihitaji kwenda na kusoma juu ya hayo na kile yanamaanisha nini kwa kina zaidi? Hayo yanabadilisha vipi vitu ninavyofanya kila siku na siku mzima na jinsi ya kujiwasilisha kikamilifu kwake.

Hivyo basi, kutoa mapenzi yetu na Bwana ni kitu tunachofanya kila siku. Siyo tendo lililosimama peke yake. Si mwisho, lakini ni mwanzo tu. Tunaweza kusema kile anachotaka kisemwe. Tunaweza kufanya kile anachotaka kifanywe. Tunaweza kuwa shahidi kwa ulimwengu wa Mwana Mpendwa wa Mungu---yote kwa sababu tunataka kufanya mambo haya. Wakati mabadiliko haya yanatendeka mioyoni mwetu, shukrani zetu kwa Upatanisho huongezeka kiasi kikubwa kwamba tunaimarishwa nayo daima.

Alma alisema, “Ikiwa mmesikia kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi, ningeuliza, mnaweza kuhisi hivyo sasa?”17

Wimbo wa upendo wa ukombozi ni wimbo wa furaha katika Upatanisho wa Yesu Kristo. Si lazima wimbo ulio na maelezo na maneno. Ni wimbo wa hisia. Maneno tunayoweza kutumia kutoa shukrani zetu tunapotaka kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi yanabadilika kila mara, kutegemea na baraka mahususi tunayopokea. Lakini hisia hii ya shukrani kwake Mwokozi ni kama wimbo. Unaweza kujicheza wenyewe tena na tena katika moyo wetu kila wakati tunapofikiria jinsi Mkombozi ametuokoa kutoka kwa kila kitu ambacho kingetuvuta chini.

Hiyo ndiyo sababu Alma aliuliza ikiwa tulihisi kuuimba sasa. Sasa ndiyo wakati unapofaa. Ikiwa tunahisi kufurahia katika Upatanisho wa Yesu Kristo sasa hivi, basi moyo wetu uko sawa. Tunatoa mapenzi yetu Kwake, Naye anaimarisha mapenzi yetu. Ikiwa tunavutiwa kwa mambo ya dunia, moyo wetu hauko sawa. Na mapenzi yetu hayaimarishwi.

Katika sehemu ya mwisho ya Kitabu cha Mormoni, Wanefi, ambao kwa mara moja walikuwa wamekuwa watu wema, waligeuka mbali na Bwana. Walianza kujivunia kwa nguvu yao wenyewe badala ya kufurahia katika nguvu ya Bwana. Waliasi kimakusudi dhidi ya Mungu. Na nini kiliwatendekea? Waliachwa kwa nguvu yao wenyewe---kwa kiwango kwamba walipoteza kila kitu.18

Hatutaki kufanya hivyo. Tunajua hatuwezi kufanikiwa pekee yetu katika maisha haya. Hatuwezi kamwe. Tunahitaji msaada wa Bwana. Tunahitaji msaada wa kila mmoja. Hatuwezi kamwe kutegemea nguvu zetu wenyewe peke yake. Mikono ya Bwana iliyonyoshwa inatukaribisha kuimarishwa Naye ili kwamba kamwe hatuachwi kwa nguvu yetu peke yake.19

Najua kwamba tunaweza kukubali mwaliko wake kuja na kuimarishwa, kuja na kusamehewa, kuja na kuhisi upendo Wake usio na kipimo. Kisha, kwa moyo ulio na tabasamu, tutataka kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi.Sio tu mara moja kwa muda. Tutakaka kuimba wimbo huu daima. Tunapohisi nguvu ya kufanya kitu kigumu, tutauimba wimbo moyoni mwetu. Tunapokubali ukweli utupata na kupanua nafsi zetu, tutauimba wimbo. Tunapohisi kusamehewa, tutauimba wimbo. Na tunapohisi upendo Wake, tutauimba wimbo.

Kila wakati tunapouimba, tutakuwa tunatoa mapenzi yetu Kwake, karama ya pekee ambayo tunayo ya kumpa. Hatakubali tu karama hii. Ataipanua na kuiimarisha. Atatufanya kujisikia kuwa na uwezo zaidi. Atatusaidia kuongeza uwezo wetu wa kupenda na kupendwa . Atatuongoza kutoka gizani hadi katika nuru. Atatuponya na kutusaidia kwa njia ambazo zinatuwezesha kusamehe na kusamehewa.

Ninashuhudia kwamba Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu . Ninashuhudia kwamba Baba Yake alitupenda zaidi ya kutosha hata kumtuma duniani ili kuishi na kufa kwa ajili yetu. Najua kwamba hili ni Kanisa Lake. Najua kwamba nabii Wake aliye hai, Rais Thomas  S. Monson, anaelewa mahitaji ya washiriki wa Kanisa na anajua jinsi ya kutusaidia kupata njia yetu ya kurudi nyumbani. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

© 2013 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Kingereza kiliidhinishwa:1/13 Tafsiri Iliidhinishwa: 1/13. Tafsiri ya I Will Give Myself to Him. Swahili PD50048935 743.

Onesha Kumbukumbu

  Muhtasari

 1.  

  1. Russell T. Osguthorpe and Lola Osguthorpe, arr. Steve Schank, “I Will Give Myself to Him” (2009).

 2.  

  2. Russell T. Osguthorpe and Lola Osguthorpe, “I Will Give Myself to Him.”

 3.  

  3. Russell M. Nelson, “Youth of the Noble Birthright: What Will You Choose?” (Church Educational System devotional, Sept. 6, 2013); LDS.org.

 4.  

  4. Neal A. Maxwell, “Remember How Merciful the Lord Hath Been,” Ensign au Liahona, May 2004, 46.

 5.  

  5.  Oxford English Dictionary, “will”; oed.com.

 6.  

  6. Jerry A. Coyne, “Why You Don’t Really Have Free Will, USA Today, Jan. 1, 2012; usatoday30.usatoday.com/news/opinion/forum/story/2012–01–01/free-will-science-religion/52317624/1.

 7.  

  7. Russell M. Nelson, “Decisions for Eternity,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 108.

 8.  

  8.  Mosia 3:19.

 9.  

  9. Ona Mosia 3:19.

 10.  

  10.  Mosia 5:2.

 11.  

  11.  Mosia 15:26.

 12.  

  12. Russell T. Osguthorpe and Lola Osguthorpe, “I Will Give Myself to Him.”

 13.  

  13. Ona Moroni 7:9.

 14.  

  14. Ona Moroni 4:3; 5:2.

 15.  

  15. Neal A. Maxwell, “Remember How Merciful the Lord Hath Been,” 46.

 16.  

  16. Henry B. Eyring, “This Day,” Ensign au Liahona, May 2007, 91.

 17.  

  17.  Alma 5:26.

 18.  

  18. Ona Helamani 4:13.

 19.  

  19. Ona Mathayo 11:28.