Kwamba “tusinywe … Kusita” (M&M 19:18)

Mkutano wa Ibada wa Vijana Wazima • Machi 3, 2013 • Chuo Kikuu cha Texas Arlington


 

Mimi nina shukrani kushiriki katika mkutano wa ibada huu pamoja na watu vijana wa Kanisa kutoka kote ulimwenguni. Nawapenda ninyi na kufurahia nafasi hii ya kuabudu pamoja.

Susan ameongea na kushuhudia juu ya kweli muhimu, na kila mmoja wetu atabarikiwa na kuimarishwa tunapotumia kila mara mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku. Susan ni mwanamke mwema, bibi mteule, na kipenzi cha maisha yangu.

Nimeshatafakari na kumsihi sana Baba yetu wa Mbinguni ili nijue jinsi ninavyoweza kuwahudumia vyema usiku wa leo. Naomba nguvu za Roho Mtakatifu ziwe pamoja na kila mmoja wetu---kwamba tuweze kufikiria kile tunahitaji kufikiria kuhisi kile tunahitaji kuhisi, na kujifunza kile tunachoweza kujifunza ili tuweze kufanya kile tunachojua kuwa tunafaa kufanya na hatimaye kuwa kile Bwana anatamani sisi tuwe.

Mfuasi wa Dhati na Mfano Kutosita

Mzee Neal A. Maxwell alikuwa mfuasi mpendwa wa Bwana Yesu Kristo. Alihudumu kama Mshiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili kwa miaka 23, kutoka mwaka wa 1981 hadi 2004. Nguvu za Kiroho za mafundisho yake na mfano wake wa ufuasi wa uaminifu uliwabariki na unaendelea kuwabariki kwa njia ya ajabu washiriki wa Kanisa la urejesho la Mwokozi na watu wa dunia.

Mnamo Oktoba 1997, Dada Bednar nami tulikuwa, tumemkaribisha Mzee na Dada Maxwell katika Chuo Kikuu cha Brigham Young---Idaho. Mzee Maxwell alikuwa awahutubie wanafunzi, wafanyakazi, na wahadhiri katika mkutano wa ibada. Kila mmoja hapo chuoni alingojea kwa hamu matembezi yake katika chuo hiki na alijitayarisha kwa hima kupokea ujumbe wake.

Mapema mwaka huo, Mzee Maxwell alikuwa amefanyiwa tibakemikali ya siku 46 kwa ugonjwa wa saratani ya damu yenye uchungu sana. Muda mfupi baada ya matibabu yake na kufutiwa kutoka hospitalini, aliongea kwa muda mfupi katika mkutano mkuu wa Kanisa wa Aprili. Kuendelea kurudi katika hali ya kawaida na kuendelea kwa tiba kuliendelea vyema kutoka miezi ya kuchipua hadi miezi ya joto, ingawa nguvu za kimwili na uthabiti wake ulikuwa umepungua wakati alipotembelea Rexburg. Baada ya kuamkuana na Mzee na Dada Maxwell katika uwanja wa ndege, Susan nami tulisafiri kwa gari hadi nyumbani kwetu kwa mapumziko na mlo wa mchana kabla ya mkutano wa ibada.

Katika hali ya mazungumzo yao siku hiyo, nilimwuliza Mzee Maxwell mafunzo gani aliyojifunza kutokana na ugonjwa wake. Nitakumbuka daima jibu wazi na la kupenya alilotoa. “Dave,” alisema, “Nimejifunza kutosita ni muhimu zaidi kuliko kustahamili.”

Jibu lake kwa maulizo yangu ilikuwa ni kanuni ambayo kwayo yeye alipata uzoefu mwingi wa kibinafsi wakati wa tibakimekali. Mzee Maxwell na mkewe walikuwa wanaendesha gari kwenda hospitalini mnamo Januari 1997, siku hiyo alikuwa amepangiwa kuanza raundi ya kwanza ya matibabu, waliegesha gari kwa maegesho na kutulia kwa wakati wa faragha pamoja. Mzee Maxwell “alivuta na kushusha pumzi na kumtazama [mkewe]. Akachukua mkono wake na kusema …, ‘Mimi sitaki kusita’” (Bruce C. Hafen, A Disciple’s Life: The Biography of Neal A. Maxwell [2002], 16).

Ujumbe wake wa mkutano mkuu wa Oktoba 1997, wenye kichwa cha “Kutumia Damu ya Upatanisho ya Kristo,” Mzee Maxwell alifunza kwa uthabiti:“Tunapokumbana na majaribu … yetu wenyewe na masumbuko, sisi pia humsihi Baba, kama vile Yesu alifanya, kwamba ‘tusiweze … kusita’---kumaanisha kurudi nyuma au kujikunja (M&M 19:18). Kutosita ni muhimu zaidi kuliko kustahamili! Hata hivyo, kunywa kikombe kichungu bila ya kuwa na machungu vivyo hivyo ni sehemu ya kufuata mfano wa Yesu” (Ensign, Nov. 1997, 22).

Jibu la Mzee Maxwell kwa swali langu lilinifanya nitafakari juu ya mafundisho ya Mzee Orson Whitney, ambaye alihudumu kama mshiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili: “Hakuna maumivu tunayoteseka, hakuna majaribu ambayo tunapata ambayo yanakuwa ni bure. Yanahudumia elimu yetu, kwa ukuaji wa sifa kama vile uvumilivu, ustahimilivu na unyenyekevu. Yale yote tunayoteseka, hutakasa mioyo yetu, hupanua nafsi zetu, na kutufanya wapole na wenye hisani, wastahiki zaidi kuitwa wana wa Mungu, … na ni kupitia kwa huzuni na kuteseka, taabu na masumbuko, ndipo tunapopata elimu ambayo tulikuja hapa kupata” (imedondolewa kutoka kwa Spencer W. Kimball, Faith Precedes the Miracle [1972], 98).

Na maandiko haya kuhusu kuteseka kwa Mwokozi alipotoa dhabihu isiyo na mwisho na ya milele ya upatanisho ikawa ya mhemko mkuu na ya maana kwangu:

“Kwa sababu hii ninakuamuru wewe kutubu—tubu, nisije nikakupiga kwa fimbo ya kinywa changu, na ghadhabu yangu, na kwa hasira yangu, na mateso yako kuwa machungu—machungu namna gani hujui, makali namna gani hujui, ndiyo, namna gani magumu kuyavumilia hujui.

“Kwani tazama, Mimi, Mungu nimeteseka mambo haya kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wasiteseke kama watatubu;

“Lakini kama hawatatubu lazima wateseke hata kama Mimi;

“Mateso ambayo yaliyosababisha Mimi mwenyewe, hata Mungu, mkuu kuliko yote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, na kuteseka mwili na roho—na kutamani nisinywe kikombe kichungu, na kusita—

“Hata hivyo, utukufu na uwe kwa Baba, na Mimi nikachukua na kukamilisha maandalizi yangu kwa wanadamu.” (M&M19:15–19).

Mwokozi hakusita huko Gethsemane au katika Golgotha.

Mzee Maxwell pia hakusita. Huyu Mtume mkuu alisonga mbele imara na alibarikiwa na muda wa ziada hapa duniani wa kupenda, kuhudumu, kufundisha, na kushuhudia. Ile miaka yake ya hitimisho la maisha yake yalikuwa alama ya mshangao dhahiri kwa mfano wake wa ufuasi wa dhati---kupitia yote maneno yake na matendo yake.

Naamini wengi wetu wangetarajia mtu wa uwezo kwa kiroho, uzoefu, na hadhi ya Mzee Maxwell kukabiliana na ugonjwa mkali na kifo kwa uelewa wa mpango wa Mungu wa furaha, akiwa na uhakikisho na neema, na staha. Na kwa kweli alifanya hivyo. Lakini madhumuni yangu leo ni kushuhudia kwamba baraka kama hizo sio tu kwa Viongozi wenye Mamlaka peke yao au washiriki wa wachache wa Kanisa walioteuliwa.

Tangu wito wangu kujaza nafasi katika Jamii ya Mitume Kumi na Wawili iliyosababishwa na kifo cha Mzee Maxwell, kazi na safari zangu zimeniwezesha kujifahamishana na Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu, washupavu na wajasiri duniani kote. Mimi nataka kuwaelezea kuhusu mvulana mmoja na msichana mmoja ambao wamebariki maisha yangu na ambao kwao nimejifunza masomo muhimu ya kiroho kuhusu kutosita na kuhusu kuruhusu mapenzi yetu yapate “kumezwa katika mapenzi ya Baba” (Mosia 15:7).

Hadithi hii ni ya kweli, na wahusika ni halisi. Hata hivyo, sitatumia majina halisi ya wahusika. Nitamwita yule mvulana John na yule msichana nitamwita Heather. Pia nitatumia kwa ruhusa taarifa zilizochaguliwa kutoka kwa shajara zao za kibinafsi.

Sio Mapenzi Yangu bali Yako Yatendeke

John ni mwenye ukuhani mstahiki na alihudumu kwa uaminifu kama mmisionari. Baada ya kurudi nyumbani kutoka kwenye misheni yake, alifanya miada na kuoana na msichana mwema na wa ajabu, Heather. John alikuwa wa miaka 23 na Heather alikuwa wa miaka 20 katika ile siku walifunganishwa kwa muda na milele yote katika nyumba ya Bwana. Tafadhali kumbuka umri wa John na Heather mtawalia hadithi inavyoendelea.

Karibu wiki tatu baada ya ndoa yao ya hekaluni, John aligunduliwa kuwa na saratani ya mifupa. Na vivimbe vya saratani pia viliguduliwa katika mapafu yake, ubashiri wa ugonjwa haukuwa mzuri.

John aliandika kwenye shajara yake: “Hii ilikuwa siku ya kuogofya katika maisha yangu. Si kwa sababu niliambiwa niko na saratani, bali kwa sababu nilikuwa nimeoa majuzi na kwa hivyo nilihisi kwamba nilikuwa nimeanguka kama mme. Nilikuwa mhifadhi na mlinzi wa familia yangu mpya, na sasa---wiki tatu katika nafasi hii---nilihisi kama nimeanguka. Najua kwamba wazo hili ni la kipuzi, lakini ni mojawapo wa vitu vya kijinga ambavyo nilijiambia katika wakati wa taabu.”

Heather aliandika: Hizi zilikuwa habari za kupasua moyo sana, na nakumbuka jinsi zilibadilisha kabisa mtazamo wetu. Nikuwa katika chumba cha kungoejea nikiandika barua za shukrani wa harusi tulipokuwa tukingojea majibu ya utafiti wa [John]. Lakini baada ya kujua kuhusu saratani ya [John], vyombo vya jikoni na masahani hayakuwa tena na umuhimu kabisa. Hii ilikuwa siku mbaya ya maisha yangu, lakini nakumbuka nikienda kitandani usiku huo na shukrani juu ya kufunganishwa kwetu hekaluni. Ingawa madaktari walimpatia [John] uwezekano wa asili mia 30 wa kunusurika, mimi nilijua kwamba ikiwa ningebakia mwaminifu ningekuwa na uwezekano wa asili mia 100 wa kuwa naye milele.”

Karibu mwezi mmoja baadaye John alianza tibakemikali. Yeye alielezea uzoefu wake: “Hii tiba ilinifanya mimi kuwa mgonjwa zaidi kuliko nilivyowahi kuwa katika maisha yangu. Nilipoteza nywele zangu, nikapoteza uzito wa ratili 41, na mwili wangu ukahisi kama unasambaratikana. Tibakemikali pia ilinidhuru kimhemko, kiakili, na kiroho. Maisha yakawa kama panda shuka katika miezi ya tibakemikali yalikuwa na uchangamfu, kuhuzunika, na kila kitu kilicho kati yake. Lakini kupitia yote haya, [Heather] nami tulidumisha imani kwamba Mungu angeniponya. Na tulijua hivyo.”

Heather aliandika mfululizo wa mawazo na hisia zake: “Mimi singevumilia kumuacha [John] alale peke yake usiku hospitalini, kwa hivyo nililala kwenye sofa ndogo iliyokuwa katika chumba chake. Tulipata marafiki wengi na wanafamilia kututembelea wakati wa mchana, usiku ilikuwa mgumu sana. Ningetazama paa na kushangaa kile Baba wa Mbinguni ametupangia sisi. Wakati mwingine akili yangu ingetanga katika sehemu za giza, na hofu ya kumpoteza [John] karibu kunishinda. Lakini nilijua mawazo haya hayakuwa yanatoka kwa Baba wa Mbinguni. Maombi yangu kwa faraja yakawa ya kila mara na Bwana alinipatia nguvu za kuendelea mbele.”

Miezi mitatu baadaye John alipasuliwa kuondoa uvimbe mkubwa kwenye mguu wake. John alisema hivi: “Upasuaji ulikuwa jambo kubwa kwetu kwa sababu utafiti wa patholojia ungefanywa kwenye uvimbe ili kuona ni kiasi gani ilikuwa hai na kiasi gani cha saratani ilikuwa imekufa. Uchanganuzi huu ungetupatia onyesho la kwanza la jinsi tibakemikali ilikuwa imefanya kazi na jinsi tungehitaji kupambana katika tiba za siku zijazo.”

Siku mbili baada ya upasuaji, nilimtembelea John na Heather hospitalini. Tukaongea kuhusu mara ya kwanza nipokutana na John katika uwanda wa misheni, kuhusu ndoa yao, kuhusu saratani, na kuhusu masomo muhimu ya milele tunayojifunza kutokana na majaribu ya maisha ya muda. Na tupohitimisha muda wetu pamoja, John aliomba ikiwa nitampatia baraka za ukuhani. Nilijibu kwamba ningependelea, kumpatia baraka kama hiyo, lakini kwanza nihitaji kwanza kuuliza maswali fulani.

Kisha nikauliza maswali ambayo sikuwa nimepanga kuuliza na kamwe sijafikiria kuuliza: “[John], Je! Wewe una imani ya kutoponywa? Ikiwa itakuwa mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni kwamba wewe uhamishe kwa kifo katika ujana wako hadi ulimwengu wa roho kuendelea na huduma yako, una imani ya kujiweka chini ya mapenzi Yake na usiponywe?”

Kwa hakika nishangazwa na maswali nilihisi kusukumwa kuuliza hasa hawa wenzi hawa. Kila mara katika maandiko Mwokozi au wafuasi Wake walitumia kipawa cha kiroho cha uponyaji (ona 1 Wakorintho 12:9;M&M 35:9; 46:20) na kujua kwamba mtu alikuwa na imani ya kuponywa (ona Matendo ya Mitume 14:9; 3 Nefi 17:8; M&M 46:19). Lakini John na Heather nami tulipokuwa tushauriana na kukabiliana na haya maswali, tulipata ongezeko la uelewa kwamba ikiwa itakuwa mapenzi ya Mungu huyu mvulana mwema aponywe, basi hiyo baraka ingeweza tu kupokelewa kama hawa wenzi wajasiri kwanza wangekuwa na imani ya kutoponywa. Katika maneno mengine, John na Heather walihitaji kushinda, kupitia Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo, yule “mtu wa kawaida” (Mosia 3:19) upole katika sisi sote wa kudai pasi uvumilivu na kusita kwa shaka juu ya baraka tunazotaka na tunazoamini tunapaswa kuwa nazo.

Tunatambua kanuni ambayo inatumika kwa kila mfuasi wa dhati: imani kuu katika Mwokozi ni kwa kujisalimisha kukubali mapenzi Yake na wakati wake katika maisha yetu---hata kama matokeo yake si kile tulitumainia au tulitaka. Hakika, John na Heather walikuwa na hamu, walitamani, na kuomba uponyaji kwa nguvu, akili, na uwezo wao wote. Lakini cha muhimu sana, walikuwa tayari “kukubali vitu vyote ambavyo Bwana anawapatia [wao], hata kama vile mtoto hunyenyekea kwa baba yake” (Mosia 3:19).Kwa kweli, wangekuwa tayari “kumtolea nafsi [zao] kama sadaka kwake (Omni 1:26) na kuomba kwa unyenyekevu, “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Luka 22:42).

Kile kilichoonekana mapema kwa John, Heather, nami kama swala la kukanganya likawa sehemu ya mpangilio ulioenea kote kama injili kinza. Fikiria onyo la Mwokozi: “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona” (Mathayo 10:39).Yeye pia alitangaza, “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza” (Mathayo 19:30). Na Bwana alishauri wafuasi Wake wa siku za mwisho, “Na kwa neno lako wengi walio juu watashushwa chini, na kwa neno lako wengi walio chini watakwezwa” (M&M 112:8). Basi, kuwa na imani ya kutoponywa inaonekana kuingiana katika mpangilio vilivyo katika mpangilio wenye nguvu wa kinza za kupenya ambazo zinatuhitaji kuuliza, kutafuta, na kugonga kile wanachoweza kupokea elimu na uelewa (ona 3 Nefi 14:7).

Baada ya kuchukua muda wa kutosha wa kutafakari juu ya maulizo yangu na kuongea na mke wake, John aliniambia: Mzee Bednar, mimi sitaki kufa. Mimi sitaki kumuacha Heather. Lakini ikiwa ni mapenzi ya Bwana nihamishwe hadi ulimwengu wa roho, basi nadhania ni sawa kwangu.” Moyo wangu kwa furaha na upendeleo nilivyoshuhudia hawa wenzi vijana wakikabiliana na mfadhaiko mkubwa wa yote ya kiroho---kusalimisha mapenzi yao kwa mapenzi ya Mungu. Imani yangu iliimarishwa niliposhuhudia hawa wenzi wakiruhusu hamu zao kubwa za kuponywa na zinazoeleweka “kumezwa na mapenzi ya Baba” (Mosia 15:7).

John alielezea kujibu kwake katika mazungumzo yetu na baraka alizopokea: “Mzee Bednar alishiriki nasi wazo kutoka kwa Mzee Maxwell kwamba ni vyema kutosita kuliko kunusurika. Mzee Bednar kisha alituuliza, ‘Najua una imani ya kuponywa, lakini je! Una imani ya kutoponywa?’ Hii ilikuwa dhana geni kwangu. Kihalisi alikuwa anauliza ikiwa nilikuwa na imani ya kukubali mapenzi ya Mungu ikiwa mapenzi ya Mungu ni kwamba sitaponywa? Ikiwa wakati unajongea kwangu kuingia katika ulimwengu wa roho kupitia kifo, mimi nilikuwa nimejitayarisha kujisalimisha na kupokea?”

John aliendelea: “Kuwa na imani kukosa kuponywa huonekana kuwa kitu kisochokuwa cha kawaida, lakini kwamba mtazamo ulibadilisha vile mke wangu nami tulifikiria na kujiruhusu kuweka imani yetu kamili katika mpango wa Baba kwetu. Tulijifunza tunahitaji kupata imani kwamba Bwana ndiye mwenye mamlaka juu chochote kitakachokuwa matokeo, na Yeye atatuongoza kutoka pale tulipo hadi pale tunahitaji kwenda. Tulioomba, maombi yetu yalibadilika kutoka ‘Tafadhali nifanye niwe mzima” hadi ‘Tafadhali nipe imani ya kukubali matokeo yoyote uliyonipangia mimi.’

“Nilikuwa na hakika kwamba kwa vile Mzee Bednar alikuwa Mtume, yeye angebariki elementi za mwili wangu kubadilika, na ningeruka kutoka kitandani na kuanza kucheza dance au kufanya kitu cha kidrama kama hicho! Lakini aliponibariki siku hiyo, nilishangazwa na maneno ambayo yeye alisema yaliyokuwa karibu na yale ya baba yangu, baba mkwe, na rais wa wangu wa misheni. Nilitambua kwamba hatimaye haijalishi ni mikono ya nani iliyo juu ya kichwa changu. Nguvu za Mungu hazibadiliki, na mapenzi Yake ujulishwa kwetu kibinafsi na kupitia watumishi Wake wenye mamlaka.”

Heather aliandika: “Siku hii ilijawa na mchanganyiko wa mihemko kwangu. Nilikuwa nimeshawishika kwamba Mzee Bednar angeweka mikono yake kwenye kichwa cha [John] na kumponya kabisa kutokana na saratani. Nilijua kwamba kupitia kwa uwezo wa ukuhani angeweza kuponywa, na nilitaka hivyo sana kutendeka. Baada ya yeye kutufunza kukosa kuponywa, nilishituka. Kufikia wakati huo, kamwe sijapata kuelewa jambo kwamba mpango wa Bwana unaweza kujumuisha kumpoteza mme wangu mpya. Imani yangu ilitegemea juu ya matokeo niliyotaka. Katika hali ya unenaji, ilikuwa upande mmoja. Ingawa ilishitua hapo mwanzoni, dhana ya kuwa na imani kukosa kuponywa hatimaye iliniweka huru kutokana na hofu. Iliniruhusu kuwa na imani kamili kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinijua mimi vyema kuliko nilivyojijua mwenyewe, na Yeye atafanya kile kilicho chema kwa kwangu na kwa John.”

Baraka ilitolewa, na wiki, miezi, na miaka ilipita. Saratani ya John kimiujiza ilififia. Yeye ameweza kumaliza masomo ya chuo kikuu na kupata ajiri ya malipo. John na Heather wameendelea kuimarisha uhusiano wao na kufurahia maisha pamoja.

Wakati fulani baadaye, nilipata barua kutoka kwa John na Heather wakinijulisha kwamba saratani imerudi. Tibakemikali imeanza na upasuaji umepangwa. John alielezea: “habari hizi hazituvunji mioyo tu [Heather] nami, bali zilitushangaza. Kuna chochote tulichofanya na hatukujifunza mara ya kwanza? Je! Bwana alitarajia kitu zaidi kutoka kwetu? Kukua kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, ilikuwa jambo la kawaida kuenda kanisa na kusikia kishazi, ‘kila jaribu Mungu analotupatia sisi kwa manufaa yetu.’ Vyema, kwa kweli, singeweza kuona jinsi haya yalikuwa yananufaisha!

Kwa hivyo, nilianza kuomba kwa ubainifu na kwamba Bwana anisaidie kuelewa kwa nini kurudi kwa saratani kulitendeka. Siku moja nilikuwa nikisoma katika Agano Jipya nilipokea jibu langu. Nilisoma taarifa ya Kristo na Mitume wake kwenye bahari wakati maji yalipochafuka. Wakiogopa mashua itazama, wafuasi walimwendea Mwokozi na kuuliza ‘Bwana, haujali kuwa sisi tutaangamia?’ Hivyo ndivyo nilivyohisi! Haujali kuwa nina saratani? Haujali kuwa tunataka kuanzisha familia? Lakini nilipokuwa nikisoma hadithi hii, nilipata jibu langu. Bwana aliwatazama na kusema “Enyi ninyi wenye imani ndogo,’ na Yeye akainyosha mikono Yake na maji yalitulia.

Wakati huo nilijiuliza mwenyewe, ‘Je! Mimi ninaamini haya? Je! Ninaamini Yeye alituliza maji siku hiyo? Au hii ilikuwa tu hadithi tamu kuisoma? Jibu ni: Naamini, na kwa sababu najua Yeye alituliza maji, mara moja nilijua Yeye anaweza kuniponya mimi. Mpaka kufikia hapo, nilikuwa na wakati mgumu kupatanisha haja ya imani yangu katika Kristo pamoja na mapenzi Yake ambayo sharti yatimizwe. Niliona mambo mawili tofauti, na wakati nikahisi kwamba moja linakinza lingine. Kwa nini ninafaa kuwa na imani ikiwa mapenzi Yake hatimaye lazima yashinde,’ nilijiuliza? Baada ya uzoefu huu, nilijua kwamba kuwa na imani---hasa katika hali yangu---haikuwa lazima kujua kwamba Yeye ataniponya mimi, bali kwamba Yeye anaweza kuniponya mimi. Nilihitaji kuamini kwamba Yeye anaweza, na basi kama itatendeka ilikuwa ni juu Yake.

“Nilipokubali haya mawazo mawili kuishi katika maisha yangu, nililenga imani yangu katika Yesu Kristo na kujiweka chini ya mapenzi Yake, nilipata faraja kubwa na amani. Imekuwa ya ajabu sana kuona mkono wa Bwana katika maisha yangu. Mambo yameingiana vyema, miujiza imetendeka, na tunaendelea kunyenyekezwa kuona mpango wa Mungu ukifumuliwa kwetu.

Narejelea taarifa ya John ili kutia mkazo, “ Nilipokubali haya mawazo mawili kuishi katika maisha yangu, nililenga imani yangu katika Yesu Kristo na kujiweka chini ya mapenzi Yake, nilipata faraja kubwa na amani.”

Wema na imani kwa hakika ni muhimu katika kuondosha milima---ikiwa kuondosha milima hukamilisha madhumuni ya Mungu na ni kulingana na mapenzi Yake. Wema na imani ni muhimu katika kuponya wagonjwa viziwi, au viwete---ikiwa uponyaji unakamilisha madhumuni ya Mungu na kulingana na mapenzi Yake. Basi, hata kwa imani kubwa, milima mingi haitaondolewa. Na sio wote wa wagonjwa au walemavu wataponywa. Ikiwa upinzani wote utaondolewa, ikiwa maradhi yote yataondolewa, basi madhumuni ya msingi ya mpango wa Baba yatazuiwa.

Masomo mengi tunayojifunza katika maisha ya muda yanaweza tu kupokelewa kupitia vitu tunavyopata uzoefu kwavyo na wakati mwingine kupatwa navyo. Na Mungu anatarajia na kuamini sisi tutakabiliana na dhiki ya maisha ya muda kwa usaidizi Wake ili tuweze kujifunza kile tunahitaji kujifunza na hatimaye kuwa kile tutakuwa katika milele.

Maana ya Vitu Vyote

Hadithi kuhusu John na Heather ni yote ya kawaida na ya ajabu. Hawa wenzi vijana wanawakilisha mamilioni wa Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu, wenye kuweka maagano kote ulimwenguni ambao wanasonga mbele katika njia iliyosonga na nyembamba kwa imani thabiti katika Kristo na matumaini kamili na angavu. John na Heather hawakuwa wanahudumu nafasi za uongozi zinazoonekana sana katika Kanisa, hawakuwa na uhusiano wowote na viongozi wenye mamlaka, na wakati mwingine walikuwa na shaka na hofu. Katika hizi hali nyingi, hadithi yao ni ya kawaida kabisa.

Kina ndugu na kina dada, huyu mvulana na msichana walibarikiwa kwa njia za ajabu ili kujifunza masomo muhimu ya milele kupitia kuteseka na ugumu. Nimeshiriki tukio hili nanyi kwa sababu John na Heather, ambao ni tu kama wengi wenu, walikuja kuelewa kwamba kutosita ni muhimu sana kuliko kunusurika. Basi, uzoefu wao haukuwa kimsingi kuhusu kuishi na kufa; bali, ulikuwa ni kuhusu kujifunza, kuishi, na kuwa.

Kiini cha kiroho cha machanganiko wa imani na juu ya jina takatifu la Yesu Kristo, cha kujisalimisha kwa mapenzi na wakati Wake, katika kusonga mbele “kwa bidii bila kuchoka (Helamani 15:6), na kutambua mkono Wake katika vitu vyote huzaa vitu vya amani katika ufalme wa Mungu ambao huleta shangwe na maisha ya milele (ona M&M 42:61). Wenzi hawa walipokuwa wanakabiliana na changamoto zilizoonekana kuzidi, waliishi “maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu” (1 Timotheo 2:2). Walitembea kwa utulivu (ona Moroni 7:4) pamoja na miongoni wa watoto wa watu. “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:7).

Kwa wengi wenu, hadithi yao ni, imekuwa au inaweza kuwa hadithi yako. Unayokabiliana nayo, umeshakabiliana nayo, au bado utakabiliana na changamoto kama hiyo katika maisha yao kwa ujasiri huo huo na mtazamo wa kiroho ambao John na Heather walikuwa nao. Sijui kwa nini watu fulani hujifunza masomo ya milele kupitia majaribu na kuteseka---hali wengine hujifunza masomo kama hayo kupitia kukombolewa na kuokolewa. Sijui sababu zote, madhumuni yote, na sijui kila kitu kuhusu wakati wa Bwana. Pamoja na Nefi, mimi na wewe tunaweza kusema kwamba sisi “hatujui maana ya vitu vyote” (1 Nefi 11:7).

Lakini vitu fulani kwa hakika navijua. Najua sisi ni wana na mabinti wa kiroho wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Najua Baba wa Milele ndiye mtungaji wa mpango wa furaha. Najua Yesu Kristo ndiye Mwokozi na Mkombozi wetu. Najua Yesu aliwezesha mpango wa Baba kupitia Upatanisho usio na mwisho na wa milele. Najua kwamba Bwana, ambaye ‘alichubuliwa, kuvunjwa, na kuraruliwa kwa ajili yetu” (Jesus of Nazareth, Savior na King,” hymns, no 181), anaweza kusaidia na kuimarisha “watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:12). Na najua kwamba mojawapo wa baraka kuu za maisha ya muda haya ni kutosita na kuruhusu mapenzi yetu binafsi ‘yamezwe na mapenzi ya Baba” (Mosia 15:7).

Ingawa sijui kila kitu kuhusu jinsi na lini na wapi na kwa nini hizi baraka hutokea, najua na nashuhudia kwamba ni halisi. Nashuhudia kwamba hivi vitu ni kweli---na kwamba sisi---tunajua vya kutosha kwa nguvu za Roho Mtakatifu kutoa ushuhuda wa kweli juu ya uungu wao, uhalisi na kufaa kwake. Ndugu na dada zangu wapendwa, nawaombeeni baraka hii: hata kwamba muweze kusonga mbele katika maisha yenu kwa imani thabiti katika Kristo, mtakuwa na uwezo wa kutosita. Nashuhudia na kuwaombeeni baraka hii katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.