Vijana wa Urithi Adimu: Mtachagua Nini?

Mkutano wa Ibada wa MEK kwa Vijana Wazima • Septemba 6, 2013 • Chuo Kikuu cha Brigham Young---Hawaii


 

Mke wangu, Wendy, nami tunashukuru sana kuwa nanyi. Kutoka kwa Cannon Activities Center kwenye kampasi ya BYU---Hawaii, tunatangaza kwa mikusanyiko ya vijana wazima duniani kote. Tena, tunatoa karibisho la kipekee kwa wale wanaohudhuria mkutano wa ibada wa MEK kwa mara ya kwanza. Mnapojisajili katika taasisi za elimu ya juu, mtataka kushiriki katika madarasa ya chuo na mikutano hii ya ibada ili kudumisha usawa wa kiroho na masomo yenu ya mambo ya kidunia. Na ikiwa hivi karibuni unaelekea misheni, tunashukuru sana. Utakuwa katika huduma ya Bwana wakati wote.

Ninaleta salamu na upendo kutoka kwa Rais Thomas  S. Monson, Rais Henry  B. Eyring, Rais Dieter  F. Uchtdorf, na washiriki wangu wapendwa katika Jamii ya Mitume Kumi na Wawili. Pia ninaleta salamu kutoka kwa Bodi ya Wadhamini ya Mfumo wa Elimu ya Kanisa, na kutoka kwa Mzee Paulo  V. Johnson, Kamishna wa Mpango wa Elimu wa Kanisa.

Tumekuwa na wanenaji watatu hapo awali katika mikutano yetu ya ibada ya MEK mwaka huu. Je, mnawakumbuka? Hotuba ya Rais Dieter  F. Uchtdorf ilikuwa na kichwa cha ujumbe “Ukweli ni Nini?” Alitufundisha jinsi ya kupata ukweli wa haki katika siku ambazo maarifa mengi yanapatikana, mengi yao ambayo si ya kweli. Kichwa cha hotuba ya Mzee David  A. Bednar kilikuwa “Ili Kwamba Tusinywee”. (M&M 19:18). Aliimarisha roho zetu alipotufundisha jinsi ya kuongeza imani kupitia swali la kina ambalo lilisaidia wanandoawachanga; mume alipokuwa akikumbana na saratani. Swali lililoulizwa na Mzee Bednar lilikuwa, “Je, unaimani ya kukosa kuponywa?” Mzee William  R. Walker aliimarisha shuhuda zetu kuhusu huduma na mfano wa ajabu wa Rais wetu mpendwa Thomas  S. Monson.

Leo, kichwa cha ujumbe wangu ni “Vijana wa Urithi Adimu1: Mtachagua Nini?”

Ninyi, kama vijana wa urithi adimu, ni wana na binti wa Mungu kihalisi, mkiwa mmezaliwa kwa wakati huu maalum katika historia ya dunia kwa kusudi tukufu. Ingawa maadili ya kitabia na kidini ya jamii yanaonekana kudhoofika duniani kote, vijana wa Kanisa hili wanakusudiwa kuwa wamiliki wa viwango vya Bwana na violeza vya mwangaza ili kuwavutia wengine Kwake. Utambulisho na kusudi lenu ni la kipekee.

Utambulisho wenu ni nini? Ninyi ni watoto wa agano. Agano gani? Lile ambalo Mungu alifanya na Baba Ibrahimu wakati Ibrahimu aliahidiwa kwamba “katika uzao wako, jamaa wote wadunia watabarikiwa.”2 Ninyi pia ni watoto wa siku ya ahadi,3 kipindi hiki cha historia ya dunia wakati Injili itakapotangazwa kwa upana katika sayari mzima.

Ni nini kusudi lenu? Ninyi akina ndugu mliteuliwa katika ulimwengu kabla ya maisha duniani kuchukua ukuhani.4 Fikirieni kuhusu hayo! Na ninyi akina dada wapendwa, mlichaguliwa kabla ya msingi wa dunia kuzaa na kuwatunza watoto wa Mungu, na katika kufanya hivyo, mnamtukuza Mungu.5 Je, nyinyi akina dada mmefikiriakwa kweli kile kinachomaanisha kuwa waumbaji wenza pamoja na Mungu?

Kila mmoja wenu ninyi wavulana na wasichana mlipewa jukumu na Baba yenu wa Mbinguni kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani hivi sasa na kuandaa watu wampokee Mwokozi wakati Yeye atakapotawala na kuongoza kama Masiya wa Milenia. Urithi wenu adimu, utambulisho, kusudi, na juhudi tukufu inawatenganisheni na wengine wote.

Lakini si urithi wenu adimu wala kuteuliwa kwenu kabla ya maisha duniani na utume unaweza kuwaokoa ama kuwatukuza. Hiyo mtafanya kupitia uamuzi wenu wa kibinafsi na mnapochagua kupokea uwezo wa Upatanisho wa Bwana katika maisha yenu. Mnajua kwamba “kila nafsi i huru kuchagua maisha yake na kile itakachokuwa.”6 Kanuni hio kuu ya milele ya wakala ni muhimu kwa mpango wa Baba yetu. Hivyo basi, ninyi vijana wa urithi adimu, mtachagua nini?

Je, mtachagua kuongezeka katika elimu?

Elimu ni yenu kuipokea. Hakuna mwingine anayeweza kuipokea kwa niaba yenu. Popote mlipo, kuza hamu ya kina ya kusoma. Kwetu sisi kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, kupata elimu si tu bahati nzuri, ni jukumu la kidini. Utukufu wa Mungu ni akili.7 Kwa kweli, elimu yetu niya milele.

“Kanuni yoyote ya akili tuipatayo katika maisha haya, itafufuka pamoja nasi katika ufufuko.

“Na kama mtu anapata maarifa zaidi na akili katika maisha haya… , atakuwa na heri ya juu zaidi katika ulimwengu ujao.”8

Mtazamo wa siku za usoni kama huo utakusaidia kufanya chaguzi njema kuhusu masomo. Ninakumbuka vyema mazungumzo miaka mingi iliyopita na mwanafunzi hodari wa miaka 16 wa shule ya upili. Alikuwa hana uhakika kuhusu sharti lake la kidini na hakuwa ameamua kuhusu kazi yake. Aliwazia kuhusu uwezekano wa kuwa daktari wa matibabu. Aliniuliza siku moja swali rahisi: “ Ilikuchukua miaka mingapi kuwa daktari wa upasuaji wa moyo?”

Nilifanya hesabu za haraka: “Kutoka wakati nilipofuzu shule ya upili hadi nilipopokea malipo kwa huduma kama daktari wa upasuaji, ilinichukua miaka 14”

“Ala!” alijibu.“Huo ni muda mrefu sana kwangu!”

Kisha nikauliza, “Utakuwa na umri gani miaka 14 kutoka sasa usipokuwa daktari wa moyo?”

“Miaka ile ile,” alijibu.“Miaka ile ile!”

Nilikuwa na maslahi maalum kwa kijana huyu. Kwa wakati mwingine nilimchukua katika gari langu kwenye njia yake ya asubuhi mapema ya kusambaza magazeti. Miaka ilivyopita imani yake ilikuwa thabiti. Alikuwa mmisionari wa ajabu. Aliamua kufuata lengo lake la kimasomo. Kwanza, alimuoa mpenzi wake hekaluni. Kisha akiwa anajifunza matibabu na upasuaji, wakawa wazazi wa watoto wanne wa kupendeza. Kwa sasa amedhibitishwa kikamilifu na bodi kama daktari wa upasuaji moyo---baada ya elimu na mafunzo ya kina katika kipindi cha miaka 14.

Akina kaka na dada, msiogope kufuata malengo yenu---hata ndoto zenu! Hakuna njia ya mkato ya mafanikio na uwezo. Elimu ndiyo tofauti kati ya kutamani ungeweza kusaidia watu wengine na kuwa unaweza kuwasaidia.

Hapa kuna swali lingine: Utachagua aina gani ya kuishi?

Ninyi, kama vijana wa urithi adimu, mnatarajiwa muishi tofauti na wengine. Mnajua kile Paulo alisema kwa kijana Timotheo: “Wewe uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo, na katika upendo, katika roho, katika imani na usafi.”9 Chagua kufikiria na kutenda tofauti na wale walio wa dunia. Chagua kuonekana tofauti na uone ushawishi wa wema utakaokuwa. Kama Dada Ardeth  G. Kapp alivyosema, “Hauwezi kuwa mwokoa---maisha, ikiwa unaonekana kama waogeleaji wengine wote kwenye ufuo.”10

Kama vijana wa urithi adimu, mnao mwanzo mzuri katika maisha. Lakini mnayo pia majukumu ya ziada. “Kwa yule ambaye amepewa mengi, mengi yanatarajiwa.”11 Sehemu ya tarajio hilo ni kuwa msajiliwa. Je, umewahi kujifikiria kama msajiliwa wa jeshi? Ulipobatizwa, ulisajiliwa upya katika jeshi la Bwana.12 Kabla ya maisha duniani, ulisimama na Yesu Kristo wakati wa Vita Mbinguni. Na sasa mapigano kati ya majeshi ya wema na maovu yanaendelea hapa duniani. Ni ya kweli! Hayo Mapigano ambayo tunashiriki sasa bado ni kati ya majeshi ya wema na majeshi ya uovu.13 Kwenye upande wa Mungu kuna Yesu Kristo, aliyeteuliwa kuwa Mwokozi wa dunia.14 Kwenye upande mwingine ni Shetani--muasi---mwangamizi wa wakala.15

Mpango wa Mungu unamwezesha adui kuwajaribu ninyi ili kwamba ninyi, mkiwa sasa katika dunia hii, mnaweza kutumia wakala wenu kuchagua wema dhidi ya uovu, kuchagua kutubu, kuchagua kumjia Yesu Kristo na kuamini mafunzo Yake na kufuata mfano Wake. Ni jukumu kubwa na wajibu mkuu jinsi gani!

Uhuru wenu wa kuchagua umeelezewa kwa uwazi katika Kitabu cha Mormoni. “Wanadamu wana uhuru wanapoishi. …  Wana haki kuchagua uhuru na uzima wa milele … au kuchagua utumwa na kifo, kulingana na utumwa na nguvu za ibilisi; kwani anataka wanadamu wote wawe na dhiki kama yeye.”16  Mtachagua nini?

Mstari mwingine unafunua kwamba “uovu hauwezi kuwa furaha.”17 vijana wengi wamejaribu kubisha ukweli huo na wameshindwa kila wakati.

Uhuru wako wa kutenda kwa ajili yako mwenyewe ni muhimu kwa maendeleo yako ya milele na furaha kwamba adui anatoa juhudi za kubwa sana za kuudhoofisha.18 Shetani kweli halali. Wengi wenu tayari mmepitia hayo!

Swali lingine ni hili hapa : Mtaanzisha vipaumbele vya kuwasaidia kufanya maamuzi yenu katika maisha?

Chaguzi zenu hazitakuwa zote kati ya wema na uovu. Nyingi zitakuwa kati ya chaguo mbili nzuri. Si kweli zote zimeundwa sawa, hivyo basi mtahitaji kuwa na vipaumbele. Katika kutafuta kwenu maarifa, jueni kwamba ukweli muhimu kabisa unaoweza kujifunza huja kutoka kwa Bwana. Katika Maombi Yake ya Upatanisho kwa Baba Yake, Mwokozi Mwenyewe alidhibitisha haya. Alisema, “Huu ni uzima wa milele, wapate kukujua wewe Mungu pekee wa kweli, na Yesu Kristo, uliyemtuma.”19 Juu ya mambo mengine yote unayojitahidi kujifunza, jitahidi kumjua Mungu, Baba yako wa Mbinguni, na Mwana Wake, Yesu Kristo. Kuja kuwajua na kuwapenda kama ninavyowapenda.

Maandiko mengine yenye kipaumbele ambayo yamenisaidia mishani mwangu ni hili: “Tafuteni kwanza kuujenga ufalme wa Mungu, na kudhibitisha haki yake, na hayo yote mtazidishiwa.”20

Zaidi ya chochote kingine duniani humu, unataka kufanya uchaguzi unaoelekeza kwa hatima ya mwisho na utukufu wa uzima wa milele. Hio ndio utukufu mkuu wa Mungu kwa ajili yako.21 Chagua uzima wa milele kama kipaumbele chako cha juu zaidi. Jifunze maandiko, kama vile sehemu ya 76 na  88 ya Mafundisho na Maagano, ili kuelewa zaidi kuhusu baraka tofauti zinazowangojea wale wanaochagua uzima wa milele na wale wasiochagua. Chagua uzima wa milele kama kipaumbele chako cha juu zaidi na utambue jinsi chaguo zingine zinaambatana vyema.

Swali lingine: Mtachagua kushirikiana na akina nani?

Kama vijana wa urithi adimu, mtashirikiana na watu wengi wema wanaoamini pia katika Mungu. Kama wao ni Wayahudi, Wakatoliki, Waprotestanti, au Waislamu, waumini wanajua kwamba kuna ukweli halisi! Katika ujumbe wa Rais Uchtdorf wa awali, alihimiza kwamba kwa kweli kuna haki na uovu, na uvunjaji wa kimakusudi wa amri za Mungu kwa kweli ni dhambi. Waumini katika Mungu pia wana dhamiri. Waumini hutii sheria ya nchi na sheria ya kiungu kwa hiari yao, hata sheria ambazo huenda vinginevyo haziwezi kutekelezwa.

Kwa sharti lako la kutii sheria za nchi na za kiungu, unasimama kwenye taa nyekundu, hata ikiwa hakuna magari mengine unayoyaona. Wewe, kama mtoto wa Mungu, jua kwamba hata ikiwa polisi hawatakushika, kwamba ukiwa utaiba, utaua, ama kutenda uzinzi, vitendo hivi ni mbaya, na Mungu hatimaye atakuwajibisha. Unajua kwamba matokeo ya kutotii masharti si tu ya muda wa ilani ya milele.

Unapoendelea kwenye safari ya maisha, utajuana pia na watu wasiomwamini Mungu. Wengi wao bado hawajapata ukweli mtukufu na hawajui mahali pa kuutafuta. Lakini ninyi vijana wa urithi adimu mnakuja kuwaokoa. Kwa idadi kubwa, mnajitokeza kwa wito wa nabii wa Mungu kwa wamisionari zaidi. Tunashukrani kabisa kwa kila mmoja! Wengi wenu tayari mmehudumu; wengine wanajitayarisha kwenda.

Mnaposhirikiana na wasioamini, fahamu kwamba huenda ikawa ku wachache ambao hawana nia bora kwako mioyoni mwao22 Mara tu unapofanya uamuzi huo-- mara tu unapobaini hayo, watoroke upesi na kabisa.23

Sasa, cha kusikitisha, mtakutanana watu ambao kutafuta kwao kwa bidii kitu ambacho kinaonekana kwao kama furaha kunawaelekeza chini kwenye mteremko telezi wa dhambi. Jihadharini na utelezi huo mwororo! Furaha yoyote katika dhambi ni ya kidunia tu, na kumbukumbu zake za dhiki zinapakwa na hatia ya kulia na kusaga. Dhambi inayopindukia ya kumbatio la kiungu lililoundwa kuunganisha mume na mke ni bandia na unafiki. Kila tukio lililo kinyume cha sheria inatolewa maana ya kina na ya kumbukumbu tamu.

Swali moja lingine: Mtachagua uhuru ama utumwa?

Misikumo isiyo ya kiungu uko kote. Mnaishi hasa katika “eneo lililotawaliwa na adui.24 Pigo la sumu ya ponografia limejaa. Linawakaba wote ambao wanakubali mkamato wake wa kudhuru kwa siri.

Hii ilitabiriwa na Bwana, aliyesema, “Na sasa nawaonyesha siri, jambo ambalo linaalikwa katika vyumba vya siri, kuleta kupita hata uharibifu wako katika mchakato wa muda, nanyi hamkulijua.”25  Kisha akaongeza onyo la pili: “Na tena, nasema kwenu kwamba adui katika vyumba vya siri anatafuta maisha yenu.”26

Sasa, zingatia ni watu wangapi, katika vyumba vingapi vya siri, wanatafuta kuharibu maisha na furaha yenu. Ikiwa ninyi akina ndugu na dada mnatazama ponografia, komeni hivi sasa! Komeni kabisa. Inaangamiza kama ukoma, inateka kama madawa ya kulevya, na babuzi kama maji magadi.

Majaribio ya kimwili si jambo jipya. Mtume Petro alionya juu ya mtego huu alipoandika:

“Wanavutia kupitia tamaa ya mwili … wale waliokuwa wasafi. …

“Wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu: maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.”27

Epukeni utumwa huo, akina ndugu na dada zangu wapendwa. Ikiwa kwa sasa unatazama ponografia, wewe koma! Na ukome sasa hivi!Tafuta usaidizi kutoka kwa askofu wako. Hakuna aliye na hekima ya kutosha kumshinda adui pekee yake, mara tu wameadhiriwa na sumu ya ponografia.

Sasa acheni tuendelee kwa swali lingine kubwa: Je,mtachagua kumfuata Bwana ama falsafa za wanadamu?

Kwa mfano, ukinzani unaenea duniani kwamba dunia imajaa watu kwa hali ya hatari na kwamba wanandoa wanapaswa wazuie idadi ya watoto wao. Je, mumesikia hayo? Hata hivyo, katika Fifth World Congress of Families, mwaka wa 2009, Dada Nelson nami tulimsikia msomi akielezea ripoti ambako alitoa kauli ya kushangaza. Alisema, “Kama kila mtu, mwanamke, na mtoto anayeishi sasa duniani angepewa robo ya ekari moja ya ardhi, watu wote bilioni 6.8 wangejaa katika nchi ya Brazili, na asilimia 20  ya Brazili bado kubaki bila watu.28 Je, hiyo inakaa kama dunia ina msongamano mkubwa?

Niliangalia hesabu hiyo. Ni sahihi. Nawasihi muamini Bwana, ambaye alisema kwamba “dunia ni kamili, na kuna ya kutosha na ya kubakisha.”29

Ukweli mwingine ni kwamba mnaishi wakati ambapo ukosefu wa ajira ni wa hali ya juu na masoko ya fedha duniani kote yana wasi wasi. Tena, suluhisho la kidunia ni kuangalia njia mbadala na mpango wa Mungu. Lakini tunajua kwamba ndoa dhabiti na familia kwa kweli husaidia uchumi kustawi. Na hatuko peke yetu katika hisia hizo.

Msomi Dk. Patrick  F. Fagan30 aliandika: “jiwe muhimu la msingi la kujengea juu yake mali ya uchumi linategemea nyumba ya wazazi waliooana---hasa familia yenye mtoto inayoabudu kila wiki. …

“… Kila ndoa inajenga nyumba mpya, kitengo cha kujitegemea cha uchumi kinachozalisha mapato, kinachonunua, kinachoweka hazina, na kuwekeza.”31

Dkt. Fagan aliongeza kuwa “mama aliyeolewa nyumbani hutoa athari zaidi kwenye uchumi kuliko vile baba aliyeoa katika sehemu za kazi. … Wakati mume anachangia uchumi wa sasa, mama anachangia uchumi wa sasa na wa siku zijazo.”32

Ripoti ya Dkt. Fagan inathibitisha dhana zilizoelezwa miaka iliyopita na Urais wa Kwanza na Mitume Kumi na Wawili katika: “Familia: Tangazo kwa Dunia.” Natumaini kwamba kila mmoja wenu ana nakala. Isome kwa makini. Wakati familia iko chini ya mashambulizi katika dunia nzima, kweli za tangazo la familia zitakuimarisha.

Ninyi vijana wa ajabu wa urithi adimu, mnafaa mfahamu matokeo yenye madhara makubwa ya mvutano wa sasa wa jamii juu ya ufafanuzi wa ndoa. Mjadala wa sasa unahusisha swali la kama watu wawili wa jinsia moja wanaweza kuoana. Kama una swali kuhusu msimamo wa Kanisa juu ya suala hili au suala lolote lingine muhimu, litafakari kwa maombi, kisha fuata ujumbe wa kinabii katika huu mkutano mkuu wa Kanisa unaokuja Oktoba hii. Jumbe hizo zenye ushawishi, pamoja na ushawishi wa Roho Mtakatifu, zitaleta kwa akili zenu ufahamu kamili na wa ukweli zaidi.

Mjadala wa ndoa ni mmojawapo tu wa utata mwingi ambao utakuwa changamoto kwenu katika siku zijazo. Kinyume na sauti kali ya adui, ninyi, kama vijana wa urithi adimu, mtachagua kusimama kwa ajili ya Bwana na ukweli Wake. Kumbuka maneno ya wimbo ulioimbwa na kwaya hii mzuri. Yarudie.Yakariri. Wimbo huu kwa kweli unawahusu ninyi:

Je! Vijana wa Sayuni watajikwaa

Katika kutetea kweli na haki?

Hali adui anashambulia,

Tutasita au kuogopa vita? La!

Ukweli kwa imani ambayo wazazi wetu walipendelea,

Ukweli kwa ukweli ambao wafia dini waliangamia,

Kwa amri ya Mungu,

Nafsi, moyo, na mkono,

Kwa uaminifu na ukweli sisi tutasimama daima.33

Mnajua kwamba Mtume Paulo alitoa unabii kuhusu masaibu ya siku zetu. Maelezo yake yanaelezwa kama tangazo letu la habari ya saa 4:00 usiku. Sikiza!

“Siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

“Wasiowapenda wa kwao,wasiotaka kufanya suluhu,wasingiziaji,wakali, wasiopenda mema,

“Wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

“Wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake: hao nao hujiepushe nao.”34

Huo ndio mwisho wa onyo lake.

Sasa, maono sahihi ya Paulo ya uharibifu wa kiroho wa siku zetu yalifuatiwa na hitimisho lake la kuliwaza, akituambia jinsi ya kukaa salama: “ Tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”35

Sasa, kwa ushauri wake ningeongeza wangu mwenyewe. Endelea kujifunza maandiko. Endelea kufanya vile vitu vinavyojenga imani katika Yesu Kristo. Kisha tambua chaguo za hekima zinazokuvutia kwa kawaida kufanya.

Imani yako katika Yesu Kristo na injili Yake itakupatia ushujaa wa kuoa na kuleta watoto katika familia yako ukiwa ungali kijana na ukiwa na uwezo wa kuwa nao. Utakapokuwa umri wangu, utawathamani watoto wako, wajukuu wako, na watoto wao, juu ya umaarufu au mali ambayo vinginevyo huenda ingekuja.

Sasa kwa swali ninaomba mtazingatia kila siku: Mtajitayarisha vipi kwa ajili ya mahojiano ya kibinafsi na Mwokozi?

Ninyi vijana wa urithi adimu si wakamilifu bado. Hakuna yeyote miongoni mwetu aliyekamili. Hivyo basi, ninyi, pamoja na sisi wengine sote, tunashukuru sana kwa ajili ya Upatanisho wa Mwokozi ambao unatoa msamaha kamili unapotubu kwa dhati. Mnajua pia kwamba makao yenu hapa duniani ni mafupi kiasi. (na zaidi unapokuwa mzee, ndio unazidi kuifahamu) Kwa muda, kila mmoja wenu atahitimu kutoka kwa hali hii ya dunia na kuendelea kwa maisha yafuatayo.

Siku ya hukumu inangoja kila mmoja wetu.Sijui kama mlango wa mbinguni ni wa lulu ama la, lakini ninajua, kama vile wanafunzi wote wa Kitabu cha Mormoni, kwamba “ mlinzi wa mlango ni yule Mtakatifu wa Israeli, na haajiri mtumishi yeyote pale; … kwani Bwana Mungu ndilo jina lake.”36 Ndio, kila moja wetu atakuwa na mahojiano ya kibinafsi na Yesu Kristo.

Kila siku duniani inawapa muda na fursa wa kujitayarisha kwa ajili ya mahojiano hayo. Tafadhali fahamu haya: Mnapochagua kuishi kwa upande wa Bwana, kamwe hamko pekee yenu. Mungu amewapa njia ya kupata usaidizi Wake mnapoendelea mbele kwenye njia hatari ya duniani. Mnapoitoa mioyo yenu Kwake kwa bidii na dhati, katika maombi ya kila siku, atatuma malaika Wake kuwasaidia.37 Na amewapa Roho Mtakatifu kuwa kando yenu mnapoishi kwa ustahiki. Amewapa maandiko ili kwamba muweze kufurahia kikamilifu maneno ya Yesu Kristo.38 Amewapa maneno ya kutii kutoka kwa manabii walio hai.

Amewapa fursa ya kupokea baraka ya baba mkuu. Itatoa ufahamu kuhusu uhusiano wenu na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo na agano lililofanywa na wao kwa ajili ya uzao wao. Baraka yenu ya baba mkuu pia inatoa ufahamu kuhusu uwezo wenu maishani hapa na katika maisha yajayo. Kila moja ya haya na misaada mingine tukufu itayokusaidia kuchagua vyema ili kwamba uweze kutamani kukutana kwako ana kwa ana na Bwana na Mwokozi wetu.

Swali langu la mwisho: Mtaweka imani yenu katika nani?

Ninyi vijana wa urithi adimu mnajua kwamba Mungu ni Baba yenu. Anawapenda. Anataka muwe na furaha. Wekeni imani yenu Kwake.39 Wekeni malengo yenu kwenye hekalu Lake tukufu. Kuweni wa kustahili kupokea endaumenti yenu na ibada tukufu ya kuunganisha. Bakini waaminifu kwa maagano hayo, na rejeeni kila mara katika hekalu. Kumbukeni, lengo lenu la thamani kabisa ni kupokea baraka kuu ya baraka zote za Mungu, ile ya uzima wa milele.40 Ibada tukufu za hekalu ni muhimu kwa baraka hio.41

Ninawaalika mjifunze kwa maombi kauli ya kimaandiko ya utambulisho wenu, kusudi na baraka, kama ilivyoandikwa katika sehemu ya  86 ya Mafundisho na Maagano. Inawahusu ninyi. Sikilizeni!

“Kwa hiyo, Bwana asema hivi kwenu ninyi [vijana wa urithi adimu], ambao ukuhani umedumu kupitia safu ya uzao wa baba zenu---

“Kwani ninyi ni warithi kisheria, kwa jinsi ya mwili, na mkafichwa kutoka ulimwenguni, pamoja na Kristo katika Mungu---

“Kwa hiyo maisha yenu na ukuhani vimedumu, na havina budi kudumu kupitia ninyi na safu ya uzao wenu hata zije zama za urejesho wa vitu vyote zilizonenwa kwa vinywa vya manabii wote watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.

“Kwa hiyo, heri ninyi kama mtakaa katika wema wangu, na nuru ya kuwa mwangaza kwa Wayunani, na kupitia ukuhani huu, mwokozi kwa watu wangu, Israeli.”42

Ndio, hakika ninyi ni vijana wa urithi adimu, walioumbwa katika mfano wa Mungu. Ninyi ni warithi kisheria, kujaribiwa na kupimwa. Mnaweza kuchagua kuwa mwangaza kwa ulimwengu, kusaidia kuokoa watoto wa Mungu, kuwa na furaha, na hatimaye kupata baraka za uzima wa milele.

Sasa, ili kuwasaidia katika chaguo hizi muhimu zilizo mbele yenu, ningependa kuwapa baraka juu yenu. Nikitumia funguo za utume mtukufu zilizokabidhiwa kwangu, Ninawabariki kwamba mfurahie maneno ya Yesu Kristo na mtumie mafundisho Yake katika maisha yenu. Nawabariki na uwezo wa kuishi kama vile angetaka ninyi muishi na, kupitia mifano yenu ya haki, muwe wa kustahili kufuatwa kama mshiriki wa Kanisa anayebeba jina Lake tukufu. Ninawabariki na ufanisi katika shughuli zenu za elimu na za kikazi, ili muweze kutoa huduma ya kustahili kwa wanadamu wenzenu. Ninawabariki na afya na nguvu mnayohitaji kutekeleza hatima tukufu ambayo Mungu amewakusudia kila mmoja wenu, ili kwamba mapenzi Yake yaweze kufanywa nanyi na kupitia ninyi.

Ninawabariki hivyo na kutoa ushuhuda wangu kwamba Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo. Hili ni Kanisa Lake. Analiongoza kupitia manabii na mitume Wake. Tunampenda na kumuidhinisha Thomas  S. Monson kama Rais wa Kanisa la Bwana siku ya leo. Ushuhuda huu na baraka ninawaachia ninyi, akina ndugu na dada zangu wapendwa, na dhibitisho langu la dhati la upendo kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

© 2013 na Intellectual Reserve, Inc. Kingereza kiliidhinishwa: 1/13 Tafsiri iliidhinishwa: 1/13 . Tafsiri ya Youth of the Noble Birthright: What Will You Choose? Lugha. PD50048932 743