2010–2019
Kuwafundisha watoto wetu kuelewa
Aprili 2012


Kuwafunza Watoto Wetu Kuelewa

Kuwafundisha watoto wetu kuelewa ni zaidi ya kupatiana maelezo. Ni kuwasaidia watoto wetu wapate mafundisho kuingia katika mioyo yao.

Miaka inapopita, utondoti mwingi katika maisha yangu unafifia zaidi na zaidi, lakini kumbukumbu zingine zinazobakia wazi sana ni kuzaliwa kwa kila mtoto wetu. Mbingu uonekana kuwa karibu sana, na kama ninajaribu, karibu kuhisi hisia zile zile za staha na za ajabu nilizopata kila wakati mmojwapo wa hawa watoto wachanga alipowekwa kwenye mikono yangu.

“Watoto wetu ni urithi wa Bwana” ( Zaburi 127:3). Yeye anamjua na kumpenda kila mmoja wao kwa upendo kamili (ona Moroni 8:17). Ni jukumu takatifu jinsi gani Baba wa Mbinguni aliloweka juu yetu kama wazazi kuwa wenzi na Yeye katika kusaidia roho Zake zenye thamani kuwa kile Yeye anachojua wanaweza kuwa.

Hii nafasi tukufu ya kulea watoto wetu ni jukumu kuu sana sisi kuweza kulifanya peke yetu bila usaidizi wa Bwana. Yeye anajua hasa kile watoto wetu wanahitaji kujua, kile wanahitaji kufanya, na kile wanahitaji kuwa, ilikurudi tena katika uwepo Wake. Yeye huwapatia kina mama na kina baba maelekezo na mwongozo mahususi kupitia maandiko, manabii Wake, na Roho Mtakatifu.

Katika ufunuo wa siku za mwisho kupitia Nabii Joseph Smith, Bwana anawaelekeza wazazi kuwafundisha watoto wao kuelewa mafundisho ya toba, imani katika Kristo, ubatizo, na kipawa cha Roho Mtakatifu. Tazama Bwana hasemi tu tunafaa “kuwafundisha mafundisho”; maelekezo Yake ni kuwafundisha watoto wetu “kuelewa mafundisho.” (OnaM&M 68:25, 28; mkazo umewekwa).

Katika Zaburi tunasoma, “Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote (Zaburi 119:34).

Kuwafundisha watoto wetu kuelewa ni zaidi ya kupatiana maelezo. Ni kuwasaidia watoto wetu wapate mafundisho kuingia katika mioyo yao kwa njia ambayo yatakuwa sehemu ya maisha yao na inaonekana katika misimamo na tabia zao maishani mwao mwote.

Nefi alifunza kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni kubeba ukweli “hata mioyoni mwa watoto wa watu” (2 Nefi 33:1). Kazi yetu kama wazazi ni kufanya yale yote tunayoweza kuleta mazingira ambapo watoto wetu watahisi ushawishi wa Roho na kisha kuwasaidia kutambua kile wanachohisi.

Nakumbuka simu niliopokea miaka kadha iliyopita kutoka kwa binti yetu Michelle. Akiwa na mhemko ororo alisema, “Mama, nimepata uzoefu wa ajabu sana na Ashley.” Ashley ni binti yake ambaye alikuwa miaka mitano wakati huo. Michelle alielezea asubuhi hiyo juu ya kuchokozana kati ya Ashley na Andrew wa miaka mitatu---ambaye hakupendelea kushiriki vitu vyake na yule mwingine, angempiga. Baada ya kuwasaidia kutatua mambo, Michelle alienda kumwangalia mtoto.

Punde, Ashley alikuja akikimbia, amekasirika kwamba Andrew hakutaka kushiriki. Michelle alimkumbusha Ashley sharti walilokuwa wameweka katika jioni ya familia nyumbani ya kuwa wakarimu mmoja kwa mwingine.

Alimuuliza Ashley kama angependa kuomba na kumuuliza Baba wa Mbinguni usaidizi, lakini Ashley akiwa bado amekasirika, alijibu, “La.” Wakati alipomuuliza kama anaamini Baba wa Mbinguni angejibu maombi yake, Ashley alisema yeye hajui. Mama alimwomba ajaribu na kuchukua mikono yake na kupiga magoti chini pamoja naye.

Michelle alimshauri Ashley kwamba amwulize Baba wa Mbinguni kumsaidia Andrew aweze kushiriki--- na kumsaidia awe mkarimu. Wazo la Baba wa Mbinguni kusaidia kakake mdogo kushiriki lazima lilisinya upendeleo wa Ashley, na alianza kuomba, kwanza akimwuliza Baba wa Mbinguni kumsaidia Andrew kushiriki. Alipokuwa akiomba alimsihi kumsaidia kuwa mkarimu, alianza kulia . Ashley alisitisha maombi na kuegemeza kichwa chake kwenye bega la mama yake. Michelle alimkumbatia na kumuuliza kwa nini alikuwa analia. Ashley alisema hakuwa akijua.

Mama yake alisema, “Nafikiria najua kwa nini unalia. Je! Unahisi vyema ndani?” Ashley aliashiria kwa kichwa na mama yake akaendelea, “Huyu ni Roho anayekusaidia kuhisi hivyo. Ni njia ya Baba wa Mbinguni ya kukwambia Yeye anakupenda na atakusaidia.”

Alimuuliza Ashley kama anaamini haya, kama anaamini Baba wa Mbinguni anaweza kusaidia. Kwa macho yake madogo yaliyojawa na machozi, Ashley alisema anaamini.

Wakati mwingine njia yenye nguvu sana ya kuwafundisha watoto wetu kuelewa mafundisho ni kufunza katika muktadha wa kile wanachopata uzoefu papo hapo. Hizi nyakati zinatokea na haziwezi kutarajiwa na zinatokea katika hali za kawaida za maisha ya familia. Zinakuja na kutoweka ghafla, kwa hivyo tunahitajika kuwa macho na kutambua nyakati za kufunza ambapo watoto wetu wanakuja kwetu na swali au shaka, wakati wana shida za kusikilizana za ndugu zao au marafiki, wakati wanapohitaji kuthibiti hasira zao, wakati wamefanya kosa, au wakati wanahitaji kufanya uamuzi. (Ona Teaching, No Greater Call: A Resource Guide for Gospel Teaching [1999], 140–41; Marriage and Family Relations Instructor’s Manual [2000], 61.)

Kama tuko tayari na tutakubali Roho atuongoze katika hali hizi, watoto wetu watafunzwa kwa juhudi na uelewa mkuu.

Na kama vile nyakati muhimu za kufunza zinazotokea, tunapanga kwa makini nyakati za kila mara kama vile maombi ya familia, masomo ya maandiko ya familia, jioni ya familia nyumbani, na zile shughuli zingine za familia.

Katika kila hali ya kufunza kujifunza kote na uelewa wote unakuzwa vyema katika mazingira ya uchangamfu na upendo ambapo Roho atakuwepo.

Karibu miezi miwili kabla ya watoto wake kufika umri wa miaka minane, baba mmoja angetenga muda kila wiki kuwatayarisha kwa ubatizo. Binti yake alisema kwamba wakati ilipofikia zamu yake, alimpatia shajara na wakakaa pamoja, wao wawili tu, wakazungumza na kushiriki hisia zao kuhusu kanuni za injili. Alimchorea chombo cha picha walipokuwa wanaendelea. Ilionyesha maisha kabla ya kuzaliwa, maisha ya duniani, na kila hatua anayohitaji kuchukua ili kurudi kuishi na Baba wa Mbinguni. Alitoa ushuhuda wake kuhusu kila hatua ya mpango wa wokovu alipokuwa akimfunza.

Wakati huyu binti alipokumbuka uzoefu huu baada kuwa mtu mzima, alisema: “Kamwe sitasahau upendo niliohisi kutoka kwa baba yangu alipotumia muda huo na mimi … naamini kwamba uzoefu huu ulikuwa sababu kuu nilipata ushuhuda wa injili wakati nilipobatizwa.” (OnaTeaching, No Greater Call,129).

Kufunza kwa ajili ya kuelewa kunahitaji juhudi za azimio na za kila mara. Kunahitaji kufunza kwa maadili na mfano na hasa kwa kuwasaidia watoto wako kuishi kile wamejifunza.

Rais Harold B. Lee alifunza, Bila kupata uzoefu wa kanuni ya injili kwa matendo, ni … vigumu sana kuamini katika hio kanuni”Teachings of Presidents of the Church: Harold B. Lee [2000], 121).

Nilijifunza mara ya kwanza kuomba kwa kupiga magoti na familia yangu katika maombi ya familia. Nilifunzwa lugha ya maombi niliposikiliza wazazi wangu wakiomba na waliponisaidia kuomba maombi yangu ya kwanza. Nilijifunza kwamba ningezungumza na Baba wa Mbinguni na kuuliza mwongozo.

Kila asubuhi bila kukosa, mama yangu na baba yangu walitukusanya pamoja katika meza ya jikoni kabla ya kiamsha kinywa, na tulipiga magoti katika maombi ya familia. Tuliomba katika kila mlo. Jioni kabla kulala, tulipiga magoti pamoja katika sebule na kufunga siku kwa maombi ya familia.

Ingawaje kulikuwa na mengi ambayo sikuelewa juu ya maombi kama mtoto, yalikuwa sehemu ya maisha yangu kwamba yalikaa ndani yangu. Bado naendelea kujifunza, na uelewa wangu wa uwezo wa maombi bado unaendelea kukua.

Mzee Jeffrey R. Holland alisema, “Tunafahamu kwamba ufanisi wa ujumbe wa injili unategemea juu ya kufunzwa na kisha kuelewa na kisha kuishi katika njia ambayo ahadi zake za furaha na wokovu zinaweza kupatikana” (“Teaching and Learning in the Church” [mkutano wa mafunzo kwa viongozi ulimwenguni kote, Feb. 10, 2007], Liahona, June 2007, 57; Ensign, June 2007, 89).

Kujifunza kuelewa kikamilifu mafundisho ya injili ni mfanyiko wa maisha yote na huja “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo” (2Nefi  28:30)‎. Kama watoto wanapojifunza na kutenda juu ya kile walichojifunza, uelewa wao utapanuka, ambavyo inaelekeza kwa kujifunza zaidi, vitendo zaidi, na hata uelewa unaozidi daima.

Tunaweza kujua watoto wetu wameanza kuelewa mafundisho wakati tunapoona ikionyeshwa kwa msimamo na matendo yao bila kulazimishwa au kuzawadiwa. Watoto wetu wanapojifunza kuelewa mafundisho ya injili, wanakuwa wa kujitegemea na kuwajibika. Wanakuwa sehemu ya suluhu kwa changamoto ya familia yako na kufanya mchango sahihi kwa mazingira ya nyumbani mwetu na ufanisi wa familia.

Tutawafunza watoto wetu kuelewa tunapochukua kila fursa ya kufunza, kualika Roho, kuweka mfano, na kuwasaidia kuishi kile walichojifunza.

Tunapotazama kwenye macho ya mtoto mchanga, tunakumbushwa wimbo:

Mimi ni mtoto wa Mungu,

Na kwa hivyo mahitaji yangu ni makuu;

Nisaidie kuelewa maneno yake

Kabla haijapata kuchelewa.

Niongoze, nielekeze, tembea pamoja nami,

Nisaidie nipate njia

Nifunze yote ambayo ni sharti nifanye

Ili niweze kuishi naye siku moja.

(“I Am a Child of God,” Hymns, no. . 301; mkazo umeongezewa)

Natufanye hivyo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.