Ruka uongozaji mkuu
Oktoba 2012 | Kuhusu Majuto na Nadhiri

Kuhusu Majuto na Nadhiri

Oktoba 2012 Mkutano Mkuu

Tunavyojitolea sana wenyewe kutafuta utakatifu na furaha, kutakuwa na uwezekano mdogo wa kuwa katika mapito ya majuto.

Kuhusu Majuto

Rais Monson, sisi tunakupenda. Asante sana kwa matangazo yenye mvuvio na ya kihistoria kuhusu ujenzi wa mahekalu mapya na huduma ya umisionari. Kwa sababu yake, nina hakika baraka kuu zitatujia sisi na kwa vizazi vingi vijavyo.

Ndugu na dada wapendwa, marafiki zangu wapendwa! Tuna miili itakayokufa. Natumaini kuwa jambo hili haliji kama la kushangaza kwa yeyote.

Hakuna yeyote kati yetu atayekuwa duniani kwa muda mrefu. Tuna miaka kadhaa ya thamani, ambayo, katika mtazamo wa milele, haibebi hata uzito kwa kufumba jicho.

Halafu tunaondoka. Roho zetu “zinachukuliwa nyumbani kwa Mungu Yule aliyetupa uhai.” 1 “Tunailaza chini miili yetu na kuyaacha nyuma mambo ya dunia tunapoendelea katika sehemu nyingine ya kuishi kwetu.

Tunapokuwa wadogo, inaonekana kwamba tutaishi milele. Tunafikiria kuwa kuna mgao usioisha wa macheo ambayo yanasuburi kupita tu kwenye upeo, na wakati wa usoni unaoonekana kwetu kama vile barabara nyoofu ambayo inaendelea bila kuwa na mwisho mbele yetu.

Lakini, jinsi tunavyozeeka, ndivyo zaidi tunavyoangalia nyuma na kushangaa jinsi gani barabara hiyo kwa kweli ni fupi. Tunashangaa jinsi gani miaka ingeweza kupita kwa haraka hivyo. Na kuanza kufikiria kuhusu maamuzi tuliyoyafanya na mambo tuliyoyafanya. Katika mchakato huo, tunakumbuka nyakati nyingi nzuri ambazo zinatupatia faraja katika nafsi zetu na furaha katika mioyo yetu. Lakini pia kumbuka majuto—mambo tunayotamani tungerudi nyuma na kuyabadilisha.

Mwuguzi aliyewatunza wanaougua magonjwa yasiyosikia dawa kila mara amekuwa akiuliza swali rahisi kwa wagonjwa wake wanapokuwa tayari kuondoka katika maisha haya.

“Una majuto yoyote?” angewauliza. 2

Kuwa karibu sana na siku ile ya mwisho ya maisha ya muda mara nyingi hutoa uwazi kwenye wazo na huleta ufahamu wa kina na mtazamo. Kwa hiyo wakati watu hawa wanaulizwa maswali kuhusu majuto yao, walifungua mioyo yao. Wakatafakari kuhusu kile wangebadili kama wangerudisha saa nyuma.

Nilipotafakari yale waliyoyasema, nilishangazwa na jinsi kanuni za kimsingi za injili ya Yesu Kristo zinaweza kuathiri mwelekeo wa maisha yetu daima, kama tutazitumia.

Hakuna cha siri kuhusu kanuni za injili. Tumejifunza haya katika maandiko, tumeyajadili katika Shule ya Jumapili, na tumezisikia kutoka katika mimbari mara nyingi. Kanuni hizi za kiungu na maadili yamenyooka na ni wazi; ni mazuri, mazito, na yana nguvu; na kwa hakika yanaweza kutusaidia kuepukana na majuto ya baadaye.

Natamani Ningetumia Muda Zaidi na Watu Ninaowapenda.

Pengine majuto ya kawaida sana ambayo watu wanaokufa walieleza ilikuwa ni kuwa walitamani wangetumia muda zaidi na wale watu wanaowapenda.

Wanaume hasa waliimba ombolezo hili la watu wote: “walijutia kutumia maisha yao [kila siku] katika kinu cha…kazi. 3 Wengi wamekosa nafasi kuwa na kumbukumbu ya muhimu ambayo inatokana na kutumia muda na familia na marafiki. Wanakosa kujenga muungano wa kina na wale wenye maana zaidi kwao.

Je! si ni kweli kwamba huwa tunakuwa na shughuli sana? Na inasikitisha kusema kwamba tunavaa kujishughulisha kwetu kama beji ya heshima kama kuwa na shughuli, kama kwamba, kujishughulisha kwenyewe kulikuwa ni mafanikio au ishara ya maisha ya hali ya juu.

Ndivyo?

Nafikiria Bwana wetu na Mfano kamili, Yesu Kristo, na maisha yake mafupi kati ya watu wa Galilaya na Yerusalemu. Nimejaribu kumfikiria akiharakisha kati ya mikutano au akifanya kazi nyingi kwa wakati mmoja kukamilisha kazi za dharura zilizo kwenye orodha ya vitu vya kufanya.

Siwezi kuiona

Badala yake, Ninamuona Mwana wa Mungu mwenye huruma na anayejali akiishi kwa madhumuni kila siku. Aliposhirikiana na wale walio karibu naye, walijihisi wa maana na wanapendwa. Alijua thamani ya milele ya watu aliokutana nao. Aliwabariki, akawatumikia . Aliwainua, akawaponya. Aliwapa karama nzuri ya muda wake.

Katika siku zetu, ni rahisi kujifanya tu kuwa tunatumia muda na wengine. Kwa kubonya puku tunaweza “kuungana” na maelfu ya “marafiki” bila ya kuonana nao uso kwa uso hata mmoja wao. Teknolojia inaweza kuwa kitu cha ajabu, na ni vizuri sana pale tunapokuwa mbali na wale tunaowapenda. Mke wangu na mimi tunaishi mbali na wale tunaowapenda; tunajua jinsi gani hiyo ilivyo. Lakini, ninaamini kuwa hatuelekei pafaapo, kibanafsi na kama jamii, wakati tupoungana na wanafamilia au marafiki sana sana kwa kuweka picha za kufurahisha, kutumiana vitu visivyo na maana, au kuwaunganisha kwenye mitandao ya interneti. Ninaamini kuna nafasi ya vitu kama hivi, lakini tunataka kutumia muda kiasi gani katika sehemu kama hii? Kama tutashindwa kujitolea nafsi zetu bora na muda usiogawanyika kwa wale ambao ni wa muhimu sana kwetu, siku moja tutajutia.

Na tuamue kuthamini wale tunaowapenda kwa kutumia muda mwingi wa maana nao, na kufanya mambo pamoja, na kukuza kumbukumbu za thamani.

Natamani Ningeliishi Kadiri ya Uwezo Wangu

Majuto mengine ambayo watu walielezea ni kwamba walishindwa kuwa watu ambao walihisi wangekuwa na walipaswa kuwa. Walipotazama nyuma kuhusu maisha yao, waligundua kuwa hawakutimiza matarajio yao, kwamba nyimbo nyingi zilibaki bila kuimbwa.

Sizungumzii hapa kuhusu mafanikio ya maisha katika kazi zetu. Ngazi hio, licha ya jinsi inavyoweza kuonekana kuwa na ukubwa gani hapa duniani, ni nadra hujumuisha hatua moja katika safari ya milele inayotusubiri.

Badala yake, nazungumzia kuwa mtu ambaye Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, amekusudia sisi tuwe.

Tunawasili katika dunia hii, kama vile mshairi alivyosema, “tukiandama michirizi ya wingu la utukufu” 4 kutoka kwa tufe ya maisha kabla kuzaliwa..

Baba yetu wa mbinguni huona uwezo wetu halisi usidhihirika. Anajua mambo kutuhusu ambayo hatuyajui. Anatushawishi katika maisha haya kutimiza kipimo cha uumbwaji wetu, kuishi maisha mazuri, na kurudi katika uwepo wake.

Kwa nini, basi, tunatenga muda mwingi na nguvu kwa mambo ambayo ni ya muda tu, yasiyo ya msingi, na ya juu juu? Je! Tunakataa kuona ujinga wa kujitahidi kutimiza yasiyo ya muhimu na ya muda mfupi?

Je! Isingekuwa ya busara kwetu “kujiwekea hazina mbinguni, kisikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi”? 5

Tunafanyaje hivi? Kwa kufuata mfano wa Mwokozi, kwa kujumuisha mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku, kwa kumpenda Mungu na watu wenzetu kwa ukweli.

Hatuwezi kufanya hivyo kwa kujiburuza, tukiangalia---saa zetu, kulalamika---tukienda katika mtazamo wetu wa ufuasi.

Inapokuja kwa kuishi injili, tusiwe kama mvulana aliyechovya kidole chake cha mguu katika maji na akasema kwamba ameenda kuogelea. Kama wana na binti wa Baba yetu wa Mbinguni, tuna uwezo wa mengi zaidi. Kwa hiyo, matarajio mema hayatoshi. Lazima tutende. Hasa cha umuhimu zaidi, lazima tuwe kile Baba yetu wa Mbinguni anatutaka tuwe.

Kuutangaza ushuhuda wetu wa injili ni vizuri, lakini kuwa mfano unaoishi wa injili iliyorejeshwa ni bora zaidi. Ukitamani kuwa mwaminifu zaidi katika maagano ni vizuri; hasa kuwa mwaminifu kwa maagano matakatifu---ikijumuisha kuishi maisha ya maadili, kulipa fungu la kumi na matoleo, kulitii Neno la Hekima na kuwatumikia wale wenye mahitaji ni bora. Kusema kwamba tutatumia muda mwingi zaidi kwa ajili ya maombi ya familia, kusoma maandiko, na shughuli nzuri za kifamilia ni vizuri; lakini hasa kufanya mambo haya yote bila kusita yataleta baraka za kiungu katika maisha yetu.

Ufuasi ni kutafuta utakatifu na furaha. Ni njia ya kuelekea kwenye ubora na furaha yetu.

Na tuamue, basi, kumfuata Mwokozi na kufanya kazi kwa bidii kuwa mtu tuliyokusudiwa kuwa. Na tusikilize na kutii ushawishi wa Roho Mtakatifu. Tunapofanya hivyo, Baba yetu wa Mbinguni atatufunulia mambo ambayo hatukuyajua kutuhusu. Atatuangazia njia yetu mbele na kutufungua macho kuona yale tusiyoyafahamu na labda vipaji visivyofikirika.

Tunavyojitolea zaidi katika kutafuta utakatifu na furaha, kutakuwa na uwezekano mdogo wa sisi kuwa katika mapito ya majuto. Tunavyotegemea rehema ya Mwokozi zaidi, tutahisi hivyo zaidi kwamba tuko katika njia ambayo Baba wetu wa Mbinguni ametupangia sisi.

Ninatamani Ningejiruhusu Kuwa na Furaha Zaidi.

Juto jingine la wale waliojua wanakufa inaweza kuwa ya kushangaza kiasi. Walitamani wangejiruhusu kuwa na furaha zaidi.

Mara nyingi tunajikuta katika udanganyifu kwamba kuna kitu tusichofikia ambacho kitatuletea furaha: hali nzuri ya kifamilia, hali nzuri ya kifedha, au mwisho wa jaribu lenye changamoto.

Tunapozeeka, ndio zaidi tunapotazama nyuma na kugundua kuwa hali ya nje haijalishi au kuukilia furaha yetu.

Sisi tuna maana.Sisi tunaukilia furaha yetu.

Wewe na mimi mwishowe tunasimamia furaha yetu wenyewe.

Mke wangu, Harriet, nami tunapenda kuendesha baiskeli. inapendeza kutoka nje na kufurahia uzuri wa mazingira. Tuna njia kadhaa tunapenda kuendeshea baiskeli, lakini huwa hatutilii mkazo ni kwa umbali gani tumesafiri au kwa mbio kiasi gani tumesarifi ukilinganisha na waendeshaji baiskeli wengine.

Lakini, mara myingine nafikiri inabidi tuwe kidogo na ushindani. Mimi hata nafikiria tunaweza kupata muda bora au kuendesha baiskeli kwa kasi zaidi kama tutajisukuma zaidi kidogo. Na kisha mara nyingine huwa nafanya kosa kubwa la kutaja wazo hili kwa mke wangu mpendwa.

Jibu lake la kawaida kwa wazo langu la namna hii kila mara ni la ukarimu sana, wazi sana, moja kwa moja sana. Hutabasamu na kusema, “Dieter, siyo mashindano, ni safari. Furahia wakati huu.”

Yu sahihi jinsi gani!

Wakati mwingine katika maisha, tunalenga sana kwenye mstari wa kumalizia kwamba tunashindwa kupata furaha katika safari hii. Siendi kuendesha baiskeli na mke wangu kwa sababu ninafuraha ya kumaliza. Naenda kwa sababu uzoefu wa kuwa naye ni mzuri na wa kufurahia.

Je! Haionekani kuwa ujinga kuharibu uzoefu mzuri na furaha kwa sababu daima tunatarajia wakati utafikia mwisho?

Je! Tunasikiliza muziki mzuri tukisubiri kidokezo cha mwisho kumalizikia kabla ya kujiruhusu kuufurahia kiukweli? La. Tunasikiliza na kuunganisha kwa mchanganyiko wa melodi, mdundo, na upatanifu kote katika utungo.

Tunatoa sala zetu kwa “amina” peke yake au kuwa na mwisho katika akili zetu? Sivyo kabisa. Tunasali tuwe karibu na Baba yetu wa Mbinguni, kupokea Roho Wake na kuhisi upendo Wake.

Tusisubiri kuwa na furaha mpaka tufikie kilele fulani cha usoni, ndipo kugundua kwamba furaha tayari ilikuwepo –wakati wote! Maisha hayamaanishi kuthaminiwa tu kwa kufikiria yaliyopita. Hii ndio siku Bwana ameifanya  … ,” Mtunga Zaburi aliandika.”Furahia na kuwa na furaha katika hiyo.”6.

Akina ndugu na dada, haijalishi hali zetu, haijalishi changamoto zetu ama majaribu, kuna kitu katika kila siku cha kukumbatia na kufurahia. Kuna kitu katika kila siku ambacho kinaweza kuleta shukrani na shangwe kama tu tutaona na kukithamini.

Labda tunapaswa kuangalia kidogo kwa macho na zaidi kwa mioyo yetu. Ninapenda nukuu hii: “Mtu huona wazi kwa moyo peke yake. Kila kitu cha muhimu hakionekani katika macho.”7

Tumeamriwa “kutoa shukrani katika kila kitu.”8 Je! Si vyema kuona kwa macho yetu na mioyo haswa kwa vitu vidogo tunavyoweza kuwa na shukrani navyo, badala ya kukuza mabaya katika hali ya sasa.

Bwana ameahidi, “Na Yule apokeaye vitu kwa shukrani atatukuzwa; na vitu vya dunia hii ataongezewa, hata mara mia.”9

Ndugu na Dada, kwa baraka nyingi za baba yetu wa Mbinguni, Mpango Wake wa ukarimu wa wokovu, ukweli mtukufu wa injili iliyorejeshwa, na mambo mengine mazuri ya maisha, safari hii ya maisha, “hatuna sababu ya kufurahia?”10

Na tuamue kuwa na furaha, bila kujali hali zetu.

Ya Nadhiri

Siku moja tutaichukua hiyo hatua isiyoepukika na kuvuka kutoka katika tufe ya maisha ya muda mpaka yajayo. Siku moja tutazama nyuma katika maisha yetu na kushangaa kama tungeweza kuwa bora zaidi, kufanya maamuzi bora, au kutumia muda wetu kwa hekima zaidi.

Ili kuepuka baadhi ya majuto ya maisha, ingekuwa busara kuweka nadhiri hizo leo. Kwa hivyo, acha sisi:

 • Tuazimie kutumia muda mwingi na wale tunaowapenda.

 • Tuazimie kujaribu kuwa mtu makini zaidi Mungu anatutaka tuwe.

 • Tuazimie kupata furaha, bila kujali hali zetu.

Ni ushuhuda wangu kwamba majuto mengi makubwa ya kesho yanaweza kuzuiwa kwa kumfuata Mwokozi leo. Kama tumetenda dhambi au kufanya makosa—kama tumefanya maamuzi ambayo tunayajutia –tuna karama nzuri ya Upatanisho wa Kristo, ambamo tunaweza kusamehewa. Hatuwezi kurudi nyuma na kubadilisha yaliyopita, lakini tunaweza kutubu. Mwokozi anaweza kufuta machozi ya majuto11 na kuondoa mzigo wa dhambi. 12 Upatanisho Wake unaturuhusu kuyaacha yaliyopita na kuendelea mbele na mikono misafi, moyo msafi13, na matazamio ya kufanya vyema na hasa kuwa bora.

Ndio, maisha haya yanapita upesi; siku zetu zinaonekana kufifia haraka; na kifo kinaogofya wakati mwingine. Hata hivyo, roho zetu zitaendelea kuishi na siku moja zitaunganishwa na miili yetu iliyofufuka kupokea utukufu usiokufa. Ninatoa ushuhuda wangu wa dhati kwa sababu ya Kristo mwenye rehema, tutaishi tena na milele. Kwa sababu ya Mwokozi na Mkombozi wetu, siku moja tutaelewa na tutafurahia katika maana ya maneno “uchungu wa kifo umemezwa katika Kristo.”14

Njia katika kutimiza kudura yetu tukufu kama watoto wa Mungu ni ya milele. Ndugu na dada zangu wapendwa, marafiki wapendwa, lazima tuanze kutembelea njia hiyo ya milele leo; hatuwezi kupoteza siku moja. Naomba kwamba hatutasubiri mpaka tuwe tayari kufa kabla ya kujifunza kikweli kuishi. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Onesha KumbukumbuFicha Kumbukumbu

  Muhtasari

  1. Alma 40:11.

  2. Ona Susie Steiner, “Top Five Regrets of the Dying,” Guardian, Feb.  1, 2012, www.guardian.co.uk/lifeandstyle/2012/feb/01/top-five-regrets-of-the-dying

  3. Bronnie Ware, in Steiner, “Top Five Regrets of the Dying

  4. “Ode: Intimations of Immortality from Recollections of Early Childhood,” The Complete Poetical Works of William Wordsworth (1924), 359

  5. Mathayo 6:20.

  6. Zaburi 118:24.

  7. Antoine de Saint-Exupéry, The Little Prince, trans. Richard Howard (2000), 63.

  8. Mosia 26:39; ona pia Mafundisho na Maagano 59:7.

  9. Mafundisho na Maagano 78:19.

  10. Alma 26:35.

  11. Ona Ufunuo 7:17.

  12. Ona Mathayo 11:28–30.

  13. Ona Zaburi 24:4.

  14. Mosia 16:8; ona pia 1 Wakorintho 15:54.