2010–2019
Msingi Thabiti
Aprili 2013


Msingi Thabiti

Hebu tukubali mwaliko wa Mwokozi kumjia. Hebu tujenge maisha yetu juu ya msingi salama na thabiti.

Mnamo Oktoba 17, 1989, nikiwa ninaendesha gari kwenda nyumbani baada ya kazi, nilikuwa ninakaribia taa ya kusimamisha katika makutano ya Market na Beale Streets kule San Francisco, California. Wakati huo nilisikia gari likitingika na kufikiria, “Lazima iwe gurudumu limetoboka.” Gari likiendelea kutingika, niliona basi karibu kabisa nami nikafikiri, “ Basi hiyo imenigonga!” Kisha gari likatingika zaidi na zaidi, na nikafikiria, “Lazima iwe magurudumu yote manne yametoboka” Lakini haikuwa magurudumu au basi---ilikuwa tetemeko la nguvu! Niliposimama katika taa nyekundu, kulikuwa na viwimbi kwenye lami kama mawimbi ya bahari yakitapaa chini Market Street. Mbele yangu jengo refu la ofisi lilikuwa likitingika upande kwa upande, na matofali yakaanza kuanguka kutoka kwa jengo zee kwa mkono wangu wa kushoto na tetemeko likiendelea kutikisika.

Tetemeko la ardhi la Loma Prieta lilipiga Eneo la San Francisco Bay saa 5:04 mchana siku hiyo na kuwawacha zaidi ya watu 12,000 bila makazi.

Tetemeko hilo la ardhi lilisababisha uharibifu mkubwa katika Eneo la San Francisco Bay, hasa kwenye udongo usio imara kule San Francisco na Oakland. Kule San Francisco, Wilaya ya Marina ilikuwa imejengwa juu ya shamba la taka lililotengenezwa na mchanganyiko wa mchanga, uchafu, vifusi, na vifaa vingine vyenye asilimia kubwa ya maji ya chini ya ardhi. Baadhi ya taka ilikuwa vifusi vilivyotupwa kwenye ghuba ya San Francisco baada ya tetemeko la ardhi la 1906 la San Francisco.”1

Mnamo 1915, majengo ya ghorofa yalijengwa kwenye shamba la taka. Kwenye tetemeko la ardhi la 1989, matope, mchanga, na vifusi vilivyojaa maji vilibadilika na kuwa kioevu maji maji, kusababisha majengo ya kuzama. Majengo hayakuwa yamejengwa kwenye msingi thabiti.

Tetemeko la ardhi la Loma Prieta liliathiri maisha ya wengi, ikiwa ni pamoja na yangu mwenyewe. Kwa kutafakari matukio ya siku hiyo ilithibitisha tena akilini mwangu na moyoni mwangu kwamba ili kufanikiwa kuhimili tufani, tetemeko, na majanga ya maisha, ni lazima tujenge juu ya msingi thabiti.

Helamani nabii wa Kinefi alitoa ufafanuzi wazi wa umuhimu wa kujenga maisha yetu kwenye msingi thabiti, hata msingi wa Yesu Kristo: “Na sasa, wana wangu, kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenga msingi wenu, kwamba ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndio, mishale yake kimbungani wakati mvua yake wa mawe na dhoruba kali itapiga juu yenu, hautakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake mmejengwa, ambapo ni msingi imara msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka” (Helamani 5:12).

Katika ujenzi wa mahekalu ya kisasa, makini hupewa uhandisi, ubuni, na matumizi ya vifaa vya ujenzi. Upimaji wa kina wa udongo na geologia hufanyika mahali ambapo hekalu litajengwa. Masomo ya mvua, upepo, na mabadiliko ya hali ya hewa ya eneo hutiliwa maanani ili hekalu lililokamilika liweze kuhimili si tu dhoruba na mabadiliko ya hali ya hewa ya kawaida katika eneo hilo, lakini hekalu huundwa na kusimamishwa ili kuhimili matetemeko yasiyotarajiwa, kimbunga, mafuriko na majanga mengine ya asili ambayo yanaweza kutokea. Katika mahekalu mengi, ruundo za saruji au chuma huendeshwa ndani ardhini ili kutia nanga msingi wa hekalu.

Kama wabuni na wajenzi wa wakati wetu, Baba yetu wa upendo na mkarimu aliye Mbinguni na Mwanawe wametayarisha mipango, nyenzo, na rasilimali nyingine kwa ajili ya matumizi yetu ili tuweze kujenga na kupanga maisha yetu kuwa ya uhakika na yasiotingika. Mpango ni mpango wa wokovu, mpango mkubwa wa furaha. Mpango ambao unatuonyesha picha ya wazi na ufahamu wa mwanzo na mwisho, na hatua muhimu, ikiwa ni pamoja na maagano, ambayo ni muhimu kwa kila mmoja wa watoto wa Baba kuwa na uwezo wa kurudi katika uwepo Wake na kuishi naye milele.

Imani, toba, ubatizo, karama ya Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho ni sehemu ya “miongozo” ya maisha. Hutusaidia kuunda vitalu sahihi vya jengo ambavyo vitashikilia maisha yetu kwa Upatanisho wa Kristo. Haya huunda na kupanga viumbo vya kuhimili vya maisha ya mtu. Kisha, kama tu vile mipango ya hekalu yana “mwongozo maalum” ambao hutoa maelekezo ya kina kuhusu namna ya kuunda na kuunganisha vipengele muhimu, kuomba, kusoma maandiko, kushiriki sakramenti, na kupokea maagano muhimu ya ukuhani huwa “mwongozo maalum” ambao husaidia kuunganisha na kufunga pamoja muundo wa maisha.

Mapatano katika matumizi ya miongozo hii maalum ni muhimu. Kwa mfano, katika mchakato wa kutengeneza tofali, viwango sahihi vya, mchanga, changarawe, saruji, na maji hutumika ili kufanikisha nguvu ya juu kabisa. Viwango visivyo sahihi au kuondolewa kwa sehemu yoyote ya viini hivi unaweza kufanya tofali kuwa dhaifu na kutoweza kufanya kazi yake muhimu.

Kwa namna hiyo hiyo, tusipotoa usawa sahihi katika maisha yetu ya maombi ya kila siku ya kibinafsi na kukaramia maandiko, uimarishaji wa kila wiki wa ushirika wa sakramenti, na ushiriki wa mara kwa mara katika maagano ya ukuhani kama vile maagano ya hekalu, sisi pia tuko hatarini kuwa dhaifu katika nguvu za kimiundo zetu za kiroho.

Paulo, katika barua kwa Waefeso alisema kwa njia hii, ambayo hutumika kwa haja ya usawa na uwiano tabia zetu na nafsi: “Katika yeye jengo lote linaunganishwa vema na kukaa hata liwe hekalu takatifu katika Bwana” ( Waefeso 2:21).

Maombi ni mojawapo ya vitalu vya kimsingi na muhimu zaidi vya ujenzi wa imani yetu na tabia. Kupitia maombi tuna uwezo wa kutoa shukrani, upendo, na ibada kwa Mungu. Kupitia maombi tunaweza kuwasilisha mapenzi yetu Kwake na kupokea nguvu kuainisha maisha yetu kwa mafundisho Yake. Maombi ni njia tunayoweza kupitia ili kutafuta ushawishi Wake katika maisha yetu, hata ufunuo.

Alma alifundisha: “Shauriana na Bwana katika matendo yako yote, na atakuongoza kwa yale mema, ndio, unapolala usiku lala katika Bwana, ili akulinde usingizini mwako, na ukiamka asubuhi ebu moyo wako ujazwe na shukrani kwa Mungu; na ukifanya vitu hivi, utainuliwa katika siku ya mwisho”(Alma 37:37).

Kushiriki mawazo yetu, hisia, na nia na Mungu kupitia maombi ya kina na ya dhati kunapaswa kuwa muhimu kwa kila mmoja wetu na ya asili kama kupumua na kula.

Kuchambua maandiko kila siku pia kutaimarisha imani yetu na tabia. Kama tunavyohitaji ili kuboresha miili yetu, roho zetu na nafsi zitajazwa tena na kuimarishwa kwa kukaramia maneno ya Kristo kama yalivyomo katika maandiko ya manabii. Nefi alifundisha, “Shiriki maneno ya Kristo; kwani tazama, maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda” (2 Nefi 32:3).

Ingawa kusoma maandiko ni kuzuri, kusoma kwenyewe hakutoshi kukamata upana kamili na kina cha mafundisho ya Mwokozi. Kuchambua, kuwaza, na kutumia maneno ya Kristo kama yalivyofundishwa katika maandiko kutaleta hekima na maarifa zaidi ya ufahamu wetu wa kidunia. Hii itaimarisha ahadi yetu na kutoa hifadhi ya kiroho kufanya kazi yetu nzuri zaidi katika hali zote.

Mojawapo wa hatua muhimu zaidi tunaweza kuchukua ili kuimarisha maisha yetu na kubaki imara katika msingi wa Mwokozi ni kushiriki sakramenti kwa kustahili kila wiki. Agano la sakramenti humpa kila mshiriki wa Kanisa fursa ya kutafakari maisha yake mapema, kuzingatia vitendo au kutotenda ambako kungehitaji kutibiwa, na kisha kwa kushiriki mkate na maji kama nembo takatifu katika kukumbuka mwili na damu ya Yesu Kristo, ushahidi wa Upatanisho Wake. Ikifanywa kwa usafi na unyenyekevu, tunapokea upya maagano ya milele, tunasafishwa na kutakaswa, na kupokea ahadi kuwa tutakuwa na Roho Wake kuwa nasi, daima. Roho hutenda kama aina ya chokaa, kiungo ambacho hakitakasi tu bali huleta mambo yote katika kumbukumbu yetu na hushuhudia mara kwa mara juu ya Yesu Kristo. Kushiriki sakramenti kwa kustahili huimarisha uhusiano wetu wa kibinafsi kwa mwamba msingi, hata kwa Yesu Kristo.

Wakati wa huduma Yake, Mwokozi alifundisha kwa upendo na ufafanuzi mafundisho, kanuni, na hatua muhimu ambayo ingeweza kuhifadhi maisha yetu na kuimarisha tabia zetu. Mwishoni mwa Mahubiri ya Mlimani, Alisema:

“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, [ambaye] aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba--

“Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma na zikaipiga nyumba ile isianguke; kwa maana msingi yake imewekwa juu ya mwamba.

Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyefanya, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga----

“Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”(3 Nefi 14:24–27; ona pia Mathayo 7:24–27).

Akina ndugu na dada, hakuna yeyote kati yetu ambaye angejenga akijua nyumba zetu, maeneo ya kazi, au nyumba za ibada takatifu juu ya mchanga, au kifusi, au bila ya mipango sahihi na vifaa. Hebu tukubali mwaliko wa Mwokozi kumjia. Hebu tujenge maisha yetu juu ya msingi salama na thabiti.

Nashuhudia kwa unyenyekevu kuwa kwa kukita maisha yetu kwa Yesu Kristo na kwa Upatanisho Wake na kwa kufuata mpango Wake kwa ajili ya furaha yetu kwa makini, ikiwa ni pamoja na maombi ya kila siku, kujifunza maandiko kila siku, na kushiriki sakramenti kila wiki, tutaimarishwa; tutapata ukuaji halisi wa kibinafsi na uongofu wa kudumu, tutakuwa tayari zaidi kufanikiwa katika kuhimili dhoruba na majanga ya maisha; tutapata furaha na shangwe iliyoahidiwa; na tutakuwa na ujasiri kwamba maisha yetu yamejengwa juu ya msingi thabiti---msingi ambao kamwe hautaanguka. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona “1989 Loma Prieta Earthquake,” wikipedia.org/wiki/1989_Loma_Prieta_earthquake.