2010–2019
Sisi ni mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni
Aprili 2013


Sisi ni Mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni

Kama mabinti wa Mungu, kila mmoja wetu ni wakipekee na tofauti katika hali zetu na uzoefu. Na bado sehemu yetu inajalisha---kwa sababu tunafaa.

Kila wiki, wasichana duniani kote hukariri dhamira ya Wasichana. Bila kujali lugha, kila mara ninaposikia maneno haya, “Sisi ni mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni, ambaye anatupenda, na sisi tunampenda,”1 Roho huthibitisha kwa nafsi yangu ya kuwa ni kweli. Na sio tu uthibitisho wa utambulisho wetu---sisi ni nani---lakini pia uthibitisho wa sisi ni wa nani. Sisi ni mabinti wa kiumbe kilichotukuzwa!

Katika kila nchi na kila bara, namekutana na wasichana wajasiri, wakujieleza wazi, waliojawa na mwanga, waliosafishwa kwa kazi ngumu na majaribu, walio na imani safi na rahisi. Wao ni wema. Wao ni waweka maagano, ambao “wanasimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote mlipo.” 2 Wao wanajua wao ni kina nani na kwamba wana wajibu muhimu wa kutenda katika kujenga ufalme wa Mungu.

Nilipokuwa katika chuo, nilikuwa mshiriki wa Wacheza Ngoma ya Jadi wa Kimataifa wa BYU. Majira moja ya joto, kundi letu lilikuwa na fursa ya kipekee ya kuzuru misheni za Ulaya. Ilikuwa majira magumu kwangu kwa sababu miezi michache kabla ya hapo baba yangu alifariki ghafla. Tulipokuwa nchini Scotland, nilihisi kuwa mpweke na nikavunjika moyo hasa. Tulicheza ngoma kanisani, na kisha baada ya maonyesho yetu, tulienda kwa nyumba ya misheni karibu na hapo. Nilipokuwa nikitembea njiani, niliona jiwe limewekwa katika bustani lililopambwa karibu na lango. Juu yake nilisoma maneno haya, “Vyo vyote ulivyo, tenda vyema sehemu yako.” Wakati huo maneno haya yalizama ndani ya moyo wangu, na nikahisi kwamba nguvu za mbinguni zilinifikia na kunipatia ujumbe. Nilijua ninajulikana na Baba yangu wa Mbinguni mwenye upendo. Nilihisi sikuwa peke yangu. Nikasimama pale katika lile bustani kwa machozi machoni mwangu. “Vyo vyote ulivyo, tenda vyema sehemu yako.” Kauli hiyo rahisi iliboresha maono yangu kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinijua mimi na alikuwa na mpango kwa maisha yangu na roho niliyohisi ilinisaidia kuelewa kwamba sehemu yangu ilikuwa muhimu.

Baadaye, nilijifunza kwamba msemo huu uliwahi kumpa motisha nabii David O. McKay alipokuwa akihudumu kama mmisionari kijana huko Scotland. Alikuwa ameuona juu ya jiwe juu ya jengo wakati wa kuvunjika moyo katika maisha na misheni yake, na maneno yaliniinua. Miaka baadaye, wakati jengo lilikuwa likibomolewa, alifanya mipango ya kupata lile jiwe na kuliweka katika bustani kwenye nyumba ya misheni.3

Kama mabinti wa Mungu, kila mmoja wetu ni wa kipekee na tofauti katika hali zetu na uzoefu wetu. Na bado sehemu yetu ni muhimu---kwa sababusisi tunafaa. Michango yetu ya kila siku ya kulea, kufundisha, na kuwajali wengine inaweza hata kuonekana kama kawaida, kupungua, ngumu, na kudhalilisha mara nyingine, na bado, tunapokumbuka mstari ule wa kwanza katika dhamira ya Wasichana---“Sisi ni mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni, anayetupenda”---italeta tofauti yote katika mahusiano yetu na majibu yetu.

Hivi majuzi, mama yangu mwema kabisa mwenye umri wa miaka 92 alifariki. Aliwacha maisha haya mafupi jinsi alivyoishi---kimya kimya. Maisha yake hayakuwa vile alivyopanga. Mumewe, baba yangu, alifariki akiwa na miaka 45, na kumwacha na watoto watatu---mimi na ndugu zangu wawili. Aliishi akiwa mjane kwa miaka 47. Alisaidia familia yetu kwa kufundisha shuleni wakati wa mchana na kufundisha masomo ya piano usiku. Alimtunza baba yake aliyezeeka, babu yangu, aliyeishi mlango uliofuta. Alihakikisha kila mmoja wetu alipata elimu ya chuo. Alisisitiza juu ya hiyo ili tuweza kuwa “wachangiaji.” Na hakuwahi kulalamika. Alitii maagano yake, na kwa sababu ya kutii, aliteremsha nguvu za mbinguni kubariki nyumba yetu na kutuma miujiza. Alitegemea nguvu ya maombi, ukuhani, na ahadi za agano. Alikuwa mwaminifu katika huduma yake kwa Bwana. Kujitolea kwake imara kulituimarisha, sisi watoto wake. Kila mara aliturudia maandiko: “Mimi, Bwana, ninafungwa wakati mnapofanya ninayosema; lakini msipofanya ninayosema, ninyi hamna ahadi.” 4 Na hio ndiyo ilikuwa kauli yake, naye alijua ilikuwa ni kweli. Alielewa maana ya kuwa mweka agano. Hakuwahi kutambuliwa na ulimwengu. Hakutaka hayo. Yeye alielewa alikuwa nani na yeye ni wa nani---binti ya Mungu. Hakika, inaweza kusemwa juu ya mama yetu kwamba alitenda vizuri sehemu yake.

Rais Gordon B. Hinckley aliwahi kusema:

“Kamwe tusisahau uwezo wa wanawake. Ni akina mama ambao huathiri maisha ya watoto wao moja kwa moja. ... Ni akina mama ambao huwalisha na kuwalea katika njia za Bwana. Ushawishi wao ni mkubwa…

“Wao ni waumbaji wa maisha. Wao ni walishaji wa watoto. Wao ni walimu wa wasichana. Wao ni wachumba wetu muhimu. Wao ni wafanyakazi wenzetu katika kujenga ufalme wa Mungu. Ni jinsi gani wajibu wao ulivyo mkubwa, mchango wao ni wa ajabu jinsi gani.” 5

Basi, kina mama na kina baba wanaweza kuingiza vipi ukweli muhimu na wa milele kwa binti kwamba yeye ni binti ya Mungu? Tunaweza kuwasaidia vipi kutoka nje ya dunia na kuingia katika ufalme wa Mungu?

Katika dunia inayodhoofisha kimaadili, wasichana wanahitaji wanawake na wanaume wa “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na mahali popote.” Kamwe hii haijawahi kuwa muhimu zaidi kuliko sasa. Wasichana wanahitaji kina mama na wanasihi wanaodhihirisha umama adilifu. Kina mama, uhusiano wako na binti yako ni wa umuhimu mkubwa, na hivyo pia mfano wako. Jinsi unavyompenda na kumheshimu baba yake, ukuhani wake, na wajibu wake wa kiuungu utajitokeza na labda kuboreshwa katika mitazamo ya binti yako na tabia.

Ni sehemu gani ambayo sisi sote ni lazima “tutende vizuri”? “Tangazo la familia kwa Ulimwengu” ni wazi:

“Kwa uumbaji wa kiuungu, kina baba wanapaswa kuongoza familia zao katika upendo na haki na wana wajibika kutoa mahitaji muhimu ya maisha na ulinzi kwa ajili ya familia zao. Kina mama wanawajibika kimsingi kwa malezi ya watoto wao. Katika majukumu haya matakatifu, baba na mama wanawajibika kusaidiana kama washirika sawa. ...

“Tunaonya kwamba watu wanaokiuka maagano ya usafi,wanaowanyanyasa wachumba wao au watoto, au wanaoshindwa kutimiza majukumu ya familia siku moja watasimama kuwajibika mbele za Mungu.”6

Katika jamii yenye maadili maovu nyakati za Mormoni, alilalamika kuwa wanawake waliibiwa kile ambacho kilipendwa sana na chenye thamani juu ya yote---wema wao na usafi.7

Tena, narudia wito wa kurudi kwa wema. Wema ni nguvu na uwezo wa mabinti wa Mungu. Ulimwengu utakuwaje ikiwa wema---mpangilio wa mawazo na tabia kulingana na viwango vya juu---ikijumuisha usafi wa maadili 8—ungerejeshwa katika jamii yetu kama kitu cha thamani ya juu zaidi? Kama uovu, picha za ngono, na unyanyasaji vingepungua, je, kungekuwa na ndoa chache zilizovunjika, maisha mbaya, na mioyo inayovunjika? Je, vyombo vya habari vinaweza kuadilisha na kuwezeshesha badala ya kupinga na kushusha hadhi ya mabinti wema wa Mungu? Ikiwa wanadamu wote wangeelewa kwa kweli umuhimu wa taarifa “Sisi ni mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni,” jinsi gani wanawake wangeonekana na kutendewa?

Miaka kadhaa iliyopita, wakati Kituo cha Mkutano kilipokuwa kinakaribia kukamilika, niliingia katika jengo hili takatifu kwenye sehemu ya roshani nikivalia kofia ngumu na miwani ya usalama, tayari kuvuta vumbi kwenye zulia ambalo mume wangu alikuwa akisaidia kuweka. Ambapo jukwaa sasa linasimama kulikuwa na gari ya kubeba taka, kumaanisha vumbi katika jengo hili lilikuwa jingi, na wakati lilipotulia, lilitulia kwenye zulia jipya. Na hivyo mimi nikavuta vumbi na nikavuta vumbi na nikavuta vumbi. Baada ya siku tatu, kivuta vumbi kidogo kiliteketea!

Alasiri kabla ya mkutano mkuu wa kwanza katika jengo hili zuri, jipya, mume wangu aliniita. Alikuwa karibu kuweka kipande cha mwisho cha zulia---chini ya jukwa hili la kihistoria.

Yeye aliuliza, “Ni maandiko gani ninafaa kuandika nyuma ya hili zulia?”

Na mimi nikasema, “Mosia 18:9: ‘Simama kama [shahidi] wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na mahali popote.’”

Katika ulimwengu ulio na changamoto sana, hivi ndivyo ninavyoona wasichana na wanawake wa Kanisa wakifanya hili. Wao ni washawishi kwa wema katika dunia. Wao ni wema na vielelezo, werevu na wenye bidii. Wanaleta tofauti kwa sababu wao ni tofauti. Wanatenda vyema katika sehemu zao.

Miaka iliyopita, nilipokuwa nikivuta vumbi kwenye zulia hili---nikijaribu kutenda vizuri sehemu yangu ndogo---sikujua kwamba siku moja nitasimama kwa miguu yangu juu ya zulia hili chini ya jukwaa hili.

Leo kama binti wa Mungu, nasimama kama shahidi kwamba Yeye yu hai. Yesu ndiye Kristo. Yeye ni Mkombozi wetu. Ni kupitia dhabihu Yake ya upatanisho usio na mipaka, ambapo siku moja nitarudi kuishi pamoja Naye---nikiwa nimethibitika, msafi, na kufunganishwa katika familia ya milele. Milele nitamsifu kwa fursa ya kuwa mwanamke, mke na mama. Nashuhudia kuwa tunaongozwa na nabii wa Mungu, Rais Thomas S. Monson, na ninashukuru kwa wanaume wema, ambao uwezo wa ukuhani wao hubariki maisha yangu. Na milele nitashukuru kwa nguvu ninazopokea kupitia kwa nguvu ya kuwezesha ya Mwokozi ninapoendelea kujitahidi “kutenda vizuri sehemu [yangu].” Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Young Women Personal Progress (booklet, 2009), 3.

  2. Mosia 18:9.

  3. Ona Matthew O. Richardson, “‘What E‘er Thou Art, Act Well Thy Part’: John Allan’s Albany Crescent Stone,” Journal of Mormon History, vol. 33 (Fall 2007), 31–61; Francis M. Gibbons, David O. McKay: Apostle to the World, Prophet of God (1986), 45.

  4. Mafundisho na Maagano 82:10.

  5. Gordon B. Hinckley, “Standing Strong and Immovable,” Worldwide Leadership Training Meeting, Jan. 10, 2004, 21.

  6. “The Family: A Proclamation to the World,” Ensign au Liahona, Nov. 2010, 129.

  7. Ona Moroni 9:9.

  8. Ona Young Women Personal Progress, 70.