2010–2019
Kuwa Mnyenyekevu na Mpole katika Moyo
Oktoba 2013


Kuwa Mnyenyekevu na Mpole katika Moyo

Kuwa mpole haimaanishi udhaifu, bali inamaanisha kuwa na tabia njema na ukarimu

Mormoni alifundisha kwamba mwanadamu “hawezi kuwa na imani na tumaini, bila kuwa na upole na unyenyekevu wa moyo.”1 Aliongeza kwamba bila ya kuwa na sifa hizo, “imani na tumaini lake ni bure, kwani hakuna yeyote anayekubaliwambele ya Mungu, isipokuwa yule aliye myenyekevu na mpolekatika moyo.”2

Upole ni sifa ya wale ambao “Wamchao Mungu, wenye haki, wanyenyekevu, wenye kufundishika na wavumilivu katika shida.”3 Wale wenye sifa hizi ni walio tayari kumfuata Yesu Kristo na kiasi chao ni tulivu, pole, vumilivu, na nyenyekevu.

Mtume Paulo alifundisha kwamba upole ni matunda ya Roho.4 Kwa hivyo, inaweza kwa urahisi kupatikana kama sisi “tutaishi katika Roho.”5 Na ili kuishi katika Roho, tabia za maisha yetu ni lazima zilingane na haki mbele za Bwana.

Tunapojichukulia juu yetu jina la Kristo, inatarajiwa kwamba tunaiga sifa Zake na kubadili tabia zetu ili zilingane na za kwake kila siku. Mwokozi, aliwaeleza mitume Wake, akisema, “Kuweni wakamilifu, kama vile Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”6 Kama “tutakuja kwa Kristo, na kujikana [wenyewe] kutoka katika uovu, na tukaamua kumpenda Mungu,” ndipo kupitia neema ya Kristo siku itakuja ambayo tunaweza kuwa wakamilifu katika Yeye.7

“Sifa kama za Kristo ni zawadi kutoka kwa Mungu. [Sifa hizi] zinakuja kama [sisi] tunatumia wakala [wetu] kwa wema. …Tukiwa na hamu ya kumpendeza Mungu, tunatakiwa kujua udhaifu wetu na kuwa tayari na tutamani kuboreka.”8

Upole ni muhimu kwetu ili kuwa kama Kristo. Bila hiyo hatuwezi kuendeleza fadhila zingine muhimu. Kuwa mpole haimaanishi udhaifu, bali inamaanisha kuwa na tabia njema na wema, kuonyesha nguvu, utulivu, uthabiti wa kujiamini na kujizuia.

Upole ulikuwa ni mojawapo ya sifa kubwa katika maisha ya Mwokozi. Yeye, Mwenyewe, aliwafundisha wafuasi Wake, “Jifunzeni toka kwangu; kwani Mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.”9

Tumebarikiwa kuzaliwa na mbegu ya upole ndani ya mioyo yetu.Tunatakiwa kuelewa kwamba si rahisi kukua na kukuza hio mbegu kwa kufumba na kufumbua bali kwa kupitia mchakato wa wakati. Kristo anatuuliza “tuuchukue msalaba [wetu] kila siku,”10 kumaanisha kwamba lazima iwe lengo na hamu ya siku zote.

Rais Lorenzo Snow, nabii wa tano wa kipindi hiki chetu alifundisha, “Ni wajibu wetu kujaribu kuwa wakamilifu, … kujiboresha kila siku, na kutathmini kile tulichofanya wiki jana, na kutenda vyema wiki hii; kutenda mambo mema leo zaidi ya tulivyotenda jana.”11 Hivyo, hatua ya kwanza ya kuwa mpole ni kujitahidi siku hadi siku. Kila siku tunahitaji kuwa bora zaidi kuliko tulivyokuwa siku iliyopita kadiri tunavyosonga mbele.

Rais Snow aliongeza:

“Tuna upumbavu na na upungufu wetu kidogo; tunapaswa kuyashinda haraka iwezekanavyo, na …. Tunapaswa [kuweka ] hisia hizi katika mioyo ya watoto wetu … ili waweze kujifunza kuwa na tabia njema mbele Zake kwa mazingira yoyote yale.

“Kama mume anaweza kuishi na mke wake siku nzima bila ya kugombana au bila ya kumtendea mtu maovu au bila ya kumsononesha Roho wa Mungu… ; yeye atakuwa mkamilifu kiasi hicho. Basi acha ajaribu kuendelea hivyo katika siku inayofuata. Lakini iwapo atashindwa kufanya hivi siku inayofuata, hiyo si sababu tosha ya kutofanikiwa kwake katika siku ya tatu.”12

Baada ya kutambua kujitolea na kuvumilia kwetu, Bwana atatupa kile ambacho hatuwezi kukipata kutokana na mapungufu na udhaifu wetu wa kibinadamu.

Hatua nyingine muhimu ya kuwa mpole ni kujifunza jinsi ya kudhibiti hasira zetu. Kwa sababu mwanadamu asili hukaa ndani ya kila mmoja wetu na kwa sababu tunaishi katika ulimwengu uliojaa shinikizo, kudhibiti hasira zetu kunaweza kuwa mojawapo wa changamoto katika maisha yetu. Fikiria kwa muda jinsi ulivyofanya wakati mtu alipofanya kinyume na matakwa yako, Na vipi kama watu wanatofautiana na mawazo yako, hata kama una uhakika yanawakilisha suluhisho halisi la tatizo? Jibu lako ni nini, wakati mtu anapokuchukiza, kukosoa juhudi lako, au hatendi haki eti kwa sababu ana hali ya kununa? Kwa wakati huu na katika hali ngumu lazima tujifunze kudhibiti hasira zetu na kueleza hisia zetu kwa uvumilivu na ushawishi wa upole. Hii ni muhimu sana nyumbani kwetu na katika mahusiano yetu na wenzi wetu wa milele. Kwa kipindi cha miaka 31 cha kuona na mke wangu mpendwa, mara nyingi amekuwa akinipa “makumbusho” kwa upole ya changamoto kali za maisha ambazo tumekumbana nazo.

Miongoni mwa maelekezo yanayopatikana katika Waraka wa Pili kwa Timotheo, Mtume Paulo alisema:

“Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

“Akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

“Wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego.”13

Kwa kudhibiti matendo yetu, kwa kuwa watulivu na wapole, na kuepuka mabishano, tutaanza kufaulu kwa karama ya upole. Raisi Henry  B. Eyring aliwahi kusema, “Kama tuna imani tunaweza kudhibiti hasira na kuacha kiburi, Roho Mtakatifu anatoa idhini, na ahadi takatifu na maagano yanatimia.”14

Hatua nyingine ya kupata upole ni kuwa mnyenyekevu. Bwana alimwagiza Thomas  B. Marsh kupitia Joseph Smith, akisema, “Jinyenyekeze; na Bwana Mungu wako atakuongoza kwa mkono, na kukupa jibu la sala zako.”15

Ninaamini, ndugu na kina dada kwamba, ni wale wanyenyekevu tu ndio wanaoweza kutambua na kuelewa majibu ya Bwana kwa sala zao. Wanyenyekevu hufundishika, wakijua jinsi wanavyomtegemea Mungu na kutamani kuwa chini ya mapenzi Yake. Wanyenyekevu ni wapole na wana uwezo wa kuwashawishi wengine kuwa vivyo hivyo. Ahadi ya Mungu kwa wanyenyekevu ni kwamba atawaongoza kwa mkono. Kwa hakika ninaamini kwamba tutaepuka kupotea njia na huzuni katika maisha yetu kama tutatembea na Bwana bega kwa bega.

Mojawapo wa mfano mzuri wa kisasa wa upole ule ninajua ni ule wa Moses Mahlangu wa uongofu wake ulianzia mwaka 1964 alipopokea nakala ya Kitabu cha Mormoni. Alikuwa na shauku wakati akisoma kitabu hiki, lakini ilikuwa hadi mwanzoni mwa miaka ya 70 alipoona bango la Kanisa la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Johannesburg, Afrika kusini, wakati akitembea mtaani.Ndugu Mahlangu alivutiwa na kuingia ndani ili kujifunza kuhusu Kanisa. Aliambiwa kwamba asingeweza kuhudhuria ibada wala kubatizwa kwa sababu sheria za nchi haikuruhusu kwa wakati huo.

Kaka Mahlangu aliukubali uamuzi ule kwa upole, unyenyekevu na bila ubishi, lakini aliendelea kuwa na hamu ya kujifunza kuhusu Kanisa. Yeye aliwaomba viongozi wa Kanisa kama wangeweza kuliacha dirisha moja la kanisa wazi siku za Jumapili ili aweze kukaa chini nje na kusikiliza ibada. Kwa miaka mingi, Familia ya Mahlangu na marafiki zake walihudhuria ibada mara nyingi kwa “kupitia dirishani.” Siku moja mwaka wa 1980 waliambiwa kwamba wanaweza kuhudhuria ibada ndani na pia kubatizwa. Ilikuwa siku tukufu kiasi gani kwa Ndugu Mahlangu.

Baadaye, Kanisa lilianzisha tawi katika kitongoji chake huko Soweto. Hii iliwezekana kwa sababu tu  ya moyo wa kujituma, kujiamini, na imani ya watu kama ya Ndugu Mahlangu ambaye aliendelea kuwa mwaminifu kwa miaka mingi katika hali ngumu.

Mmoja wa marafiki wa Ndugu Mahlangu, aliyejiunga na Kanisa wakati mmoja, alinielezea habari hii nilipotembelea kigingi cha Soweto. Mwishoni mwa maongezi yetu, alinikumbatia. Wakati ule, ndugu na kina dada, nilijisikia kama nimezungukwa na mikono ya upendo wa Bwana. Upole ulijionyesha machoni mwa Ndugu huyu mwema. Akijawa na moyo wa wema na shukrani nyingi, aliniomba kama ningeweza kumwambia Rais Thomas S. Monson jinsi alivyo na shukrani na alivyobarikiwa yeye na na wengine kwa kuwa na injili ya kweli katika maisha yao. Mfano wa upole wa Ndugu Mahlangu na rafiki yake kwa hakika ulishawishi maisha mazuri kwa wengi --- hususani yangu.

Akina ndugu na dada, ninaamini Yesu Kristo ni mfano mzuri wa unyenyekevu. Hata katika siku za mwisho za uhai Wake, akiwa ametuhumiwa na kuhukumiwa pasipo haki, kwa maumivu aliubeba msalaba Wake hadi Golgotha, akidhiakiwa na kulaaniwa na maadui Zake, akiwa ameachwa pekee na watu waliomjua na kushuhudia miujiza Yake, alisulubiwa msalabani.

Hata baada ya mateso makali sana ya kimwili, Bwana alimgeukia Baba Yake na kunena kutoka kina cha moyo Wake wa upole na unyenyekevu. “Baba, wasamehe; kwani hawajui walitendalo.”16 Kristo alikumbana na mateso makali sana ya kimwili na kiroho, akitupatia sisi nafasi ya kubadilisha silka yetu ya kiroho na kuwa wapole kama yeye alivyo.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu. Ninashuhudia kwenu kwamba, kwa sababu ya upendo Wake, inawezekana kubadilika. Inawezekana kuacha udhaifu wetu. Inawezekana kukataa ushawishi wa uovu katika maisha yetu, kudhibiti hasira zetu, kuwa wapole, na kukuza sifa kama za Mwokozi wetu. Yeye alituonyesha njia. Yeye alituonyesha mfano mzuri na kutuamuru kila mmoja wetu kuwa kama Yeye alivyo. Mwaliko Wake kwetu ni wa kumfuata Yeye, kufuata mfano Wake, na kuwa kama Yeye. Kwa kweli hizi, ninatoa ushuhuda katika jina Lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.