2010–2019
Dai baraka za Maagano yako
Oktoba 2013


Dai baraka za Maagano yako

Tunapoweka upya na kuyaheshimu maagano yetu, mizigo yetu inaweza kuwa miepesi, na tunaweza kuendelea kutakaswa na kuimarishwa

Akina dada, ni furaha iliyoje kuwa nanyi tena.

Hivi karibuni nilikutana na mwanamke aliyekuwa akijiandaa kubatizwa. Jumapili hiyo aliwasili kanisani akiwa ametembea kilometa  3 kwenye matope. Mara moja akaenda bafuni, akavua nguo zake zenye matope, akaoga, na kuvaa nguo safi za Jumapili. Kwenye kipindi cha wanawake alielezea juu ya uongofu wake. Niliguswa na matamanio yake ya kutaka kuwa msafi kupitia njia ya toba na dhabihu ya upatanisho wa Mwokozi na utashi wake wa kuyaacha maisha ya kale ili kuweka maagano tukufu na Baba yetu wa Mbinguni. Alikuwa ameachana na mchumba wake, alikuwa akijaribu kushinda uraibu, kutii neno la Hekima, kuacha kufanya kazi Jumapili ili aende kanisani, na aliwakosa marafiki zake baada ya kutangaza nia yake ya kubatizwa. Alikuwa na furaha ya kuziacha dhambi zake, ili aweze kuoshwa kuwa msafi na kuwa na upendo wa ukombozi wa Mwokozi. Asubuhi ile nilihamasishwa na nia yake ya kuwa msafi kimwili na kiroho.

Tunajua kuwa wengi wenu mmefanya jambo kama hili pale mlipohisi ushahidi wa Roho Mtakatifu na mkataka kutubu, kubatizwa, na kuwa wasafi. Inawezekana hapakuwa na muda mwingine tuliohisi upendo mtukufu wa Mwokozi ukiwa mwingi kama ule wakati ambao tunatubu na kuhisi mikono yake ya upendo ikitukumbatia na kutuhakikishia upendo Wake na kukubaliwa.

Jumapili chache zilizopita nikiwa nasikiliza sala ya sakramenti, niliguswa kwa jinsi kuhani alivyokuwa akitamka kila neno kwa hisia nzuri. Baadaye nikamwita yule kuhani na kumshukuru kwa kuifanya sakramenti iwe ya kiroho kwangu na kwa washiriki wote. Hakuwepo nyumbani, lakini mama yake alijibu, “Oh, atakuwa nafuraha sana kusikia ulipiga simu! Hii ilikuwa ni siku yake ya kwanza kubariki sakramenti, na tulikuwa tunaandaa pamoja, tukizungumzia umuhimu wa sakramenti na kwa haki tukikumbuka maagano yetu ya ubatizo ya Bwana. Ninampenda sana mama huyu mpendwa kwa kumfundisha mwanawe kuhusu nguvu za maagano ya ubatizo na nafasi aliyo kuwa nayo ya kuwasaidia wanachama wa ile kata kuhisi ule uwezo.

Mama mwingine ninayemfahamu alikuwa anakaa kanisani peke yake kwa miaka mingi pamoja na watoto wake wadogo wanne. Akiwa nadra sana kuweza kuwa makini juu ya Mwokozi wakati wa sakramenti, aliandaa mpango. Sasa anajaribu kuwa na muda kila Jumamosi akiitafakari wiki yake na akitafakari kuhusu maagano yake na kile anachotaka kutubu. “Ndipo” akasema, “bila kujali uzoefu nilionao kuhusu watoto wangu siku ya Jumapili, nimejiandaa kushiriki sakramenti, kujikumbusha maagano yangu, na kujisikia utakazo wa nguvu za upatanisho.

Kwa nini Mwokozi anaweka umuhimu katika sakramenti, akina dada wapendwa? Huku kuyafanya upya maagano yetu ya ubatizo kila wiki kuna umuhimu gani katika maisha yetu? Tunautambua uwezo wa Mwokozi wa utakaso wetu kamili wa kila wiki pale tunapokuwa wasafi wa kushiriki sakramenti? Raisi Boyd  K. Packer alishuhudia, “Hiyo ni ahadi ya injili ya Yesu Kristo na Upatanisho: … ambapo mwisho wa maisha yetu tunaweza kupitia kwenye pazia tukiwa tumetubu dhambi zetu na tukiwa tumesafishwa kwa njia ya damu ya Kristo.”1

Urais wetu unafuraha kuona dada zetu na familia zao wanafanya maagano na kuyaweka, lakini mioyo yetu inahuzuni kwa ninyi mnaokumbana na shida katika maisha yenu kwa sababu ya maagano yaliyovunjwa na wale muwapendao. Nabii Jacob, kaka mdogo wa Nefi, aliamuriwa na Bwana kuongea na ndugu zake kuhusu wanawake na watoto wema wa siku hizi. Ninashuhudia kwamba maneno yake yametunzwa hususani kwa ajili ya siku yetu. Anaongea nasi kama vile Bwana mwenyewe alikuwa anaongea. Jacob alikuwa na “wasiwasi … mwingi” wakati akitoa ushuhuda kwa waume na akina baba.

“Ninahuzunika kwamba yanilazimu kutumia sauti ya ujasiri … mbele ya wake zenu na watoto wenu, wengi wao wakiwa na hisia changa na wasafi na maridadi. …

“… vilio vya mioyo yao kwa sababu yenu vinamfikia Mungu. … mioyo mingi ilikufa, ikiwa imedungwa na vidonda vikubwa.”2

Kwa wale waweka maagano wanawake na watoto wa siku hizi, Jacob aliahidi:

“Mtegemeeni Mungu kwa mawazo yenu yote, na mmuombe, kwa imani kuu, na atawafariji katika mateso yenu, …

“… inueni vichwa vyenu na kupokea neno la kupendeza la Mungu, na kusherekea upendo wake.”3

Kina dada, mimi nashuhudia juu ya uwezo na nguvu za maombi pale tunapoonyesha machungu na hamu yetu kwa Baba yetu wa Mbinguni na majibu ambayo tunayapokea pale tunaposoma maandiko matakatifu na maneno ya manabii waliohai.

Karibu miaka mitatu iliyopita moto uliteketeza ndani kwenye nyumba inayopendwa, ya tabanakulo ya kihistoria ya Provo Utah. Hasara yake ilikuwa kubwa kwa jamii na washiriki wa Kanisa. Wengi walishangaa, “Kwa nini Bwana aliacha haya yatokee? Hakika angeweza kuzuia moto au angamizo lake.”

Miezi kumi baadaye, wakati wa mkutano mkuu wa Oktoba 2011, kulikuwa na kelele wakati Rais Thomas S. Monson alipotangaza kwamba tabanakulo lililoteketea linakuwa hekalu takatifu—nyumba takatifu ya Bwana! Ghafla tungeweza kuona kile ambacho Bwana amekijua mara nyingi! Hakuleta moto, lakini aliruhusu moto uangamize mle ndani. Aliliona Tabanakulo kama hekalu lililopendeza---nyumba ya kudumu kwa ajili ya kuweka maagano matakatifu ya milele.4

Wapendwa dada zangu, Bwana anatuacha tujaribiwe, wakati mwingine kwa kiwango cha juu. Tumeona maisha ya tuwapendao---na hata pengine yetu binafsi yakichomwa moto na tunakuwa tukijiuliza ni kwa nini Baba wa Mbinguni atupendaye na kutujali anaweza kuruhusu vitu kama hivi vitokee. Lakini hatuachi kwenye jivu, Anasimama na mikono iliyowazi, huku akitamani kutukaribisha Kwake. Anayajenga maisha yetu kwenye mahekalu mazuri ambamo Roho Wake anaweza kukaa milele.

Katika Mafundisho na Maagano 58:3–4, Bwana anatuambia sisi:

“Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu juu ya mambo yale ambayo yatakuja hapo baadaye, na utukufu utakaofuata baada ya taabu kubwa.

“Kwani baada ya taabu kubwa huja baraka. Kwa hiyo siku yaja ambayo ninyi mtavikwa utukufu mkubwa.”

Akina dada, ninashuhudia kwamba Bwana ana mpango katika maisha yetu. Hakuna kinachotokea kwa mshtuko au mshangao Kwake. Yeye anajua yote na anapenda sana. Anatamani kutusaidia, kutufariji, na kuyapunguza maumivu yetu pale tunapotegemea nguvu za Upatanisho na kuyatii maagano yetu. Ninajua hili. Majaribu na mateso tunayokumbana nayo yaweza kuwa ndiyo mwongozo wetu wa kumjia Yeye na kushikilia maagano yetu ili tuweze kurudi kwenye uwepo wake na kupokea yote ambayo Baba anayo.

Mwaka uliopita nimehitaji na kutaka kuhisi upendo wa Bwana zaidi, kupata ufunuo wa kibinafsi, kuelewa vyema maagano yangu ya hekaluni, na kuifanya mizigo yangu kuwa miepesi. Kama nilivyoomba hususani kwa ajili ya hizi baraka, nimehisi mwongozo wa Roho ukiniongoza kwenda hekaluni na kusikiliza kwa ukaribu kila neno la baraka lililotolewa kwangu. Ninashuhudia kwamba nimesikiliza kwa makini na kujaribu kuitumia imani yangu, kwani Bwana amekuwa mwingi wa huruma kwangu na amenisaidia kuifanya mizigo yangu kuwa miepesi. Amenisaidia kuhisi amani kuhusu maombi ambayo bado hayajajibiwa. Tunamwamini Bwana katika kuziweka ahadi Zake pale tunapotii maagano yetu na kuonyesha imani yetu. 5 Njooni hekaluni, akina dada wapendwa, na kudai baraka zenu!

Pia ningependa kugusia njia nyingine inayoweza kutupatia imani na kujiamini. Sisi wakati mwingine, kama wanawake, tuna tabia ya kujihukumu wenyewe. Kipindi cha wakati huu tunahitaji Roho na kuuliza,“Hivi ndivyo Bwana anataka mimi nijifikirie au shetani anajaribu kuniangusha? Kumbuka asili ya Baba yetu wa Mbinguni, upendo wake ni kamili na usio na mwisho.6 Yeye anataka kutuimarisha, na sio kutukatisha tamaa.

Kama washiriki wa Kanisa, wakati mwingine tunaweza kuhisi kwamba tunahitaji kuwa sehemu ya familia ya Watakatifu wa Siku za Mwisho halisi ili kukubaliwa na Bwana. Mara nyingi tunajisikia kama siyo wakamilifu kama tunahisi kuwa si-familia ya WSM. Akina dada wapendwa, hatimaye, kile kitakachokuwa cha maana kwa Baba aliye Mbinguni itakuwa ni jinsi tulivyoweza kuyaweka maagano yetu na jinsi tulivyojaribu kufuata mfano wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Kwa sababu ya dhabihu ya upatanisho Wake, tunaweza kuoshwa kila wiki pale tunapopokea sakramenti Yake. Tunapoweka upya na kuyaheshimu maagano yetu, mizigo yetu inaweza kuwa miepesi, na tunaweza kuendelea kutakaswa na kuimarishwa ili hapo mwisho wa maisha yetu tuweze kuhesabiwa wema ili tupate kuinuliwa, na uzima wa milele. Ninashuhudia mambo haya katika jina la Yesu Kristo, amina.