2010–2019
Unalala Wakati wote wa Urejesho?
Aprili 2014


Unalala Wakati wote wa Urejesho?

Kuna mambo mengi hatarini kwetu binafsi, kama familia, na kama Kanisa la Kristo kutoa tu nusu ya juhudi zetu katika kazi hii tukufu.

Karibu miaka 200 iliyopita, habari fupi ya Mmarekani “Rip Van Winkle” ikawa maarufu mara moja. Mchezaji mkuu, Rip, ni mtu asiye na makuu ambaye alikuwa hodari wa kuepuka vitu viwili: kazi na mke wake.

Siku moja, akiwa akirandaranda mlimani na mbwa wake, aligundua kundi la watu waliovaa kiajabu wakinywa na kucheza michezo. Baada ya kukubali baadhi ya pombe yao, Rip akaanza kuchoka na kufumba macho yake kwa muda. Alipofumbua tena macho yake, alishangaa kuona mbwa wake ametoweka, bunduki yake imeshika kutu, na sasa ana ndevu ndefu.

Rip anaanza safari ya kurudi kijijini kwake huku akigundua kwamba kila kitu kimebadilika. Mke wake, rafiki zake wameondoka, na sanamu ya Mfalme George III katika klabu ya pombe imebadilishwa na kuwekwa ya mtu asiyemjua—ya Jemadari George Washington.

Rip van Winkle alikuwa amelala kwa miaka 20! Na, katika mchakato huo, alikuwa amekosa moja kati ya vipindi muhimu katika historia ya nchi yake—alikuwa amelala katika kipindi cha mapinduzi ya Marekani.

Mnamo Mei 1966, Dr. Martin Luther King Jr. alitumia habari hii kama ilivyoainishwa kwenye hotuba yake ya “Usilale Wakati wa Mapinduzi.”1

Hivi leo, ningependa kuchukua mada hiyo hiyo na kuuliza swali kwa wote ambao wana ukuhani wa Mungu: Je! Tunalala wakati wote wa Urejesho?

Tunaishi katika Kipindi cha Urejesho.

Wakati mwingine tunafikiri Urejesho wa injili kama kitu kilichokamilika, tayari upo nyuma yetu—Joseph Smith alitafsiri Kitabu cha Mormoni, alipokea funguo za ukuhani, Kanisa likaanzishwa. Lakini ukweli ni, Urejesho ni tendo la kuendelea; tunaishi katika kipindi hicho sasa. Unajumuisha “yale yote ambayo Mungu ameyafunua, yale yote anayoyafunua sasa,” na vitu vingi vizuri na Muhimu” ambavyo “Yeye atavifunua”2. Ndugu, maendeleo yote mazuri ya leo ni sehemu ya maandalizi ambayo yalinenwa hapo kale kwamba yataishia katika Ujio wa Pili wa Mwokozi, Yesu Kristo.

Hiki ni mojawapo wa vipindi muhimu vya historia ya ulimwengu! Manabii wa kale walipenda kuiona siku yetu.

Wakati maisha haya yatakapokwisha, ni uzoefu gani ambao tunaweza kuuelezea juu ya mchango wetu katika kipindi hiki kigumu cha maisha yetu na kuiendeleza kazi ya Bwana? Tutaweza kusema kwamba tulikunja mikono ya mashati yetu na kufanya kazi kwa moyo wetu wote, nguvu, mawazo na uwezo wetu wote? Au tunaweza kukiri kwamba majukumu yetu yalikuwa kama ya yule mtazamaji?

Ninatumaini kuna sababu nyingi za kwa nini hatutaki kujihusisha katika kuujenga ufalme wa Mungu. Acheni nitaje sababu tatu kuu. Ninapofanya hivi, ninawaalikeni kutafakari kama kuna lolote linalowahusu. Kama unaona nafasi ya kujirudi, ninawaombeni kufikiria kile kinachoweza kufanyika ili mbadilike kuwa bora.

Ubinafsi

Kwanza, ubinafsi.

Wale walio wabinafsi wanataka vitu kwa faida yao wenyewe na starehe juu ya vitu vyote. Swali la msingi kwa mtu mbinafsi ni “Mimi nafaidika nini?

Ndugu, nina hakika kuwa mnaweza kuona tabia hii dhahiri inapingana na roho inayotakiwa kujenga ufalme wa Mungu

Tunapohitaji kujiridhisha badala ya kuwatumikia wengine, kipaumbele chetu kinakuwa kujipatia umaarufu na sifa.

Vizazi vilivyopita vilikuwa na matatizo yake na aina tofauti ya majivuno, lakini leo nafikiri tunawapatia ushindani mkali. Je! Ni sadfa kuwa Kamusi ya Oxford hivi majuzi ilitangaza “selfie” kama ni neno la mwaka? 3

Kwa asili, sote tuna tamaa ya kujulikana, na hakuna ubaya kujipumzisha na kujifurahisha wenyewe. Lakini wakati tunapojitafutia “faida na sifa za ulimwengu” 4 inakuwa ni sehemu muhimu ya hamasisho letu, tunakosa uzoefu wa ukombozi na furaha ambayo huja wakati tunajitolea wenyewe kwa ukarimu katika kazi ya Bwana.

Tiba ni nini?

Jibu, kama ilivyo kila mara, lipo katika maneno ya Kristo.

“Yeyote ajaye kwangu, mwache ajikane mwenyewe, na aubebe msalaba wake, na anifuate.

“Kwani yeyote atakayeokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na injili yangu, naye ataokolewa.”5

Wale wanaoyatoa maisha yao kwa moyo wao wote kwa Mwokozi wetu na kumtumikia Mungu na watu wenzao hupata utajiri na ukamilifu wa maisha ambao mtu mwenye ubinafsi hawezi kupata. Wasio na ubinafsi hujitolea wenyewe. Hizi zinaweza kuwa zawadi ndogo za hisani ambazo zinachochea mazuri: tabasamu, kushikana mkono, kukumbatia, kusikilizana, neno la kutia moyo, au mtazamo wa kujali. Tabia zote hizi za wema zinaweza kubadili moyo na maisha. Tunapochukua nafasi ya muda usio na kikomo wa kuwapenda na kuwatumikia wenzetu, wakiwemo wenza wetu na familia zetu, uwezo wetu wa kumpenda Mungu na kuwatumikia wengine utaongezeka pakubwa.

Wale wanaowatumikia wengine hawatalala wakati wa Urejesho.

Uraibu

Kitu kingine ambacho kinaweza kutufanya sisi tulale katika huu msimu muhimu wa ulimwengu ni uraibu

Uraibu mara nyingi huanza kidogo kidogo. Uraibu ni kamba nyembamba za matendo ambayo yanayorudiwa ambazo hujisuka zenyewe kuwa kamba nene za tabia. Tabia hasi huweza kuleta uraibu unaotawala.

Minyororo hii yenye kufunga ya uriabu inaweza kuwa ya aina mbalimbali, kama vile picha za ngono, pombe, uzinzi, madawa, tumbaku, kamari, chakula, kazi, tovuti, au ukweli taswira. Shetani, adui yetu, ana vifaa vingi anavyotumia kutulaghai sisi ili tusiweze kukamilisha kazi yetu katika ufalme wa Bwana.

Inamsikitisha Baba yetu wa Mbinguni kuona jinsi kwa hiari baadhi ya wanawe wateule wakinyoosha mikono yao kupokea minyororo ya tabia angamizi.

Ndugu, tuna ukuhani wa milele wa Mwenyezi Mungu. Sisi kwa kweli ni wana wa Aliye Juu na tumetawazwa kwa mambo makubwa. Tumeandaliwa kulingana na uwezo wetu. Hatukuumbwa ili tufanywe mateka wa dunia, kufungwa na vizuizi vya kujitakia wenyewe.

Tiba ni nini?

Kitu cha kwanza tunachotakiwa kuelewa ni kwamba uraibu ni rahisi kuukinga kuliko kuutibu. Katika maneno ya Bwana, “Msiache mambo haya yaingie moyoni mwenu.”6

Miaka kadhaa iliyopita, Rais Thomas S. Monson nami tulipata nafasi kutembelea Air force One —ndege ya kifahari inayombeba Rais wa Marekani. Kulikuwa na ulinzi mkali, nami nikatabasamu kidogo wakati Askari Maalum walipomwendea nabii wetu mpendwa kabla hajapanda.

Kisha rubani mkuu aliniomba mimi nikae kwenye kiti cha kapteni. Ulikuwa ni wakati mzuri sana kukaa tena katika kiti cha mashine irukayo kama ile niliyowahi kuirusha kwa miaka mingi. Kumbukumbu za kurusha ndege kuvuka bahari na mabara zilijaa moyoni na akilini mwangu. Nilifikiria kupaa na kushuka kunakosisimua katika viwanja vya ndege duniani kote.

Hata bila ya kufikiria, niliweka mikono yangu kwenye usukani wa 747. Ndipo hapo, sauti ya upendo isiyo na shaka ikasikika nyuma yangu—sauti ya Thomas S. Monson.

“Dieter,” alisema, “wala usifikirie hivyo.”

Mimi sikiri lolote, lakini huenda ikawa Rais Monson aliyabaini mawazo yangu.

Tunapojaribiwa kufanya mambo tusiyotakiwa, naomba tusikilize onyo lenye upendo toka kwa familia, marafiki, nabii wetu mpendwa, na Mwokozi daima.

Njia nzuri ya kujilinda na uraibu ni kutouanza kabisa.

Vipi kwa wale wanaojikuta wenyewe katika mtego wa uraibu?

Tafadhali fahamu, kwanza kabisa, kuna tumaini. Tafuta msaada toka kwa wale uwapendao, viongozi wa Kanisa, na washauri waliopata mafunzo. Kanisa linatoa huduma ya waathiriwa wa matatizo kupitia viongozi wa Kanisa, tovuti,7 na katika maeneo mengine, kupitia LDS Family Services.

Kila mara kumbuka, kwa msaada wa Mwokozi, unaweza kuepukana na uraibu. Inaweza kuwa safari ndefu na ngumu, lakini hatuwezi kushindwa kwa ajili yenu. Yesu Kristo aliteseka kwa Upatanisho ili kukusaidia wewe ubadilike, kukuokoa kutoka kwenye kifungo cha dhambi.

Kitu muhimu sana ni kuendelea kujaribu—wakati mwingine inachukua kujaribu mara nyingi kabla ya watu kufanikiwa. Hivyo usikate tamaa. Uweke moyo wako karibu na Bwana, na Yeye atakupa nguvu ya ukombozi. Atakufanya uwe huru.

Ndugu zangu wapendwa, nyakati zote kaeni mbali na tabia ambazo zinaweza kuwaongoza katika uraibu. Wale wafanyao hivyo wataweza kutoa mioyo, mawazo, akili na nguvu zao katika huduma ya Mungu.

Hawatalala wakati wa Urejesho.

Vipaumbele vyenye Ushindani

Kizuizi cha tatu ambacho kinatuzuia katika kujihusisha kikamilifu katika kazi hii ni vipaumbele vyenye ushindani tunavyokumbana navyo. Baadhi yetu tunashughulika hata tunahisi kama tunavuta mkokoteni unaopaswa wanyama kumi na wawili wa kazi hii—kila mnyama akijaribu kwenda njia tofauti. Nguvu nyingi zinahitajika, lakini mkokoteni hauendi kokote.

Mara nyingi tunafanya kazi nyingi katika mazoea yetu, michezo, ujuzi wa kielimu, na kijamii au maswala ya kisiasa. Vitu hivi vyote vinaweza kuwa vizuri na vyenye kuheshimika, lakini je, vinatuachia muda na nguvu kwa ajili ya vipaumbele vya juu zaidi?

Tiba ni nini?

Kwa mara ingine, inatoka katika maneno ya Mwokozi:

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

“Hii ndiyo amri ya kwanza na iliyo kuu.

“Na ya pili inafanana na hiyo, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”8

Kila kitu katika maisha lazima kiwe ni cha pili katika hivi vipaumbele vikuu viwili.

Hata katika utumishi wa Kanisa, ni rahisi kutumia muda mwingi kufanya mambo bila ya moyo au tabia ya ufuasi.

Ndugu, sisi kama makuhani tumejitoa kuwa watu wenye kumpenda Mungu na jirani zetu na ambao tuko radhi kuonyesha upendo huo kwa maneno na vitendo. Hicho ni kiini cha kuonyesha sisi ni kina nani kama wafuasi wa Yesu Kristo.

Wale wanaoishi kwa kufuata kanuni hizi hawatalala wakati wa Urejesho.

Wito wa Kuamka

Mtume Paulo aliandika, “Amkeni enyi mlalao, na simameni toka kwenye umauti, na Kristo atawapa mwanga.”9

Wapendwa rafiki zangu, mjue kwamba ninyi ni wana wa mwanga.

Msiuruhusu ubinafsi! Msiruhusu tabia ambazo zinaweza kuwaongoza kwenye uraibu! Msiruhusu vipaumbele vyenye ushindani kuwaongoza ninyi katika hali ya kutojali au kujiondoa toka kwenye ufuasi wenye baraka na kuziacha kazi ya ukuhani!

Kuna mambo mengi hatarini kwetu binafsi, kama familia, na kama Kanisa la Kristo kutoa tu nusu ya juhudi zetu katika kazi hii tukufu.

Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo siyo juhudi za mara moja kwa wiki au mara moja kwa siku. Ni juhudi za muda wote.

Ahadi ya Bwana kwa makuhani Wake wa kweli ni kubwa sana kuielewa.

Wale walio wema katika Ukuhani wa Haruni na Melkidezeki na kuipanua miito yao “wanatakaswa na Roho katika kuifanya upya miili yao.” Kwa hiyo, vyote alivyonavyo Baba vitatolewa kwao.10

Ninashuhudia kwamba nguvu za kutakasa za Upatanisho wa Yesu Kristo na nguvu za Roho Mtakatifu zinaweza kuponya na kumwokoa binadamu. Ni nafasi yetu, kazi yetu takatifu, na furaha kuitikia wito wa Mwokozi, wa kumfuata Yeye kwa upendo na moyo wenye lengo. Na “Jifungueni minyororo ambayo imewafunga, na mtoke fumboni, na muinuke kutoka mavumbini.”11

Na tuamke na tusichoke kutenda mema, kwani sisi tunaweka msingi wa kazi kubwa,”12 hata kuandaa ujio wa Mwokozi. Ndugu, tunapoongeza mwanga wa mfano wetu kama mashahidi wa uzuri na nguvu za ukweli uliorejeshwa, hatutalala wakati wa Urejesho. Juu ya haya ninashuhudia na kuwaachieni baraka zangu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.