2010–2019
Kristo aliye Mkombozi
Aprili 2014


Kristo aliye Mkombozi

Dhabihu [ya Mkombozi] ilibariki kila mtu, kutoka kwa Adamu, binadamu wa kwanza, hadi binadamu wa mwisho.

Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alizaliwa na kufa katika hali za kipekee. Aliishi na kukulia katika hali nyenyekevu, bila vitu vya kidunia. Alisema kujihusu Mwenyewe, “Mbweha wana mapango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake” (Luka 9:58).

Hakuwahi kupokea heshima, usaidizi, utambuzi, wala kutendewa kwa mapendeleo kutoka kwa viongozi wa kisiasa wa dunia, wala kutoka kwa viongozi wa dini wa siku Zake. Wala hakuketi mbele katika masinagogi.

Mahubiri yake yalikuwa rahisi, na hata ingawa watu wengi walimfuata, utumishi wake daima ulijumuisha kubariki watu mmoja baada ya mwingine. Alitenda miujiza mingi sana miongoni mwa wale waliomkubali kama aliyetumwa na Mungu.

Aliwapa Mitume Wake mamlaka na uwezo kutenda miujiza “na kazi kubwa” kuliko zile alizotenda (Yohana 14:12), lakini hakuwahi kunaibisha kwao fursa ya kusamehe dhambi. Maadui zake walikasirishwa walipomsikia akisema, “Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:11) ama “Umesamehewa dhambi zako” (Luka 7:48). Haki hiyo ilikuwa ni Yake peke yake kwa sababu Yeye ni Mwana wa Mungu na kwa sababu angelipia dhambi hizo na Upatanisho Wake.

Uwezo Wake wa Kushinda Kifo

Uwezo wake wa kushinda kifo ulikuwa ni sifa ingine ya kiungu. Yairo Mkuu, mtawala wa sinagogi, alisihi “kwamba aingie nyumbani kwake; kwa kuwa binti yake yu katika kifo, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili” (Luka 8:41–42). Bwana alisikia kilio chake, na walipokuwa wanatembea, mfanyikazi alimjia Yairo na kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue Mwalimu” (Luka 8:49). Alipoingia nyumbani, Yesu aliomba kuwa kila mtu atoke inje, na mara moja, akimchukua kwa mkono, Alimwambia yeye, “Inuka” (Luka 8:54).

Wakati mwingine, alipokuwa safarini kuelekea mjini Naini, alikutana na kikundi cha waombolezi wakitembea kuelekea mahali ambapo wangemzika aliyekufa, mjane akiomboleza kifo cha mwanawe wa pekee. Akiwa amejawa na huruma, aligusa kilili cha jeneza, na kusema, “Kijana nakuambia, Inuka” (Luka 7:14). Watu walipoona muujiza huo, walisema, “Nabii mkuu ametokea kwetu; na, … Mungu amewaangalia watu wake” (Luka 7:16). Muujiza huu ulikuwa wa ajabu zaidi kwa sababu walikuwa wamesha mtangaza kisheria kijana yule kuwa hakika amekufa na walikuwa njiani kwenda kumzika. Na vijana wawili kufufuliwa, ushahidi wa mamlaka Yake na uwezo wa kushinda kifo uliwashangaza waaminio na kuwafanya wale waliomchukia kuwa na hofu.

Mara ya tatu ambapo Yesu alifufua mtu ilikuwa ya ajabu zaidi. Martha, Mariamu, na Lazaro walikuwa ndugu ambao Kristo angewatembelea mara kwa mara. Watu walipompasha kwamba Lazaro alikuwa amegonjeka, alibaki siku mbili kabla ya kuondoka kwenda kwa familia. Katika kumfariji Martha baada ya kifo cha kakaye, Alimshuhudia kwa uwazi, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” (Yohana 11:25).

Mwokozi alipowaambia waombolezi watoe jiwe kutoka kaburini, Martha alimwambia kwa sauti ndogo, “Bwana, ananuka sana; maana amekuwa maiti siku nne” (Yohana 11:39).

Kisha Yesu akamkumbusha kwa upendo, “Sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?” (Yohana 11:40). Na baada ya kusema hayo, alipaza sauti kuu:

“Lazaro, njoo huku nje”

“Na akatoka nje yule aliyekufa” (Yohana 11:43–44).

Baada ya siku nne za Lazaro kaburini, maadui wa Mwana wa Mungu walikabiliwa na ushahidi ambao hawangekana, hawangepuuza, dharau, ama kubadilisha ili kupotosha, na wakiwa hawana busara na kwa nia mbaya “tangu siku ile walifanya shauri la kumwua” (Yohana 11:53).

Amri Mpya

Baadaye, Kristo aliye hai alisheherekea katika Yerusalemu, akiwa na Mitume Wake, Karamu Yake ya mwisho ya Pasaka, akaanzisha Ibada ya sakramenti, na kuwapa amri kupendana kwa kutumikiana kwa dhati.

Uchungu wake katika Gethsemane

Baada ya hayo, kwa maonyesho makuu ya upendo Wake kwa wanadamu, na akitenda kulingana na matakwa Yake mwenyewe, alitembea kwa ujasiri na uamuzi kukabiliana na majaribu Yake magumu. Katika Bustani ya Gethsemane, akiwa pekee yake kabisa, Aliteseka kwa uchungu mwingi sana, damu ikimtiririkia kutoka kwa kila kinyweleo. Akiwa amemtii kabisa Baba Yake, alilipia dhambi zetu na pia akachukua juu Yake magonjwa yetu na mateso ili kwamba ajue jinsi ya kutusaidia. (ona Alma 7:11–13).

Tuna mzigo mkubwa wa madeni Kwake na kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa sababu dhabihu Yake ilibariki kila mtu, kutoka kwa Adamu, binadamu wa kwanza, hadi binadamu wa mwisho.

Kuhukumiwa na Kusulubiwa kwa Mwokozi

Wakati mateso aliyopitia Gethsemane kukamilika, alijitolea mwenyewe kwa maadui Wake. Akiwa amesalitiwa na mmoja wa watu Wake, alihukumiwa kwa haraka, kwa njia iliyokuwa si ya haki na isiyofuata sheria, katika majaribio ya hila na yasiyokamili. Usiku huo huo alishtakiwa kosa la kukufuru na kuhukumiwa kifo. Wakiwa na chuki na haja kuu ya kilipiza kisasi ---kwa sababu aliwashuhudia kwamba alikuwa Mwana wa Mungu ---maadui Wake walipanga na Pilato kumhukumu. Ili kutekeleza mpango huo, walibadilisha mashtaka kutoka kwa mashtaka ya kukufuru na kuwa uasi hivyo kwamba kifo chake kingekuwa kwa kusulubiwa.

Hukumu Yake miongoni mwa Warumi ilikuwa ya kikatili zaidi: kejeli zao na matusi kuhusu ufalme Wake wa Kiroho, kufedheheshwa na taji ya miiba, kupigwa Kwake kwa mijeledi, na uchungu wa muda mrefu wa kusulubiwa Kwake hadharani kulikuwa kwote ni onyo wazi kwa watu wote ambao wangethubutu kujitangaza kuwa mwanafunzi Wake.

Katika kila wakati wa mateso Yake, Mkombozi wa dunia alionyesha kujizuia wa kipekee. Yeye daima alifikiria juu ya kuwabariki wengine; kwa wema na huruma, Alimshihi Yohana amtunze mamake, Mariamu. Alimwomba Baba Yake wa Mbinguni awasamehe waliokuwa wanamuuwa ambao walimsulubisha. Kazi Yake duniani ikiwa imetimia, aliiweka roho Yake kwa Mungu na kupumua kwa mara ya mwisho. Mwili wa Kristo ulipelekwa kaburini na kubaki huko siku tatu.

Kazi ya Mkombozi miongoni mwa Wafu

Wakati wanafunzi wake walikuwa wakiteseka kutokana na huzuni, kuvunjika moyo, na kutokuwa na uhakika, Mwokozi wetu, katika awamu ingine ya mpango mtukufu wa Baba Yake, alipanua huduma yake katika njia mpya. Katika kipindi kifupi cha siku tatu, Yeye alifanya kazi bila kuchoka kuandaa kazi kubwa ya wokovu miongoni mwa wafu. Siku hizo zilikuwa baadhi ya siku zilizojawa tumaini kwa familia ya Mungu. Wakati wa ziara hiyo aliwapanga wafuasi Wake waaminifu ili waweze kubeba habari njema ya ukombozi kwa wale ambao katika maisha hawakujua mpango mtukufu ama ambao waliukataa. Sasa wangekuwa na nafasi ya kuwa huru kutokana na utumwa wao na kukombolewa na Mungu wa wote walio hai na wafu (ona M&M 138:19, 30–31).

Limbuko lao Waliolala

Kazi yake ikiwa imekamilika katika ulimwengu wa kiroho, alirudi duniani ---kuunganisha roho Yake na mwili Wake milele. Hata ingawa alikuwa ameonyesha kwa kuaminika uwezo Wake wa kushinda kifo, hadithi za maandiko ya wale Yeye alifufua kabla ya Ufufuo Wake zinaonyesha kwamba wao walikuwa tu wanarudi katika maisha ambayo yalikuwa kimiujiza yamerefushwa; wangeweza bado kufa.

Kristo alikuwa wa kwanza kufufuka na kamwe kutokufa tena, milele kuwa na mwili kamilifu, wa milele. Katika hali yake ya kufufuka, alimtokea Mariamu ambaye mara tu alipomtambua, alianza kumwabudu. Mkombozi Wetu, kwa huruma kubwa, alimuonya kuhusu hali Yake mpya na tukufu: “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba” (Yohana 20:17)—kutoa ushahidi wa ziada kwamba huduma yake katika ulimwengu wa kiroho ilikuwa ya kweli na kamili. Kisha, akitumia maneno yaliyothibitisha ukweli wa Ufufuo Wake, alisema, “Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu, naye ni Mungu wenu” (Yohana 20:17). Baada ya kwenda kwa Baba Yake, alirudi tena na akawatokea Mitume Wake, “akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana” (Yohana 20:20).

Mkombozi Atarudi

Ninashuhudia kwamba Kristo atarudi kwa njia tofauti sana na ujio Wake wa kwanza. Atakuja kwa nguvu nyingi na utukufu na Watakatifu wote waliowema na waaminifu. Atakuja kama Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana, kama Mkuu wa Amani, Masiya aliyeahidiwa, Mwokozi na Mkombozi, kuwahukumu walio hai na wafu. Ninampenda na kumtumikia na moyo wangu wote, na nasihi kwamba tuhudumu kwa furaha na kujitolea na kwamba tuweze kubaki waaminifu Kwake mpaka mwisho. Katika jina Lake, Yesu Kristo, amina.