Ruka uongozaji mkuu
Aprili 2014 | “Usiogope; Maana Mimi ni Pamoja Nawe’

“Usiogope; Maana Mimi ni Pamoja Nawe’

Aprili 2014 Mkutano Mkuu

Tunapokuza matumaini makuu na imani katika Bwana, tunaweza kupata nguvu Zake za kutubariki na kutokomboa.

Hisia chache zinazoweza kulinganishwa na hisia njema za kuwa mzazi. Hakuna kitu kitamu kuliko kupokea mtoto mpendwa, moja kwa moja kutoka mbinguni. Mmoja wa ndugu zangu alipitia hisia hii kwa njia ya uchungu. Mtoto wake wa kwanza alizaliwa mbichi na alikuwa na uzito wa paundi 2 na aunsi 14 (1.3 kg) tu. Hunter alichukua miezi yake miwili ya kwanza ya maisha katika kitengo cha watoto walio mahututi cha hospitali. Miezi hiyo ilikuwa ya majaribu kwa familia yote tulipotumaini na kumwomba Bwana kwa msaada Wake.

Mtoto Hunter alikuwa mtegemezi. Alijitahidi ili kupata nguvu muhimu ya kuishi. Mkono wa nguvu wa baba yake mwenye upendo mara nyingi ilifikia mkono mdogo wa mwanawe ili kuhimiza mtoto wake mdogo mwenye shida.

Na hivyo ndivyo ilivyo kwa watoto wote wa Mungu. Baba yetu aliye Mbinguni humfikia kila mmoja wetu kwa upendo Wake usio na mwisho. Yeye ana nguvu juu ya kila kitu na anatamani kutusaidia kujifunza, kukua, na kurudi Kwake. Hii inafafanua lengo la Baba yetu: “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”1

Tunapokuza imani zaidi na matumaini katika Bwana, tunaweza kupata nguvu Zake ili kutubariki na kutuokoa.

Kitabu cha Mormoni husuka mada hii nzuri ya nguvu ya Bwana ya kuwaokoa watoto Wake katika kurasa zake. Nefi aliitanguliza katika sura ya kwanza ya kitabu hiki. Katika aya ya 20, tunasoma, “Tazama, mimi, Nefi, nitawaonyesha nyinyi kuwa ana huruma nyororo juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani, kuwatia nguvu hata kwenye uwezo wa ukombozi.” .”2

Miaka mingi iliyopita nilikuja kujua kwa njia ya kibinafsi zaidi kweli zilizoonyeshwa katika mstari huu. Nilikuja kujua jinsi Baba yetu wa Mbinguni alivyo karibu na ni kiasi gani Yeye ana hamu ya kutusaidia.

Jioni moja usiku ulipokuwa ukiingia, mimi pamoja na watoto wangu tulikuwa tukiendesha gari. nilipomwona mvulana akitembea kando ya barabara isiyo na watu. Baada ya kumpita, nilipata hisia tofauti kuwa napaswa kurudi nyuma na kumsaidia. Lakini nilikuwa na wasiwasi angeshtuka kuona mgeni akisimama karibu naye wakati wa usiku, niliendelea kuendesha gari. Hisia hiyo kali ilirudi tena pamoja na maneno katika akili yangu: “Nenda umsaidiye mvulana huyo!”

Nilirudi nyuma na kuuliza, “Je, unahitaji msaada? nilikuwa na hisia kuwa ninafaa nikusaidie.”

Aligeuka kutuangalia na machozi yakitiririka mashavuni mwake akisema, “Je, utaweza? Nimekuwa nikiomba mtu aweze kunisaidia.”

Maombi yake kwa msaada yalijibiwa kwa maongozi kutoka mbinguni yaliyokuja kwangu. Uzoefu huu wa kupokea maelekezo wazi kama haya kutoka kwa Roho uliacha fikra zisizoweza kusaulika ambazo bado ziko kwenye moyo wangu.

Na sasa baada ya miaka 25 kupitia rehema ororo, mimi nilikutana tena na mvulana huyu kwa mara ya kwanza miezi michache iliyopita. Niligundua kwamba tukio hilo sio hadithi yangu tu---ni hadithi yake pia. Deric Nance sasa ni baba mwenye familia yake mwenyewe. Yeye pia hajawahi kusahau tukio hilo. Sisi sote tumelitumia katika kufundisha watoto wetu kwamba Mungu anatulinda sisi. Sisi hatuko peke yetu. Lilitusaidia kuweka msingi wa imani kwamba Mungu husikia na hujibu maombi yetu. Sote wawili tuliutumia kuwafundisha watoto wetu kwamba Mungu anatutunza. Sisi hatuko peke yetu.

Usiku huo, Deric alibakia kwa shughuli baada ya shule na kukosa basi la mwisho. Kama kijana mdogo, alihisi kujiamini kuwa angeweza kufanikiwa kurudi nyumbani, hivyo akaanza kutembea.

Saa moja na nusu ilikuwa imepita akitembea kwenye barabara peke yake. Ikiwa bado maili kadha kutoka nyumbani na pasipoonekana nyumba yoyote, alijawa na hofu. Kwa kukata tamaa, alienda nyuma ya mrundo ya changarawe, akapiga magoti, na kuomba Baba wa Mbinguni msaada. Dakika chache tu baada ya Deric kurudi barabarani, nilisimama kutoa msaada muhimu aliouomba.

Miaka hii mingi baadaye, Deric anakumbuka: “Bwana alinikumbuka, mvulana mkondefu, asiyeona mbali. Na licha ya kila kitu kingine kinachoendelea ulimwenguni, Yeye alifahamu hali yangu na kunipenda ya kutosha kunitumia msaada. Bwana amejibu maombi yangu mara nyingi tangu ile barabara yenye upweke. Majibu yake mara zote si haraka na wazi hivi, lakini ufahamu Wake juu yangu ni dhahiri leo kama ilivyokuwa usiku ule wa upweke. Wakati vivuli vyeusi vya maisha vinafunika ulimwengu wangu, Najua kila wakati ana mpango wa kunirudisha nyumbani salama tena.”

Kama vile Deric alivyoeleza, sio kila maombi hujibiwa hivyo haraka. Lakini kwa kweli Baba yetu anatujua na husikia kilio cha mioyo yetu. Yeye hutimiza miujiza Yake, ombi moja kwa wakati mmoja, mtu mmoja kwa wakati.

Tunaweza kuamini kwamba atatusaidia, si lazima kwa njia tutakayo lakini kwa njia ambayo itakuwa bora kutusaidia kukua. Kuyaweka mapenzi yetu chini ya Yake inaweza kuwa vigumu, lakini ni muhimu katika kuwa kama Yeye na kupata amani anayotupatia sisi.

Tunaweza kuja kuhisi, kama C. S Lewis alivyoeleza: “Naomba kwa sababu siwezi kujisaidia mwenyewe. Naomba kwa sababu haja hutiririka kutoka kwangu wakati wote, nikiamka na kulala. Haimbadilishi Mungu. Hunibadilisha mimi.”3

Kuna hadithi nyingi katika maandiko ya wale ambao wameweka imani yao katika Bwana na ambao wamesaidiwa na kukombolewa Naye. Fikiria juu ya kijana Daudi, aliyenusurika kifo dhahiri katika mkono wa Goliathi kwa kumtegemea Bwana. Fikiria Nefi, ambaye maombi yake kwa Mungu kwa imani yalileta ukombozi kutoka kaka zake ambao walitaka kuutoa uhai wake. Kumbuka kijana Joseph Smith, ambaye kwa maombi alitafuta msaada wa Bwana. Alikombolewa kutokana na nguvu za giza na kupokea jibu la kimiujiza. Kila mmoja alipitia changamoto halisi na ngumu. Kila mmoja alitenda kwa imani na kuweka imani yake katika Bwana. Kila mmoja alipokea msaada Wake. Na bado katika siku zetu, nguvu na upendo wa Mungu ni wazi katika maisha ya watoto Wake.

Nimeiona hivi karibuni katika maisha ya Watakatifu wenye imani kule Zimbabwe na Botswana. Katika mkutano wa mfungo na ushuhuda katika Tawi dogo, nilinyenyekezwa na kuvutiwa na ushuhuda wa watoto, vijana, na watu wazima vilevile. Kila moja alidhihirisha onyesho kuu la imani katika Bwana Yesu Kristo. Wakizungukwa na changamoto na hali ngumu, wanaishi kila siku kwa kuweka imani yao katika Mungu. Wanatambua mkono Wake katika maisha yao na kila mara inaonyeshwa kwa kishazi “Nashukuru sana kwa Mungu.”

Miaka michache iliyopita familia aminifu ilionyesha mfano kwa washiriki wa kata yetu imani hiyo hiyo katika Bwana. Arn na Venita Gatrell walikuwa wakiishi maisha ya furaha na familia ya ajabu. Arn alikuwa na kazi nzuri, na kisha, bila kutarajia, alipatikana na ugonjwa wa saratani kali. Ubashiri haukuwa mzuri---alikuwa na wiki chache tu kuishi. Familia ilitaka kuwa pamoja kwa mara ya mwisho. Hivyo watoto wote walikusanyika, wengine kutoka maeneo ya mbali. Walikuwa tu na masaa 48 ya thamani ya kuwa pamoja. Wana Gatrell kwa uangalifu walichagua kile cha muhimu zaidi kwao---picha ya familia, chakula cha jioni cha familia, na kikao katika Hekalu la Salt Lake. Venita alisema, “Tulipotoka nje ya milango ya hekalu, ilikuwa ni mara ya mwisho tutakayo kuwa pamoja katika maisha haya.”

Lakini waliondoka kwa uhakika kwamba kuna zaidi kwao kuliko tu maisha haya. Kwa sababu ya ahadi takatifu za hekalu, wanaweza kuwa na tumaini katika ahadi za Mungu. Wanaweza kuwa pamoja milele.

Miezi miwili iliyofuata ilijawa na baraka nyingi mno kwa kusimulia. Imani na matumaini ya Arn na Venita kwa Bwana yalikuwa yanaongezeka kama ilivyoshuhudiwa katika maneno ya Venita: “Nilibebwa. Nilijifunza kwamba unaweza kuhisi amani katika machafuko. Nilijua Bwana alikuwa akitulinda. Kama utaamini katika Bwana, kweli unaweza kushinda yoyote kati ya changamoto za maisha.”

Mmoja wa mabinti zake aliongeza, “Tuliwatazama wazazi wetu na kuona mfano wao. Tuliiona imani yao na jinsi walivyoichukua. Kamwe singeweza kuomba jaribio hili, lakini siwezi kamwe kuitupilia mbali. Tunazingirwa na upendo wa Mungu.”

Bila shaka, kufa kwa Arn haikuwa ​​matokeo ambayo wana Gatrell walitarajia. Lakini shida yao haikuwa shida ya imani. Injili ya Yesu Kristo si orodha ya mambo ya kufanywa; badala yake, huishi katika mioyo yetu. Injili “sio uzito; ni mabawa.”4 Hutubeba sisi. Iliwabeba wana Gatrell. Walihisi amani katikati ya dhoruba. Walishikana pamoja na kuzingatia maagano ya hekalu waliyoyafanya na kuweka. Walikuwa katika uwezo wao wa kuamini katika Bwana na waliimarishwa na imani yao katika Yesu Kristo na katika uwezo Wake wa upatanisho.

Popote tunapojipata katika njia ya ufuasi, pasipokujali wasiwasi na changamoto zetu zitakazokuwa, sisi hatuko peke yetu. Sisi hatujasahauliwa. Kama Deric, Watakatifu wa Afrika, na familia ya Gatrell, tunaweza kuchagua kufikia mkono wa Mungu katika mahitaji yetu. Tunaweza kukabiliana na changamoto zetu kwa sala na imani katika Bwana. Na hatimaye tunakuwa zaidi kama Yeye.

Akiongea na kila mmoja wetu, Bwana akisema, “Usiogope; … mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu; … Nitakusaidia; naam, Nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”5

Nashiriki ushuhuda wangu mnyenyekevu bali wa hakika kwamba Mungu Baba yetu anatujua sisi binafsi na hufikia kutusaidia. Kupitia kwa Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, tunaweza kushinda changamoto za dunia hii na kurejeshwa nyumbani salama. Na tuweze kuwa na imani kumtumaini Yeye, naomba katika jina la Yesu Kristo, amina.

Left
Onesha KumbukumbuFicha Kumbukumbu

  Muhtasari

  1. Moses 1:39.

  2. 1 Nefi 1:20.

  3. Ilisemwa kwa hulka ya C. S. Lewis kama ilivyoonyeshwa William Nicholson, Shadowlands (1989), 103.

  4. Harry Emerson Fosdick, Twelve Tests of Character (1923), 88.

  5. Isaya 41:10.