Ruka uongozaji mkuu
Aprili 2014 | Kama Mnapungukiwa na Hekima

Kama Mnapungukiwa na Hekima

Aprili 2014 Mkutano Mkuu

Mungu atafunua ukweli kwa wale wanaoutafuta kama ilivyoandikwa katika maandiko.

Hivi majuzi, mwanangu mwenye umri wa miaka 10 alikuwa anasoma kuhusu akili ya binadamu kwenye Intaneti. Anataka kuwa daktari wa upasuaji siku moja. Si vigumu kutambua kwamba ni mwerevu zaidi kunishinda.

Tunapenda Intaneti. Nyumbani sisi huwasiliana na familia na marafiki kupitia mitandao ya kijamii, barua pepe, na njia zinginezo. Watoto wangu hufanya zaidi ya kazi zao za shule kupitia Intaneti.

Haijalishi ni swali gani, ikiwa tunahitaji habari zaidi, sisi huitafuta kwenye mtandao. Kwa sekunde tunazo taarifa nyingi. Hili ni jambo zuri la ajabu.

Intaneti inatupa fursa nyingi za kujifunza. Hata hivyo, Shetani anatutaka tuwe na huzuni, naye huharibu madhumuni halisi ya vitu. Yeye hutumia chombo hiki kikuu kukuza shaka na hofu, na kuangamiza imani na matumaini.

Na yale yote yanayopatikana kwenye Intaneti, mtu lazima azingatie kwa makini mahali pa kuweka juhudi zake. Shetani anaweza kutushughulisha, kutupotosha, na kutuathiri kupitia kwa kupekua habari nyingi zake ambazo huenda zikawa ni takataka kabisa.

Mtu hapaswi atangetange ndani ya takataka.

Sikiliza mwongozo huu, uliotolewa katika maandiko: “Kwani tazama, Roho ya Kristo imetolewa kwa kila mtu, ili ajue mema na maovu; kwa hivyo, ninawaonyesha njia ya kuhukumu; kwani kila kitu kinachokaribisha kufanya mema, na kushawishi kuamini katika Kristo, kinasababishwa na uwezo na thawabu ya Kristo; kwa hivyo mgejua...ni cha Mungu.”1

Kwa hali halisi, sisi hukabiliwa na mtanziko ule ule ambao Joseph Smith alikumbana nao katika ujana wake. Mara nyingi sisi hujipata tukiwa tumepungukiwa na hekima.

Katika ufalme wa Mungu, utafutaji wa ukweli unakaribishwa, unahimizwa, na huwa hauzimwi ama kuogopewa kwa njia yoyote. Washiriki wa Kanisa hushauriwa kwa nguvu na Bwana Mwenyewe kutafuta maarifa.2 Alisema, “Tafuteni kwa bidii… ; ndiyo, tafuteni kutoka kwenye vitabu vizuri maneno ya hekima; tafuteni maarifa, hata kwa kujifunza na pia kwa imani.”3 Hata hivyo, tunawezaje kutambua ukweli katika dunia ambayo zaidi inashambulia moja kwa moja mambo ya Mungu?

Maandiko yanatufundisha jinsi:

Kwanza, tunaweza kujua ukweli kwa kutazama matunda yake.

Wakati wa Mahubiri Yake makuu Mlimani, Bwana alisema:

“Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. …

“Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.”4

Nabii Mormoni alifundisha kanuni hii hii aliposema: “Kwa matunda yao mtawatambua; kwani kama matunda yao ni mema, basi ni wema pia.”5

Tunawakaribisha wote wafanye utafiti wa matunda na vitendo vya Kanisa hili.

Wale ambao wana hamu ya ukweli wataweza kutambua tofauti ambayo Kanisa na washiriki wake huleta katika jamii ambapo wapo. Watatambua pia uboresho katika maisha ya wale ambao hufuata mafundisho yake. Wale ambao wanafanya utafiti wa matunda haya watagundua kwamba matunda ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni matamu na ya kuvutia.

Pili, tunaweza kupata ukweli kwa kujaribu juu ya maneno wenyewe.

Nabii Alma alifundisha:

“Tutalinganisha neno kwa mbegu. … Ikiwa mtatoa nafasi, ili mbegu ipandwe ndani ya moyo wako, tazama ikiwa itakuwa mbegu ya kweli, [na] ... ikiwa hamtaitupa nje kwa kutoamini kwenu, ... tazama, itaanza kuvimba ndani ya vifua vyenu; na ... mtaanza kusema ndani yenu---inawezekana kwamba hii ni mbegu nzuri, ... kwani inaanza kukua ndani ya nafsi yangu; ndio, inaanza kuangaza kuelewa kwangu, ndio, inaanza kunipendeza mimi. …

“... Sasa tazama, … si hii itaongeza imani yenu? Ninawaambia, Ndio. …

“... Kwani kila mbegu huzaa mfano wake.”6

Ni mwaliko mzuri jinsi gani kutoka kwa nabii wa Bwana! Hii inaweza kulinganishwa na utafiti wa kisayansi. Tunaalikwa tujaribu neno, tunapewa vigezo, na tunaambiwa matokeo ya jaribio, ikiwa tutafuata maelekezo.

Hivyo basi, maandiko yanatufundisha kwamba tunaweza kujua ukweli kwa kuchunguza matunda yake; ama, kwa kujaribu kibinafsi, tukitoa nafasi ya neno katika mioyo yetu, na kulikuza, kama vile mbegu.

Hata hivyo, kunayo bado njia ya tatu ya kujua ukweli, na hiyo ni kupitia ufunuo wa kibinafsi.

Mafundisho na Maagano sehemu ya 8 hufundisha kwamba ufunuo ni---“maarifa ya chochote kile [tutakachokiomba] kwa imani, na moyo mnyoofu, [sisi] tukiamini kwamba [sisi] tutapata .”7

Na Bwana anatuambia jinsi tutapata ufunuo. Anasema, “Nitakujulisha wewe akilini mwako na katika moyo wako, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye atakujia na ambaye atakaa moyoni mwako.”8

Basi, tunafundishwa kwamba ufunuo unaweza kupatikana kwa kuomba kwa imani, na moyo mnyoofu, na tukiamini kwamba tutapata.

Lakini kumbuka kwamba Bwana alieleza wazi alipoonya, “Kumbuka kwamba pasipo imani huwezi kufanya lolote; hivyo basi omba kwa imani.”9 Imani inahitaji matendo---kama vile kuchunguza katika akili yako, ndipo umulize katika maombi kama ni sahihi.

Bwana alisema:

“Kama ni sahihi nitaufanya moyo wako uwake ndani yako; kwa njia hiyo, utahisi kuwa hiyo ni sahihi.

Lakini kama siyo sahihi hautapata hisia za namna hiyo, bali mzubao wa mawazo ambayo yatakufanya usahau kitu kile kisicho sahihi.”10

Imani isipokuwa ina matendo, imekufa.11 Basi, “omba kwa imani, pasipo shaka yoyote.”12

Nina rafiki, ambaye si wa dini yetu, ambaye alinieleza kwamba yeye si mtu wa kuthamini mambo ya roho. Hatasoma maandiko ama kuomba kwa sababu anasema hawezi kuelewa maneno ya Mungu, wala hana uhakika kwamba Mungu yupo. Mtazamo huu unaeleza kukosa kwake kuthamini mambo ya kiroho na utaelekeza kwa kile kilicho kinyume cha ufunuo, kama vile ilivyoelezwa na Alma: Alisema, “Na kwa hivyo, yule ambaye atashupaza moyo wake, huyo atapokea sehemu ndogo ya neno.”

Lakini, Alma aliongezea, “yule ambaye hatashupaza moyo wake, huyo anapewa sehemu kubwa ya neno, hadi awezeshwe kufahamu siri za Mungu hadi azielewe kikamilifu.”13

Alma na wana wa Mosia ni vielelezo vya kanuni kwamba imani inahitaji matendo. Katika Kitabu cha Mormoni, tunasoma:

“Walikuwa wameyapekua maandiko kwa bidii, ili wajue neno la Mungu.

“Lakini haya sio yote; kwani walikuwa wamejitoa kwa sala, na kufunga; kwa hivyo walikuwa na roho ya ufunuo.”14

Kuomba kwa moyo mnyoofu ni muhimu pia katika jitihadi hii. Ikiwa tunatafuta ukweli kwa dhati, tutafanya yote kadri ya uwezo wetu kuupata, ambayo inaweza kujumuisha kusoma maandiko, kwenda kanisani, na kufanya tuwezavyo kutii amri za Mungu. Inamaanisha pia kwamba tuko tayari kufanya mapenzi ya Mungu tutakapoyajua.

Matendo ya Joseph Smith alipokuwa anatafuta hekima ni mifano mizuri ya kile kinachomaanisha kuwa na moyo mnyoofu. Alisema alitaka kujua ni lipi kati ya madhehebu yale yote lilikuwa sahihi, ili angejua lipi angejiunga nayo.”15 Hata kabla aombe, alikuwa tayari kutendea ambalo angepata.

Lazima tuulize kwa imani na kwa moyo mnyoofu. Lakini hii haitoshi. Lazima pia tuamini kwamba tutapokea ufunuo. Lazima tumuamini Bwana na tutumainie ahadi Zake. Kumbuka kile kilichoandikwa: “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atawapa.”16 Ni baraka ya ajabu jinsi gani!

Ninawaalika nyote mtafute ukweli kutoka kwa yoyote kati ya njia hizi lakini hasa kutoka kwa Mungu kupitia ufunuo wa kibinafsi. Mungu atafunua ukweli kwa wale wanaoutafuta kama ilivyoelezwa katika maandiko. Inahitaji bidii zaidi kuliko tu kutafuta kwenye Intaneti, lakini ni ya thamani.

Ninatoa ushuhuda wangu kwamba hili ndilo Kanisa la Yesu Kristo la kweli. Nineona matunda yake katika jamii na maisha ya maelfu ya watu, ikiwa ni pamoja na wana familia; hivyo basi ninajua kuwa ni la kweli. Mimi pia nimejaribu neno hili katika maisha yangu kwa miaka mingi na mimi nimehisi athari yake kwa nafsi yangu; hivyo basi ninajua ni la kweli. Lakini muhimu kabisa, nimejifunza juu ya ukweli wake mwenyewe kwa ufunuo kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu; hivyo basi ninajua ni kweli. Ninawaalika ninyi nyote kufanya vivyo hivyo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Onesha KumbukumbuFicha Kumbukumbu