Ruka uongozaji mkuu
Aprili 2014 | Mzigo wa Furaha wa Ufuasi

Mzigo wa Furaha wa Ufuasi

Aprili 2014 Mkutano Mkuu

Kuwaidhinisha viongozi wetu ni fursa; huja na jukumu la kibinafsi la kushiriki mizigo yao na kuwa wafuasi wa Bwana.

Mnamo Mei 20 mwaka jana, kimbunga kikubwa kilikumba viunga vya Mji wa Oklahoma, katika kitovu cha Marekani, kuchora njia zaidi ya maili moja (1.6 km) kwa upana na maili 17 (27 km) kwa urefu. Dhoruba hii, shambulizi la kimbunga kali, lilibadilisha sura ya nchi na maisha ya watu katika njia yake.

Wiki moja tu baada ya dhoruba kubwa kupiga, nilitumwa kutembelea eneo hilo ambapo nyumba na mali zilitapakaa katika vitongoji vya jirani vilivyoharibiwa vibaya.

Kabla ya kuondoka, niliongea na nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, anayependezwa na kazi kama hiyo kwa ajili ya Bwana. Kwa heshima inayotokana si tu kwa ofisi yake lakini pia kwa wema wake, niliuliza, “Je, unataka nifanye nini? Je, unataka niseme nini?

Kwa upole alishika mkono wangu, kama vile angefanya kwa kila mmoja wa waathiriwa na kila moja anayesaidia katika uharibifu kama angekuwapo pale, na akasema:

“Kwanza, waambie ninawapenda.

“Pili, waambi ninawaombea.

“Tatu, tafadhali washukuru wale wote ambao wanasaidia.”

Kama mshiriki wa Urais wa Sabini, ningeweza kuhisi uzito juu ya mabega yangu kwa maneno ambayo Bwana alinena na Musa:

“Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli ambao wewe unawajua kuwa ndio wazee wa watu, na maakida juu yao; …

“Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako [Musa], na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu pamoja nawe, ili usichukue wewe peke yako.”1

Haya ni maneno kutoka nyakati za kale, lakini njia za Bwana hazijabadilika.

Hivi sasa katika Kanisa, Bwana ameita Sabini 317, wakihudumu katika jamii 8, ili kuwasaidia Mitume Kumi na Wawili katika kubeba mzigo uliowekwa kwenye Urais wa Kwanza. Nahisi kwa furaha wajibu huo katika kina cha nafsi yangu, kama wafanyavyo Ndugu zangu. Hata hivyo, sio sisi peke yetu tunaosaidia katika kazi hii tukufu. Kama washiriki wa Kanisa duniani kote, sisi sote tuna nafasi ya ajabu ya kubariki maisha ya wengine.

Nilikuwa nimejifunza kutoka kwa nabii wetu mpendwa kile watu waliosukwasukwa na dhoruba walihitaji---upendo, sala, na shukrani kwa mikono ya kusaidia.

Mchana huu kila mmoja wetu atainua mkono wake wa kulia mraba na kuidhinisha Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili kama manabii, waonaji, na wafunuaji wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Huu sio mwenendo tu wa kawaida, wala haujawekwa kwa ajili ya wale walioitwa kwa huduma ya kawaida. Kuidhinisha viongozi wetu ni fursa; inakuja ikiwa pamoja na wajibu wa kibinafsi wa kushiriki mzigo wao na kuwa wafuasi wa Bwana Yesu Kristo.

Rais Monson amesema:

“Tumezungukwa na wale wanaohitaji mawazo yetu, mahimizo yetu, msaada wetu, faraja yetu, wema wetu---kama wao ni wanafamilia, marafiki, jamaa, au wageni. Sisi ni mikono ya Bwana hapa duniani, na mamlaka ya kutumikia na kuinua watoto Wake. Yeye anategemea kila mmoja wetu. ...

“‘… Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu … , mlinitendea mimi’ [Mathayo 25:40].”2

Je, tutaweza kujibu kwa upendo wakati nafasi ipo mbele yetu ya kufanya matembezi au kupiga simu, kuandika barua, au kutumia siku kukidhi mahitaji ya mtu mwingine? Au tutakuwa kama kijana ambaye alishuhudia kufuata amri zote za Mungu:

“Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

“Yesu akamwambia, ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.”3

Kijana huyo alikuwa anaitwa kwa huduma kuu zaidi katika upande wa Bwana ili kufanya kazi ya ufalme wa Mungu duniani, lakini alipuuza, “kwa maana alikuwa na mali nyingi.”4

Ni nini kuhusu mali yetu hapa duniani? Tunaweza kuona kile kimbunga kinaweza kufanya nayo kwa dakika tu. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujitahidi na kujiwekea hazina yetu ya kiroho mbinguni kwa kutumia wakati wetu, talanta, na wakala katika utumishi wa Mungu.

Yesu Kristo anaendelea kueneza mwito “Njoo Unifuate.”5 Alitembea nchi Yake na wafuasi Wake kwa njia ya kujitolea. Anaendelea kutembea na sisi, kusimama na sisi, na kutuongoza. Kufuata mfano Wake kamili ni kutambua na kumheshimu Mwokozi, aliyebeba mizigo yetu yote kupitia kwa Upatanisho Wake mtakatifu na wenye kuokoa, kitendo cha mwisho cha huduma. Kile anauliza kila mmoja wetu ni kuwa na uwezo na nia ya kuchukua “mzigo” wa furaha wa ufuasi.

Nilipokuwa Oklahoma, nilikuwa na fursa ya kukutana na familia chache zilizoathirika kutokana na vimbunga vikali. Nilipokuwa nikitembelea familia ya Sorrels, niliguswa hasa na matukio ya binti yao, Tori, wakati huo akiwa wa gredi tano katika Shule ya Msingi ya Plaza Towers. Yeye na mama yake wako pamoja nasi hapa leo.

Tori na marafiki wake wachache wakijifinyilia katika choo kwa ajili ya makazi wakati kimbunga kikivuma kupitia kwa shule. Sikiliza ninaposoma, katika maneno ya Tori mwenyewe, matukio ya siku hiyo:

“Nilisikia kitu kikigonga paa. Nilidhani ilikuwa inanyesha tu mvua ya mawe. Sauti iliendelea kuwa kubwa zaidi na zaidi. Nilisema maombi kwamba Baba wa Mbinguni angetulinda sisi sote na kutuweka salama. Ghafla tulisikia sauti kubwa ya mvuto, na paa likatoweka juu ya vichwa vyetu. Kulikuwa na upepo mwingi na taka ziliruka kwote na kupiga kila sehemu ya mwili wangu. Ilikuwa giza nje na ilionekana kama anga ilikuwa nyeusi, lakini haikuwa nyeusi---ilikuwa ndani ya kimbunga. Nilifunga tu macho yangu, nikitumaini na kuomba kwamba itaisha hivi karibuni.

“Kwa ghafla kukawa kimya.

“Nilipofungua macho yangu, niliona ishara ya kusimama mbele ya macho yangu! Ilikuwa karibu kugusa pua yangu.”6

Tori, mama yake, ndugu zake watatu, na marafiki wengi ambao walikuwa pamoja naye pia shuleni, walinusurika kimbunga kimiujiza; saba kati ya wanafunzi wenzao hawakunusurika.

Wikendi hiyo ndugu wa ukuhani walitoa baraka nyingi kwa washiriki ambao waliathirika katika dhoruba. Nilinyenyekezwa kumpa Tori baraka. Nilipoweka mikono yangu juu ya kichwa chake, andiko nilipendalo likaja akilini mwangu: “Nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho Wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika zangu watawazingira, ili kuwabeba juu.”7

Nilimshauri Tori kukumbuka siku ambayo mtumishi wa Bwana aliweka mikono yake juu ya kichwa chake na kutamka kwamba yeye alikuwa amelindwa na malaika katika dhoruba.

Kufikia kuokoa mtu mwingine, chini ya hali yoyote, ni kipimo cha milele cha upendo. Hii ndio huduma nilioshuhudia Oklahoma wiki hiyo.

Mara nyingi sisi hupewa fursa ya kuwasaidia wengine katika wakati wao wa mahitaji. Kama washiriki wa Kanisa, tuna jukumu takatifu la “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi,”8 “kuomboleza na wale wanaoomboleza,”9 na kuinyoosha mikono iliyolegea na kuimarisha magoti yaliyodhaifu.”10

Ndugu na dada, jinsi gani Bwana ana shukrani kwa kila mmoja wenu, kwa masaa yasiohesabika na matendo ya huduma, iwe ni makubwa au madogo, ambayo unatoa kwa ukarimu na neema kila siku.

Mfalme Benjamini alifundisha katika Kitabu cha Mormoni, “Mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.”11

Kulenga kuwahudumia ndugu na dada zetu kunaweza kutuongoza sisi kufanya maamuzi matakatifu katika maisha yetu ya kila siku na kutuandaa kuthamini na kupenda kile Bwana anapenda. Kwa kufanya hivyo, tunashuhudia kwa maisha yetu kwamba sisi ni wafuasi Wake. Tunapojumuika katika kazi yake, tunahisi Roho wake pamoja nasi. Tunakuwa kwa ushuhuda, imani, tumaini, na upendo.

Najua ya kuwa Mkombozi wangu yu hai, hata Yesu Kristo, na kwamba humwongelesha nabii Wake na kutuongelesha kupitia nabii Wake, Rais mpendwa Thomas S. Monson, katika siku hizi zetu.

Na tuweze sote kupata furaha inayotokana na huduma takatifu ya kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine hata ile rahisi na midogo, ni ombi langu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Onesha KumbukumbuFicha Kumbukumbu