2010–2019
Ongozwa Salama Nyumbani
Oktoba 2014


Ongozwa Salama Nyumbani

Tunatazama mbinguni kwa ajili ya ile hisia isiokwisha ya mwelekeo, ili kwamba tuweze kuweka na kufuata njia nzuri

Ndugu, tumekusanyika kama muungano mkuu wa ukuhani, hapa katika Kituo cha Mkutano Mkuu na katika maeneo kote duniani. Ninashukuru na bado kunyenyekezwa na jukumu ambalo ni langu kuwahutubia jumbe chache. Ninaomba Roho wa Bwana aniongoze ninapofanya hivyo.

Miaka sabini na tano iliyopita, mnamo Februari  14, 1939, kule Hamburg, Ujerumani, sikukuu ya umma ilisherekewa. Miongoni mwa hotuba za dhati, umati wa watu ukishangilia, na kucheza kwa nyimbo za kitaifa, meli mpya ya vita Bismarck iling’oa nanga katika Mto wa Elbe. Hii, meli kuu zaidi ya zote majini, ilikuwa onyesho la mshangao kwa silaha na mashine. Ujenzi ulihitaji miongozo 57,000 ya mizinga miwili ya milimita 380, bunduki zinazoelekezwa na rada. Meli ilikuwa na maili 28,000 (45,000km) ya mizunguko ya umeme. Tani elfu thelathini na tano ya mabamba yaliyoimarishwa. Ilionekana ya Kifahari, Kubwa kwa ukubwa, mzuri kwa uwezo wa silaha, meli hiyo kubwa ilizingatiwa kuwa haiwezi kuzamishwa.

Wakati wa Bismarck kukutana na hitima yake ulikuja zaidi ya miaka miwili iliyofuata, ambapo mnamo Mei  24, 1941, meli kuu za vita katika Jeshi la Maji la Uingereza, Prince of Wales na Hood, zilipigana na Bismarck na mashua ya Ujerumani Prinz Eugen. Katika dakika tano Bismarck ilikuwa imezamisha Hood katika Atlantika na kila mfanyikazi katika meli ila tu watatu kati ya 1,400. Meli ile ingine ya Uingereza, Prince of Wales, ilikuwa imeharibiwa sana na ikageuka na kurudi.

Katika siku tatu zilizofuata, Bismarck ilipigana tena, wakati huu na meli na ndege za vita za Uingereza. Yote pamoja, Waingereza walikusanya nguvu za meli tano za vita, ndege mbili, meli za vita zenye kasi 11, na meli ndogo za vita 21 katika jitihada ya kuipata na kuizamisha Bismarck kuu.

Wakati wa vita, makombora mengi yaliharibu Bismarck tu juu juu. Je, ilikuwa haiwezi kuzamishwa kweli? Kisha topido ikaigonga vizuri, pigo lililokwamisha usukani wa Bismarck. Jitihada za kurekebisha hazikufua dafu. Na bunduki tayari kufiatuliwa na wanamaji wakiwa gangari, Bismarck ingezunguka duara tu pole pole. Karibu tu kulikuwa na kikosi kikuu cha anga cha Ujerumani.  Bismarck haingeweza kufika bandari ya nyumbani salama. Wala haingetoa mahali pa kujificha palipohitajika, kwani Bismarck ilikuwa imepoteza uwezo wa kusonga mbele. Bila usukani; bila usaidizi; bila bandari. Mwisho ulikaribia. Mizinga ya Uingereza ilipokuwa inafyatuliwa, wanamaji wa Ujerumani wakatawanywa na meli kuzamishwa ambayo kwa wakati fulani ilionekana kuwa haiwezi kuharibiwa. Mawimbi ya Atlantika yenye njaa yaligonga upande wa meli na kisha yakameza kiburi ya kikosi cha wanamaji wa Ujerumani. Bismarck ikawa haiko tena.1

Kama Bismarck, kila mmoja wetu ni muujiza wa uhandisi. Kuumbwa kwetu, hata hivyo, hakukupunguzwa na uerevu wa binadamu. Mwanadamu anaweza kujenga mashine ya ubunifu wa hali ya juu sana lakini hawezi kuzipa maisha ama kuzipa uwezo wa kufikiria na kudadisi. Hizi ni karama za kiungu, zinazotolewa tu na Mungu.

Kama usukani muhimu wa meli, ndugu, tumepewa njia ya kuamua mwelekeo tunaosafiri. Mnara wa taa wa Bwana unaelekeza wote tunaposafiri katika bahari ya maisha. Kusudi letu ni kusafiri katika njia isiyobadilika kuelekea lengo tunalolitamani---hata ufalme wa Mungu wa selestia. Mtu asiyekuwa na kusudi ni kama meli isiyo na usukani, isiyo na uwezekano kamwe kufika kwenye bandari ya nyumbani. Kwetu kunakuja ishara: amua njia unataka kwenda, jitayarishe kwenda, weka ukusani wako vyema, na endelea.

Kama vile na Bismarck, kuu, ndivyo ilivyo na mwanadamu. Msukumo wa tabo na nguvu ya rafadha hazina maana bila mwelekeo, kule kutumia nguvu zile, kule kuelekeza nguvu inayotolewa na usukani, uliofichika, ulio mdogo kwa kulinganisha, lakini muhimu sana kimatumizi.

Baba yetu alitoa jua, mwezi, na nyota---makundi ya nyota mbinguni kuwaongoza mabaharia ambao wanasafiri njia za bahari. Kwetu sisi, tunapotembea mapito ya maisha, anatoa ramani wazi na kuonyesha njia kuelekea kwa hitimio letu tunalotamani. Anaonya: tahadhari vipotoshi njia, hatari, mitego. Hatuwezi kudanganywa na wale ambao wangetupotosha, wale wajanja wapigao filimbi ya dhambi wakiitana hapa ama pale. Badala yake, tunasimama kuomba; tunasikiliza sauti ile ndogo na tulivu ambayo inazungumzia kwa kina cha nafsi zetu aliko pole la Mwalimu, “Njoo, unifuate.”2

Bado kuna wale ambao hawasikilizi, ambao hawatatii, ambao wanapendelea kutembea njia waliyojitengenezea wenyewe. Mara nyingi wao hukosa kupinga majaribio yanayozingira kila mmoja wetu na ambayo yanaweza kuonekana kuvutia sana.

Kama wenye ukuhani, tumewekwa duniani katika nyakati za shida. Tunaishi katika dunia tata na mawimbi ya vita kila mahali kupatikana. Mipango ya kisiasa inaharibu utulivu wa mataifa, kushika kwa nguvu utawala kwa viongozi wabaya, na makundi ya jamii yanaonekana milele kunyanyaswa, kunyimwa fursa, na kuachwa na hisia ya kushindwa. Falsafa za wanadamu zinasikika kila mara, dhambi inatuzingira.

Letu ni jukumu la kuwa wastahiki kwa baraka zote kuu ambazo Baba yetu wa Mbinguni ametuhifadhia. Popote tuendapo, ukuhani wetu huenda nasi. Je, tunasimama katika mahali patakatifu? Tafadhali, kabla ujiweke wewe na ukuhani wako mashakani kwa kwenda mahali ama kushiriki katika shughuli ambazo hazistahili kwako ama kwa ukuhani huo, tua ili kuzingatia matokeo.

Sisi ambao tumetakaswa kwa ukuhani wa Mungu tunaweza kuleta mabadiliko. Tunapohimili usafi wetu wa kibinafsi na kuheshimu ukuhani wetu, tunakuwa mifano miema kwa wengine kufuata. Mtume Paulo alishauri: “Kuwa kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”3 Aliandika pia kwamba wafuasi wa Kristo wanapaswa wawe “kama mianga katika ulimwengu.”4 Kutoa mfano wa wema kunaweza kutoa mwangaza kwa dunia inayoongezeka kuwa na giza.

Wengi wenu mtamkumbuka Rais N. Eldon Tanner, ambaye alihudumu kama mshauri kwa wanne wa Marais wa Kanisa. Alitoa mfano usiobadilika wa wema kupitia kazi yake katika viwanda, wakati wa huduma katika serikali ya Kanada, na kama Mtume wa Yesu Kristo. Alitupa ushauri wake uliovuviwa: “Hakuna kitakacholeta shangwe zaidi na mafanikio kuliko kuishi kulingana na mafundisho ya injili. Kuwa mfano; kuwa ushawishi wa wema.”

Aliendelea: Kila mmoja wetu amechaguliwa awali kwa ajili ya kazi fulani kama mtumishi wa Mungu aliyechaguliwa ambapo juu yake ameona sawa kumtolea ukuhani na nguvu kutenda katika jina lake. Kumbuka daima kwamba watu wanakutazamia kwa ajili ya uongozi na unashawishi maisha ya watu binafsi aitha kwa wema ama kwa mabaya, ushawishi ambao utahisiwa kwa vizazi vijavyo.”5

Tunaimarishwa na ukweli kwamba nguvu kuu duniani leo ni nguvu ya Mungu inavyotumiwa kupitia wanadamu. Ili kusafiri kwa usalama katika maisha duniani, tunahitaji mwongozo wa Baharia wa Milele---hata Yehova mkuu. Tunafikia, tunainuka, ili kupata usaidizi wa mbinguni.

Mfano unaojulikana vyema kabisa wa mmoja ambaye hakuinuka ni ule wa Kaini, mwana wa Adamu na Hawa. Akiwa na uwezo mkuu lakini mnyonge katika nia, Kaini alikubali uchoyo, wivu, uasi, na hata mauaji kuharibu ule usukani wa kibinafsi ambao ungemwongoza kwa usalama na kuadhimishwa. Kutazama chini kulibadilisha kutazama juu; Kaini alianguka.

Katika wakati mwingine na kupitia mfalme muovu, mtumishi wa Mungu alijaribiwa. Akiwa anasaidiwa na uvuvio wa mbinguni, Danieli, mwana wa Daudi, alimtafsiria mfalme maandishi kwenye ukuta. Kuhusu zawadi aliyoahidiwa---hata nguo ya kifalme, mkufu wa dhahabu, na nguvu ya kisiasa---Danieli alisema, “Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine.”6 Mali na uwezo mkuu ulikuwa utolewa kwa Danieli, zawadi zilizowakilisha mambo ya dunia na si ya Mungu. Danieli alikataa na kubaki mwaminifu.

Baadaye, Danieli alipomwabudu Mungu licha ya amri iliyotangaza hayo kuwa haramu, alitupwa katika tundu la simba. Maelezo ya Biblia yanatuambia kwamba asubuhi iliyofuata, “Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini … Mungu wake.”7 Katika wakati wa haja kubwa, uamuzi wa Danieli kubaki kwenye njia dhahiri ulitoa ulinzi wa kiungu na ulitoa mahali pa usalama. Ulinzi huo na usalama unaweza kuwa wetu tunapoendelea katika njia hiyo dhahiri kuelekea nyumba yetu ya milele.

Saa ya historia, kama mchanga katika shisha, inaonyesha kifungu cha wakati. Watu wapya wanachukuwa nafasi kwenye jukwa la maisha. Matatizo ya siku zetu yanaonekana kutisha mbele yetu. Katika historia yote ya dunia, Shetani amefanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya uangamizi wa wafuasi wa Mwokozi. Tukikubali uvutio wake, sisi---kama meli kuu Bismarck ---tutapoteza huo usukani ambao unaweza kutuongoza hadi kwenye usalama. Badala yake, tukiwa tumezingirwa na vitu vizuri vya maisha ya kisasa, tunatazama mbinguni kwa ajili ya ile hisia isiyokwisha ya mwelekeo, ili kwamba tuweze kuweka na kufuata njia nzuri. Baba yetu wa Mbinguni hatawacha maombi yetu ya dhati bila majibu. Tunapotafuta usaidizi wa mbinguni, usukani wetu, tofauti na ule wa Bismarck, hautashindwa.

Tunaposafiri kwenye safari zetu za kibinafsi, tusafirini kwa usalama bahari za maisha. Tuwe na ujasiri wa Danieli, ili kwamba tuweze kubaki wakweli na waaminifu licha ya dhambi na majaribio yanayotuzingira. Shuhuda zetu ziwe za kina na za nguvu kama zile za Yakobo, kaka ya Nefi, ambaye, alipokabiliwa na mmoja aliyetaka kwa njia zote kuangamiza imani yake, alisema, “Singetetemeshwa”8

Na usukani wa imani ukiongoza njia yetu, ndugu, sisi pia tutapata njia yetu ya usalama nyumbani---nyumbani kwa Mungu, kuishi Naye milele. Hayo yawe hivyo kwa kila mmoja wetu, ninaomba katika jina takatifu la Yesu Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu, amina.