2010–2019
Zaeni, Mkaongezeke, na Muitiishe Nchi
Aprili 2015


Zaeni, Mkaongezeke, na Muitiishe Nchi

Baba wa Mbinguni ametuamuru na kutubariki tuzaane, tuongezeke, na tuituishe nchi ili kwamba tuweze kuwa kama Yeye.

Asanteni, Kwaya Tabernacle, kwa kutukuza kutamu kwa Mwokozi wa ulimwengu.

Katika siku hiyo Mungu Baba alipomuita Mwanawe Mpendwa wa Pekee kumuumba mwanadamu katika mfano Wao na sura Yao, Aliwabariki watoto Wake, akisema, “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale ... kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”1 Hivyo basi, safari yetu duniani ilianza na jukumu la kiungu na baraka. Baba anayetupenda alitupa jukumu na baraka kuzaa na kuongezeka na kutawala ili tuweze kuendelea na kuwa hata kama Yeye alivyo.

Ndugu na dada zangu, jioni ya leo, ninaalika imani na maombi yenu kwa niaba yangu ninaposhiriki nanyi mawazo machache kuhusu sifa tatu za msingi za asili yetu ya kiungu. Ombi langu ni kwamba sote tuweze kutambua kikamilifu zaidi na kutekeleza wajibu wetu mtakatifu –amri ya Baba yetu –kuendeleza asili yetu ya kiungu ili tuweze kuongoza safari yetu kwa mafanikio zaidi na kupokea hatima yetu ya kiungu.

Kwanza, Mungu Alitupa Jukumu la Kuzaa

Sehemu muhimu katika kuzaa matunda ambayo wakati mwingine hupuuzwa ni ile ya kujenga ufalme wa Mungu duniani. Mwokozi alifundisha:

“Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi: akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana: maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. …

“Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.

“Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.”2

Tunazaa matunda tunapokaa katika Kristo na “tunapojichukulia juu [yetu jina Lake] [na] ... kumtumikia hadi mwisho”3 kwa kuwasaidia wengine kuja Kwake.

Katika siku zetu, manabii na mitume walio hai wanaendelea kupaza sauti zao kualika kila mmoja wetu kujishughulisha kikamilifu katika kazi ya wokovu kulingana na uwezo wetu na fursa.

Chanzo cha itiko linalozaa matunda mengi ni kuwa “mnyenyekevu na mpole katika moyo.”4 Ndipo tunaweza kuja kwa Kristo kwa ukamilifu zaidi tukikubali ushawishi wa Roho Mtakatifu na kutii maagano yote tuliyoweka.5 Tunaweza kutafuta na kupokea karama ya hisani na kuwa na nguvu za kualika familia zetu, mababu zetu, na majirani wetu ambao ni waumini wa kanisa na wasio-waumini na marafiki kupokea injili ya Yesu Kristo.

Kufanya kazi katika roho ya hisani si jukumu, ila ni furaha. Matatizo yanakuwa fursa za kujenga imani. Tunakuwa “mashahidi wa [uzuri wa] Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote [tulipo], hata hadi kifo.”6

Sote tunaweza na tunapaswa kushughulika kikamilifu katika kazi ya wokovu. Mwokozi ametupa jukumu lifuatalo na ahadi: “Ni Mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”7

Pili, Mungu Alitupa Jukumu la Kuongezeka

Miili yetu ni baraka kutoka kwa Mungu. Tuliipokea kwa kusudi la kutekeleza kazi ya Baba wa Mbinguni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”8 Mwili ndio njia ambapo tunaweza kupokea uwezo wetu wa kiungu.

Mwili huwawezesha watoto watiifu wa kiroho wa Baba wa Mbinguni kupata uzoefu wa maisha duniani.9Kuzaa watoto kunawapa watoto wengine wa kiroho wa Mungu fursa ya kufurahia pia maisha duniani. Wote waliozaliwa duniani wana fursa ya kuendelea na kuinuliwa wakitii amri za Mungu.

Ndoa kati ya mwanaume na mwanamke ndio ushirika ambao Mungu aliuweka wakfu kwa ajili ya utekelezaji wa jukumu la kuongezeka. Uhusiano wa jinsia moja hauna uwezo wa kuongeza.

Ndoa halali na ya kisheria iliyofungishwa hekaluni na ambapo maagano ya kufunganisha yanaheshimiwa huwapa wazazi na watoto wao fursa ya uzoefu bora zaidi wa upendo na maandalizi ya maisha ya mafanikio. Huwapa mazingira bora ambapo wanaweza kuishi maagano yao waliyofanya na Mungu.

Kwa sababu ya upendo Wake kwetu, Baba wa Mbinguni amewezesha kwamba watoto Wake wote waaminifu ambao hawana ama hawawezi kufurahia baraka za ndoa ya agano na watoto ama ukamilifu wa baraka hizo kwa sababu ambazo si zakujitakia, katika wakati uliopangwa na Bwana, nao pia wafurahie baraka hizi.10

Manabii na mitume walio hai wamewashauri wote ambao wana fursa ya kuingia katika agano la ndoa ya milele kusonga mbele kwa hekima na imani. Hatupaswi kuchelewesha wakati wa siku hiyo takatifu kwa sababu ya shughuli za kidunia ama kuweka matarajio yetu ya mwenzi anayefaa kwa kiwango kinachomwondoa kila mchumba ambaye angetufaa.

Ahadi kwa wote waliounganishwa katika agano la ndoa ya milele na wanaozaa matunda kwa njia ya kutii maagano yao ni kwamba adui kamwe hatakuwa na nguvu ya kuharibu msingi wa uhusiano wao wa milele.

Tatu, Mungu Alituamuru Kudhibiti Dunia

Kuitiisha nchi na kutawala kila kitu kilicho na uhai ni kudhibiti vitu hivi ili vitekeleze mapenzi ya Mungu11 na kutekeleza malengo ya watoto Wake. Kudhibiti kunajumuisha kuidhibiti miili yetu wenyewe.12haijumuishi kuwa waathiriwa wanyonge wa vitu hivi ama kuvitumia kinyume na matakwa ya Mungu.13

Kukuza uwezo wa kuvitiisha vitu vya nchi hunaanza na unyenyekevu wa kutambua upungufu wetu wa kibinadamu na nguvu tunayopata kupitia Kristo na Upatanisho Wake. Kwani “Kristo amesema: Ikiwa mtakuwa na imani ndani yangu mtakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote ambacho ni muhimu kwangu.”14 Nguvu hii inapatikana kwetu tunapochagua kutenda kwa utiifu amri Zake. Tunaongeza uwezo wetu kwa kutafuta kipawa cha Roho na kwa kukuza talanta zetu.

Nilizaliwa na kulelewa katika hali ya umaskini kama ilivyo jambo la kawaida kwa familia nyingi huko Afrika. Nilipata uwezo wa kujiinua kutoka katika hali hizo kwa kutafuta na kupata, na kwa msaada wa wazazi wangu wenye kujali, elimu nzuri. Kuendeleza ono la kwamba mimi ninaweza kuwa nani lilikuwa muhimu kwa maendeleo yangu. Baadaye, kama wenzi wachanga, mke wangu na mimi tulipata injili ya urejesho, inayoendelea kubariki maisha yetu na mwongozo wa kiroho. Kama ilivyo kwa kila familia, sisi tuna majaribu na changamoto zetu. Lakini tunapomtegemea Bwana kwa msaada, tumepata majibu ambayo yamelete amani na faraja, na hatuhisi kushindwa na vitu hivi.

Changamoto zinazokabili jamii ya wanadamu leo, zinajumuisha uovu, ponografia, vita, uchafuzi, matumizi ya madawa ya kulevya, na umaskini, zinazidi kwa sababu wengi duniani wamejisamilisha kwa hiari “kwenye nia ya ibilisi na mwili”15 badala ya mapenzi ya Mungu. “Hawamtakii Bwana kuendeleza kazi zake, bali kila mtu huenda katika njia zake mwenyewe, na akifuata mfano wa mungu wake mwenyewe, ambaye ni mfano wa kitu cha duniani.”16

Hata hivyo, Mungu anawaalika watoto Wake wote kupokea msaada Wake ili kushinda na kustahimili changamoto za maisha haya kwa maneno haya:

“Mimi ndimi Mungu; niliyeufanya ulimwengu, na watu kabla hawajawa katika mwili.

“… Kama utanigeukia, na kuisikiliza sauti yangu, na kuamini, na kutubu uvunjaji sheria wako, na kubatizwa, hata katika maji, katika jina la Mwanangu wa Pekee..., ninyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, mkiomba mambo yote katika jina lake, na lolote mtakaloliomba, mtapewa.”17

Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu wanaoelewa uwezo wao wa kiungu na kutegemea kwa dhati nguvu inayopatikana kupitia Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo wanaimarishwa katika upungufu wao wa asili na “wanaweza kufanya vitu vyote.”18Wanawezeshwa kushinda ushawishi wa uovu ambao umewaweka wengi katika ufungwa kwa adui. Paulo alifundisha kwamba:

“Mungu ni mwaminifu, [na] hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”19

“Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.”20

Baba wa Mbinguni ametuamuru na kutubariki kuzaa matunda, kuongezeka, na kuitiisha nchi ili kwamba tuweze kuwa kama Yeye. Ametoa usaidizi ili sote tuweze, kulingana na uchaguzi wetu binafsi, kuwa kama Yeye alivyo. Ni ombi langu kwamba sote tuweze kuishi maisha yetu tukiongozwa na ono la asili yetu ya kiungu, tukililia baraka zetu zote za kiungu, na kufikia hatima yetu ya kiungu.

Ninashuhudia kwamba Mungu Baba na Mwanawe Mpendwa, Mwokozi wetu Yesu Kristo, kweli wanaishi; ukweli juu ya mpango Wao mtukufu wa furaha; na juu ya funguo ambazo zimeshikiliwa na nabii aliye hai duniani leo, hata Thomas S. Monson. Ni ombi langu kwamba tuweze kuwa na nguvu za kufurahia utimilifu wa baraka Zake katika jina la Yesu Kristo, amina.