2010–2019
Baraka za Hekalu
Aprili 2015


Baraka za Hekalu

Tunapohudhuria hekalu, kunakuja kwetu kipimo cha kiroho na hisia za amani.

Ndugu na dada zangu wapendwa, nina furaha jinsi gani kuwa pamoja nanyi asubuhi hii nzuri ya Pasaka, wakati ambao mawazo yetu yanamgeukia Mwokozi wa Ulimwengu. Ninatoa upendo wangu na salamu kwa kila mmoja wenu na ninaomba Baba yetu wa Mbinguni ayafunue maneno yangu.

Mkutano huu unaadhimisha miaka saba tangu niliposimikwa kuwa Rais wa Kanisa. Imekuwa miaka ya shughuli nyingi, ambayo hazikuwa na changamoto tu bali pia na baraka tele. Mojawapo ya baraka hizi za kuvutia na takatifu zilikuwa ni fursa niliyopata kuweka wakfu mahekalu mapya na ya zamani.

Hivi majuzi zaidi, Novemba iliyopita ilikuwa ni nafasi yangu kuliweka wakfu Hekalu jipya nzuri la Phoenix Arizona. Niliambatana na Rais Dieter F. Uchtdorf, Mzee Dallin H. Oaks, Mzee Richard J. Maynes, Mzee Lynn G. Robbins, na Mzee Kent F. Richards. Jioni kabla ya kuweka wakfu, sherehe nzuri za kitamaduni zilikuwa zikifanyika ambapo zaidi vijana 4,000 wa Kanisa kutoka katika wilaya ambayo hekalu lipo walicheza. Siku iliyofuata hekalu likawekwa wakfu katika vipindi vitatu vitakatifu vya kutia moyo.

Ujenzi wa mahekalu ni ishara tosha ya kukua kwa Kanisa. Hadi sasa tuna mahekalu 144 yanayofanya kazi duniani kote, 5 kati ya hayo yakiwa yanafanyiwa ukarabati na 13 mengine yanajengwa. Zaidi ya hayo, mahekalu mengine 13 ambayo yalitangazwa hapo awali yapo katika ngazi tofauti za maandalizi kabla ujenzi kuanza. Mwaka huu tunatarajia kuyaweka tena wakfu mahekalu mawili na kuweka wakfu mahekalu mapya matano ambayo yamepangiwa kukamilishwa.

Katika maika miwili iliyopita, tulivyokuwa tunazingatia juhudi zetu katika kukamilisha mahekalu yaliyotangazwa mapema, tumekuwa tumesitisha mipango kwa mahekalu zaidi. Asubuhi hii, hata hivyo, ninafurahia kutangaza mahekalu matatu mpya ambayo yatajengwa katika maeneo yafuatayo: Abidjan, Ivory Coast; Port-au-Prince, Haiti: na Bangkok, Thailand. Ni baraka za ajabu jinsi gani zinazowasubiri waumini wetu wengi katika maeneo haya na, pale mahekalu yalipo kote ulimwenguni.

Mchakato wa kutathmini haja na kutafuta maeneo kwa ajili ya mahekalu mengine unaendelea, kwani tunatamani kwamba waumini wengi iwezekanavyo wawe na nafasi ya kuhudhuria hekalu bila ya dhabihu kubwa ya muda na fedha. Kama tulivyofanya hapo kale, tutawataarifuni pale uamuzi utakapotolewa juu ya swala hili.

Ninapofikiria kuhusu mahekalu, mawazo yangu yanageukia kwenye baraka nyingi tunazozipata ndani yake. Tunapoingia kupitia milango ya hekalu, tunaacha nyuma mashaka na ghasia za ulimwengu. Ndani ya hekalu hili takatifu, tunapata uzuri na mpangilio. Kuna sehemu ya kupumzika kwa ajili ya nafsi zetu na pumziko dhidi ya maisha yetu.

Tunapohudhuria hekalu, panaweza kutokea kwetu mwelekeo wa kiroho na hisia za amani ambayo itashinda hisia nyingine ambazo zinaweza kuja katika moyo wa mwanadamu. Tutaelewa maana sahihi ya maneno ya Mwokozi pale Aliposema: “Nawaachieni amani, nawapeni amani yangu….Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.”1

Amani ya aina hiyo inaweza kuwa kwa kila moyo yote---mioyo ambayo inasumbuka, mioyo inayosumbuliwa na huzuni, mioyo yenye mchafuko, mioyo inayoomba msaada.

Hivi majuzi nilijifunza mwenyewe juu ya kijana aliyekwenda hekaluni na moyo uliokuwa ukiomba msaada. Miezi mingi hapo awali alipata wito wake wa kutumikia misheni huko Amerika ya Kusini. Hata hivyo, visa yake ilicheweshwa kwa kipindi kirefu hata akabadilishiwa wito kwenda kwenye misheni ya Marekani. Ijapokuwa alivunjika moyo kwa kutotumikia katika eneo lake la awali, pamoja na hivyo alifanyakazi kwa bidii kwenye uteuzi wake mpya, alijitolea kutumikia kwa kadiri ya uwezo wake. Akakatishwa tamaa, hata hivyo, kwa sababu ya uzoefu aliopata kwa wamisionari walioonekana kupenda kuwa na wakati mzuri kuliko kushiriki injili.

Miezi michache baadaye kijana huyu alikumbwa na changamoto mbaya ya kiafya ambayo ilimwacha akiwa amepooza upande, na hivyo akarudishwa nyumbani kwa likizo ya matibabu.

Miezi kadhaa baadaye kijana yule alipona kabisa, na kupooza kulitoweka. Aliarifiwa kwamba kwa mara nyingine tena angeweza kutumikia kama misionari, baraka ambayo alikuwa akiiomba kila siku. Kilichokuwa cha kuvunja moyo tu ni kwamba alitakiwa kurudi kwenye misheni ile ile aliyokuwepo awali, ambako alihisi tabia na mtazamo wa baadhi ya wamisionari hazikuwa nzuri kama walivyotarajiwa.

Alikuwa amekuja hekaluni ili kutafuta ufariji na uhakikisho kwamba angeweza kuwa na wakati mzuri kama mmisionari. Wazazi wake pia walisali ili safari hii ya hekalu iweze kutoa msaada ambao mwana wao alikuwa akiuhitaji.

Wakati kijana alipoingia katika chumba cha selestia baada ya kipindi, alikaa kwenye kiti na akaanza kusali kwa ajili ya mwongozo kutoka kwa Baba yake wa Mbinguni.

Mwingine aliyeingia chumba cha selestia muda mchache baadaye alikuwa kijana aliyeitwa Landon. Alipoingia kwenye chumba, mara moja akamwona kijana amekaa kwenye kiti, akiwa amefumba macho na akiomba. Landon alipokea mwongozo dhahiri kuwa alipaswa kuongea na yule kijana. Hakutaka kukatiza sala yake, hata hivyo, aliamua kusubiri. Baada ya dakika kadhaa kupita na kijana akiendelea kusali, Landon alijua asingeweza kuahirisha mwongozo wake. Alimjia kijana na kwa upole akamgusa bega lake. Kijana akafumbua macho yake, alishtuka kuona kwamba alibughudhiwa. Landon alisema kwa upole, “Nimehisi ushawishi kwamba nahitaji kuongea na wewe, ijapokuwa sijui ni kwa nini.”

Walipoanza kuongea, kijana alieleza yote ya moyoni mwake kwa Landon, alielezea hali yake na kumalizia na matamanio yake ya kupata ufariji na kutiwa moyo juu ya misheni yake. Landon, aliyerudi toka kwenye misheni yenye mafanikio mwaka mmoja nyuma, alielezea juu ya uzoefu wa misheni yake mwenyewe, changamoto na matatizo aliyokumbana nayo, njia ambayo aliitumia kumgeukia Bwana kwa msaada, na baraka alizozipata. Maneno yake yalikuwa ya ufariji na uhakikisho, na furaha yake ya kutumikia misheni ikamgusa kijana. Hatimaye, wakati woga ulipomwondoka, mawazo ya amani yakamjia kijana yule. Alijawa na shukrani wakati alipogundua sala yake ilikuwa imejibiwa.

Vijana wale wawili walisali kwa pamoja, na kisha Landon alijiandaa kuondoka, akifurahi kwa kufuata mwongozo ambao ulikuja kwake. Aliposimama kuondoka, kijana alimwuliza Landon, “Wewe ulitumikia wapi misheni yako?” Kwa wakati huu, hakuna hata mmoja kati yao aliyetaja kwa mwenzake jina la misheni ambayo alitumikia. Wakati Landon alipojibu kwa kutaja jina la misheni yake, machozi yalijaa kwenye macho ya yule kijana. Landon alikuwa ametumikia katika misheni ile ile ambayo kijana ilibidi arudi kutumikia!

Katika barua ya hivi karibuni kwangu, Landon alishiriki nami maneno ambayo kijana aliyasema kwake: “Nilikuwa na imani Baba wa Mbinguni angenibariki, lakini sikuweza kufikiri kwamba angemtuma mtu kuja kunisaidia mimi mtu ambaye ametumikia kwenye misheni yangu mwenyewe. Sasa ninajua kila kitu kitakuwa sawa.”2 Sala ya unyenyekevu ya moyo wa kweli imesikika na kujibiwa.

Ndugu na dada zangu, katika maisha yetu tutakuwa na majaribio; tutakuwa na majaribu na changamoto. Tunapokwenda hekaluni, tunapokumbuka maagano tunayoyaweka kule, tutaweza kushinda hayo majaribu na kuvumilia majaribu yetu. Katika hekalu tunaweza kupata amani.

Baraka za hekalu zina thamani. Moja ya baraka ninayoshukuru kwa sababu yake kila siku ya maisha yangu ni ile ambayo mke wangu mpendwa, Frances, na mimi niliipokea wakati tulikuwa tumepiga magoti katika madhabahu matakatifu na kuweka maagano yaliyotuunganisha pamoja kwa milele yote. Hakuna baraka yenye thamani kwangu zaidi ya amani na ufariji ninaoupata kwamba yeye na mimi tutakuwa pamoja milele.

Naomba Baba yetu wa Mbinguni atubariki ili tuweze kuwa na roho wa kuabudu hekaluni, ili tuweze kuwa watiifu katika amri Zake, na kwamba tuweze kufuata kwa uangalifu hatua za Bwana na Mwokozi, Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba Yeye ni Mkombozi wetu. Yeye ni Mwana wa Mungu. Yeye ndiye aliyekuja kutoka kaburini siku ile ya kwanza ya Pasaka, akileta pamoja naye zawadi ya uzima wa milele kwa watoto wote wa Mungu. Katika siku hii nzuri, tunaposherehekea tukio muhimu, naomba tusali kwa shukrani kwa ajili ya zawadi yake nzuri na ya ajabu kwetu. Ili iwe hivyo, ninaomba katika jina Lake takatifu, amina.

Muhtasari

  1. Yohna 14:27.

  2. Mawasiliano yaliyo katika umiliko wa Thomas S. Monson.