2010–2019
Chagua Kuamini
Aprili 2015


Chagua Kuamini

Mwokozi hutoa injili Yake kama nuru ya kuongoza wale ambao wamechagua kumwamini.

Januari iliyopita, Sailor Gutzler mwenye umri wa miaka saba na familia yake walikuwa wanasafiri kutoka Florida kuelekea Illinios katika ndege ya kibinafsi. Babake Sailor alikuwa anaiendesha ndege. Punde baada ya giza kufika, ndege ilipata shida za kimekaniki na kuanguka katika milima iliyojaa giza ya Kentucky, upande wa juu ukiwa chini katika upeo wenye kuparuza. Watu wote walikufa katika ajali hii isipokuwa Sailor. Kifundo chake kilivunjika katika ajali. Alipata majeraha ya kukatwakatwa, kugwaruzwagwaruzwa na alikuwa amepoteza viatu vyake. Halijoto ilikuwa digrii 38 Farenhaiti (digrii 3 Selisiasi) Ilikuwa usiku baridi, kulikuwa kunanyesha Kentucky na Sailor alikuwa amevaa kaptula tu, shati, na soksi moja.

Aliwaita wazazi wake, lakini hakuna aliyemjibu. Akitumia ujasiri wote aliokuwa nao, alitembea kwa mguu bila viatu kupitia mashambani akitafuta usaidizi, akipitia vijito, akivuka mashimo, na akipita vikwazo vya mitemba ya bluberi. Kutoka upeo wa kilima kimoja kidogo, Sailor aliona nuru kwa umbali, karibu umbali wa maili moja. Akiangukaanguka katika giza na miti kuelekea kwenye nuru, hatimaye alifika kwenye nyumba ya mtu mkarimu ambaye kamwe hajawahi kutana naye aliyeharakisha kumsaidia. Sailor alikuwa salama. Punde alipelekwa hospitalini na akasaidiwa hata akapona.1

Sailor aliendelea kuishi kwa sababu aliona nuru kwa umbali na kjitahidi kuifikia---bila kujali mashamba pori, kina cha janga alilopitia, na majeraha aliyokuwa amepata. Ni vingumu kufikiria jinsi Sailor alichoweza kufanya usiku huo. Lakini kile tunajua ni kwamba alitambua kuwa katika nuru ya nyumba iliyokuwa mbali kuilikuwa na nafasi ya kuokolewa. Kulikuwa na tumaini. Alifanya kwa ukweli kwamba bila kujali jinsi mambo yalikuwa mabaya, angeokolewa katika nuru hiyo.

Wachache wetu watawahi kupitia matukio ya dhiki kama ile ya Sailor. Lakini kila mmoja wetu atalazimika, wakati moja au mwingine, kupitia majanga yetu ya kiroho na kupitia safari zetu ngumu za kihisia. Katika nyakati hizo, bila kujali jinsi zipo na giza na kutokuwa na tumaini, tukiitafuta, daima kutakuwa na nuru ya kiroho inayotuita, ikitupa tumaini ya kuokolewa na kusaidiwa. Nuru hiyo inang’aa kutoka kwa Mwokozi wa binadamu wote, ambaye ni Nuru ya Ulimwengu.

Kutambua nuru ya kiroho ni tofauti na kuona nuru ya kimwili. Kutambua nuru ya kiroho ya Mwokozi huaanza na utayari wetu wa kuamini. Mungu anataka mwanzoni tutamani angalau kuamini. “Ikiwa mtaamka na kuziwasha akili zenu ... na kutumia chembe ya imani” nabii Alma anafundisha, “ndio, hata ikiwa hamwezi ila kutamani kuamini, acha hamu hiyo ifanye kazi ndani yenu, hata mpaka muamini kwa njia ambayo mtatoa nafasi kwa sehemu ya maneno ya [Mwokozi].”2

Wito wa Alma kwetu kutamani kuamini na “kutoa nafasi” katika mioyo yetu kwa maneno ya Mwokozi unatukumbusha kwamba sadiki na imani inahitaji uchaguzi wetu wa kibinafsi na vitendo. Lazima “tuamke na kuziwasha akili [zetu].” Tunaomba kabla tupewe; tunatafuta kabla tupate; tunabisha kabla tufunguliwe. Tunapewa ahadi hii: “Kwani kila mmoja ambaye huuliza, hupata; na yule anayetafuta, huvumbua; na yule ambaye hubisha, hufunguliwa.”3

Hakuna ombi la dhati kwetu kuamini limekuja kuliko kutoka kwa Mwokozi Mwenyewe, wakati wa huduma yake duniani alipowasihi wasikilizaji Wake wasioamini:

“Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini.

“Lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziamini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.”4

Kila siku kila mmoja wetu hukumbana na jaribio. Ni jaribio la maisha: je tutachagua kumwamini Yeye na kuruhusu nuru ya injili Yake kuwa ndani yetu, ama tutakataa kuamini na kung’ang’ana na kusafiri peke yetu gizani? Mwokozi hutoa injili yake kama nuru ya kuwaongoza wale wanaochagua kuamini na kumfuata Yeye.

Baada ya ajali, Sailor alikuwa na uchaguzi. Angechagua kubaki kando ya ndege gizani, peke yake na akiwa na uoga. Lakini kulikuwa na usiku mrefu mbele, na kungezidi tu kuwa baridi. Alichagua njia nyingine. Sailor alipanda juu ya mlima na hapo akaweza kuona mwangaza katika upeo wa macho yake.

Pole pole, alipokuwa akitembea usiku kuelekea kwenye nuru, nuru ilizidi kung’aa. Bado, lazima kuwe kulikuwa na nyakati ambazo hakuweza kuiona. Pengine hakuweza kuiona alipokuwa katika korongo ama nyuma ya miti ama vichaka, lakini aliendelea mbele. Wakati wowote aliweza kuona nuru, alikuwa na ushahidi kwamba alikuwa kwenye njia sawa. Hakujua kwa uhakika nuru ile ilikuwa nini, lakini aliendelea kutembea kuifikia kulingana na kile alichojua akitumaini na kuamini angeiona tena kama angeendelea kusonga katika mwelekeo sahili. Kwa kufanya hivyo, huenda angeokoa maisha yake.

Maisha yetu yanaweza kuwa hivyo pia. Huenda kukawa na nyakati ambazo tumeumia, wakati tumejaribiwa, na wakati maisha yetu yanaonekana kuwa na giza na baridi. Huenda kukawa na nyakati ambazo hatuwezi kuona nuru yoyote kwenye upeo wa macho, na huenda tukajihisi kukata tamaa. Ikiwa tuko tayari kuamini, ikiwa tunatamani kuamini, tukichagua kuamini, basi mafundisho ya Mwokozi na mfano utatuonyesha njia ya kwenda.

Chagua Kuamini

Kama vile Sailor alivyohitaji kuamini kwamba angepata usalama katika nuru hiyo iliyo mbali, ndivyo lazima tuchague kufungua mioyo yetu kwa ajili ya ukweli mtukufu wa Mwokozi na nuru Yake ya milele na huruma Wake wa uponyaji. Manabii wa karne zote wametuhimiza na hata kutuomba tuamini katika Kristo. Mafunzo yao yana msingi katika ukweli wa msingi: Mungu hatulazimishi kuamini. Badala yake Yeye hutualika kuamini kwa kuwatuma manabii walio hai na mitume kutufundisha, akitoa maandiko, na kwa kutuita kupitia Roho Yake. Sisi ndio tunaohitaji kuchagua kukubali mualiko huo wa kiroho, tukichagua kuona na macho ya kiroho, nuru ya kiroho ambayo anatumia kutuita. Uamuzi wa kuamini ni chaguo la muhimu zaidi tunalofanya. Unaadhiri maamuzi yetu yote mengine.

Mungu hatulazimishi kuamini zaidi hata ya vile anatulazimisha kutii amri yoyote, licha ya nia Yake kamilifu ya kutubariki. Lakini bado wito wake kwetu kumwamini Yeye kutumia hiyo chembe ya imani na kutoa nafasi kwa maneno Yake hubaki kwetu hata leo. Kama vile Mwokozi alivyosema, “Ninashuhudia kwamba Baba huamuru watu wote, kila mahali, kutubu na kuniamini.”5

Kusadiki, ushuhuda na imani si kanuni zisizo na vitendo. Hazitendeki kwetu tu. Kusadiki ni kitu tunachochagua tunakitumaini, tunakifanyia kazi, na tunajitolea kwa ajili yake. Hatuta kuja kuamini kwa bahati katika Mwokozi na injili Yake zaidi ya vile tutakavyoomba ama kulipa zaka kwa bahati. Tunachagua kusadiki kwa vitendo, kama vile tunapochagua kutii amri zingine.

Weka Imani katika Vitendo

Sailor hangejua kwa mara ya kwanza kama kile alichokuwa anakifanya alipokuwa akiendelea mbele vichakani kingefaulu. Alikuwa amepotea na kujeruhiwa; kulikuwa na giza na baridi. Lakini aliondoka mahali pa ajali na kwenda nje katika tumaini ya kuokolewa, akigaagaa na kutambaa kwenda mbele hadi alipoona nuru kwa umbali. Mara tu alipokuwa ameiona, alifanya awezavyo kuisogelea, akikumbuka kile alichokuwa amekiona.

Sisi vile vile lazima tutoe nafasi kwa ajili ya tumaini kwamba tutapata nuru ya kiroho kwa kukumbatia imani kuliko kuchagua kuwa na mashaka. Vitendo vyetu ndivyo ushahidi wa imani yetu na vinakuwa kiini cha imani yetu. Tunachagua kuamini tunaposali. Tunachagua kuamini tunaposoma maandiko. Tunachagua kuamini tunapofunga, tunapoitakasa Sabato, tunapoabudu hekaluni, na tunaposoma maandiko. Tunachagua kuamini tunapobatizwa na tunapokula sakramenti.Tunachagua kuamini pale tunapotubu na kutafuta msamaha wa kiungu na upendo wa uponyaji.

Katu Usikate Tamaa

Wakati mwingine maendeleo katika mambo ya kiroho yanaweza kuonekana kuwa polepole ama bila mfuatano. Wakati mwingine huenda tukahisi tumepoteza msimamo na kwamba jitihada zetu bora za kumtafuta Mwokozi hazifanyi kazi. Kama unahisi hivi, tafadhali usikate tamaa kamwe. Endelea mbele na kumwamini Yeye, injili Yake na Kanisa Lake. Linganisha matendo yako na imani yako. Katika nyakati hizo ambapo nuru ya imani yenu imepunguka acha tumaini lako kwa upendo na neema ya Mwokozi, vipatikanavyo katika injili Yake, na Kanisa Lake viyashinde mashaka yako. Ninakuahidi kuwa Yeye amesimama tayari kukupokea. Baada ya muda utakuja kuona kwamba umefanya uchaguzi bora ambao hukutegemea. Uamuzi wako wa ujasiri wa kumwamini Yeye utakubariki bila kipimo na milele yote.”

Baraka za Kusadiki

Nimesikia upendo wa huruma wa Mwokozi katika maisha yangu. Nimemtafuta Yeye katika nyakati zangu za giza naye amenifikia kwa nuru yake iponyayo. Moja katika furaha kubwa katika maisha yangu imekuwa ni kusafiri pamoja na mke wangu Kathy kukutana na waumini wa Kanisa hili katika kona nyingi za dunia. Kukutana huku kwa kupendeza kumenifundisha juu ya upendo wa Mungu kwetu sisi. Wamenionyesha uwezekano usio na kikomo wa furaha ambayo huja kuwa baraka kwa wale wote wanao chagua kufuata mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Nimejifunza kwamba kumwamini Yeye na katika nguvu Zake za ukombozi ndiyo njia ya kweli kuelekea kwenye “amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao.”6

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye chanzo cha nuru na tumaini kwetu sote. Ninaomba kwamba sote tuweze kuchagua kumwamini. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhktasari

  1. Ona Lindsey Bever, “How 7-Year-Old Sailor Gutzler Survived a Plane Crash,” Washington Post, Jan. 5, 2015, washingtonpost.com; “Girl Who Survived Plane Crash Hoped Family ‘Was Just Sleeping,’” Jan. 4, 2015, myfox8.com; “Kentucky Plane Crash: Four Killed, Little Girl Survives,” Jan. 4, 2015, news.com.au; Associated Press, “Young Girl, Sole Survivor of Kentucky Plane Crash,” Jan. 3, 2015, jems.com.

  2. Alma 32:27; himizo imeongezwa.

  3. 3 Nefi 14:8; ona pia mstari wa 7.

  4. Yohana 10:37–38.

  5. 3 Nefi 11:32.

  6. Mafundisho na Maagano 59:23.