2010–2019
Kurejea kwenye Imani
Aprili 2015


Kurejea kwenye Imani

Kila mmoja wetu anaweza kuimarisha imani yetu katika Yesu Kristo katika safari yetu binafsi na kupata furaha.

Katika asubuhi hii ya Pasaka, Rais Monson, tunashukuru sana kusikia sauti ya nabii wetu anayeishi. Tunathamini maneno yako, ikijumuisha ushauri wako: “Tafuta furaha katika safari”1 na “Siku zako za usoni zitang’ara kama imani yako.”2

Mwaka huu watoto wa Msingi wanashiriki nasi furaha na uangavu wa imani yao katika Yesu Kristo wanapoimba wimbo “I Know That My Savior Loves Me.” Wanaimba ukweli: “Najua anaishi! … Moyo wangu ninampa Yeye.”3 Kama watoto wa Msingi, kila mmoja wetu anaweza kuimarisha imani katika Yesu Kristo katika safari yetu binafsi na kupata furaha.

Katika mkutano wa Muungano wa Usaidizi wa kina Mama hivi majuzi nilimsikiliza mama kijana akishiriki nasi safari yake ya uongofu. Alikuwa amekulia katika Kanisa akiwa na wazazi ambao walimfundisha injili. Alihudhuria madarasa ya Msingi, Wasichana, na seminari. Alipenda kujifunza na kugundua ukweli. Jitihada zake za mara kwa mara zilikuwa ni kujua kwa nini.Mzee Russell M. Nelson amesema, “Bwana anaweza kuifundisha tu akili inayouliza.”4 Na msichana huyu alikuwa anafundishika.

Baada ya shule ya upili alihudhuria chuo kikuu, akaunganishwa hekaluni na mmisionari aliyerejea kutoka misheni, na akabarikiwa kupata watoto warembo.

Kwa roho ya kuuliza, mama huyu aliendelea kuuliza maswali. Lakini maswali yalivyokuwa magumu, na ndivyo majibu yalivyokuwa. Na wakati mwingine hakukuwa na majibu—au hakukuwa na majibu ambayo yalileta amani. Mwishowe kadiri alivyojitahidi kupata majibu, maswali zaidi na zaidi yaliibuka na akaanza kutilia shaka baadhi ya misingi halisi ya imani yake.

Wakati huu wa kuchanganyikiwa, baadhi ya waliokuwa wanamzunguka walisema, “Wewe egemea kwenye imani yangu,” lakini akafikiria, “Siwezi. Hamuelewi; hamuhusiki na mambo haya.” Alielezea, “Nilikuwa radhi kuwastahi wale wenye shaka, kama wangenistahi.” Na wengi walifanya hivyo.

Alisema, “Wazazi wangu walijua moyo wangu na kuniachia nafasi. Walichagua kunipenda wakati nikijaribu kutafuta majibu mimi mwenyewe.” Hivyo hivyo, askofu wa huyu mama kijana mara kadhaa alikutana naye na kuzungumzia ujasiri aliokuwa nao.

Waumini wa kata vile vile hawakusita kutoa upendo, na akajiona mwenye kuhusishwa. Kata yake haikuwa sehemu ya watu wenye kujifanya wakamilifu, ilikuwa sehemu ya kuleana.

“Ilikuwa inafurahisha,” alikumbuka. “Wakati huu nilihisi uhusiano mzito na wa kweli na kina bibi na babu zangu ambao walikuwa wamekwisha fariki. Walikuwa wananitia moyo na kuniomba niendelee kujaribu. Nilihisi walikuwa wananiambia, ‘Zingatia katika kile unachokijua.”

Licha ya kundi kubwa la watu waliokuwa wanamtia moyo, akageuka kuwa hahudhurii kikamilifu. Alisema, “Sikujitenga kutoka kanisani kwa sababu ya tabia mbaya, kutokujali vitu vya kiroho, kutafuta sababu za kutoishi amri, au kutafuta njia rahisi ya kuundoka. Nilihisi nahitaji jibu kwa swali ‘Ni nini hasa ninachoamini?’”

Katika kipindi hiki alisoma kitabu cha maandishi ya Mama Teresa, ambaye alikuwa ametoa hisia kama hizo. Katika barua ya mwaka 1953, Mama Teresa aliandika: “Tafadhali niombeeni haswa mimi nisiharibu kazi Yake na kwamba Bwana Wetu ajioneshe Mwenyewe—kwani kuna kiza kinene ndani yangu, kama vile kila kitu kimekufa. Imekuwa hivi kwa kiwango kinachotofautiana kutoka nilipoanza ‘kazi.’ Mwombeni Bwana Wetu anipe mimi ujasiri.”

Askofu Mkuu Périer alijibu: “Mungu akuongoze, Mama mpendwa; hauko sana kizani kama unavyofikiri. Njia inayotakiwa kufuatwa haiwezi kuwa safi mara moja. Omba kwa ajili ya mwanga, usiamue kwa haraka, wasikilize wengine wanasemaje, fikiria sababu zao. Utapata tu kitu cha kukusaidia. … Ukiongozwa kwa imani, maombi na kwa sababu kukiwa na dhumuni sahihi unavyo vya kutosha.”5

Rafiki yangu alifikiria kama Mama Teresa aliweza kuishi dini yake bila majibu yote na bila hisia sahihi ya kila kitu, labda naye angekuwa hivyo pia. Angeweza kupiga hatua rahisi moja mbele kwa imani—na kisha nyingine. Angeweza kuzingatia kweli ambazo aliziamini na kuacha kweli hizo kuijaza akili na moyo wake.

Alipofikiria huko nyuma, alisema, “Ushuhuda wangu umekuwa kama rundo la majivu. Ulikuwa wote umeungua. Kitu pekee kilichokuwa kimebaki ilikuwa ni Yesu Kristo.” Aliendelea, “Lakini Yeye hakuachi wakati una maswali. Wakati mtu yeyote anapojaribu kutii amri, mlango umefunguliwa wazi kabisa. Maombi na kujifunza maandiko inakuwa na umuhimu mkubwa kiajabu.

Hatua yake ya kwanza katika kujenga imani yake ilikuwa ni kuanza na kweli za msingi za injili. Alinunua kitabu cha nyimbo cha watoto na kuanza kusoma maneno ya nyimbo. Yalikuwa ni ya thamani kwake. Aliomba kwa ajili ya imani ili kuinua uzito aliouhisi.

Aligundua kwamba alipokutana na kauli iliyomsababishia kutia shaka, angeacha, akaangalia picha kamili, na kuifanya injili kuwa yake binafsi.” Alisema, “Ningeuliza, Je hii ni njia sahihi kwangu na familia yangu?’ Wakati mwingine ningejiuliza, ‘Ninataka nini kwa ajili ya wanangu?’ Ninagundua ninawataka wawe na ndoa za hekaluni. Hapo ndio kuamini kukarudi katika moyo wangu.’”

Mzee Jeffrey R. Holland alisema, “Unyenyekevu, imani, na ushawishi wa Roho Mtakatifu daima [itakuwa] vipengele katika kila jitihada ya kutafuta ukweli.”6

Ingawa alikuwa na maswali kuhusu jinsi gani Kitabu cha Mormoni kilikuja, hakuweza kukana kweli alizojua kutoka katika Kitabu cha Mormoni. Alikuwa amelenga katika kujifunza Agano Jipya ili kumwelewa Mwokozi vyema. “Lakini mwishowe,” alisema, “Nilijikuta nimerudi tena katika Kitabu cha Mormoni kwa sababu nilipenda nilichojisikia wakati ninasoma kuhusu Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

Alihitimisha, “Unatakiwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe wa kiroho katika kweli zilizopo katika kitabu hicho,” na alikuwa anazipata. Alielezea, “Nilisoma katika Mosia na kuhisi kuongozwa kabisa. ‘Mwamini Mungu; amini kwamba yupo, na kwamba aliumba vitu vyote … ; amini kwamba ana hekima yote na uwezo wote, mbinguni na ardhini; mwanini kwamba mwanadamu hafahamu vitu vyote ambavyo Bwana anavyoweza kufahamu.’7

Katika wakati huu wito ulikuja ili kutumikia kama mpiga kinanda wa Msingi. “Ilikuwa ni salama.” Alisema. “Nilitaka kuwa na watoto wangu kwenye kipindi cha Msingi, na sasa niliweza kuwa nao. Na nilikuwa bado sijakuwa tayari kufundisha.” Alipotumikia, aliendelea kujionea mwenyewe kutoka kwa wale waliomzunguka: “Njoo, tunakutaka bila kujali uko katika kiwango gani, na tutakutana nawe pale. Tupe chochote unachoweza kutupa.”

Akipiga kinanda nyimbo za Msingi, mara nyingi alikuwa akifikiria mwenyewe: “Hapa kuna kweli ninazipenda. Bado ninaweza kutoa ushuhuda. Ninaweza kusema mambo haya ambayo ninayajua na kuyaamini. Inawezekana isiwe matoleo kamilifu, lakini itakuwa ni matoleo yangu. Kile ninachokizingatia kinapanuka ndani yangu. Ni vizuri kurudia kanuni za msingi za injili na kuhisi uwazi.

Katika Jumapili hiyo asubuhi, nilipokuwa namsikiliza dada huyo kijana akishiriki nasi hadithi ya safari yake, nilikumbushwa kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu ambapo lazima tujenge msingi wetu.8 Nilikumbushwa pia juu ya ushauri wa Mzee Jeffrey R. Holland: “Shikilia sana kile ambacho tayari unakijua na simama imara mpaka ufahamu wa ziada utakapokuja.”9

Wakati wa somo lake, nilijikuta najua zaidi kwamba majibu katika maswali yetu ya dhati yanakuja pale tunapotafuta kwa bidii na tunapoishi amri. Nilikumbushwa kwamba imani yetu inaweza kufika mbali zaidi ya vikomo vya sababu za sasa.

Na, ee, jinsi gani nataka kuwa kama wale waliomzunguka mama huyu kijana, wakimpenda na kumpa msaada. Kama Rais Dieter F. Uchtdorf alivyosema: “Sisi sote ni mahujaji tukitafuta nuru ya Mungu tunaposafiri katika njia ya ufuasi. Hatushtumu wengine kwa ajili ya kiasi cha nuru ambayo wanaweza kuwa nayo au wasiwe nayo; bali, tunalea na kutia moyo nuru zote mpaka zitakapoonekana wazi, angavu na kweli.”10

Wakati watoto wa Msingi wanapoimba “Sala ya Mtoto,” wanamwomba: “Baba wa Mbinguni, je kweli upo? Na je unasikia na kujibu sala ya kila mtoto?”11

Na sisi pia tunaweza kushangaa, “Je! Baba wa Mbinguni kweli yupo?” kufurahia tu—kama rafiki yangu alivyofurahia—wakati majibu yalipomjia kimya kimya, na uhakika sahihi. Ninashuhudia hakiki hizo rahisi zinatoka kama mapenzi yake yanavyokuwa yetu. Ninashuhudia kwamba ukweli upo duniani leo hii na injili yake inapatikana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Thomas S. Monson, “Finding Joy in the Journey,” Ensign au Liahona, Nov. 2008, 85.

  2. Thomas S. Monson, “Be of Good Cheer,” Ensign au Liahona, May 2009, 92.

  3. “I Know That My Savior Loves Me,” katika I Know My Savior Lives: 2015 Outline for Sharing Time (2014), 29.

  4. Russell M. Nelson, in M. Russell Ballard, “What Came from Kirtland” (Brigham Young University fireside, Nov. 6, 1994); speeches.byu.edu.

  5. In Mother Teresa: Come Be My Light; The Private Writings of the Saint of Calcutta, ed. Brian Kolodiejchuk (2007), 149–50; vituo vya maandishi vimesanifishwa.

  6. Jeffrey R. Holland, “Be Not Afraid, Only Believe” (evening with Elder Jeffrey R. Holland, Feb. 6, 2015); lds.org/broadcasts.

  7. Mosia 4:9.

  8. Ona Helamani 5:12.

  9. Jeffrey R. Holland, “Lord, I Believe,” Ensign au Liahona, May 2013, 94.

  10. Dieter F. Uchtdorf, “Receiving a Testimony of Light and Truth,” Ensign au Liahona, Nov. 2014, 22.

  11. “A Child’s Prayer,” Children’s Songbook, 12.