2010–2019
Mithali ya Mpanzi
Aprili 2015


Mithali ya Mpanzi

Ni juu ya kila mmoja wetu kuweka vipaumbele na kufanya vitu ambavyo vitarutubisha udongo wetu na kufanya mavuno yetu kuwa mengi.

Mada za hotuba za mkutano mkuu hupangwa---siyo kwa mamlaka ya binadamu bali kwa misukumo ya Roho. Mada nyingi hupendekezwa na masuala ya binadamu tunayoshiriki sote. Lakini kwa vile Yesu hakufundisha jinsi ya kushinda changamoto za kibinadamu au udhalimu wa kisiasa wa siku Zake, Yeye kwa kawaida huwafunulia watumishi Wake kuongea kuhusu kile wafuasi Wake wanaweza kufanya ili kurekebisha maisha yetu binafsi kujitayarisha kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Ninahisi msukumo wa kuongea kuhusu mafundisho yenye thamani na ya milele katika mojawapo ya mithali za Yesu.

Mithali ya mpanzi ni mojawapo ya idadi ndogo ya mithali zilizosemwa katika maandishi yote matatu ya Injili. Pia ni mojawapo ya hata vikundi vidogo vya mithali Yesu alielezea kwa wanafunzi Wake. Mbegu ambayo ilipandwa ilikuwa ni “neno la ufalme” (Mathayo 13:19), “neno” (Marko 4:14), au “neno la Mungu” (Luka 8:11)---mafundisho ya Bwana na watumishi Wake.

Udongo tofauti ambako mbegu zilianguka huashiria njia tofauti ambazo kwazo binadamu hupokea na kufuata mafundisho haya. Basi, mbegu ambazo “zilianguka karibu na njia” (Marko 4:4) hazikufikia udongo mzuri ambapo zingeweza kukua. Zinakuwa kama mafundisho ambayo yanaanguka kwenye moyo mgumu au ambao haujatayarishwa. Sitasema mengi zaidi ya hayo. Ujumbe wangu unahusu wale wenu ambao mmeweka sharti kuwa wafuasi wa Kristo. Je! Tunafanya nini na mafundisho ya Mwokozi tunapoishi maisha yetu?

Mithali ya mpanzi hutuonya juu ya hali na mitazamo ambayo inaweza kumzuia mtu ambaye ameshapokea mbegu ya ujumbe wa injili kutozaa matunda mema.

I. Mwambani, Hakuna Mizizi

Mbegu nyingine “ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba: hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka” (Marko 4:5–6).

Yesu alisema kwamba hii inaelezea “wale ambao wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha,” lakini kwa sababu wao “hawana mizizi ndani yao, … kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa” (Marko 4:16–17).

Ni nini kinawasababisha wasikiaji “kuwa hawana mzizi ndani yao”? Hii ndiyo hali ya waumini wapya ambao wameongolewa kwa ajili ya wamisionari au sifa nyingi za kuvutia za Kanisa au matunda mengi makuu ya ushiriki wa Kanisa. Hawajakita mzizi katika neno, wakati upinzani unapozuka wanaweza kuchomwa na kuyayuka. Basi hata wale ambao wamelelewa katika Kanisa---waumini wa muda mrefu---wanaweza kuteleza katika hali ambapo hawana mzizi ndani yao. Mimi nawajua baadhi ya hawa---waumini wasio na uongofu thabiti na wa kudumu katika injili ya Yesu Kristo. Kama hatuna mizizi katika mafundisho ya injili na hatufuati desturi zake, yeyote wetu anaweza kukuza moyo mgumu, ambao ni mwamba kwa mbegu za kiroho.

Chakula cha kiroho ni muhimu kwa kustahimili kiroho, hasa katika ulimwengu ambao unasonga mbali na imani katika Mungu na uhuru wa sahihi na kosa. Katika kipindi kinachotawaliwa na Intaneti ambayo hupanua ujumbe ambao unatishia imani, ni sharti sisi tuongeze uzoefu wetu wa ukweli wa kiroho ili tuimarishe imani yetu na kukita mizizi katika injili.

Vijana, kama hilo fundisho linaonekana kuwa la jumla sana, hapa kuna mfano mahususi. Kama nembo za sakramenti zinapitiswa na ninyi mnatuma ujumbe mfupi au mnanong’onezeana au kucheza michezo ya video au mnafanya kingine chochote kujinyima chakula muhimu cha kiroho, mnakatakata mizizi yenu ya kiroho na kujipeleka hata kwenye mwamba. Mnajihatarisha wenyewe kunyauka wakati mtakabiliana na dhiki kama vile kutengwa, kutishwa, au kukejeliwa. Hiyo pia ni kwa watu wazima.

Kiangamizi kingine cha mizizi ya kiroho---kikichochewa na tekinolojia mpya bali si cha kipekee---ni mtazamo wa kuchungulia injili au Kanisa kupiti kwa tundu la ufunguo. Huu mtazamo finyu unalenga mafundisho au desturi fulani au mapungufu yanayofikiriwa ya viongozi na kupuuza picha yote ya mpango wa injili na matunda ya kibinafsi na jumla ya mavuno yake. Rais Gordon B. Hinckley alitoa maelezo wazi kabisa ya aina moja ya huu mtazamo wa kuchungulia. Aliiambia hadhara ya BYU kuhusu wachanganuzi wa kisiasa “walio na ghadhabu” juu ya habari za tukio la majuzi. “Kwa umahiri walimwaga siki chachu ya ubunifu ya ghadhabu na hasira. … ‘Hakika.’” Alihitimisha, “‘Hiki ni kipindi na mahali pa wacheshi wenye talanta.’”1 Kinyume, ili tuwe tumekita mizizi katika injili ni sharti tuwe wastani na kiasi katika uhakiki na tutafute daima mtazamo mpana wa kazi tukufu ya Mungu.

II. Miiba; Shughuli za Dunia Hii na Udanganyifu wa Mali

Yesu alifunza kwamba “nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda” (Marko 4:7). Alielezea kwamba hawa ni wale “watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai” (Marko 4:18–19). Hili hakika ni onyo sisi sote tunalopaswa kulisikiza.

Nitazungumza kwanza kuhusu udanganyifu wa mali. Wakati wowote tunapokuwa katika safari yetu ya kiroho---hali yoyote ile ya uongofu wetu---sisi sote hujaribiwa nayo. Wakati mitazamo na vipaumbele vinapolenga kupata, kutumia, au kuwa na mali, sisi tunaita hivi unyakinifu. Mengi yameshasemwa na kuandikwa kuhusu unyakinifu hivi kwamba ni kidogo sana kinaweza kuongezewa.2 Wale wanaomini kile kinachoitwa teolojia ya mali wanaugua kutokana na “udanganyifu wa mali.” Kuwa na utajiri au kipato cha juu siyo ishara ya baraka za mbinguni, na ukosefu wake siyo ushahidi wa kukosekana kwa baraka za mbinguni. Wakati Yesu aliwaambia wafuasi waaminifu kwamba angerithi uzima wa milele kama angelitoa tu yote aliyokuwanayo kwa maskini (ona Marko 10:17–24), Yeye hakuwa anasema kuna uovu katika kuwa na mali bali uovu uliokuwa katika mtazamo wa wafuasi katika mali. Kama tunavyojua sote, Yesu alimsifu Msamaria mwema ambaye alitumia fedha zizi hizi kumuhudumia mwanadamu mwenzake ambazo Yuda alitumia kumsaliti. Shina la uovu wote siyo fedha bali ni kupenda fedha (ona 1 Timotheo 6:10).

Kitabu cha Mormoni kinaelezea juu ya wakati ambapo Kanisa la Mungu “lilianza kukosa kuendelea”(Alma 4:10) kwa sababu “watu wa kanisa walianza … kuweka mioyo yao katika utajiri na vitu vya ulimwengu”(Alma 4:8). Yeyote yule, mwenye wingi wa vitu yuko katika hatari ya “kuduwazwa” kiroho na mali na vitu vingine vya ulimwengu.3 Huu ni utangulizi ufaao wa mafundisho ya Mwokozi wa yanayofuata.

Miiba fiche sana kueleweka inayosonga athari za neno la injili katika maisha yetu ni nguvu za kilimwengu ambazo Yesu anaziita “shughuli na mali na anasa za maisha haya” (Luka 8:14). Hizi ni nyingi sana kuzikariri. Mifano fulani itafaa.

Wakati mmoja Yesu alimkemea Mtume Wake mkuu, akimwambia Petro, “Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” (Mathayo 16:23; ona pia M&M 3:6–7; 58:39). Kuyawaza mambo ya wanadamu humaanisha kuweka shughuli za ulimwengu huu mbele ya mambo ya Mungu katika matendo yetu, vipaumbele vyetu, na kufikiria kwetu.

Tunajisalimisha kwa “anasa za maisha haya” (1)  wakati tunapopatwa na uraibu, ambao hudhoofisha vipawa vya thamani vya Mungu vya wakala; (2)  wakati tunapodanganyika na vishawishi duni, ambayo vinatuvutia mbali kutoka kwa vitu vya umuhimu wa milele; na (3)  wakati tunapokuwa na mtazamo wa sisi ndiyo tunaofaa, ambao hudhoofisha ukuaji wa kibinafsi unaofaa kutuhitimisha kwa kudra yetu ya milele.

Tunashindwa na “shughuli … za maisha haya” wakati tunapoganda kwa hofu kuhusu siku za usoni, ambayo huzuia kwenda mbele kwetu katika imani, kuamini katika Mungu na ahadi Zake. Miaka ishirini na tano iliyopita mwalimu wangu aliyeheshimika wa BYU, Hugh W. Nibley, alizungumza juu ya hatari za kujisalimisha kwa shughuli za ulimwengu. Aliulizwa katika mahojiano kama hali za ulimwengu na wajibu wetu wa kuhubiri injili inahitaji kutafuta njia za “kukubali ulimwengu katika kile tunachofanya katika Kanisa.”4

Jibu lake: “Hiyo imekuwa hadithi yote ya Kanisa, ama sivyo? Sharti uwe radhi kuudhi, sharti uwe radhi kudhubutu. Hapo ndipo imani inapohitajika. … Sharti letu linahitajika kuwa mtihani, linafaa kuwa gumu, linatakiwa kuwa haliwezekani katika mtazamo wa ulimwengu huu.”5

Kipaumbele hiki cha injili kilithibitishwa katika chuo cha BYU miezi michache iliyopita na kiongozi aliyeheshimika Mkatoliki, Charles J. Chaput, kasisi mkuu wa Philadelphia. Akiongoea juu ya mambo ambayo yanashughulikiwa na jamii za WSM na Katoliki, kama vile “kuhusu ndoa na familia, asili ya ujinsia wetu, utakatifu wa uzima wa binadamu, na umuhimu wa uhuru wa dini,” alisema:

“Ningetaka kusisitiza tena umuhimu wa kuishi kihalisi kile tunachodai kuamini. Kile kinachohitaji kuwa kipaumbele---siyo tu katika maisha yetu binafsi na maisha ya familia bali katika makanisa yetu, chaguo zetu za kisiasa, shughuli zetu za biashara, utendaji wetu kwa maskini; kwa maneno mengine, katika kila kitu tunachofanya.”

“Hapa kuna sababu kwa nini hiyo ni muhimu,” [aliendelea]. “Jifunze kutoka kwa uzoefu wa Kikatoliki. Sisi Wakatoliki tunaamini kwamba kazi yetu ni kuwa chachu katika jamii. Lakini kuna tofauti dhahiri sana katika kuwa chachu katika jamii, na kumezwa na jamii.”6

Onyo la Mwokozi dhidi ya kuacha shughuli za ulimwengu huu zisonge neno na Mungu katika maisha yetu kwa kweli inatutia changamoto sisi kulenga vipaumbele vyetu---kuweka mioyo yetu---kwenye amri za Mungu na uongozi wa Kanisa Lake.

Mifano ya Mwokozi inaweza kutufanya tufikirie juu ya mithali hii kama mithali ya udongo. Uzuri wa udongo hutegemea moyo wa kila mmoja wetu ambaye amepatiwa mbegu ya injili. Ukitathimini mafundisho ya kiroho, mioyo mingine imeganda na si tayari, mioyo mingine ni miamba kutokana na kutotumika, na mioyo mingine imewekwa katika vitu vya ulimwengu.

III. Ilianguka kwenye Udongo Mzuri na Kuzaa Matunda

Mithali ya mpanzi iliishia na maelezo ya Mwokozi ya mbegu ambazo “zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa” kwa viwango tofauti (Mathayo 13:8). Je! Tunaweza kujitayarisha wenyewe vipi kuwa ule udongo mzuri na kuwa na mavuno mazuri?

Yesu alielezea “penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyoofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia” (Luka 8:15). Tuna mbegu ya neno la injili. Ni juu ya kila mmoja wetu kuweka vipaumbele na kufanya mambo ambayo yanafanya udongo kuwa mzuri na mavuno yetu kuwa mengi. Ni sharti tutafute kukita mizizi kabisa na kuongolewa katika injili ya Yesu Kristo (ona Wakolosai 2:6–7). Tunapata uongofu huu kwa maombi, kwa kusoma maandiko, kwa kuhudumu, na kupokea sakramenti kila mara ili daima Roho Yake awe nasi. Ni sharti pia tutafute yale mabadiliko makubwa ya moyo (ona Alma 5:12–14) ambayo hubadilisha tamaa mbaya na ubinafsi na upendo wa Mungu na hamu ya kumtumikia Yeye na watoto Wake.

Ninashuhudia juu ya ukweli wa vitu hivi, na ninashuhudia juu ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ambaye mafundisho yake yanaonyesha njia na ambaye Upatanisho Wake hufanya yote yawezekane, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Gordon B. Hinckley, “Let Not Your Heart Be Troubled” (Brigham Young University devotional, Oct. 29, 1974), 1; speeches.byu.edu.

  2. Ona, kwa mfano, Dallin H. Oaks, “Materialism,” chapter 5 in Pure in Heart (1988), 73–87.

  3. Nina deni kwa Neal A. Maxwell kwa ajili ya picha yenye kumbukumbu; ona “These Are Your Days,” Ensign, Oct. 2004, 26).

  4. James P. Bell, in “Hugh Nibley, in Black and White,” BYU Today, May 1990, 37.

  5. Hugh Nibley, in “Hugh Nibley, in Black and White,” 37–38.

  6. Charles J. Chaput, “The Great Charter at 800: Why It Still Matters,” First Things, Jan. 23, 2015, firstthings.com/web-exclusives/2015/01/the-great-charter-at-800; see also Tad Walch, “At BYU, Catholic Archbishop Seeks Friends, Says U.S. Liberty Depends on Moral People,” Deseret News, Jan. 23, 2015, deseretnews.com/article/865620233/At-BYU-Catholic-archbishop-seeks-friends-says-US-liberty-depends-on-moral-people.html. Askofu Mkuu Chaput alisema pia kwamba “baadhi ya vyuo vyetu bora vya Kikatoliki vimepoteza au kiasi kikubwa vimelegeza sura ya dini yao.  …Brigham Young ni chuo kikuu cha aina ya kipekee … kwa sababu ni kituo cha masomo kilichorutubishwa na sura ya dini yake. Msisahau hilo” (“The Great Charter at 800”).