2010–2019
Mungu Yuko kwenye Usukani
Oktoba 2015


Mungu Yuko kwenye Usukani

Amri na maagano ni kweli na mafundisho ya thamani kuu yanayopatikana katika Meli Sayuni ya Zamani, ambapo Mungu yuko kwenye usukani.

Katika mkutano mkuu wa Oktoba iliyopita, niliwaalika wasikilizaji kufuata ushauri wa Brigham Young wa kubaki kwenye Meli Sayuni ya Zamani ambayo ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na kushikilia kwa mikono yote miwili.1 Kuanzia hapo, nina furaha kujua kwamba baadhi ya watu wa familia yangu na wengine walikuwa wanasikiliza na wameniuliza, “Nini kilichopo kwenye meli ya zamani tunachoweza kushikilia?” Ninawakumbusha alichosema Rais Young: “Tupo kwenye meli Sayuni ya zamani.  ... [Mungu] yuko kwenye usukani na ataendelea kuwa hapo. … Anaamuru, anaongoza na kuelekeza. Kama watu watakuwa wa kujiamini zaidi katika Mungu wao, bila kuacha maagano yao wala Mungu wao, Yeye atatuongoza vema.”2

Ni dhahiri kuwa, Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo wameisheheni Meli Sayuni ya zamani ikiwa na kweli wazi na rahisi za milele ambazo zitatusaidia kupitia njia ya maji  yaliyochafuka ya maisha ya duniani. Hizi ni baadhi chache tu.

Kanisa la Yesu Kristo daima limeongozwa na manabii na mitume walio hai. Japokuwa ni wanadamu na si wakamilifu, watumishi wa Bwana hupewa maongozi ili kutusaidia sisi kuepuka vikwazo ambavyo vinahatarisha maisha ya kiroho na kutusaidia kupita salama katika maisha haya hadi ya mwisho, hatimaye, makao ya mbinguni.

Kwa kipindi cha takribani miaka 40 ya uhusiano wangu wa karibu na wao, nimekuwa shahidi binafsi wa vyote maongozi ya kimya kimya na ufunuo muhimu ambapo ulisababisha hatua kuchukuliwa na manabii na mitumie, viongozi wengine wakuu, viongozi wa makundi ya saidizi. Japokuwa si wakamilifu wala hawakosi dosari, wanaume na wanawake hawa wazuri wamekuwa wakijitolea kuingoza kazi ya Bwana isonge mbele kama alivyoelekeza.

Na usisahau, Bwana anaongoza Kanisa Lake kupitia manabii na mitume walio hai. Hii ndiyo njia ambayo daima amekuwa akifanya kazi Yake. Kwa hakika, Mwokozi alifundisha, “Amini, amini, nawaambia, Yeye ampokeaye mtu yeyote niliyemtuma anipokea mimi.”3Hatuwezi kumtenganisha Kristo na watumishi Wake. Bila ya Mitume Wake wa kwanza, tusingekuwa na ushahidi wa mafundisho Yake mengi, Utumishi Wake, mateso Yake katika bustani ya Gethsemane, na kifo Chake msalabani. Bila ya shuhuda zao, tusingekuwa na ushahidi wa kitume wa kaburi tupu na Ufufuko.

Aliwaamuru wale Mitume wa kwanza:

“Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu:

”Mkiwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi.”4

Kazi hii kubwa iliwekwa tena katika siku zetu wakati Bwana alipomwita Joseph Smith kulirejesha Kanisa, pamoja na Mitume waliotawazwa ili kuitangaza injili Yake kwa mara ya mwisho kabla hajaja tena.

Kila mara pamekuwa na changamoto kwa ulimwengu kuwatambua na kuwakubali manabii na mitume, lakini ni muhimu kufanya hivyo ili kuelewa kabisa Upatanisho na mafundisho ya Yesu Kristo na kupata utimilifu wa baraka za ukuhani zinazotolewa kwa wale Aliowachagua.

Watu wengi wanafikiria viongozi na waumini wa Kanisa wanapaswa kuwa wakamilifu au kuwa karibu wakamilifu. Wamesahau kwamba neema ya Bwana yatosha kukamilisha kazi Yake kupitia wanadamu. Viongozi wetu wana nia nzuri, lakini wakati fulani tunafanya makosa. Hiki si kitu cha kipekee katika mahusiano ya Kanisa, wakati kitu kama hicho kikitokea katika uhusiano wetu na marafiki, majirani, kazini na kati ya wenza na katika familia.

Kuangalia udhaifu wa mwanadamu kwa wengine ni rahisi sana. Hata hivyo, tunafanya kosa kubwa kuangalia tabia ya asili ya mwanadamu na kushindwa kuona mkono wa Mungu ukitenda kazi kwa wale Alioita.

Kuzingatia tu jinsi Bwana huwatia moyo viongozi Wake wateule na jinsi huwapeleka Watakatifu kufanya mambo mazuri bila kujali ubinadamu wao ni njia moja ambayo tunaishikilia injili ya Yesu Kristo na kubaki salama safarini katika Meli Sayuni ya Kale.

Ukweli wa pili ni mafundisho ya mpango wa wokovu. Kupitia Nabii Joseph Smith, Mungu alimpa Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na mafundisho mengine mengi ya Kanisa. Hii inajumuisha elimu ya mpango wa wokovu, ambayo ni ramani ituonyeshayo tumetoka wapi, malengo yetu ya kuwepo hapa duniani, na tunakwenda wapi baada ya kufa. Mpango pia unatupa matarajio mazuri ya baadaye kwamba sisi ni watoto wa kiroho wa Mungu. Kwa kuelewa Baba yetu wa Mbinguni ni nani na uhusiano wetu na Yeye, na Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, tutakubali amri Zao na kuweka maagano pamoja Nao ambayo yatatuongoza kurudi katika uwepo Wao wa milele.

Kila wakati ninapomshika mtoto mchanga, nimekuwa nikishangaa: “Wewe mtoto mdogo ni nani? Utakuwa nani kupitia Upatanisho wa Kristo?”

Tunajiuliza maswali ya tafakari kama haya wakati mtu tumpendaye anapokufa: “Wako wapi? Wanaona na kuhisi nini? Je, maisha yanaendelea? Uhusiano wetu wa kiasili tunaoupenda utakuwaje katika ulimwengu mkuu wa roho za wafu?

Katika ulimwengu huo, familia yetu ina wajukuu wawili wa kike, Sara na Emily, na mjukuu wa kiume, Nathan. Katika kila kifo cha mjukuu, sisi kama familia tunashikilia ukweli wa injili kwa mikono yetu miwili. Maswali yetu yalijibiwa kwa ufariji na uhakika kupitia Upatanisho wa Mwokozi. Japokuwa tunawakosa wajukuu wetu, tunajua wanaishi, na tunajua tutawaona tena. Tunashukuru sana kwa injili hii kwa ajili ya uelewa  wa kiroho wakati wa msukosuko wa binafsi na kifamila.

Ukweli mwingine muhimu katika Kanisa ni kwamba Baba wa Mbinguni alimuumba Adamu na Hawa kwa malengo matakatifu. Ilikuwa ni kazi yao—na hatimaye kazi vizazi vyao—kuumba miili ya duniani kwa ajili ya watoto wa kiroho wa Mungu ili wapate uzoefu wa duniani. Kwa kitendo hiki, Baba wa Mbinguni anawaleta watoto wake wa kiroho hapa duniani kujifunza na kukua kupitia uzoefu wa maisha ya duniani. Kwa sababu Yeye anatupenda watoto Wake, Mungu huwatuma wajumbe Wake na Mitume kuwafundisha juu ya kazi muhimu ya Yesu Kristo kama Mwokozi.

Kwa karne nyingi, manabii wametimiza wajibu wao walipowaonya watu juu ya hatari zilizopo mbele yao. Mitume wa Bwana wana majukumu ya kutunza, kuonya, na kuwasaidia wale wanaohitaji majibu ya maswali ya maisha.

Miaka ishirini iliyopita, Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walitoa “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Katika hati lile, tulimalizia na yafuatayo: ”Tunaonya kwamba watu wanaovunja maagano ya usafi, wanaodhulumu wenzi au uzao, au wanaokosa kutimiza majukumu ya familia siku moja wataweza kusimama kuwajibika mbele ya Mungu. Zaidi ya hayo, tunaonya kwamba kutengana na familia kutamletea mtu binafsi, jumuiya, na mataifa majanga yaliyotabiriwa na manabii wa kale na sasa.”5

Kama Mitume, tunarudia kusisitiza hili onyo zito kwa mara nyingine leo. Tafadhali kumbuka kwamba amri na maagano ni kweli na mafundisho ya thamani kuu yanayopatikana katika Meli Sayuni ya Kale, ambapo Mungu yuko kwenye usukani.

Fundisho jingine muhimu ambalo tunapaswa kushikilia ni kuitukuza siku ya Sabato. Hii inatusaidia sisi kubaki bila mawaa hapa duniani, inatupa pumziko la mwili, kumpa kila mmoja burudani ya kiroho ya kumwabudu Baba na Mwana kila Jumapili.6Tunapoitukuza siku ya Sabato, ni ishara ya upendo wetu Kwao.7

Kama sehemu ya juhudi zetu za kuifanya Sabato kuwa ya kufurahiwa, tuliwaomba viongozi wenyeji na waumini wa Kanisa wakumbuke kwamba mkutano wa sakramenti ni wa Bwana na lazima ujengwe kwenye mafundisho Yake. Ibada ya sakramenti ni wakati wa kufanya upya maagano na kuthibitisha upendo wetu kwa Mwokozi na kukumbuka dhabihu Yake na Upatanisho Wake.

Roho hiyo hiyo lazima ijeze mikutano yetu ya kila mwezi ya kufunga na ushuhuda. Mkutano huu wa sakramenti umewekwa kwa waumini kutoa kwa ufupi shukrani, upendo, na kumthamini Baba yetu wa Mbinguni, Yesu Kristo, na injili iliyorejeshwa na kutoa ushahidi binafsi wa mambo haya. Mkutano wa kufunga na ushuhuda ni wakati wa kushiriki mawazo na hisia za kiroho na kutoa ushuhuda wa dhati. Siyo wakati wa kutoa hotuba.

Watoto wadogo lazima wafanye mazoezi ya kutoa ushuhuda katika darasa la Msingi na pamoja na wazazi wao katika Mkutano wa Jioni wa familia ya nyumbani hadi pale watakapoelewa umuhimu na maana ya ushuhuda.

Msisitizo wa hivi karibuni wa kuifanya Sabato iwe ya furaha ni matokeo ya moja kwa moja ya mwongozo toka kwa Bwana kupitia viongozi wa Kanisa. Washiriki wa baraza la Kata wanapaswa kuusaidie uaskofu wiki kadhaa mapema kwa kupitia muziki na mada ambazo zimepitishwa kwa kila mkutano wa sakramenti.

Sisi wote tunabarikiwa wakati Sabato inapojaa upendo kwa ajili ya Bwana nyumbani na kanisani. Wakati watoto wetu wanapofundishwa kwa njia ya Bwana, na wanapojifunza kuhisi na kumjibu Roho Wake. Sisi sote tunatamani  kuhudhuria kila Jumapili kupokea sakramenti tunapohisi Roho wa Bwana. Na wote, watoto na wazee, wenye mizigo mizito watahisi kuinuliwa kiroho na faraja inayokuja siku ya Sabato ya tafakari ya dhati juu ya Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani, Kristo daima yu karibu, akisubiri na yupo radhi kutusaidia tunapokuwa tayari kutubu na kuja Kwake.

Sasa, tunapotafakari kweli hizi chache na vipawa vilivyopo katika Meli Sayuni ya Kale, acha tubaki ndani na tukumbuke kwamba, kwa ufafanuzi, meli ni chombo, na lengo la chombo ni kutupeleka hadi tamati ya safari.

Tamati ya safari ya meli yetu ni baraka kamili za injili, ufalme wa mbinguni, utukufu wa selestia, na uwepo wa Mungu!

Mpango wa Mungu umeanzishwa. Yeye yupo kwenye usukani, na meli Yake kuu na yenye nguvu inaelea kuelekea kwenye wokovu na kuinuliwa. Kumbukeni sisi hatuwezi kufika huko kwa kurukia toka kwenye boti na kujaribu kuogelea mpaka huko wenyewe.

Kuinuliwa ni lengo la safari hii ya mwili, na hakuna hafikaye kule bila ya kuwa na injili ya Yesu Kristo: Upatanisho Wake, ibada, na kanuni zinazoongoza ambazo zinapatikana Kanisani.

Ni Kanisani ndipo tunapojifunza kazi ya Mungu na kukubali neema ya Bwana Yesu Kristo ambayo inatuokoa. Ni Kanisani ambapo tunaweka ahadi na maagano ya familia za milele ambayo yanakuwa pasipoti ya kuelekea kwenye kuinuliwa. Ni Kanisa ambalo linaongozwa kwa ukuhani kutupeleka kutupitisha katika  maji yasiyotabirika ya duniani.

Na tuwe na shukrani kwa ajili ya Meli ya Sayuni ya Kale, kwani bila hiyo tutatupwa nje, peke yetu bila msaada, tukisombwa na maji bila usukani ama kasia, kusombwa na mikondo mikali ya upepo na mawimbi ya adui.

Shikilia kwa nguvu, na usafiri katika meli hii tukufu, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na tutafikia hatima yetu ya milele. Huu ndiyo ushuhuda wangu na maombi yangu kwa ajili yetu wote katika jina la Yeye ambaye Meli Sayuni ya Kale inaitwa jina Lake, hata Bwana na Mwokozi, Yesu Kristo, amina.