2010–2019
Hapa Kuhudumia Lengo la Haki
Oktoba 2015


Hapa Kuhudumia Lengo la Haki

Na tuweze kuchagua kuhudumu lengo la haki kama wajumbe jasiri wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Nina shukrani kwamba tunaweza kukusanyika pamoja na wanawake waaminifu, kama Lisa, wenye mioyo safi, wanaompenda Bwana na kumtumikia Yeye, hata nyakati za majaribio yao. Simulizi ya Lisa inanikumbusha kuwa lazima tupendane na kuona katika mmoja na mwingine uzuri wa nafsi. Mwokozi alifundisha, ”Kumbuka thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu.”1 Iwapo tuna umri wa miaka 8 au 108, kila mmoja wetu ni ”mwenye thamani machoni [Mwake].”2 Anatupenda. Sisi ni mabinti wa Mungu. Sisi ni dada katika Sayuni. Tuna asili ya uungu, na kila mmoja wetu ana kazi tukufu ya kutekeleza.

Wakati wa majira ya joto nilimtembelea mama mwema kijana wa mabinti. Alinieleza hisia zake kuwa wasichana wetu wanahitaji lengo, kitu ambacho kitawasaidia kuhisi wanathaminiwa. Alifahamu kuwa tunaweza kugundua thamani yetu binafsi ya milele kwa kutenda kulingana na lengo letu tukufu katika maisha duniani. Usiku wa leo, hii kwaya ya ajabu imeimba maneno ambayo yanafunza madhumuni yetu. Kupitia kujaribiwa na majaribio, hata kupitia uoga na katika kukata tamaa, tuna mioyo jasiri. Tumeamua kutatekeleza majukumu yetu. Tuko hapa kuhudumia lengo la haki.3 Akina dada, katika lengo hili tunathaminiwa. Sisi sote tunahitajika.

Lengo la haki tunalohudumu ni lengo la Kristo. Ni kazi ya wokovu.4 Bwana Alifundisha, ”Hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”5 Sisi ndiyo sababu Yesu Kristo aliteseka, na kutokwa na damu katika kila kinyweleo, na katika upendo kamili akautoa uhai Wake. Lengo Lake ni habari njema, ”habari njema, ... kwamba alikuja duniani, hata Yesu, ili kusulubiwa kwa ajili ya ulimwengu, na kuchukua dhambi za ulimwengu, na kuutakasa ulimwengu, na kuusafisha kutokana na udhalimu wote; ili kupitia kwake yeye wapate kuokolewa.”6 Mwokozi wetu ”ameweka ishara mapito na kuongoza kwenye njia.”7 Ninashuhudia kuwa tunapoofuata mfano Wake, kumpenda Mungu, na kutumikia kila mmoja wetu kwa ukarimu na upendo, tunaweza kusimama katika usafi,”pasipo lawama mbele za Mungu siku ile ya mwisho.”8 Tunachagua kumtumikia Bwana katika lengo Lake la haki ili tuweze kuwa kitu kimoja na Baba na Mwana.9

Nabii Mormoni alitangaza kwa ujasiri kuwa, ”Tuna kazi ya kufanya wakati tungali kwenye hekalu la udongo, kwamba tuweze kumshinda adui wa haki yote, na kupumzisha nafsi zetu katika ufalme wa Mungu.”10 Viongozi wa mbeleni wa Kanisa na watangulizi wa nyakati zilizopita waliendelea kwa bidii kwa ujasiri na kishujaa na msimamo wa imani kuanzisha injili iliyorejeshwa na kujenga hekalu ambamo maagizo ya kuinuliwa yanaweza kutendeka. Watangulizi wa sasa, kumaanisha wewe na mimi, pia tunaendelea kusonga mbele katika imani, ”kufanya kazi katika shamba la [Bwana] la mzabibu kwa ajili ya wokovu wa roho za wanadamu.11 Na, kama Rais Gordon B. Hinckley alifundisha, ”Siku za baadaye zitakuwa zenye kupendeza sana jinsi gani, Mwenyezi anapoendeleza kazi Yake tukufu ... kupitia huduma isiyo ya kibinafsi kwa wale ambao mioyo yao imejawa na upendo wa Mkombozi wa dunia.”12 Tunajiunga na kina dada waaminifu wa siku zilizopita, wa sasa, na wa kizazi kinachochipuka katika kazi ya wokovu!

Kabla hatujazaliwa, tulikubali mpango wa Baba wa Mbinguni ”ambao kupitia kwake [sisi] tungeweza kupata mwili na kupata tajriba ya dunia ya kuwawezesha kuendelea mbele hadi ukamilifu na hatimaye kugundua hatima yao tukufu kama warithi wa uzima wa milele.”13 Kuhusu agano hili la maisha kabla dunia, Mzee John A. Widtsoe alieleza: ”Tulikubali, papo hapo, kuwa sio tu waokozi wetu binafsi lakini pia … waokozi wa familia mzima ya wanadamu. Tuliingia katika ushirikiano na Bwana. Kazi ya mpango huo ikawa sio tu kazi ya Baba, na kazi ya Mwokozi bali pia kazi yetu. Mdogo kabisa kati yetu, aliye mnyenyekevu kabisa, yuko katika ushirikiano na Mwenyezi katika kutekeleza lengo la milele la mpango wa wokovu.”14

Hapa katika maisha ya duniani tumeagana tena kumtumikia Mwokozi katika kazi ya wokovu. Kwa kushiriki katika ibada takatifu ya ukuhani, tunaahidi kwamba tutaanza kumtumikia Mungu kwa moyo, uwezo, akili na nguvu.15 Tunampokea Roho Mtakatifu na kutafuta msukumo Wake ili aelekeze jitihada zetu. Haki inaenea duniani wakati tunapoelewa kile ambacho Mungu anahitaji tufanye halafu tunakitimiza.

Ninamjua mtoto wa Msingi ambaye alimwambia mwenzake akiwa amesimama kwenye kituo cha basi, ”Ewe! Unafaa kuja kanisani nami na ujifunze kuhusu Yesu!”

Niliwaona wasichana katika darasa la Wasichana wakishikana mikono kisha kuahidi kuhudumiana mmoja na mwingine na kupanga njia mwafaka ya kumsaidia msichana aliyekuwa akisumbuliwa na uteja fulani.

Nimewahi kuwaona kina mama vijana wakijitolea kwa kila kitu cha muda wao, talanta zao, na nguvu zao ili kufunza kwa kuwa mfano wa kanuni za injili kwa watoto wao, kama wana wa Helamani, waweze kusimama imara na kwa imani kwenye majaribio, majaribu, na dhiki.

Pengine cha kunyenyekeza sana kwangu mimi ilikuwa kusikia dada kijana mzima akitamka kwa moto wa ushuhuda msafi kuwa kazi ya maana sana ambayo tunayoweza kufanya ni kujitayarisha kwa ndoa na familia. Ingawaje hakuwa ametimiza haya, anajua ya kwamba familia ni kitovu hasa cha kazi ya wokovu. ”Mpango mtakatifu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuendelea baada ya kifo.”16 Tunaheshimu mpango wa Baba na kumtukuza Mungu tunapoimarisha na kuadilisha huo uhusiano katika agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa. Tunachagua kuishi maisha safi na ya adilifu ili fursa zinapotokezea, tuwe tayari kufanya na kushika hilo agano takatifu la milele katika nyumba ya Bwana.

Sisi sote tunapitia katika nyakati na vipindi maishani mwetu. Lakini iwapo tuko shuleni, kazini, katika jamii, na hasa nyumbani, sisi ni mawakala wa Bwana na tuko katika kazi Yake.

Katika kazi ya wokovu hakuna nafasi ya kulinganisha, upinzani, au lawama. Haihusu umri, tajriba, au kusifiwa. Kazi hii takatifu inahusu kuwa na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, na hiari ya kutumia vipawa vya kiroho na talanta zetu za kipekee kufanya kazi ya Bwana katika njia Yake. Ni unyenyekevu wetu wa kupiga magoti na kusema, ”Ee Baba yangu, ... si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”17

Kwa nguvu zake Bwana ”tunaweza kufanya vitu vyote.”18 Tunazidi kutafuta ushauri Wake katika maombi, kwenye maandiko, na minong’ono ya Roho Mtakatifu. Dada mmoja, aliyekabiliwa na kazi ngumu kabisa aliandika, ”Mara nyingine mimi hushangaa ikiwa akina dada mwanzoni mwa historia ya Kanisa, kama sisi, hawakuweka vichwa vyao kwenye mto usiku na kuomba, ’Chochote kijacho kesho, Utanisaidia?’” Kisha akaandika, ”Mojawapo ya baraka ni [kwamba] tuko na kila mmoja wetu na tuko katika haya pamoja!19 Katika hali yoyote, popote tulipo katika njia ya wokovu, tunaungana kama kitu kimoja katika ahadi yetu ya kumfuata Mwokozi. Tunahimiliana mmoja na mwingine katika huduma Yake.

Picha
Ella Hoskins anajaza Maendeleo ya Kibinafsi

Hivi majuzi, mnaweza kuwa mlisoma kuhusu Dada Ella Hoskins, ambaye akiwa na umri wa miaka 100 aliitwa kuwasaidia wasichana katika kata yake na Maendeleo ya Kibinafsi.20 Karibu miaka miwili baadaye, akiwa 102 Dada Hoskins alipata Tunzo la Utambulisho ya Wasichana ya Uanamama. Wasichana, urais wa Wasichana na urais wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama katika kata na vigingi, na familia zao walikusanyika pamoja kusherehekea ufanikishaji wake. Mipaka ya rika, mipangilio, na hali ya ndoa ilififia katika huduma aminifu. Wasichana walitoa shukrani kwa Dada Hoskins, kwa ufundishaji na kwa mfano wake wa haki. Wanataka kuwa kama yeye. Baadaye, nilimuuliza Dada Hoskins, ”Ni kwa jinsi gani ulifanya hivyo?”

Alijibu kwa papo hapo, ”Mimi hutubu kila siku.”

Kutoka kwa bibi mpole, aliyejawa na Roho wa Bwana kiasi cha kuwa aling’aa kwa mwangaza halisi, nilikumbushwa kwamba ili kung’aa kwa urembo wa utakatifu, ili kusimama pamoja na Mwokozi na ili kuwabariki wengine, lazima tuwe wasafi. Kuwa msafi inawezekana kupitia katika Kristo tupojinyima ubaya wote na kuchagua kumpenda Mungu kwa uwezo, akili, na nguvu.21 Mtume Paulo alifundisha, ”Zikimbie ... tamaa za ujanani: ... ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.”22 Hakuna mmoja wetu aliyekamilika. Sisi wote tumefanya makosa. Lakini tunatubu ndio tuweze kuwa bora na ”kudumisha jina [la Kristo] likiwa limeandikwa daima mioyoni mwetu.”23 Tunapohudumu katika jina la Bwana, na usafi wa moyo, tunakisi upendo wa Mwokozi na kuwaonyesha wengine mbinguni kidogo tu.

Na tuweze kuchagua kuhudumu lengo la haki kama wajumbe jasiri wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na tusimame sote pamoja na ”kwa wimbo mioyoni mwetu tusonge mbele, tukiishi injili, tukimpenda Bwana, na kuujenga ufalme Wake.”24 Nashuhudia kwamba katika kazi hii tukufu, tunaweza kujua upendo msafi wa Mungu. Tunaweza kupokea furaha ya kweli na kupata utukufu wote wa milele. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.