2010–2019
Shikilia Njia Yako
Oktoba 2015


Shikilia Njia Yako

Muweke Mungu mbele, bila kujali majaribu yanayokukumba. Mpende Mungu. Kuwa na imani katika Kristo, na ujikabidhi Kwake kwa mambo yote.

Machi 11, 2011, Nilikuwa nimesimama kwenye ulingo katika kituo cha garimoshi cha Tokyo Shinagawa nikienda kutembelea Misheni ya Kobe Japan. Takribani saa 8:46 mchana, tetemeko kubwa la ardhi lenye kiwango cha 9.0 likatokea. Sikuwa na uwezo wa kusimama kwa sababu ya kutingishika kwa nguvu, na nikashikilia kwa nguvu chuma cha ngazi. Taa za dari zilizokuwa karibu nami zilianza kuanguka sakafuni. Mji mzima wa Tokyo ulikuwa na hofu.

Kwa bahati, sikuumia, na masaa manne baadaye, nilipata nafuu kujua kuwa familia yangu yote ilikuwa salama.

Kwenye televisheni, kulikuwa na mfululizo wa picha za kuogofya na kushtua. Tsumani kali ilikurupuka kwenye eneo la Misheni ya Sendai—ikifagia kila kitu kwenye njia yake: magari, nyumba, viwanda, na mashamba. Nilifadhaishwa na picha za maafa hayo, na nikalia. Na niliomba kwa bidii kuwa ulinzi na usaidizi wa Baba yetu wa Mbinguni uwe kwa wale watu walioishi katika eneo hili ninalolipenda sana.

Baadaye, ilifahamika kuwa wamisionari wote na waumini wote wa Kanisa walikuwa salama. Lakini, waumini wengi waliathiriwa, kupoteza watu wa familia zao, nyumba, na mali ya nyumbani. Zaidi ya watu 20,000 waliangamia, miundombinu iliharibiwa, na watu wengi walilazimika kuyahama makazi yao kama matokeo ya ajali ya mtambo wa nishati ya nyuklia.

Maafa kama haya yanasababisha uharibifu mkubwa katika sehemu nyingi duniani siku hizi, na kusababisha vifo vya watu wengi. Tumeonywa kuwa majanga, vita, na magumu mengi yasiyohesabika yatatokea duniani.

Wakati majaribu kama haya yanapokuja kwetu ghafla, tunaweza kujiuliza, ”Ni kwa nini haya yananitokea mimi? au ”Ni kwa nini nateseka?”

Kwa muda mrefu baada ya kuongoka katika injili, sikuwa na jibu dhahiri kwa swali ”Ni kwa nini napewa majaribu?” Nilielewa sehemu ya mpango wa wokovu kwamba tutajaribiwa. Hata hivyo, katika hali halisi, lilipokuja kwa swali hili, sikuwa na msimamo thabiti wa kujibu swali hili kikamilifu. Lakini ulikuja wakati maishani mwangu ambapo nami pia nilipata jaribu kubwa.

Nilipokuwa na miaka 30, nilikuwa ninatembelea misheni ya Nagoya kama sehemu ya majukumu yangu. Baada ya mkutano, rais wa misheni kwa ukarimu alifanya mpango wa wazee wamisionari kunisafirisha hadi kwenye kiwanja cha ndege. Hata hivyo, tulipofika kwenye njia panda chini ya kilima kirefu, lori kubwa lilikuja kwa kasi mno nyuma yetu. Likagonga nyuma ya gari letu na kutusukuma mbele zaidi ya futi 70 (mita 20). Cha kuogofya ni kuwa hapakuwepo na dereva. Upande wa nyuma wa gari ulibonyezwa hadi kuwa nusu ya ukubwa wake wa asili. Kwa bahati, wazee wamisionari na mimi tulinusurika.

Hata hivyo, siku iliyofuata, nilianza kuhisi maumivu shingoni na mabegani na nikawa na maumivu makubwa ya kichwa. Kutoka siku hiyo sikuweza kulala, na nililazimika kuishi kila siku na maumivu ya kimwili na ya kiakili. Niliomba kwa Mungu aweze kuniponya uchungu wangu, lakini dalili hizi ziliendelea kwa karibu miaka 10.

Kwa wakati huu, hisia za wasiwasi zilianza kupenya akilini mwangu na nikashangaa, ”Ni kwa nini nateseka sana kwa uchungu huu wote?” Hata hivyo, ingawaje uponyaji niliotaka haukutolewa, nilijitahidi  kutii amri za Mungu kwa uaminifu. Niliendelea kuomba kuwa niwe na uwezo wa kusuluhisha maswali niliyokuwa nayo kuhusu majaribu yangu.

Kulikuwa na wakati ambapo nilijikuta nikipambana na suala jipya la kibinafsi, na nilikuwa na wasiwasi kwa vile sikujua jinsi ya kuvumilia hili jaribu jipya. Nilikuwa naomba nipate jibu. Lakini sikupata jibu mara moja. Kwa hivyo nilienda nikazungumza na kiongozi wa Kanisa niliyemwamini.

Tulipokuwa tukizungumza, kwa upendo katika sauti yake, alisema, ”Ndugu Aoyagi, si lengo lako la kuwa duniani humu ni kupitia jaribio hili? Haitoshi kukubali majaribu yote ya maisha haya vile yalivyo na mengine kumuachia Bwana? Haufikirii kuwa shida hii itatatuliwa wakati tutakapofufuka?”

Niliposikia maneno haya, nilihisi Roho wa Mungu kwa nguvu sana. Nilikuwa nimesikia fundisho hili mara nyingi, macho ya uelewa wangu hayakuwa yamewahi kufunguka kiasi ambacho yalikuwa yamefunguka kwa wakati huu. Nilielewa kuwa hili ndilo jibu nililokuwa nikitafuta kutoka kwake Bwana katika maombi yangu. Niliweza kuelewa dhahiri mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni na kuelewa upya hii kanuni muhimu.

Katika Ibrahimu, Bwana Mungu alitangaza, ”Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru.”1

Kanuni ni kuwa yule Mungu ambaye aliumba mbingu na dunia anafahamu usanifu mkuu wa dunia hii, kwamba Yeye anatawala vitu vyote mbinguni na duniani, na ili atimize mpango wa wokovu, anatupa uzoefu mwingi tofauti —ndiyo kusema kwamba, majaribu—wakati bado tungali duniani.

Na Bwana akasema yafuatayo kwake Joseph Smith:

”Fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.

”Kwa hiyo, shikilia njia yako ..., kwani Mungu atakuwa pamoja nawe milele na milele.”2

Majaribu ya dunia hii—pamoja na magonjwa na kifo—ni sehemu ya mpango wa wokovu na matukio ambayo hayawezi kuepukika. Ni muhimu kwetu ”kushikilia njia [yetu]” na kuyakubali majaribu yetu kwa imani.

Hata hivyo, lengo la maisha yetu sio tu kuvumilia majaribu. Baba wa Mbinguni alimtuma Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, awe Mwokozi na Mkombozi wetu, ili tuweze kushinda majaribu yanayotukabili katika dunia hii; hii ina maana kwamba, Anafanya vitu dhaifu kuwa vyenye nguvu,3 Anapatanisha dhambi zetu na makosa yetu, na anafanya kuwe na uwezekano kwetu kupata kutokufa na uzima wa milele.

Rais Henry B. Eyring alisema: “Lakini jaribio ambalo Mungu mwenye upendo ameweka mbele yetu sio kuona ikiwa tunaweza kuvumilia matatizo. Ni kuona ikiwa tutavumilia vyema. Tunapita jaribio kwa kuonyesha kuwa tulimkumbuka Yeye na amri alizotupa.”4

”Shikilia njia yako” ni chaguo muhimu wakati wa majaribu. Geuza moyo wako kwake Mungu, hasa wakati tunapitia kwenye majaribu. Kwa unyenyekevu tii amri za Mungu. Onyesha imani ili kupatanisha hamu za mtu na mapenzi ya Mungu.

Wacha sasa tuzingatie ile ajali ya gari kule Nagoya. Ningalifariki katika ile ajali. Hata hivyo, kupitia neema yake Bwana, nilinusurika kimiujiza. Na najua kuwa mateso yangu yalikuwa kwa kujifunza kwangu na kukua kwangu.5 Baba wa Mbinguni alinifunza kuwa na subira, kuwa na uwezo wa kuhisi maono ya mwingine, na kuwafariji wale ambao wanapitia katika mateso. Nilipogundua haya, moyo wangu ulijawa na hisia za shukrani kwake Baba yangu wa Mbinguni kwa majaribu haya.

Muweke Mungu mbele, bila kujali majaribu yanayokukumba. Mpende Mungu. Kuwa na imani katika Kristo, na ujikabidhi kwake katika mambo yote. Moroni anatoa ahadi ifuatayo kwa watu kama hao: ”Na ikiwa mtajinyima ubaya wote, na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi neema yake inawatosha, kwamba kwa neema yake mngekamilishwa kwa Kristo.”6

Kwa kweli nashuhudia kuwa Mungu Baba na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, wako hai na ahadi za Mungu kwa wale ambao wana ”shikilia njia [Yao]” na kumpenda zitatimizwa hata wakati ambapo wanapitia kwenye majaribu, katika jina la Yesu Kristo, amina.