2010–2019
Inafanya Kazi Vyema!
Oktoba 2015


Inafanya Kazi Vyema!

Mimi naomba kwamba sisi tutazingatia “urahisi ambao upo katika Kristo” na turuhusu neema Yake ituinue na kutubeba.

Wapendwa kaka na dada zangu, marafiki zangu wapendwa, ni furaha kuwa nanyi hii leo. Tunahuzuni kuviona viti vitatu vikiwa tupu huku mbele. Tutawakosa Rais Packer, Mzee Perry, na Mzee Scott; tunawapenda wao. Tunawapenda wao, tunawaombea afya njema kwa familia zao.

Katika wikendi hii ya mkutano huu, tutakuwa na nafasi ya kuwakubali watu watatu walioitwa na Bwana kuchukua nafasi zao miongoni mwa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

Sala zenu kwa niaba yao zitawaimarisha watakapobeba jukumu takatifu la utume.

Je, Injili Inafanya kazi Kwako?

Si muda mrefu niliona nukuu ambayo ilinifanya nisimame na kufikiri. Ilisema hivi: “Mwambie mtu kuna trilioni za nyota katika anga, naye atakuamini. Mwambie kuna rangi mbichi kwenye ukuta, naye atagusa ili kupata uhakika.”

Si sisi wote kwa kiasi fulani tuko hivyo? Baada ya huduma za kitabibu, madaktari wangu wenye uwezo walielezea nilichotakiwa kufanya ili nipone vizuri. Lakini kwanza nilitakiwa kujifunza upya kuhusu mwenyewe kile nilichotakiwa kuwa nimekijua muda mrefu uliopita: kama mgonjwa, mimi sio mvumilivu.

Kwa sababu hii niliamua kuharakisha tendo la uponyaji kwa kufanya utafiti binafsi kwenye tovuti. Nahisi nilitegemea kugundua ukweli ambao madaktari wangu hawakuujua au walijaribu kunificha.

Ilinichukua muda kidogo kabla nigundue kejeli niliyokuwa nikifanya. Hakika, kufanya utafiti sisi wenyewe siyo kitu kibaya. Lakini nilikuwa siuamini ukweli niliopaswa kuutegemea na badala yake nikajikuta mwenyewe nikikimbilia kwenye tovuti ambako hakuna taarifa sahihi.

Wakati mwingine, ukweli unaweza tu kuonekana wazi sana, na rahisi sana kwetu kuthamini thamani yake kubwa. Hivyo tunayaacha yale tuliyoyazoea na kujua kuwa ni kweli kufukuzia mambo ya kimiujiza ama taarifa kanganyishi. Hatimaye tunaweza kujifunza kwamba tunapofukuzia vivuli, tunatafuta mambo ambayo yanafaida na thamani ndogo tu.

Inapokuja kwenye ukweli wa kiroho, tunawezaje kujua kwamba tupo katika njia sahihi?

Njia moja ni kuuliza maswali sahihi---yale yanayoweza kutusaidia kutafakari maendeleo yetu na kutathimini jinsi mambo yanavyotuendea sisi. Maswali kama:

“Hivi maisha yangu yana maana?”

“Hivi ninamwamini Mungu?”

“Hivi ninaamini kwamba Mungu ananijua na Ananipenda?

“Nina amini kwamba Mungu ananisikia na kujibu maswali yangu?”

“Nina furaha hakika?”

“Je, juhudi zangu zinaniongoza katika malengo ya juu ya kiroho na ya thamani katika maisha?”

Maswali mzito kama haya yanayohusu sababu ya maisha yamewaongoza watu wengi binafsi na familia ulimwenguni kote kutafuta ukweli. Mara nyingi kutafuta huko kumewaongoza katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kwenye injili iliyorejeshwa.

Nashangaa kama sisi, kama waumini wa Kanisa, tunaweza kufaidika kwa kujiuliza mara kwa mara: “Hivi uzoefu wangu katika Kanisa unanisaidia? Unanileta karibu na Kristo? Unanibariki mimi na familia yangu kwa amani na furaha iliyoahidiwa katika maandiko?”

Alma aliuliza maswali kama haya kwa waumini wa Kanisa huko Zarahemla pale alipouliza: “Mmeshuhudia mabadiliko haya makuu katika mioyo yenu? …[Na] [ninyi] mnaweza kuhisi hivyo sasa?”1 Maswali ya aina hii yanaweza kutusaidia au kupanga upya juhudi zetu za mpango mtukufu wa wokovu.

Waumini wengi watajibu kwa furaha kwamba uzoefu wao kama waumini wa Kanisa unafanya kazi vizuri kwa ajili yao. Watashuhudia kwamba iwe katika nyakati za ufukara au utajiri, mambo yawapo mazuri au machungu, wanapata maana ya kweli, amani, na furaha katika maisha kwa sababu ya kujituma kwao kwa Bwana na utumishi wao wa kujitolea katika Kanisa. Kila siku ninapokutana na waumini wa Kanisa waliojawa na furaha angavu sana na ambao wanaonyesha kwa maneno na matendo kwamba maisha yao yamebarikiwa na injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Lakini pia ninatambua kwamba kuna wengine wenye uzoefu usioridhisha sana---wanaohisi kwamba uumini wao katika Kanisa wakati mwingine siyo kile walichotarajia.

Hili linanihuzunisha, kwa sababu ninajua kabisa jinsi injili inavyoweza kumwimarisha na kuifanya upya roho ya mtu---jinsi inavyoweza kuijaza mioyo yetu na fikra zetu na nuru. Ninajua mwenyewe jinsi matunda ya baraka za injili ya Yesu Kristo inavyoweza kubadilisha maisha toka ya kawaida na yenye huzuni kwenda kuwa maisha yasiyo ya kawaida na ya maisha ya juu.

Lakini kwa nini inaonekana mambo mazuri kwa baadhi kuliko wengine? Kuna tofauti gani kati ya wale wanaopata uzoefu Kanisani wakisikia nafsi zao zikiimba wimbo wa upendo wa ukombozi2 na wale wanaohisi kwamba kuna kitu kinachokosekana?

Kadiri nilivyotafakari maswali haya, mafuriko ya mawazo yakaja kwenye fikra zangu. Leo, ningependa kushiriki nanyi mambo mawili.

Rahisisha

Kwanza: tunaufanya ufuasi wetu kuwa changamani?

Injili hii nzuri ni rahisi sana hata mtoto anaweza kuielewa, hata hivyo ni ngumu na pana sana na itachukua muda mrefu—hata milele yote—kwa kujifunza na kugundua na kuielewa kwa ukamilifu.

Lakini wakati mwingine tunachukua yungiyungi nzuri ya ukweli wa Mungu na kuifunika kwa tabaka la mawazo mazuri, mipango, na matarajio ya mwanadamu. Kila moja, peke yake, yaweza kusaidia na kuwa sahihi kwa muda na hali fulani, lakini yanapowekwa juu ya jingine, yanaweza kujenga mlima wa masimbi ambao huwa mnene na mzito kiasi kwamba huleta hatari ya kutoliona ua zuri ambalo mwanzo tulilipenda sana.

Kwa hivyo, kama viongozi lazima tulilinde Kanisa na injili yake katika usafi na uwazi wake na kuepuka kuweka mizigo isiyo ya lazima kwa waumini wetu.

Na sisi wote kama waumini wa Kanisa, sisi tunahitaji kuweka juhudi makini ili kujitolea nguvu na muda wetu katika mambo yanayofaa, huku tukiwainua wenzetu na tukiujenga ufalme wa Mungu.

Dada mmoja, mwalimu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, alijulikana kwa kuandaa masomo mazuri. Wakati mmoja, aliamua kutengeneza blanketi ambalo lingetumika vizuri katika mada ya somo lake. Lakini hali ilibadilika—kulikuwa na watoto wa kachukuliwa shuleni, kuna jirani aliyehitaji msaada wa kuhama, mume alikuwa na homa, na rafiki mpweke. Siku ya somo ilikaribia, na blanketi halikukamika. Mwishowe, usiku kabla ya somo lake, hakupata usingizi mzuri akifuma lile blanketi usiku mzima.

Siku iliyofuata alikuwa amechoka na kushindwa kupangilia mawazo yake, lakini kwa ujasiri alisimama kufundisha somo lake.

Na blanketi lilikuwa zuri sana—mishono ilikuwa mizuri, rangi ziling’aa, muundo ulikuwa mzuri na wakupendeza. Na katikati ya blanketi palikuwa na neno moja ambalo kwa furaha lilibeba mada ya somo lake: “Rahisisha.”

Akina kaka na akina dada, kuishi injili hakuhitaji kuwe kwa uchangamani.

Ni kweli iliyo wazi. Ingeweza kuelezeka hivi:

  • Kulisikia neno la Mungu kwa makini kunatuongoza kumwamini Mungu na kuamini ahadi Zake.3

  • Kadiri tunavyomwamini Mungu, ndivyo mioyo yetu inavyojawa na upendo Kwake na kwa kila mmoja wetu.

  • Kwa sababu ya upendo wetu kwa Mungu, tunatamani kumfuata Yeye na kutenda mambo yanayoendana na neno Lake.

  • Kwa sababu tunapenda Mungu, tunataka kumtumikia Yeye na kufikia kubariki maisha ya wengine na kuwasaidia maskini na wenye mahitaji.

  • Kadiri tunavyotembea katika njia hii ya ufuasi, ndivyo tunavyojifunza neno la Mungu.

Na ndivyo iendavyo, kila hatua inatuongoza katika nyingine na kutujaza ongezeko la milele la imani, tumaini na hisani.

Ni rahisi sana, na inafanyakazi vizuri sana.

Kaka zangu na dada zangu, kama uliwahi kufikiria kwamba injili haifanyi kazi vizuri kwako, ninakuomba rudi nyuma, yaangalie maisha yako, na rahisisha mwenendo wako wa uanafunzi. Zingatia katika mafundisho ya msingi, kanuni, na matumizi ya injili. Ninawaahidi kwamba Mungu atawaongoza na kuwabariki katika njia zenu ya maisha ya kuridhisha, na injili itafanyakazi vizuri kwenu.

Anza Pale Ulipo

Ushauri wangu wa pili ni: anza pale ulipo.

Wakati mwingine tunahisi kukata tamaa kwa sababu hatuko “zaidi” kitu kama---kiroho zaidi, kuheshimiwa, wenye akili, afya, tajiri, urafiki, au wenye kuweza. Kwa kawaida, hakuna kibaya katika kutaka kuboresha. Mungu alituumba ili tukue na tusonge mbele. Lakini kumbuka, udhaifu wetu unaweza kutusaidia kuwa wanyenyekevu na kumgeukia Kristo, ambaye atafanya vitu dhaifu kuwa vya nguvu.”4 Shetani, kwa upande mwingine, anatumia udhaifu wetu katika hali ambayo tunakatishwa tamaa hata tusijaribu.

Nilielewa maishani mwangu kwamba: hatuhitaji kuwa “zaidi” ya kitu chochote ili kuanza kuwa mtu ambaye Mungu angependa sisi tuwe.

Mungu atakuchukua kama ulivyo wakati huu na kuanza kufanya kazi nawe. Unachohitaji ni moyo uliotayari, kutamani kuamini, na kumwamini Bwana.

Gidioni alijiona mwenyewe kama mkulima maskini, mdogo katika nyumba ya baba yake. Lakini Mungu alimwona kama mtu shupavu wa ujasiri.5

Wakati Samueli alipomchagua Sauli kuwa mfalme, Sauli alimshawishi asimchague. Sauli alikuwa akitoka katika kabila dogo la wana wa Israeli. Angewezaje kuwa mfalme?6 Lakini Mungu alimwona kama “kijana mteule.”7

Hata nabii mkuu Musa alihisi hivyo na kukata tamaa wakati fulani kwamba akataka kuacha na afe.8 Lakini Mungu hakukata tamaa na Musa.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, kama tunajiangalia kwa macho yetu ya kimwili, hatuwezi kujiona kama tu wazuri. Lakini Baba wa Mbinguni anatuona kama tulivyo, na wale watu tunaweza kuwa. Anatuona kama wana na binti zake, kama viumbe wa nuru ya milele na wenye hatima takatifu.9

Dhabihu ya Mwokozi ilifungua mlango wa wokovu kwa wote kurudi kwa Mungu. Neema Yake inatosha watu wote ambao hujinyenyekeza mbele ya [Mungu].”10 Neema yake ni nguvu inayowezesha kuingia katika ufalme wa Mungu wa wokovu. Kwa sababu ya neema Yake, sisi wote tutafufuka na kuokolewa katika ufalme wa utukufu.

Hata utukufu wa ufalme wa chini---utukufu wa telestia, “ipitayo akili zote,”11 na idadi ya watu wasio hesabika wataurithi wokovu huu.12

Lakini neema ya Mwokozi inaweza kufanya zaidi kwetu. Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunatamani kitu kizuri zaidi. Ni kuinuliwa katika ufalme wa selestia. Ni uzima wa milele katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni. Ni zawadi kubwa ya Mungu.13 Katika ufalme wa selestia, tunapata: ukamilifu Wake, na utukufu Wake.”14 Hakika, yale yote aliyonayo Baba atatupa sisi.15

Kuinuliwa ndiyo lengo letu; ufuasi ni safari yetu.

Unapotumia imani yako ndogo na kuanza kutembea kama mfuasi mwenye amani wa Bwana Yesu Kristo, moyo wako utabadilika.16 Nafsi yako itajazwa na nuru.17

Mungu atakusaidia uwe mkuu kuliko ulivyowahi kufikiria itawezekana. Na utagundua kwamba injili ya Yesu Krsito kwa hakika inafanya kazi katika maisha yako. Inafanya kazi.

Inafanya kazi!

Kaka zangu na dada zangu, marafiki wapendwa, ninaomba kwamba tulenge katika “urahisi uliopo katika Kristo”18 na kuwezesha neema Yake kutuinua na kutubeba wakati wa safari yetu toka hapa tulipo kwenda kwenye hatima ya utukufu katika uwepo wa Mungu.

Tunapofanya hivyo, na mtu atakapotuuliza, “Inakusaidiaje wewe kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho?” tutakuwa tayari kusema kwa ufahari na furaha kubwa, “Ni vizuri sana! Nashukuru kwa kuniuliza! Je, ungependa kujua zaidi?”

Haya ni matumaini yangu, sala yangu, ushuhuda wangu na baraka zangu katika jina la Yesu Kristo, amina.