2010–2019
Kwamba Daima Wamkumbuke Yeye
Oktoba 2015


Kwamba Daima Wamkumbuke Yeye

Ninapenda kujifunza na kutafakari maisha Yake aliyetoa kila kitu kwa ajili yangu na kwa ajili ya sisi sote.

Naupenda wimbo wa Msingi ambao unasema:

Nisimulie hadithi za Yesu napenda kuzisikia.

Vitu ningetaka kumuuliza yeye aniambie kama angalikuwa hapa.

Mandhari ya njiani, simulizi za bahari,

Hadithi za Yesu, nisimulie juu yake.1

Ninaamini kwamba kuanzisha desturi ya kusimulia hadithi za Yesu kwa watoto wetu na familia zetu ni njia maalum sana ya kuitukuza Siku ya Sabato katika nyumba zetu.

Hii hakika italeta roho wa kipekee katika nyumba zetu na kuleta katika familia zetu mifano toka kwa Mwokozi Mwenyewe.

Ninapenda kujifunza na kutafakari maisha Yake aliyetoa kila kitu kwa ajili yangu na kwa ajili ya sisi sote.

Ninapenda kusoma vifungu vya maandiko juu ya maisha Yake yasiyo na dhambi, na baada ya kusoma maandiko ambayo yanaelezea matukio Yeye aliyoyapitia, ninafumba macho yangu na kujaribu kuweka taswira ya matukio matakatifu ambayo yananifundisha na kuniimarisha kiroho.

Nyakati kama:

  • Alipotema mate chini na, kufanya tope kutokana na mate, akampaka machoni mtu kipofu na kumwambia, “Nenda, kanawe katika birika ya Siloamu.” Naye akatii, akaenda kunawa, akarudi anaona.2

  • Wakati Yeye aliponya mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu na aliyegusa pindo la vazi lake, kwa kuamini kwamba kwa kugusa kwake tu angeweza kuponywa.3

  • Wakati alipojitokeza kwa wafuasi Wake, akitembea juu ya bahari.4

  • Wakati alipokwenda pamoja na wafuasi wake barabara iendayo Emausi na kufungua uelewa wao kwenye maandiko.5

  • Wakati alipowatokea watu katika Amerika na kuwaambia waje Kwake na waingize mikono yao na kuitia kwenye ubavu Wake na pia kwamba waguse alama za misumari katika mikono Yake na katika miguu Yake, ili wajue Yeye ndiye “Mungu wa Israeli, na Mungu wa ulimwengu wote, na aliuawa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.”6

Ninafurahi kujua kwamba kuna wazazi wanaosimulia hadithi za Kristo kwa watoto wao. Niligundua hili ninawatazama watoto Kanisani, katika onyesho la Msingi, na katika matukio mengine.

Ninawashukuru wazazi wangu kwa kunifundisha kuhusu Kristo, Naendelea kuona jinsi mfano wa Mwokozi wetu unavyomsaidia mke wangu mpendwa na mimi wakati tunapowafundisha watoto wetu.

Moyo wangu umejawa na furaha ninapowaona watoto wangu wakisimulia hadithi za Kristo kwa wajukuu wangu Inanikumbusha moja ya maandiko niyapendayo, yanayopatikana katika 3  Yohana, aya ya 1, mstari wa 4, ambao unasomeka, “Sina furaha iliyo kuu kuliko hii kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli,” na kwa nini isiwe kwa wajukuu wetu pia? Na kwa nini wajukuu wetu pia?

Ninawashukuru viongozi wetu ambao mara zote wanatufundisha juu ya Kristo, juu ya kuitakasa Siku ya Sabato, na juu ya kupokea sakramenti kila Jumapili kwa kumtukuza Mwokozi.

Tunaweza kufurahia zaidi Sabato na sakramenti kwa kujifunza hadithi za Kristo, Na kwa kufanya hivyo, tunajenga desturi ambayo inajenga imani yetu na ushuhuda wetu na pia kuilinda familia yetu.

Wiki kadhaa zilizopita, wakati nikisoma tena ujumbe uliotolewa na Rais Russell  M. Nelson kwenye mkutano mkuu uliopita, wakati nikitafakari juu ya siku ya Sabato, nahisi shukrani kwa ajili ya baraka na nafasi ya kuweza kupokea sakramenti. Kwa upande wangu, ni wakati mtukufu sana, mtakatifu na wa kiroho. Ninapenda sana mkutano wa sakramenti.

Katika kutafakari kwangu, nilijifunza kwa makini kubariki mkate na kubariki maji. Nilisoma na kufikiria kwa makini sala ya sakramenti na ibada ya sakramenti. Nilianza kurudia tena katika akili yangu na moyo wangu matukio ambayo yameunganika kwenye sakramenti.

Katika hali ya kutafakari, nilifikiria kwamba siku ile, siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati Yeye, akijibu swali la wafuasi wake kuhusu wapi waandae Pasaka, aliwajibu, akisema, “Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Bwana asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka na wanafunzi wangu.7

Nilijaribu kufikiria katika akili yangu wafuasi wakinunua chakula na kuandaa meza vizuri ili wale pamoja Naye katika siku ile maalum: meza ya watu 13, Yeye na wanafunzi Wake 12, ambao aliwapenda.

Nililia wakati nilipofikiria Kristo akila pamoja nao, wakati aliposema, “Amini nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”8

Nilifikiria kuhusu wafuasi wenye huzuni wakimwuliza, “Bwana, ni mimi?”9

Na wakati Yuda alipomwuliza swali hilo hilo, Alijibu kwa upole, “Wewe umesema.”10

Niliweza kuona ile mikono iliyoponya, iliyofariji, iliyojenga, na iliyobaribiki, iliyomega mkate, na Yesu akisema, “Twaeni, mle; huu ni mwili wangu.”11

Kisha akakitwaa kikombe kilichojaa divai na akashukuru na akawapa kikombe, akisema, “Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”12

Katika akili yangu, niliwaangalia wafuasi, mmoja baada ya mwingine, na kutazama shaka machoni mwao juu ya Mwalimu, ambaye walimpenda sana. Ilikuwa kama nimekaa pale pamoja nao, nikiangalia kila kitu. Nilijisikia uchungu mwingi moyoni mwangu, huzuni na masikitiko makubwa kwa yale yaliyotarajiwa kutokea Kwake.

Nafsi yangu ilijawa na matamanio makubwa ya kuwa mtu mzuri. Kupitia toba na huzuni, nilitamani kuweza kuzuia na kuepusha umwagikaji hata matone machache ya damu Yake katika Gethesmane.

Kisha nikatafakari juu ya sakramenti tunayopokea kila wiki katika ukumbusho Wake. Na nikifanya hivyo, nikatafakari kila neno la kubariki mkate na maji. Kwa kina niliakisi kuhusu maneno “na daima kumkumbuka” katika kubariki mkate, na “kwamba daima wamkumbuke” katika kubariki mkate.13

Mimi nilitafakari nini maana ya “daima wamkumbuke Yeye.”

Kwangu, ina maana:

  • Kukumbuka maisha Yake kabla ya kuja duniani, wakati dunia hii nzuri ilipokuwa ikiumbwa na Yeye.14

  • Kukumbuka kuzaliwa Kwake kwa unyenyekevu kwenye hori la ng’ombe, katika Bethlehemu ya Yudea.15

  • Kukumbuka wakati, akiwa mvulana wa miaka 12 tu, Aliwafundisha na kuwahubiria walimu wa dini hekaluni.16

  • Kukumbuka wakati Alipokwenda faraghani huko nyikani, kujiandaa kwa utumishi Wake duniani.17

  • Na wakati alipobadilika sura mbele ya wafuasi Wake.18

  • Kukumbuka wakati alipoanzisha sakramenti, katika Karamu ya Mwisho na wafuasi Wake.19

  • Kukumbuka wakati Alipokwenda kwenye Bustani la Gethsemane na kuteseka sana kwa ajili ya dhambi zetu, maumivu, kukata tamaa, magonjwa ambayo hata kwamba akatokwa na damu kila kinyweleo.20

  • Kukumbuka wakati, baada ya mateso mengi na maumivu makali, hata hivyo huko Gethsemane, Alisalitiwa kwa busu na mmoja wa wafuasi Wake aliyemwita rafiki.21

  • Kukumbuka wakati alipopelekwa kwa Pilato na kwa Herodi ili ahukumiwe.22

  • Kukumbuka wakati alipofedheheshwa, akapigwa makofi, akatemewa mate, akapigwa, na kupigwa mijeledi hadi kuchuna ngozi ya mwili Wake.23

  • Kukumbuka wakati taji la miiba likiwekwa kikatili juu ya kichwa Chake.24

  • Kukumbuka kwamba Alitakiwa kuubeba msalaba Wake mwenyewe kwenda Gologotha na kwamba alipigiliwa msalabani, akiteseka kila aina ya maumivu kimwili na kiroho.25

  • Kukumbuka akiwa msalabani, moyo Wake ukiwa umejaa hisani, Aliwaangalia wale waliokuwa wakimsulubisha na akainua macho Yake mbinguni, akiomba, “Baba, wasamehe; kwani hawajui watendalo.”26

  • Kukumbuka wakati Yeye, akijua ametimiza kazi Yake ya kuwaokoa wanadamu, akaiweka Roho Yake mikononi mwa Baba Yake, Baba yetu.27

  • Kukumbuka Ufufuko Wake, ambao unatuhakikishia ufufuko wetu wenyewe na uwezekano wa kuisha karibu Yake kwa milele yote, ikitegemea chaguzi zetu.28

Na zaidi ya hapo, kutafakari juu ya sala ya sakramenti na umuhimu na maneno ya maana ya sala, kupokea ahadi, wakati wa kubariki sakramenti, kwamba daima tumkumbuke Yeye, ili Roho Wake daima apate kuwa pamoja nasi.29

Ninaamini Bwana ana wakati Wake wa lini atatoa ufunuo kwetu. Nilielewa hili vizuri sana wakati nikijifunza Mhubiri 3:1, 6ambayo inasema:

“Katika kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu: …

“Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; wakati wa kuweka na wakati wa kutupa.”

Sakramenti pia ni muda kwa Bwana wa Mbinguni kutufundisha kuhusu Upatanisho wa Mwanawe Mpendwa—Mwokozi wetu, Yesu Kristo, na kwa ajili ya sisi kupata ufunuo juu ya hilo. Ni wakati wa “kupiga hodi, na kufunguliwa,”30 kuomba na kupokea elimu hii. Ni wakati wetu kumwomba sana Mungu kwa ajili ya elimu hii. Na kama tutafanya hivi, sina shaka kwamba tutapokea elimu hii, ambayo itabariki maisha yetu bila kipimo.

Ninaipenda Sabato, sakramenti, na maana yake. Ninampenda Mwokozi kwa nafsi yangu yote. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.