2010–2019
Kupitia Macho ya Mungu
Oktoba 2015


Kupitia Macho ya Mungu

Ili kuweza kuwahudumia wengine kwa ufanisi, ni lazima tuwatazame kupitia macho ya mzazi, kupitia macho ya Baba wa Mbinguni.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, asanteni sana kwa kunikubali jana kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Ni vigumu sana kwangu mimi kueleza maana ya hayo yote. Hususani nilikuwa mwenye shukrani hasa kwa kura ya wanawake wawili wasio wa kawaida maishani mwangu: mke wangu, Ruth, na mpendwa, mpendwa, binti yetu mpendwa, Ashley.

Wito wangu unatoa ushahidi wa kutosha juu ya ukweli wa maelezo ya Bwana mapema katika kipindi hiki cha injili: “Kwamba utimilifu wa injili yangu upate kutangazwa na watu walio dhaifu na wa kawaida hata miisho ya ulimwengu.”1 Mimi ni mmoja wa walio dhaifu na wa kawaida. Miongo michache iliyopita, wakati nilipoitwa kuwa askofu wa kata moja huko mashariki mwa Marekani, kaka yangu, mkubwa wangu kidogo na mwenye hekima zaidi yangu, alinipigia simu. Yeye alisema, ”Unahitaji kujua kwamba Bwana hajakupa wito kwa sababu ya chochote ulichokitenda. Katika hali yako, huenda ikawa ni licha ya yale uliyotenda. Bwana amekupa wito kwa ajili ya yale anayohitaji Yeye kutenda kupitia kwako, na hayo yatatendeka tu ikiwa wewe utafanya hivyo katika njia Yake.” Ninatambua kuwa hekima hii kutoka kwa kaka mkubwa inafaa zaidi hata leo hii.

Jambo la ajabu hufanyika katika huduma ya mmisionari wakati anapogundua kwamba wito wake sio juu yake yeye; bali, ni juu ya Bwana, kazi Yake, na juu ya watoto wa Baba wa Mbinguni. Ninahisi kwamba hilo pia ni kweli kwa Mtume. Wito huu sio juu yangu. Ni juu ya Bwana, kazi Yake, na watoto wa Baba wa Mbinguni. Bila kujali ni kazi au wito upi katika Kanisa, ili kuhudumu kwa ustadi, mtu lazima ahudumu akifahamu kuwa kila tunayemhudumia “ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kama ndivyo, ... ana asili na hatima ya kiungu.”2

Katika taaluma yangu ya awali, nilikuwa daktari bingwa wa moyo niliyebobea katika kutibu ugonjwa wa moyo kushindwa na kupandikiza moyo mwingine, na nikiwa na wagonjwa wengi waliokuwa mahututi. Mke wangu kwa utani husema kwamba ilikuwa ishara mbaya ya utabiri ya kuwa mmoja wa wagonjwa wangu. Nikiweka utani wote kando, niliona watu wengi wakiaga dunia, na nikaja kuwa mbali na hisia za mshtuko wakati mambo hayakwenda sawasawa. Kwa njia hiyo, hisia za huzuni na kuvunjika moyo zilipungua.

Katika mwaka wa 1986 kijana mmoja kwa jina Chad alipatwa na tatizo la moyo kushindwa na akapokea upandikizaji wa moyo. Aliendelea vizuri kwa muda wa muongo mmoja na nusu. Chad alifanya kila aliloweza kuwa na afya njema na kuishi maisha ya kawaida iwezekanavyo. Alihudumu misheni, akafanya kazi, na alikuwa mwana aliyejitoa kwa wazazi wake. Miaka michache ya mwisho wa maisha yake, ijapokuwa, ilikuwa na changamoto, na alipelekwa hospitalini mara kwa mara.

Jioni moja, aliletwa katika idara ya dharura ya hospitali kwa sababu ya mshtuko kamili wa moyo. Washirika wangu pamoja nami tulifanya kazi kwa muda mrefu ili kurejesha mzunguko wake wa damu. Hatimaye, ilikuwa wazi kwamba Chad hangeweza kufufuliwa. Tulisitisha jitihada zetu ambazo hazikuwa na ufanisi, na nikamtangaza mfu. Ingawaje mwenye huzuni na masikitiko, nilidumisha mtazamo wa mtaalam. Niliwaza mwenyewe, ”Chad ametunzwa vyema. Amekuwa na miaka mingi zaidi ya maisha kuliko ilivyotarajiwa .” Umbali ule wa kutokuwa na hisia punde ulikatizwa na wazazi wake walipoingia katika chumba cha dharura na kumwona mwana wao aliyeaga dunia akiwa amelazwa juu ya machela. Katika wakati huo, nilimwona Chad kupitia macho ya mama yake na baba yake. Niliona matumaini na matarajio makuu waliyokuwa nayo kwake, hamu waliyokuwa nayo kwamba angeliishi tu kwa muda mrefu kidogo na siha nzuri kidogo. Kwa kugundua haya, nilianza kulia. Katika hali ya kinyume cha wajibu na katika kitendo cha huruma sitosahau kamwe, wazazi wake Chad walinifariji mimi.

Hivi sasa nimegundua kwamba katika Kanisa, ili kuweza kuwahudumia wengine kwa ufanisi, ni lazima tuwatazame kupitia macho ya mzazi, kupitia macho ya Baba wa Mbinguni. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuelewa thamani halisi ya nafsi. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuhisi upendo alionao Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake wote. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuona hisia za Mwokozi katika kuwajali wao. Hatuwezi kutimiza kikamilifu wajibu wetu wa agano la kuomboleza na wale wanaoomboleza na kuwafariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa isipokuwa tumewatazama kupitia macho ya Mungu.3 Mtazamo huu ulio mpana utafungua mioyo yetu kwa ajili ya masikitiko, hofu, na huzuni kubwa ya wengine. Lakini Baba wa Mbinguni atatusaidia na kutufariji, kama vile wazazi wake Chad walivyonifariji mimi miaka mingi iliyopita. Tunahitaji kuwa na macho yanayoona, masikio yanayosikia, na mioyo inayofahamu na kuhisi kama tunataka kutimiza uokozi ambao mara kwa mara Rais Thomas  S. Monson anatuhamasisha.4

Ni wakati tu tunapotazama kupitia macho ya Baba wa Mbinguni tunaweza kujawa na “upendo safi wa Kristo.”5 Kila siku tunapaswa kumsihi Mungu atupe upendo huu. Mormoni alitoa mawaidha, “Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo.”6

Kwa moyo wangu wote ninataka kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.7 Ninampenda. Ninamuabudu. Ninashuhudia juu ya ukweli wa kuishi Kwake. Ninashuhudia kwamba yeye ndiye Mpakwa Mafuta, Masiya. Mimi ni shahidi wa rehema, huruma na upendo Wake usioweza kulinganishwa. Ninaongeza ushuhuda wangu kwa ule wa Mitume ambao, katika mwaka wa 2000 walisema ”kwamba Yesu ndiye Kristo Aliye Hai, Mwana asiyekufa wa Mungu. … Yeye ni nuru, uzima, na tumaini la ulimwengu.”8

Ninashuhudia kwamba katika siku ile mwaka wa 1820 katika kichaka kilicho katika wilaya iliyo nje ya New York, Bwana mfufuka alionekana, pamoja na Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, kwake Nabii Joseph Smith, kama vile Joseph Smith alivyosema kuwa Wao walimtokea. Funguo za ukuhani zipo duniani leo kuwezesha ibada za wokovu na kuinuliwa. Ninajua hayo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 1:23.

  2. ”Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Liahona, Nov. 2010, 129; ilisomwa na Rais Gordon B. Hinckley kama sehemu ya ujumbe wake wakati wa mkutano mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama mnamo Septemba 23, 1995, kule Jijini Salt Lake City, Utah.

  3. Ona Mosia 18:8–10.

  4. Ona, kwa mfano, Thomas S. Monson, “Kwa Uokozi,” Liahona, Julai 2001, 57–60; “Wajibu Wetu Kuokoa,” Liahona, Okt. 2013, 4–5. Rais Monson alisisitiza dhana hizi katika ujumbe wake kwa Viongozi Wakuu Wenye Mamlaka mnamo Septemba 30, 2015, akiwakumbusha wale waliokuwa wamekusanyika kuwa alikuwa akisisitiza tena ujumbe aliokuwa ameutoa kwa Viongozi Wakuu wenye Mamlaka na Sabini wa Maeneo katika mikutano ya mafunzo wakati wa mkutano mkuu wa Aprili 2009.

  5. Moroni 7:47.

  6. Moroni 7:48.

  7. Ona Mafundisho na Maagano 18:27–28:

    ”Na hao Kumi na Wawili watakuwa wanafunzi wangu, na wao watajichukulia juu yao jina langu; na hao Kumi na Wawili ni wale ambao hutamani kujichukulia juu yao jina langu kwa dhamira ya moyo wao wote.

    ”Na kama wao hutamani kujichukulia juu yao jina langu kwa dhamira ya moyo wao wote, hao wameitwa kwenda ulimwenguni kote kuhubiri injili yangu kwa kila kiumbe.”

  8. ”Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume,” Liahona, Apr. 2000, 3. Kwa kudondoa haya hapa, kitaswira ninaweka saini yangu kwenye hati hiyo, nikishuhudia ushuhuda ule ule uliotolewa na Mitume wale.