2010–2019
Mimi Nimepungukiwa na Nini?
Oktoba 2015


Mimi Nimepungukiwa na Nini?

Kama tukiwa wanyenyekevu na wenye kufundishika, Roho Mtakatifu atatuongoza kwenda nyumbani, lakini tunahitaji kumwomba Bwana maelekezo tukiwa njiani.

Nilipokuwa kijana, nilianza kuchunguza juu ya Kanisa. Kwanza nilivutiwa na injili kwa mifano ya marafiki zangu wa Watakatifu wa Siku za Mwisho, lakini hatimaye nilivutiwa na mafundisho. Nilipojifunza kwamba wanaume na wanawake waaminifu wanaweza kuendelea na hatimaye  kuwa kama wazazi wao wa mbinguni, nilishangazwa. Nilipenda wazo hilo; lilionekana kuwa kweli kwangu.

Mara baada ya ubatizo wangu, nilikuwa najifunza Mahubiri ya Mlimani, na kugundua kwamba Yesu alifundisha ukweli huo huo juu ya kuendelea milele katika Biblia. Alisema, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”1

Nimekuwa muumini kwa zaidi ya miaka 40 sasa, na ninaposoma mstari huu wa maandiko, ninakumbushwa malengo yetu hapa duniani. Tulikuja kujifunza na kuendelea hadi tutakapokuwa tumetakaswa au kukamilishwa katika Kristo.

Safari ya ufuasi si rahisi. Imeitwa “hatua za maboresho endelevu.”2 Tunapotembea katika njia iliyosonga na nyembamba, Roho kila mara anatupa changamoto ili tuwe watu wema na tupande juu zaidi. Roho Mtakatifu anakuwa mwenza mzuri katika safari. Kama tu wenye unyenyekevu na kufundishika, atatushika kwa mkono Wake na kutuongoza nyumbani.

Hata hivyo, tunahitaji kumwomba Bwana kwa ajili ya mwongozo njiani. Tunatakiwa kujiuliza maswali fulani magumu, kama “Nini nahitaji kubadilika?” “Nawezaje kubadilika?” “Ni udhaifu gani unahitaji kuimarishwa?”

Acha tufikirie Agano Jipya juu ya mtawala kijana tajiri. Alikuwa kijana mwema ambaye alikuwa tayari amezishika Amri Kumi, lakini alitaka awe mwema zaidi. Lengo lake lilikuwa uzima wa milele.

Alipokutana na Mwokozi, alimwuliza, “Mimi nimepungukiwa na nini?”3

Yesu akamjibu mara moja, akitoa ushauri ambao ulitakiwa hususani kwa kijana tajiri. “Yesu akamwambia, “Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, na uwape maskini, na  … njoo na unifuate.”4

Kijana alishangazwa, hajawahi kamwe kufikiria dhabihu kama hiyo. Alikuwa mnyenyekevu na kuweza kumwuliza Bwana lakini hakuwa mwaminifu kuufuata ushauri mtakatifu aliopewa. Lazima tuwe tayari kutenda wakati tunapopokea jibu.

Rais Harold B. Lee alifundisha: “Kila mmoja wetu, kama tunahitaji kufikia ukamilifu, lazima wakati fulani tujiulize wenyewe swali hili: “Mimi nimepungukiwa na nini?”5

Nilimjua mama mwaminifu aliyejinyenyekeza na kuuliza, “Nini kinanifanya nisiendelee?” Katika hali yake, majibu kutoka kwa Roho yakaja mara moja; “Acha kulalamika.” Jibu hili lilimshangaza; kamwe hajawahi kufikiria kama yeye ni mlalamishi. Hata hivyo, ujumbe kutoka kwa Roho Mtakatifu ulikuwa wazi. Katika siku zilizofuata, alikuja kujua tabia yake ya kulalamika. Shukrani kwa msukumo wa kuboreka, alikuwa na nia ya kuhesabu baraka zake na si changamoto zake. Siku kadhaa, alihisi idhinisho changamfu la Roho.

Kijana mnyenyekevu, ambaye hakuonekana kama kupata mchumba sahihi, alikwenda kwa Bwana kwa ajili ya msaada: “Nini kinanifanya mimi nisiwe mtu sahihi?“ aliuliza. Jibu hili likamjia kwenye fikra na moyo wake: “Safisha lugha yako.” Kwa wakati huo, aligundua kwamba maneno kadhaa yasiyofaa yalikuwa ni sehemu ya misamiati yake, na aliahidi kubadilika.

Dada mmoja mseja aliuliza swali zuri: “Nini nahitaji nibadilishe?” na Roho akamnong’oneza, “Usiingilie watu wanapoongea.” Roho Mtakatifu hakika anatoa ushauri mahususi. Ni mwenza mkweli daima na atatuambia vitu ambavyo hakuna mtu yeyote ajuaye au mwenye ujasiri wa kusema.

Mmisionari aliyemaliza kutumikia alijikuta akikabiliwa na ratiba ngumu. Alikuwa anajaribu kutafuta muda wa kufanya kazi, kusoma, familia, wito wa Kanisa. Alimwomba Bwana ushauri: “Nawezaje kuhisi amani kwa yote ninayohitaji kufanya?” Jibu halikuwa lile alilolitarajia;  alipokea mwongozo kwamba alitakiwa kuwa mwangalifu zaidi katika kuitii siku ya Sabato na kuishika kitakatifu. Aliamua kuifanya Jumapili kuwa siku ya huduma ya Mungu—kuweka pembeni kazi za shule katika siku hiyo na kujifunza injili badala yake. Marekebisho haya madogo yalileta amani na uwiano aliokuwa anauhitaji.

Miaka iliyopita, nilisoma katika jarida la Kanisa habari juu ya msichana aliyekuwa anaondoka nyumbani na kwenda chuoni. Alikuwa nyuma darasani mwake, maisha ya kijamii siyo yale aliyoyatarajia, na alikosa furaha. Mwishowe siku moja, alipiga magoti na kulia, “Nini nifanye ili maisha yangu yawe mazuri?” Roho Mtakatifu alinong’ona, “Simama nenda kasafishe chumba chako.” Mwongozo huu ulikuja kama mshangao, lakini ulikuwa mwanzo aliouhitaji. Baada ya kuchukua muda kupanga na kuweka vitu vyake vizuri, alihisi Roho akikijaza chumba chake na kuinua moyo wake.

Roho Mtakatifu hatuambii tujirekebishe kwa kila kitu mara moja. Kama angefanya hivyo, tungekuwa tumekatishwa tamaa. Roho anafanyakazi kwetu kwa kasi yetu wenyewe, hatua moja kwa wakati, au kama Bwana alivyofundisha, “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri,  … na heri wale wanaosikiza kanuni zangu,  … kwani kwa yule atakayepokea nitampatia zaidi.”6 Kwa mfano, kama Roho Mtakatifu amekuongoza kusema asante mara nyingi, na unajibu kulingana na mwongozo ule, Anaweza kufikiri ni muda wa kusonga mbele katika jambo lenye changamoto – kama vile kujifunza kusema, “Samahani, hilo lilikuwa kosa langu.”

Picha
Familia ikipokea sakramenti

Muda mzuri wa kujiuliza, “Mimi nimepungukiwa na nini?” ni wakati tunapopokea sakramenti. Mtume Paulo alifundisha kwamba huu ni wakati kwa kila mmoja wetu kujipima mwenyewe.7 Ni katika mazingira ya staha mawazo yetu yanapogeukia mbinguni, Bwana kwa upole anatuambia tunachohitaji kukifanya.

Kama wewe, nimepokea ujumbe mwingi toka kwa Roho kwa miaka mingi ukinionyesha jinsi ambavyo ningeweza kufanya vizuri zaidi. Acha nishiriki mifano binafsi ya ujumbe ambao niliukubali moyoni. Miongozo hii ni pamoja na:

  • Usipaze sauti yako.

  • Jipange vizuri; tengeneza orodha ya vitu vya kufanya kila siku.

  • Utunze mwili wako kwa kula zaidi matunda na mboga.

  • Ongeza mahudhurio yako ya hekalu.

  • Pata muda wa kutafakari kabla ya kusali.

  • Omba ushauri wa mke wako.

  • Na kuwa mvumilivu wakati ukiendesha gari; usivuke mwendo uliowekwa. (Bado ninafanyia kazi hili la mwisho.)

Upatanisho ndio unaoufanya ukamilifu au utakaso uwezekane. Hatuwezi kamwe kujifanyia wenyewe, bali neema ya Mungu inatosha kutusaidia. Kama Mzee David  A. Bednar alivyowahi kusema: “Wengi wetu tunaelewa kwamba Upatanisho ni kwa ajili ya wenye dhambi. Sina uhakika, hata hivyo, kama tunajua na kuelewa kwamba Upatanisho pia ni kwa watakatifu—kwa wanaume na wanawake wema ambao ni watiifu, wema, na waangalifu na wale wanaojaribu kuwa wema.”8

Picha
Mwanamke Akisali

Ningependa kushauri kwamba kila mmoja wenu ashiriki katika zoezi la kiroho hivi karibuni, ikiwezekana hata leo usiku wakati wa kusali. Kwa unyenyekevu mwulize Bwana swali lifuatalo: “Nini kinanifanya mimi nisiendelee?” Kwa maneno mengine: “Mimi Nimepunukiwa na nini?” Kisha subiri kimya kimya kwa ajili ya majibu. Kama una moyo safi, jibu litakuja wazi. Utakuwa ni ufunuo uliokusudiwa kwa ajili yako.

Huenda Roho atakuambia kwamba unahitaji kumsamehe mtu. Au unaweza kupokea ujumbe wa kuwa makini katika kuchagua filamu za kuangalia au muziki wa kusikiliza. Wewe unaweza kujisikia kuongozwa kuwa mkweli zaidi katika biashara zako au shughuli zako au kuwa mkarimu katika matoleo ya mfungo. Kuna uwezekano wa aina nyingi.

Roho anaweza kutuonyesha udhaifu wetu, lakini pia anaweza kutuonyesha nguvu zetu. Wakati mwingine yatupasa kuuliza juu ya mazuri tunayoyafanya ili Bwana aweze kutuinua na kutuhamasisha. Tunaposoma baraka zetu za baba mkuu, tunakumbushwa kwamba Baba yetu wa Mbinguni  anajua uwezo mtakatifu. Anafurahia kila wakati tunapopiga hatua mbele. Kwake, mwelekeo wetu ni muhimu kuliko kasi yetu.

Shikeni msimamo, akina kaka na dada, lakini msikate tamaa. Tutahitaji kufanya kazi ya ziada kabla hatujafa ili tuwe wakamilifu, lakini katika maisha haya tunaweza kuweka msingi. “Ni jukumu letu kuwa wazuri leo kuliko tulivyokuwa jana, na wazuri kesho zaidi ya tilivyo leo.”9

Kama kukua kiroho siyo kipaumbele katika maisha yako, kama hatupo kwenye njia ya kuboreka daima, tutakosa uzoefu muhimu ambao Mungu anataka atupe.

Miaka iliyopita nilisoma maneno ya Rais Spencer  W. Kimball, ambayo yalileta faida kwangu. Alisema. “Nimejifunza kwamba penye moyo wa maombi, wenye kutamani kutenda mema, wenye kukataa dhambi, na wemye kutiifu kwa amri za Mungu, Bwana anatoa nuru zaidi na zaidi hadi mwisho kuna nguvu za kuchoma pazia la mbinguni.  ... Mtu mwenye wema wa aina hiyo ana ahadi zenye thamani ambapo siku moja ataiona sura ya Bwana na kujua kwamba yupo.”10

Ni maombi yangu kwamba uzoefu huu unaweza kuwa wetu siku moja, tunapomruhusu Roho Mtakatifu kutuongoza nyumbani. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mathayo 5:48.

  2. Neal A. Maxwell, “Testifying of the Great and Glorious Atonement,” Liahona, Apr. 2002, 9.

  3. Mathayo 7:20 PM.

  4. Mathayo 7:21 PM.

  5. Teachings of Presidents of the Church: Harold B. Lee (2000), 197.

  6. 2  Nefi 28:30.

  7. Ona 1(nb} Wakorintho 11:28

  8. David A. Bednar, “The Atonement and the Journey of Mortality,” Liahona, Apr. 2012, 14.

  9. Joseph Fielding Smith, Doctrines of Salvation, comp. Bruce R. McConkie, 3 vols. (1954–56), 2:18.

  10. Spencer W. Kimball, “Give the Lord Your Loyalty,” Tambuli, Feb. 1981, 47.