2010–2019
Kuwa Mnyenyekevu
Aprili 2016


Kuwa Mnyenyekevu

Unyenyekevu unatuwezesha kuwa wazazi, wana na mabinti, waume na wake, majirani na marafiki bora.

Tumebarikiwa Kanisani kuwa na mkusanyiko wa nyimbo zinazotusaidia kuabudu kwa kupitia nyimbo. Katika mikutano yetu ya kanisani, “nyimbo zinaalika Roho wa Bwana, kutengeneza roho wa utulivu, kutuunganisha kama waumini, na kutupa njia ya kumsifu Bwana. Baadhi ya mahubiri makubwa yanahubiriwa kwa kuimba nyimbo.”1

Miaka michache tu baada ya kanisa kuundwa, ufunuo ulipokelewa na Nabii Joseph Smith kwa ajili ya mke wake Emma. Bwana alimuelekeza “achague baadhi ya nyimbo tukufu, kama atakavyopewa, ambazo zinampendeza yeye, kusikika katika kanisa lake.”2

Emma Smith aliweka pamoja mkusanyiko wa nyimbo ambazo mara ya kwanza zilitokea katika kitabu hiki cha nyimbo cha Kirtland mnamo mwaka 1836.3 Kulikuwa na nyimbo 90 tu zilizojumuishwa katika kijitabu hiki chembamba. Nyingi zilikuwa ni nyimbo kutoka katika imani ya Kiprotestanti. Ishirini na sita kati ya hizo zilitungwa na William W. Phelps, ambaye baadaye aliziandaa na kuzichapisha nyimbo hizo. Nyimbo peke yake ziliandikwa; hapakuwa na sauti zilizorandana na maneno haya. Kitabu hicho kidogo cha nyimbo kilidhihirisha kuwa baraka kwa waumini wa mwanzo wa Kanisa.

Picha
Ukurasa kutoka kwenye kitabu cha nyimbo cha Emma Smith
Picha
Ukurasa wa Kichwa kutoka kwenye kitabu cha nyimbo cha Emma Smith

Toleo la hivi karibuni kabisa la kitabu katika lugha ya kiingereza lilichapishwa mnamo mwaka wa 1985. Nyingi kati ya chaguo za Emma alizozichagua miaka mingi awali bado zimejumuishwa katika kitabu cha nyimbo, kama vile, “I know that My Redeemer Lives” na “How Firm a Foundation.”4

Wimbo mmoja ambao ulikuwa mpya katika kitabu cha1985 ni “Be Thou Humble.”5 Wimbo huu mahiri uliandikwa na Grietje Terburg Rowley, ambaye alifariki mwaka uliopita. Alijiunga na Kanisa mnamo mwaka 1950 kule Hawaii, ambapo alikuwa anafundisha shuleni. Dada Rowley alihudumu katika Kamati Kuu ya Muziki na akasaidia katika kutohoa nyimbo katika lugha mbali mbali. Alikita maandishi yake ya “Be Thou humble” kwenye mistari miwili ya maandiko: Mafundisho na Maagano 112:10 na Ether 12:27. Mstari huo katika Etheri unasema: “Na ikiwa watu watakuja kwangu nitawaonyesha udhaifu wao. Ninawapatia watu udhaifu ili katika udhaifu wao wawe wanyenyekevu; … kwani wakijinyenyekeza mbele yangu, na kuwa na imani ndani yangu, ndipo nitafanya vitu dhaifu kuwa vya nguvu kwao.

Kama ilivyo katika nyimbo za Kanisa, “Be thou Humble” unatufundisha ukweli rahisi na mkamilifu. Unatufundisha kwamba kama tukijinyenyekeza, maombi yetu yatajibiwa; tunafurahia amani ya roho; tunahudumu vyema sana katika miito yetu; na kama tutaendelea kuwa waaminifu, mwishowe tutarudi katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni.

Mwokozi alifundisha kuwa wafuasi Wake sharti wajinyenyekeze kama mtoto mdogo ili waweze kuingia mbinguni.6 Tunapolea watoto wetu, inabidi kuwasaidia waendelee kuwa wanyenyekevu wanapokua na kukomaa kuelekea utu uzima. Hatufanyi hivi kwa kuvunja mioyo yao kupitia kutokuwa wapole au kwa kuwa wenye ukali katika nidhamu zetu. Wakati tunakuza ujasiri binafsi na kujiamini, tunahitaji kuwafundisha thamani ya kujitegemea, upole, uraia wema, utiifu, kutokuwa na kiburi, kuelimika, na kutojifanya. Tunahitaji kuwafundisha kuwa na furaha katika mafanikio ya ndugu zao na marafiki. Rais Howard W. Hunter alifundisha kwamba “Haja yetu kuu ni mafanikio ya wenzetu.”7 Kama sivyo, watoto wetu wanaweza kupenda sana kujiinua na kufanya mengi kuwapita wengine, wivu, na kutofurahia ushindi wa wengine. Ninamshukuru mama ambaye, aliponiona kwamba ninajigamba sana, angesema, “mwanangu, unyenyekevu kidogo sasa hivi ungekupeleka mbali sana.”

Lakini unyenyekevu si kitu kilichowekwa kufundisha watoto tu. Lazima sote tujitahidi kuwa wanyenyekevu zaidi. Unyenyekevu ni muhimu sana katika kupata baraka za injili. Unyenyekevu unatuwezesha kuwa na mioyo iliyovunjika tunapotenda dhambi au kufanya makosa na kutuwezesha kutubu. Unyenyekevu unatuwezesha kuwa wazazi, wana na mabinti, waume na wake, majirani na marafiki bora.

Kwa upande mwingine, kiburi kinaweza kutenganisha mahusiano ya jamii, kuvunja ndoa, na kuharibu urafiki. Ni umuhimu sana kukumbuka unyenyekevu pale unapokaribia kuwa na ubishi ndani ya nyumba. Fikiria maumivu ya Roho unayoweza kuepuka kwa kujinyenyekeza kwa kusema “Samahani”, “Sikukufanyia vyema”; “Ungependa nifanye nini?”; “Nilikuwa sifikirii”; au “Ninajivunia wewe sana.” Kama vishazi hivi vifupi vingetumiwa kinyenyekevu, kungekuwa na mikwaruzano kidogo na amani tele katika nyumba zetu.

Kuishi maisha kwa urahisi kunaweza kuwa na mara nyingi ni uzoefu wa kunyenyekeza. Ajali na magonjwa, vifo vya wapendwa wetu, matatizo katika mahusiano, hata kurudi nyuma kiuchumi kunaweza kutunyenyekeza. Iwe uzoefu huu mgumu unatokana na makosa yetu wenyewe au kupitia kwa maamuzi na hukumu mbaya, majaribu haya yananyenyekeza. Kama tutachagua kuwa katika mawasiliano na roho na kuendelea kuwa wanyenyekevu na wakufundishika, sala zetu zinakubalika sana na imani na ushuhuda wetu unakua tunapoyashinda majaribu katika maisha yetu ya hapa duniani. Sisi sote tunatazamia kuinuliwa, lakini kabla ya hili kutokea, lazima tuvumilie kile kilichoelezewa kama “bonde la unyenyekevu.”8

Miaka mingi iliyopita, mtoto wetu Eric mwenye umri wa miaka 15 alipata majeraha mabaya kichwani. Nilipomuona kwenye wodi ya wagonjwa mahututi moyo wangu ulivunjika. Madaktari walituambia kwamba hawakuwa na uhakika nini kingetokea baadaye. Dhahiri, tulifurahi sana tulipoona kuwa alikuwa anapata fahamu. Tulifikiria sasa kwamba kila kitu kingekuwa sawa, lakini tulikosea.

Alipoamka, hakuweza kuongea, kutembea au kujilisha. Kibaya zaidi, hakuweza kukumbuka chochote. Aliweza kukumbuka karibu kila kitu kabla ya ajali, lakini alikuwa hana uwezo wa kukumbuka matukio baada ya, hata vitu ambayo vimetokea dakika chache awali.

Kwa muda, tulijawa na hofu kwamba tungekuwa na mwana aliyefungiwa katika akili ya mtoto wa miaka 15. Mambo yalikuwa rahisi kwa mwana wetu kabla ya ajali. Alikuwa mtu wa michezo, anajulikana, na alifanya vizuri shuleni. Kabla, maisha yake ya siku za usoni yalionekana kung’ara, sasa tulikwa na hofu kuwa hakuwa hata na maisha siku za usoni, angalau mmoja angekumbuka. Sasa hivi anajitahidi kujifunza jinsi ya kufanya vitu vya kimsingi. Huu ulikuwa ni muda wa kunyenyekeza sana. Ulikuwa ni muda wa kunyenyekeza kwa wazazi wake.

Hakika tulishangaa kwa nini kitu kama hicho kilitokea. Kila wakati tulikuwa tumejitahidi kufanya kitu sahihi. Kuishi injili ilikuwa ni jambo la kipaumbele katika familia yetu. Hatukuelewa kwa nini kitu cha uchungu kama hicho kingetokea kwetu. Tulilazimika kusali kwenye magoti mara tu baada ya kugundua kwamba kurekebishwa kungechukua miezi, hata miaka. Kigumu zaidi ilikuwa ni kugundua kidogo kidogo kwamba asingeweza kuwa kama alivyokuwa mwanzoni.

Wakati huu, machozi mengi yalitoka na sala zetu zikawa zinatolewa kwa dhati. Kupitia jicho la unyenyekevu, pole pole tulianza kuona, muujiza mdogo kwa mtoto wetu alioupata wakati huu wa uchungu. Akaanza kupata nafuu. Tabia yake na mtazamo wake ukabadilika.

Leo, mtoto wetu Eric amemuoa mwenza wake mwema, na wana watoto watano. Ni mwalimu mwenye upendo na anashiriki kwenye jamii, na kanisani vile vile. Cha muhimu, anaendelea kuishi katika roho ile ile ya unyenyekevu alioupata miaka mingi iliyopita.

Lakini je kama tungekuwa wanyenyekevu kabla ya kupitia “bonde la unyenyekevu”? Alma alifundisha:

“Heri wale ambao hunyenyekea wenyewe bila kulazimishwa kunyenyekea.”

“Ndio, wanabarikiwa sana zaidi kuliko wale wanaolazimishwa kuwa wanyenyekevu.”9

Ninashukuru kwa manabii, kama vile Alma, ambaye ametufundisha umuhimu wa sifa hii kuu. Spencer W. Kimball, Rais wa 12 wa Kanisa, alisema: “Je mtu anakuwaje mnyenyekevu? Kwangu mimi, kila mmoja wetu lazima akumbushwe utegemezi wetu. Tunamtegemea nani? Bwana. Tunajikumbushaje? Kwa maombi dhabiti, yenye msimamo, na shukrani.”10

Si ajabu kwamba wimbo alioupenda Rais Kimball “Nina Haja Nawe.”11 Mzee Dallin H. Oaks alitoa ripoti kwamba huu ulikuwa ni wimbo uliokuwa ukiimbwa mara nyingi kama wimbo wa kufungulia katika mahekalu miaka ya mwanzoni akiwa katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Weka taswira kwenye msisimuko wa kiroho uliojaa mkono wa watumishi wa Bwana wanapoimba wimbo huo kabla ya kusali kwa ajili ya mwongozo katika kutimiza wajibu wao mkubwa.”12

Ninashuhudia umuhimu wa unyenyekevu katika maisha yetu. Ninashukuru kwa watu kama Dada Grietje Rowley ambao wameendelea kuwainua watu kupitia maneno na muziki ambao unatusaidia kujifunza mafundisho ya injili ya Yesu Kristo, ambayo inajumuisha unyenyekevu. Ninashukuru kuwa tuna urithi wa nyimbo, ambao hutusaidia kuabudu kupitia nyimbo, na ninashukuru kwa ajili ya unyenyekevu. Ni maombi yangu kwamba tujitahidi kuishi kwa unyenyekevu katika maisha yetu ili tuweze kuwa wazazi, wana na mabinti, na wafuasi wa mwokozi. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Dibaji ya Urais wa Kwanza,” Hymns of The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints (1985), ix.

  2. Mafundisho na Maagano 25:11.

  3. Huu ukurasa wa kichwa wa toleo la kwanza la kitabu cha nyimbo ni la mwaka wa 1835, lakini halikukamilika na kuwezekana kupatikana mpaka 1836 mapema.

  4. Nyimbo 26 ambazo zilikuwepo katika kitabu cha nyimbo cha 1835 zimejumuishwa katika kitabu chetu cha sasa (ona Kathleen Lubeck, “The New Hymnbook: The Saints Are Singing!” Ensign, Sept. 1985, 7).

  5. “Be Thou Humble,” Hymns, no. 130.

  6. Ona Mathayo 18:1–4.

  7. Howard W. Hunter, “The Pharisee and the Publican,” Ensign, May 1984, 66.

  8. Anthon H. Lund, in Conference Report, Apr. 1901, 22.

  9. Alma 32:16, 15.

  10. The Teachings of Spencer W. Kimball, ed. Edward L. Kimball (1982), 233.

  11. Ona “I Need Thee Every Hour,” Hymns, no. 98; Brent H. Nielson, “I Need Thee Every Hour,” Ensign, Apr. 2011, 16.

  12. Dallin H. Oaks, “Worship through Music,” Ensign, Nov. 1994, 10.