2010–2019
Uchaguzi
Aprili 2016


Uchaguzi

Natuweze daima kuchagua yaliyo magumu ya haki, badala ya yaliyo rahisi ya makosa.

Ndugu na dada, kabla ya kuanza ujumbe wangu rasmi leo hii, ningependa kutangaza mahekalu manne mapya ambayo, katika miezi na miaka ijayo, yatajengwa katika maeneo yafuatayo: Quito, Ecuador; Harare, Zimbabwe; Belém, Brazil; na hekalu la pili katika Lima, Peru.

Wakati nilipopewa mwito kuwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili mwaka wa 1963, kulikuwepo na mahekalu 12 yaliyokuwa yakitumika katika Kanisa zima. Pamoja na kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Provo City Center wiki mbili zilizopita, kunayo mahekalu 150 yanayotumika kote duniani. Ni shukrani iliyoje tuliyo nayo kwa baraka tunazopokea katika nyumba hizi takatifu.

Sasa, ndugu na dada, ningependa kutoa shukrani kwa nafasi ya kushiriki mawazo kadhaa nanyi asubuhi ya leo.

Nimekuwa nikifikiria hivi majuzi kuhusu chaguzi. Imesemekana kwamba mlango wa historia hugeuka kwenye mabawaba madogo, na hivyo pia maisha ya watu. Chaguzi tunazofanya huamua hatima yetu.

Tulipoondoka katika maisha kabla ya hapa duniani na kuingia katika mauti, tulikuja na zawadi ya uhuru wa kujiamulia. Lengo letu ni kupata utukufu wa selestia, na uchaguzi tunaofanya utaweza, pakubwa, kuamua ikiwa tutafikia lengo letu au la.

Wengi wenu mnafahamu Alice katika riwaya ya Lewis Carroll ya Alice’s Adventures in Wonderland. Mtakumbuka kwamba anapatana na njia panda na njia mbili mbele yake, kila moja ikinyooka kwenda mbele lakini kwenye mwelekeo kinyume. Huku akitafakari upande gani wa kuelekea, anakabiliwa na yule paka Cheshire, ambaye Alice anamuuliza, “Njia ipi nitafuata?

Yule paka anajibu, “Inategemea na wapi unapotaka kwenda. Kama hujui mahali unapotaka kwenda, haijalishi njia utakayochagua.”1

Tofauti na Alice, tunajua tunapotaka kwenda, na inajalisha njia ambayo tutachagua, kwa vile njia tunayofuata maishani humu inaelekea hadi hatima yetu katika maisha yajayo.

Na tuweze kuchagua kujenga imani ndani yetu, imani kubwa na yenye nguvu ambayo itakuwa kinga yetu yenye ufanisi zaidi dhidi ya mipango ya adui—imani ya kweli, aina ya imani ambayo itatuimarisha na itasaidia hamu yetu ya kuchagua haki. Bila imani kama hii, hatuendi popote. Tukiwa nayo, tunaweza kutimiza malengo yetu.

Ingawa ni lazima tuchague kwa busara, kuna wakati ambapo tutafanya uchaguzi usio wa busara. Zawadi ya kutubu, iliyotolewa na Mwokozi wetu, inatuwezesha kurekebisha mwelekeo wetu, ili tuweze kurudi katika njia ambayo itatuongoza hadi kwenye ule utukufu selestia tunaoutafuta.

Natuweze kuendelea kuwa na ujasiri wa kupinga yanayokubaliwa na wengi. Natuweze daima kuchagua yaliyo magumu ya haki, badala ya yaliyo rahisi ya makosa.

Tunapotafakari uamuzi tunaofanya maishani mwetu kila siku—kama ni kufanya uchaguzi huu au ule mwingine—ikiwa tutamchagua Kristo, tutakuwa tumefanya uchaguzi sahihi.

Kwamba hili na liweze kuwa hivyo ni sala yangu ya dhati na ya unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, amina.

Muhtasari

  1. Imetolewa kutoka Lewis Carroll, Matukio ya Alice kule Wonderland (1898), 89.