2010–2019
Familia za Milele
Aprili 2016


Familia za Milele

Majukumu yetu ya ukuhani ni kuziweka familia zetu na familia za wale wanaotuzunguka katikati ya mawazo yetu.

Nina shukrani kuwa pamoja nanyi jioni hii katika kikao kikuu cha ukuhani cha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Huu ni wakati mzuri katika historia ya Kanisa. Miaka mia moja na themanini na mbili iliyopita katika mwaka 1834, huko Kirtland, Ohio, makuhani wote waliitwa kukusanyika pamoja kwenye nyumba ya shule ya futi-14-kwa-14 (mita 4.2 kwa 4.2) ililojengwa kwa mbao. Katika mkutano huo Nabii Joseph Smith inaripotiwa akisema: “Hamjui kamwe hatma ya Kanisa na ufalme huu kuliko mtoto aliye mapajani mwa mama yake. Hamuelewi. … Ni wachache tu kidogo wenye Ukuhani mnaoweza kuwaona hapa usiku wa leo, lakini Kanisa hili litaijaza Amerika ya Kaskazini na Kusini—litaijaza dunia.”1

Mamilioni ya wenye ukuhani, katika zaidi ya nchi 110, wamekusanyika kwa kikao hiki. Huenda Nabii Joseph aliuona wakati huu na ule mzuri wa baadaye mbele yetu.

Ujumbe wangu jioni hii ni jaribio la kuelezea wakati wa usoni na tunachotakiwa kufanya ili kuwa sehemu ya mpango wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni aliouandaa kwa ajili yetu. Kabla hatujazaliwa, tuliishi katika familia pamoja na Baba yetu wa mbinguni aliye wa milele aliyeinuliwa. Aliutawaza mpango ambao unatuwezesha kuendelea na kuwa kama Yeye. Alifanya hivyo kwa upendo Wake kwetu. Lengo la mpango huu lilikuwa ni kutuwezesha kupata nafasi ya kuishi milele kama aishivyo Baba yetu wa Mbinguni. Mpango huu wa injili ulitupa sisi maisha ya mwili ambayo tunaweza kujaribiwa. Ahadi ilitolewa kwamba kupitia kwa Upatanisho wa Yesu Kristo, kama tulitii sheria na ibada za ukuhani za injili, tutakuwa na uzima wa milele, zawadi kuu ya zawadi Zake zote.

Uzima wa milele ni aina ya maisha ambayo Mungu Baba wa Milele huishi. Mungu amesema kwamba lengo Lake ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa wanadamu” (Musa 1:39). Lengo kubwa la kila mwenye ukuhani ni kusaidia katika kazi ya kuwasaidia watu kuinukia kwenye uzima wa milele.

Kila jitihada ya ukuhani na kila ibada ya ukuhani ina nia ya kusaidia watoto wa Baba wa Mbinguni wabadilishwe kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo kuwa wana wa vitengo vya familia kamilifu. Hivyo basi “kazi kubwa ya kila mtu ni kuamini injili, kutii amri, na kujenga na kuimarisha kitengo cha familia,”2 na kuwasaidia wengine wafanya vivyo hivyo.

Kwa kuwa huo ni ukweli, kila kitu tunachokifanya lazima ndoa ya selestia iwe kitovu na lengo lake. Hiyo ina maana kuwa ni lazima tujitahidi kuunganishwa na mwenza wa milele katika hekalu la Mungu. Lazima pia tuwatie moyo wengine kufanya na kutii maagano ambayo yanawaunganisha pamoja mume na mke pamoja, pamoja na familia yao, katika maisha haya na ulimwengu ujao.

Kwa nini jambo hili ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu—kijana au mzee, shemasi au kuhani mkuu, mwana au baba? Ni kwa sababu majukumu yetu ya ukuhani ni kuziweka familia zetu na familia za wale wanaotuzunguka katikati ya kitovu cha uzingativu. Kila uamuzi mkubwa unatakiwa kuzingatia athari itakayo kuwa juu ya familia ili kufuzu kuishi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Hakuna kitu muhimu katika huduma ya ukuhani zaidi ya hilo.

Acheni niwaambie hii ina maana gani kwa shemasi anayesikiliza jioni hii kama mshiriki wa kitengo cha familia na mshiriki wa akidi.

Katika familia yake, huenda pakawa au pasiwe na sala ya familia au mkutano wa Jioni wa familia ya nyumbani kila mara. Kama baba yake, akihisi majukumu haya, aiite familia pamoja kwa ajili ya sala au kusoma maandiko, shemasi anaweza kukimbilia kushiriki akiwa na tabasamu. Anaweza kuwatia moyo kaka na dada zake kushiriki na kuwasifia wanapofanya hivyo. Anaweza kumwomba baba yake baraka wakati shule zinapoanza au wakati mwingine wa shida.

Huenda hana baba mwaminifu. Lakini tamanio la moyo wake kwa yale matukio litaleta nguvu za mbinguni kwa wale wanaomzunguka kwa sababu ya imani yake. Watatafuta maisha ya familia ambayo shemasi anataka kwa moyo wake wote.

Mwalimu katika Ukuhani wa Haruni anaweza kuona katika wajibu wake wa ualimu wa nyumbani nafasi ya kumsaidia Bwana kubadilisha maisha ya familia. Bwana alishauri katika Mafundisho na Maagano:

“Kazi ya mwalimu ni kuliangalia kanisa daima, na kuwa nalo, na kuwaimarisha;

“Na kuona kwamba hakuna uovu katika kanisa, wala kuzozana baina yao, wala kudanganya, kusengenya, wala kusemana mabaya” (M&M 20:53–54).

Vivyi hivyo, kuhani katika Ukuhani wa Haruni anapewa wajibu:

“Kazi ya kuhani ni kuhubiri, kufundisha, kuelezea, kushawishi, na kubatiza, na kuhudumia sakramenti,

“Na kutembelea nyumba ya kila muumini, na kuwashawishi kusali kwa sauti na kwa siri na kushiriki kazi zote za familia”(M&M 20:46–47).

Unaweza kushangaa, kama nilivyofanya nilipokuwa mwalimu kijana na kuhani, jinsi ulimwenguni uliweza kuzikabili changamoto hizo. Sikuwa na uhakika kamwe jinsi mimi ningeweza kuwahimiza kwa njia ambayo ingeweza kuipeleka familia kuelekea uzima wa milele bila kuwakwaza au kuonekana kukosoa. Nimejifunza kwamba ni kusihi ambako kunabadilisha mioyo hutoka kwa Roho Mtakatifu. Hayo hutokea mara nyingi tunapotoa ushahuda wa Mwokozi, ambaye alikuwa na ni mwana familia mkamilifu. Tukiwa tunalenga upendo wetu Kwake, maelewano na amani itakua katika nyumba tunazotembelea. Roho Mtakatifu atakuwa nasi katika huduma yetu kwa familia.

Kijana mwenye ukuhani anaweza, kwa jinsi anavyoomba, kwa jinsi anavyoongea, na kwa jinsi anavyowapa moyo wanafamilia, kuleta ushawishi na mfano wa Mwokozi katika akili zao na mioyo yao.

Mmoja wa viongozi wa ukuhani mwenye hekima alinionyesha mimi kwamba alielewa hilo. Alimwomba kijana wangu mdogo kuongoza katika matembezi ya ualimu wa nyumbani. Alisema kwamba familia inaweza kukinza ushawishi wake, lakini alifikiri mafundisho rahisi na ushuhuda wa kijana unaweza kupenyeza ndani ya mioyo yao migumu.

Ni nini kijana anaweza kufanya kusaidia katika uumbaji wa familia za milele? Anaweza akawa karibu aende misheni. Anaweza kuomba kwa moyo wake wote kwamba aweza kutafuta, fundisha, na kubatiza familia. Bado ninamkumbuka kijana mwema akiwa na bi arusi wake na mabinti zao wawili wakiwa wamekaa nami na mmisionari mwenzangu siku moja. Roho Mtakatifu alinijia na kuwashuhudia kwamba injili ya Yesu Kristo imerejeshwa. Waliamini kabisa hata waliomba kama tungewapa mabinti zao wawili baraka kama walivyoona kwenye kipindi cha sakramenti. Tayari walikuwa wametamani watoto wao wapate baraka, lakini walikuwa bado hawaelewi kwamba baraka za kweli zingewezekana tu katika mahekalu ya Mungu baada ya kuweka maagano.

Bado ninahisi maumivu kufikiria juu ya wale wana ndoa na wale mabinti, huenda sasa wamekua, bila ya ahadi ya familia milele. Wazazi wao angalao walikuwa na fununu ya baraka ambazo zingeweza kupatikana kwao. Tumaini langu ni kwamba wao kwa namna fulani, mahali fulani wanaweza kuwa na fursa ya kufuzu kuwa familia ya milele.

Wazee wengine waendao misheni watakuwa na uzoefu wa furaha kama wa Matthew mwana wangu. Yeye na mwenza wake walikutana na mjane mwenye watoto nane wakiishi katika umaskini. Alitaka wao wapate kile mnachotaka—kuwa na familia ya milele. Kwa mwana wangu, ilionekana haiwezekani au kwa kipindi kile tu.

Nilizuru mji ule mdogo miaka kadhaa baada ya mwana wangu kumbatiza yule mjane, na yeye alinialika kukutana na familia yake. Ilibidi nisubiri kidogo kwa sababu watoto wake, na wajukuu wake wengi, walikuja kutoka nyumba kadhaa za ibada katika eneo. Mwana mmoja alikuwa akihudumu kwa uaminifu kwenye uaskofu, na kila mmoja wa watoto wake alibarikiwa na maagano ya hekalu na kuunganishwa katika familia ya milele. Nilipoondoka kutoka kwa dada huyu mpendwa, aliweka mikono yake kiunoni mwangu (alikuwa mfupi sana, hata angeweza kufikia kiunoni mwangu) na alisema, “Tafadhali, mwambie Mateo aje Chile kabla sijafa.” Alikuwa amepewa, kwa sababu ya wale wazee watiifu, matarajio ya baraka kuu kati ya zote zilizo kuu za Mungu.

Kuna mambo ambayo mzee, anaporudi toka misheni, lazima afanye kuwa mkweli katika dhamira ya kupata uzima wa milele kwake mwenyewe wale awapendao. Hakuna dhamira muhimu zaidi katika wakati au katika milele kuliko ndoa. Mmesikia shauri la hekima kuipa ndoa kipaumbele katika mipango ya mapema baada ya misheni. Mtumishi mkamilifu wa ukuhani atatenda kwa hekima.

Katika kufikiria ndoa, ataona kwamba anachagua wazazi wa watoto wake na urithi watakao kuwa nao. Atafanya uchaguzi kwa uchambuzi wa kina na kwa maombi. Yeye atahakikisha kwamba mtu anayemuoa anashiriki mawazo yake juu ya familia, imani yake ya kusudi kwa Bwana kwa ajili ya ndoa, na kwamba yeye ni mtu ambaye angekuwa tayari kuamini furaha ya watoto wake.

Rais N. Eldon Tanner alitoa ushauri wa busara: “Wazazi ambao utawaheshimu kuliko wengine ni wale wazazi wa watoto wako watarajiwa. Wale watoto wanastahili kuwa na wazazi wema kitu ambacho kinawezekana kuwapa—wazazi wasafi.”3 Usafi utakuwa kinga na kinga ya watoto wote. Una deni lao la hizo baraka.

Sasa, kuna waume na akina baba wanaosikiliza usiku huu. Unaweza kufanya nini? Tumaini langu ni kwamba tamanio lako limeongezeka la kufanya mabadiliko muhimu kwako na familia yako kuishi katika ufalme wa selestia siku moja. Kama baba mwenye ukuhani, ukiwa na mke wako pembeni, unaweza kugusa mioyo ya kila mwana familia ili kuwahamasisha kuitazamia siku ile. Utahudhuria mikutano yako ya sakramenti na familia yako, utakuwa ukifanya mikutano ya familia ambayo Roho Mtakatifu anaalikwa, utakuwa ukiomba na mke na familia yako, na kujiandaa kuipeleka familia yako hekaluni. Utatembea nao pamoja kwenda nyumba ya familia ya milele.

Utamtendea mke na watoto wako kama vile Baba wa Mbinguni alivyokutendea wewe. Utafuata mfano na mwongozo wa Mwokozi ili kuiongoza familia yako katika njia Yake.

“Hakuna nguvu au uwezo unaoweza au upaswao kudumishwa kwa njia ya ukuhani, isipokuwa tu kwa njia ya ushawishi, kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki;

“Kwa wema, na maarifa safi, ambayo yataikuza sana nafsi isiyo na unafiki, na isiyo na hila—

“Kukemea kwa ukali kwa wakati wake, utakapokuwa umeongozwa na Roho Mtakatifu; na halafu baadaye kuonyesha ongezeko la upendo kwa yule uliyemkemea, asije akakudhania wewe kuwa ni adui yake” (M&M 121:41–43).

Bwana amewaambia akina baba wenye ukuhani wanatakiwa kuwa akina baba na waume wa aina gani. Anasema. “Mpende mke wako kwa moyo wako wote, na utaambatana na yeye tu na siyo mwingine” (M&M 42:22). Wakati Bwana anapoongea na wote mume na mke, anaamuru, “usi … zini, … wala kufanya kitu kama hicho” (M&M 59:6).

Kwa vijana, Bwana ameweka kiwango. “Watoto, watiini wazazi wenu: kwani hili lampendeza Bwana” (Wakolosai 3:20), na “waheshimu baba yako na mama yako” (Kutoka 20:12).

Wakati Bwana anaponena na wote katika familia, ushauri Wake ni kupendana na kusaidiana.

Anatutaka sisi “kujitahidi kuimarisha maisha ya kila [mwanafamilia]; kuimarisha wadhaifu; kuwarudisha [wale] wapendwa waliopotea, na kufurahi kwa nguvu zao mpya za kiroho.”4

Bwana pia anataka kwamba tufanye kila tuwezalo ili kuwasaidia wale mababu zetu kuwa pamoja nasi katika nyumba ya milele.

Kiongozi wa makuhani wakuu aliyefanyakazi kwa bidii kuwasaidia watu kuwatafuta mababu zao na kuyapeleka majina hekaluni ili kuwaokoa wale waliotangulia. Kutakuwa na shukrani katika ulimwengu ujao kwa wale makuhani wakuu, na kwa wale wanaotoa ibada, kwa sababu hawakusahau familia zao zinazosubiri katika ulimwengu wa roho.

Manabii wamesema: “Kazi ya Bwana iliyo muhimu sana ambayo utaweza kuifanya itakuwa ni kazi unayoifanya ndani ya kuta za nyumba yako mwenyewe. Ualimu wa Nyumbani, kazi ya uaskofu, na kazi nyingine za kanisa zote ni muhimu, lakini kazi iliyo muhimu sana ipo ndani ya kuta za nyumba yako mwenyewe.”5

Katika nyumba zenu, na katika huduma zetu za ukuhani, thamani kubwa itakuwa kwenye matendo madogo yanayotusaidia sisi na wale tunaowapenda kuelekea maisha ya milele. Matendo hayo yaweza kuonekana madogo katika maisha haya, lakini yataleta baraka za milele.

Tunapokuwa waaminifu katika kuhudumu kwetu kuwasaidia watoto wa Baba wa Mbinguni kurudi Kwake, tutastahili kwa salamu ambazo wote tunazihitaji kuzisikia tunapomaliza utumishi wetu wa duniani. Haya ndiyo maneno: “Vema, mtumishi mwema na mwaminifu: umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakufanya kuwa mtawala juu ya mambo mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mathayo 25:21).

Miongoni mwa hayo “mambo mengi” ni ahadi ya vizazi visivyo na mwisho. Sala yangu ni kwamba sote tuweze kustahili na kuwasaidia wengine wastahili baraka hizo katika nyumba ya Baba Yetu wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 137.

  2. Bruce R. McConkie, in Conference Report, Apr. 1970, 26.

  3. N. Eldon Tanner, Church News, Apr. 19, 1969, 2.

  4. Bruce R. McConkie, in Conference Report, Apr. 1970, 27.

  5. Harold B. Lee, Decisions for Successful Living (1973), 248–49.