2010–2019
Baraza za Familia
Aprili 2016


Baraza za Familia

Wakati wazazi wamejitayarisha na watoto kusikiliza na kushiriki katika mjadala, baraza la familia kwa kweli linafanya kazi!

Akina ndugu na dada, suala la kejeli kuhusu kuwa wazazi ni kwamba sisi huwa wazazi bora baada ya watoto kuwa wakubwa. Nitashiriki nanyi alasiri hii kitu ambacho ninatamani kwamba ningelikuwa nimeelewa vyema wakati Barbara nami tulipoanza kuwalea watoto wetu wenye thamani.

Wakati wa huduma yangu ya utume, mara nyingi nimesisitiza nguvu na umuhimu wa mabaraza ya Kanisa, pamoja na misheni, kigingi, kata na mabaraza saidizi.

Ninaamini ya kwamba mabaraza ni njia bora ya ufanisi ya kupata matokeo halisi. Kwa kuongezea, ninajua mabaraza ni njia ya Bwana na kwamba aliumba vitu vyote ulimwenguni kupitia baraza la mbinguni, kama ilivyotajwa katika maandiko matakatifu.1

Kufikia sasa, hata hivyo, sijawahi kuzungumza katika mkutano mkuu kuhusu la msingi zaidi—na pengine la muhimu zaidi—kati ya mabaraza yote: baraza la familia.

Mabaraza ya familia yamehitajika kila mara. Na hakika, ni ya milele. Tulikuwa washiriki katika baraza la familia katika maisha kabla ya ulimwengu, wakati tulipoishi na wazazi wetu wa mbinguni kama watoto wao wa kiroho.

Baraza la familia, linapoendeshwa kwa upendo na kwa sifa kama za Kristo, litakabiliana na athari za teknolojia za kisasa ambazo kila mara hutuzuia kutokana na kuwa na wakati mwema na kila mmoja wetu na pia huelekea kuleta mabaya nyumbani mwetu.

Tafadhali kumbukeni kwamba mabaraza ya familia ni tofauti na mkutano wa Jioni na familia nyumbani kila Jumatatu. Mikutano ya jioni kimsingi hulenga mafundisho ya injili na shughuli za familia. Mabaraza ya familia, kwa upande mwingine, yanaweza kufanyika siku yoyote ya wiki, na kimsingi ni mkutano ambao wazazi husikiliza—kila mmoja wao na watoto wao.

Ninaamini ya kwamba kunayo aina nne ya mabaraza ya familia:

Kwanza, baraza kuu la familia linalojumuisha kila mshiriki wa familia.

Pili, baraza tendaji la familia linalojumuisha mama na baba.

Tatu, baraza ndogo la familia linalojumuisha wazazi na mtoto mmoja.

Nne, baraza la mmoja kwa mmoja la familia linalojumuisha mzazi mmoja na mtoto mmoja.

Katika mazingira haya yote ya baraza la familia, vifaa vya kielektroniki vinahitaji kuzimwa ili kila mtu aweze kutazama na kusikiliza kila mmoja. Wakati wa mabaraza ya familia na wakati mwingine unaofaa, waweza kutaka kuwa na kikapu cha vifaa vya elektroniki ili wakati familia inapokutana, kila mtu—pamoja na mama na baba—wanaweza kuweka simu zao, tarakilishi, na vifaa vya MP3 vya kucheza muziki ndani ya kikapu hicho. Baada ya hapo, wanaweza kushauriana bila ya kujaribiwa kujibu ujumbe wa Facebook, ujumbe mdogo wa simu, Instagram, Snapchat, au viashiria vya barua pepe.

Acheni nishiriki nanyi kwa kifupi jinsi aina hii ya mabaraza ya familia inaweza kufanya kazi.

Kwanza, baraza zima la familia linajumuisha washiriki wote wa familia.

Kijitabu cha Kanisa kinachoitwa Familia Yetu kinasema, “Baraza hili linaweza kukutana kujadiliana shida za familia, kujadili kuhusu fedha, kufanya mipango, kusaidia na kuimarisha kila mmoja, kuombea kila mmoja na familia.”2

Baraza hili linafaa kukutana kwa wakati uliotengwa na kwa kawaida linakuwa rasmi kuliko aina nyingine yoyote ya baraza la familia.

Linafaa kuanza kwa maombi, au laweza kuwa muendelezo wa mazungumzo ambayo yalikuwa yameanza katika mazingira tofauti. Tafadhali fahamu kwamba baraza la familia linaweza kutokuwa na mwanzo au mwisho rasmi siku zote.

Wakati wazazi wamejitayarisha na watoto kusikiliza na kushiriki katika mjadala, baraza la familia kwa kweli linafanya kazi!

Haijalishi hali ya familia yetu, ni muhimu tuelewe hali ya kipekee ya kila mshiriki wa familia. Ingawaje twaweza kuwa tunashiriki DNA sawa, kunaweza kuwa na hali miongoni mwetu ambazo zinaweza kutufanya tuwe tofauti kabisa na kila mmoja wetu na ambazo zinaweza kuhitaji ushirikiano wa huruma wa baraza la familia.

Kwa mfano, mazungumzo yote na kushiriki na upendo wote duniani hauwezi kutatua shida za kimatibabu au shida ya kihisia ambayo mshiriki mmoja wa familia au zaidi wanaweza kuwa wanakabiliana nayo. Kwa wakati kama huu, baraza la familia huwa mahala pa umoja, uaminifu, na usaidizi wa upendo huku usaidizi wa nje ukijumuishwa katika kutafuta suluhisho.

Ndugu, hasa walio na umri mkubwa, wanaweza kuwa washauri wa nguvu kwa watoto wadogo ikiwa wazazi watatumia baraza la familia kujumuisha usaidizi wao wakati wa shida na shinikizo.

Katika njia hii, familia ni kama kata. Wakati askofu anapojumuisha washiriki wa baraza la kata, anaweza kutatua shida na kukamilisha mema katika njia ambazo kamwe hangeweza bila usaidizi wao. Katika njia hiyo hiyo, wazazi wanahitaji kujumuisha kila mshiriki wa familia katika kukabiliana na changamoto na shida. Kwa njia hiyo, nguvu ya baraza la familia inafanya kazi. Wakati washiriki wa familia wanahisi wamejumuishwa katika uamuzi, wao huunga mkono na matokeo mazuri yanaweza kupatikana.

Si kila baraza la familia linajumuisha wazazi wawili na watoto. Baraza la familia yenu laweza kuwa tofauti na jinsi baraza la familia yetu lilikuwa wakati tulipokuwa tukiwalea watoto wetu saba. Leo baraza la familia yetu linajumuisha Barbara na mimi, isipokuwa tunapokuwa na baraza la familia pana ambalo linajumuisha watoto wetu wakubwa, wake na waume zao, na mara nyingine wajukuu wetu na vitukuu.

Wale ambao hawajafunga ndoa na hata wanafunzi wanaoishi mbali na nyumbani wanaweza kufuata utaratibu mtakatifu wa baraza kwa kukutana na marafiki na wale wanaoishi nao kushauriana pamoja.

Zingatia namna mazingira katika ghorofa ingebadilika ikiwa wanaoishi pamoja wangekutana mara kwa mara kuomba, kusikiliza, kujadiliana, na kupanga vitu pamoja.

Kila mtu anaweza kuanza kuwa na baraza la familia na kufaidika na utaratibu huu mtakatifu ulioanzishwa na Baba wa Mbinguni mwenye upendo.

Kama ilivyosemwa hapo awali, mara kwa mara baraza la familia pana linaweza kuwa lenye manufaa. Baraza familia pana linaweza kuwa na kina babu na watoto wazima wasioishi nyumbani. Hata kama kina babu au watoto wazima wanaishi mbali, wanaweza kushiriki katika mabaraza ya familia kwa njia ya simu, Skype, au FaceTime.

Unaweza kutaka kuzingatia kuwa na baraza la jumla la familia Jumapili, ambayo ni siku ya kwanza ya wiki; familia zinaweza kufanya mapitio ya wiki iliyopita na kufanya mipango ya wiki ijayo. Hii inaweza kuwa hasa kile familia yako inahitaji kuifanya Sabato kuwa tukio la kupendeza.

Aina ya pili ya baraza la familia ni baraza tendaji la familia ambalo linahusisha tu wazazi. Wakati huu pamoja, wazazi wanaweza kufanya mapitio ya mahitaji na maendeleo ya kimwili, kihisia, na kiroho ya kila mtoto.

Baraza tendaji la familia pia ni wakati mzuri wa wake na waume zao kuzungumza kuhusu uhusiano wao kibinafsi na kila mmoja wao. Wakati Mzee Harold B. Lee alipotuunganisha, alitufundisha kanuni ambayo ninaamini kila wanandoa wataipata kuwa yenye usaidizi. Alisema, “Msiwahi kwenda kulala bila kupiga magoti pamoja, kushikana mikono, na kusali. Sala kama hizi humwalika Baba wa Mbinguni kutushauri kupitia nguvu ya Roho.”

Aina ya tatu ya baraza la familia ni baraza ndogo la familia. Hapa, wazazi wote huwa na wakati na mtoto mmoja binafsi katika mazingira rasmi au yasiyo rasmi. Hii ni nafasi ya kuwa na mazungumzo kuhusu kufanya uamuzi mapema kuhusu mambo kama ni nini atafanya au hatafanya katika siku zijazo. Wakati uamuzi wa aina hii unapofanywa, anaweza kutaka kuurekodi kwa kumbukumbu za baadaye ikihitajika. Ikiwa mwana wako au binti yako atakutambua kama msaidizi wake wa dhati, mkutano huu wa baraza unaweza kuanzisha malengo ya siku zijazo. Huu pia ni wakati wa kusikiliza kwa makini kuhusu wasiwasi mkubwa na changamoto ambazo mtoto anaweza kuwa anakumbana nazo kama ukosefu wa kujiamini, unyanyasaji, uonevu, au hofu.

Aina ya nne ya baraza la familia baraza la mmoja kwa mmoja la familia linalojumuisha mzazi mmoja na mtoto mmoja. Aina hii ya baraza la familia kwa ujumla hufanyika tu. Kwa mfano, mzazi na mtoto wanaweza kufaidika kwa nafasi zisizo za rasmi wakati ambapo wanasafiri garini au wanapofanya kazi nyumbani. Matembezi na mtoto mmoja pamoja na baba au mama yanaweza kutoa nafasi maalum ya kiroho au kihisia ya kuwa na uhusiano wa karibu. Weka kwenye kalenda haya mapema ili watoto waweze kutarajia wakati maalum pekee yao na Mama au Baba.

Sasa, kina ndugu na kina dada, kuna wakati ambapo kuta za nyumbani zilitoa kinga yote tuliyohitaji dhidi ya kuingiliwa na ushawishi wa nje. Tulifunga milango, tukafunga madirisha: tukafunga malango, na tukajihisi salama, na tuliolindwa katika kimbilio letu ndogo kutokana na ulimwengu.

Siku hizo sasa zimepita. Kuta, milango, ua, na malango ya nyumba zetu hayawezi kuzuia uvamizi usioonekana kutokana na Mtandao wa mawasiliano, Wi-Fi, simu za mikono, mitandao. Inaweza kuingia katika nyumba zetu kupitia tu kubonyeza na kuandika.

Kwa bahati nzuri, Bwana ametoa njia ya kukabiliana na uvamizi mbaya wa teknolojia ambao unaweza kutuzuia kutokana na kuwa na wakati mwema na kila mmoja wetu. Amefanya hivi kwa kuleta mfumo wa baraza kuimarisha, kukinga, kulinda, na kukuza uhusiano wetu wa thamani kubwa zaidi.

Watoto wanahitaji sana wazazi ambao wako tayari kuwasikiliza, na baraza la familia linaweza kutoa nafasi ambapo washiriki wa familia wanaweza kujifunza kuelewa na kupendana.

Alma alifundisha, “Shauriana na Bwana kwenye matendo yako yote, na atakuongoza kwa yale mema.”3 Kumwalika Bwana kushiriki katika baraza lenu la familia kupitia maombi kutaboresha uhusiano wetu na kila mmoja wetu. Tunaweza, kwa usaidizi wa Baba wa Mbinguni na Mwokozi, kuwa wavumilivu, wazingativu, wenye kutoa usadizi, wenye kusamehe, na kuelewa tunaposali tupate usaidizi. Pamoja na usaidizi wao, tunaweza kufanya nyumbani mwetu kuwa kiasi kidogo cha mbinguni hapa duniani.

Baraza la familia linalofuata utaratibu kama mabaraza ya mbinguni, yaliyojazwa na upendo kama wa Kristo, na kuongozwa na Roho wa Bwana litatusaidia kulinda familia zetu dhidi ya mambo ambayo yanaweza kupoteza wakati wetu wa thamani wa kuwa pamoja na kutulinda kutokana na maovu ya dunia.

lkijumuishwa na maombi, baraza la familia litaalika uwepo wa Mwokozi, kama alivyoahidi. “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, mimi nipo papo hapo katikati yao.”4 Kumwalika Roho wa Bwana kushiriki katika mabaraza yetu ya familia huleta baraka zisizoweza kuelezeka.

Hatimaye, tafadhali kumbukeni ya kwamba baraza la familia ambalo hufanywa mara kwa mara litatusaidia kutambua shida za familia mapema na kuzitatua mapema; mabaraza yatampa kila mshiriki wa familia hisia ya kuwa na thamani na umuhimu; na zaidi ya yote yatatusaidia kuwa na mafanikio zaidi na furaha katika uhusiano wetu wa thamani, nyumbani kwetu. Na Baba wa Mbinguni atubariki familia zetu tunaposhauriana pamoja, ni maombi yangu ya unyenyekevu katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.