2010–2019
Kimbilio kutoka kwa Tufani
Aprili 2016


Kimbilio kutoka kwa Tufani

Kipindi hiki hakielezi sifa bainifu za wakimbizi, lakini mjibizo wetu utasaidia kueleza sifa zetu bainifu.

“Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; Nalikuwa na kiu, mkaninywesha; Nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

“Nilikuwa uchi, mkanivika. …

“… Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”1

Inakadiriwa kunao wakimbizi milioni 60 duniani kufikia sasa, hii ina maana kwamba “1 katika kila watu 122 … amelazimika kutoroka nyumbani kwao”2 na nusu ya hawa ni watoto.3 Inashtua kuzingatia idadi hii na kutafakari kuhusu maana ya haya katika maisha ya kila mmoja. Kazi yangu sasa hivi iko kule Ulaya, ambapo milioni moja na robo ya wakimbizi hawa wamewasili mwaka jana kutoka sehemu za mapigano makali kule Mashariki ya Kati na Afrika.4 Tunaona wengi wao wakija tu na zile nguo ambazo wamevalia na kile wanachoweza kubeba katika mfuko mmoja mdogo. Sehemu kubwa kati yao wamesoma vizuri, na wote imewabidi kutoroka nyumbani, shule, na kazi.

Chini ya uongozi wa Urais wa Kwanza, Kanisa linafanya kazi pamoja na mashirika 75 katika nchi 17 za Ulaya. Mashirika haya yanajumuisha taasisi kubwa za kimataifa na miradi midogo ya kijamii, kutoka mashirika ya serikali hadi miradi ya hisani ya dini na ya kilimwengu. Tuna bahati kushirikiana na kujifunza kutoka wengine ambao wamekuwa wakifanya kazi na wakimbizi kote duniani kwa miaka mingi.

Kama waumini wa Kanisa, kama binadamu, hatuhitaji kutazama nyuma sana katika historia yetu kuakisi juu ya wakati ambapo tulikuwa wakimbizi, tukifukuzwa kikatili kutoka nyumba zetu na mashamba yetu tena na tena. Wikiendi iliyopita akizungumza juu ya wakimbizi, Dada Linda Burton aliwauliza wanawake wa Kanisa kuzingatia “Kama hadithi yao ingekuwa hadithi yangu ?”5 Hadithi yao ni hadithi yetu, siyo miaka mingi iliyopita.

Kuna mijadala mikali serikalini katika jamii mbali mbali kuhusu kueleza sifa bainifu za mkimbizi na jambo linaloweza kufanywa kuwasaidia wakimbizi. Usemi wangu kwa njia yoyote ile hauna lengo la kujihusisha mijadala hii mikali, wala kusema juu ya sera za uamiaji, lakini badala kuwalenga watu ambao wamefukuzwa kutoka nyumbani kwao na nchini mwao kwa sababu ya vita ambavyo hawakuvianzisha.

Mwokozi anajua jinsi ilivyo kuwa mkimbizi—alikuwa mmoja. Kama mtoto mdogo, Yesu na familia yake walikimbilia Misri kutoroka panga za mauaji za Herodi. Na katika nyakati mbali mbali katika huduma Yake, Yesu alijipata akiwa ametishwa na maisha Yake yakiwa hatarini, hatimaye akajisalimisha kwa mipango ya binadamu waovu ambao walikuwa wamepanga kifo Chake. Pengine, wakati huo, ni ajabu zaidi alitufundisha tena na tena kupendana, kupenda jinsi anavyopenda, kupenda jirani yetu kama tunavyojipenda. Kwa kweli, “dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao”6 na “kuwaangalia maskini na wenye shida, na kuwapatia msaada ili kwamba wasiteseke.”7

Imetia msukumo kushuhudia vitu ambavyo waumini wa Kanisa kote ulimwenguni wametoa kwa ukarimu ili kuwasaidia watu binafsi na familia ambazo zimepoteza mengi sana. Kote kule Ulaya hasa, nimewaona waumini wengi wa Kanisa ambao wamehisi msisimko wa furaha na kujengwa kwa nafsi wakati ambapo wamejibu ile hamu ya ndani ya kutaka kuwahudumia wale walio na mahitaji makuu karibu nao. Kanisa limetoa makazi na huduma ya kimatibabu. Vigingi na misheni vimekusanya maelfu ya vifaa vya usafi. Vigingi vingine vimetoa vyakula na maji, mavazi, makoti ya mvua, baisikeli, vitabu, mifuko ya mabegani, na zaidi.

Watu binafsi kutoka Scotland na Sicily wametoa huduma ya kila aina inayoweza kufikirika. Madaktari na wauguzi wamejitolea na kutoa huduma mahala ambapo wakimbizi wanawasili wakiwa wamelowa maji, wakihisi baridi, na mara nyingi wakiwa na kiwewe kutokana na safari yao baharini. Wakati wakimbizi wanapoanza mchakato wa kupata makazi mapya, waumini katika maeneo hayo wanawasaidia kujifunza lugha ya nchi enyeji, huku wengine wakiinua roho za wazazi na watoto kwa kuwapa vitu vya kuchezea, vifaa vya sanaa, muziki, na michezo. Wengine wanachukua nyuzi zilizotolewa, sindano za kufuma, na kufundisha ujuzi huu kwa wakimbizi wazee kwa vijana.

Waumini wa Kanisa wenye uzeofu mwingi ambao wamehudumu kwa miaka mingi na katika uongozi wanaweza kushuhudia kwa ukweli kwamba kuhudumia watu hawa walio na mahitaji ya dharura kumewapa uzoefu makuu wenye hisia za kutimiza zaidi katika huduma yao kufikia sasa.

Uhalisi wa hali hizi ni lazima uonekane ili uweze kuaminika. Katika majira ya baridi nilikutana, miongoni mwa wengine wengi, mama mjamzito kutoka Siria katika kambi ya kupitia tu ya wakimbizi akitafuta kuhakikishiwa kwamba hangehitajika kujifungua mtoto wake kwenye sakafu baridi ya ukumbi mkubwa ambapo alikuwa amepewa makazi. Kule Siria alikuwa profesa wa chuo kikuu. Kule Ugiriki nilizungumza na familia ambayo ilikuwa bado imelowa maji, ikitetemeka, na kutishika kutokana na kuvuka kutoka Uturuki kwenye boti ndogo ya mpira. Baada ya kutazama machoni mwao na kusikiliza simulizi zao, za hofu ambayo walitoroka na za safari yao ya hatari kutafuta kimbilio, kamwe sitasalia nilivyokuwa.

Kutoa utunzaji na msaada ni baadhi ya kazi zinatolewa na wafanya kazi wa msaada, wengi wao ni wa kujitolea. Nilimwona muumini mmoja wa Kanisa ambaye, kwa miezi mingi, alifanya kazi usiku mzima, akitoa msaada kwa mahitaji ya dharura ya wale waliokuwa wakiwasili kutoka Uturuki wakiingia Ugiriki. Miongoni mwa juhudi zingine zisizohesabika, alitoa huduma ya kwanza kwa wale waliohitaji sana msaada muhimu wa kimatibabu, alihakikisha kwamba wanawake na watoto waliokuwa wakisafiri pekee yao walihudumiwa, aliwakumbatia wale waliokuwa wamefiwa safarini, na alifanya kila juhudi kugawa rasilimali kidogo kwa mahitaji watu chungu mzima. Yeye, kama wengi sawa naye, amekuwa malaika wa kweli wa kuhudumu ambaye matendo yake hayajasahaulika na wale ambao aliwahudumia, wala Bwana, ambaye ni kazi Yake alikuwa akiifanya.

Wote ambao wamejitolea kupunguza mateso ya walio karibu nao wako kama watu wa Alma: “Na hivyo, hata katika hali yao ya kufanikiwa hawakumfukuza yeyote aliyekuwa uchi, au walio na njaa, au walio na kiu, au wale ambao walikuwa wagonjwa, au wale ambao hawakuwa wamelishwa; …walikuwa wakarimu kwa wote, wote wazee kwa vijana, wote watumwa na walio huru, wote wanaume kwa wanawake, washiriki wa kanisa na wale wasio washiriki wa kanisa, bila kubagua wale wote walio na shida.”8

Ni lazima tuwe waangalifu kwamba habari ya hatma ya wakimbizi kwa namna fulani isije ikawa kawaida, wakati mshtuko wa awali unapodidimia, na bado vita vinaendelea na familia zinazidi kuja. Mamilioni ya wakimbizi kote duniani, ambao simulizi zao hazifiki kwenye vyombo vya habari, wangali wanahitaji msaada kwa dharura.

IIkiwa unauliza, “Ni nini naweza kufanya?” na tukumbuke kwanza tusihudumu kwa kutelekeza familia zetu na majukumu mengine,9 wala tusitarajie viongozi wetu watupangie miradi. Lakini kama vijana, wanawake, na familia, tunaweza kushiriki katika juhudi hii kubwa ya kibinadamu.

Katika kujibu mwaliko kutoka Urais wa Kwanza kushiriki katika huduma kama ya Kristo kwa wakimbizi kote duniani,10 urais mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, Wasichana, na Msingi wamepanga juhudi za usaidizi ziitwazo “Nilikuwa Mgeni.” Dada Burton aliwasilisha haya kwa wanawake wa Kanisa wikiendi iliyopita katika kikao kikuu cha wanawake. Kunayo mawazo mbali mbali yanayoweza kusaidia, rasilimali, na mapendekezo ya kutoa huduma kwenye IWasAStranger.lds.org.

Anza kwa kupiga magoti katika maombi. Kisha fikiria kuhusu kufanya jambo karibu na nyumbani, katika jamii zenu, ambapo utapata watu ambao wanahitaji usaidizi kukabiliana na mazingira yao mapya. Lengo muhimu la kutoa huduma kwa wale wanaohitaji msaada ni kuwawezesha kuwa wachapakazi na kuwa na maisha ya kujitegemea.

Nafasi zetu za kutoa msaada ni nyingi mno. Unaweza kuwasaidia wakimbizi waliopewa makazi kujifunza lugha ya nchi enyeji, kuboresha ujuzi wao wa kazi, au kufanya mazoezi ya mahojiano ya kazi. Unaweza kujitolea kuwa mnasihi wa familia au mama aliye mzazi wa pekee wanapojaribu kutengamana na tamaduni geni, hata kwa kitu rahisi kama vile kuambatana nao hadi sokoni au shuleni. Baadhi ya kata na vigingi tayari vina mashirika ya kuaminika ya kushirikiana nayo. Na, kulingana na hali yako, unaweza kutoa msaada kwa juhudi za ajabu za kibinadamu za Kanisa.

Kila mmoja wetu anaweza kuongeza ufahamu wetu wa matukio ya dunia ambayo hufanya familia hizi kutoroka nyumbani kwao. Ni lazima tuchukue msimamo dhidi ya kutovumiliana na tutetee heshima na uelewano miongoni mwa tamaduni na mila. Kukutana na familia za wakimbizi na kusikiliza simulizi zao kwa masikio yako, na sio kutoka kwa televisheni au gazetini, kunaweza kukubadilisha. Uhusiano halisi utakua na kudumisha urafiki na utengamano uliofanikiwa.

Bwana ametuagiza kwamba vigingi vya Sayuni vinafaa kuwa “ngome” na “kimbilio wakati wa tufani.”11 Tumetengeneza kimbilio. Acheni tuondoke kwenye sehemu zetu salama na tugawe, kutoka neema zetu, matumaini ya siku bora zijazo, imani katika Mungu na wanadamu wenzetu, na upendo ambao unatazama zaidi ya tofauti zetu za kitamaduni na kiitikadi hadi kwenye ukweli mtukufu kwamba sisi sote ni watoto wa Baba yetu wa Mbinguni.

“Maana Mungu hakutupa Roho ya uwoga; bali ya nguvu, na ya upendo.”12

Kuwa mkimbizi kunaweza kuwa wakati wa maumuzi katika maisha ya wale ambao ni wakimbizi, lakini kuwa mkimbizi hakuelezi sifa zao. Kama maelfu wasiohesabika mbele yao, hiki kitakuwa ni kipindi—tunatumai muda mfupi—maishani mwao. Baadhi yao watakuja kuwa washindi wa tuzo ya Nobel, wafanyikazi wa umma, madaktari, wanasayansi, wanamuziki, wasanii, viongozi wa kidini, na wachangiaji katika nyanja mbali mbali. Hakika, wengi wao walikuwa vitu hivi vyote kabla ya kupoteza kila kitu. Kipindi hiki hakielezi sifa zao bainifu, lakini mjibizo wetu utasaidia kueleza sifa zetu bainifu.

“Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”13 Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Kwa marejeo zaidi, ona IWasAStranger.lds.org na mormonchannel.org/blog/post/40-ways-to-help-refugees-in-your-community.