2010–2019
Kusimama pamoja na Viongozi wa Kanisa
Aprili 2016


Kusimama pamoja na Viongozi wa Kanisa

Swali linaloendelea leo lipo wazi: je, unasimama pamoja na viongozi wa Kanisa katika ulimwengu wa giza ili uweze kueneza Nuru ya Kristo?

Tunawakaribisha kwa dhati Viongozi Wakuu wapya walioitwa, Wale wa Sabini wa Eneo, na urais mkuu wa Msingi mpya. Kwa shukrani za dhati, tunawashukuru wale waliopumzishwa. Tunawapendeni, kila mmoja.

Akina ndugu na dada zangu wapendwa, sisi tumeshiriki katika uzoefu wenye baraka tukiwa tumenyoosha mikono yetu kuwaidhinisha manabii, wafunuzi na waonaji na viongozi wengine na maafisa wakuu walioitwa na Mungu katika siku hizi. Sijawahi kamwe kuchukulia kwa wepesi au juu juu fursa ya kuidhinisha na kuongozwa na watumishi wa Bwana. Na nikiwa na muda wa miezi tu katika wito wangu mwenyewe kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, kwa unyenyekevu nashukuru kwa kura zenu na imani ya kuniunga mkono. Ninathamini hiari yenu kusimama nami na pamoja na viongozi hawa wakuu.

Mara baada ya kuidhinishwa mwezi Oktoba mwaka jana, nilisafiri kwenda Pakistan, kwenye majukumu na, nikiwa kule, nilikutana na Watakatifu waliojitolea wa nchi hiyo. Walikuwa wachache kiidadi, lakini wengi kiroho. Mara baada ya kurudi nyumbani, nilipata ujumbe ufuatao toka kwa Kaka Shakeel Arshad, muumini mpendwa niliyekutana naye katika safari yangu. “Asante, Mzee Rasband, kwa kuja Pakistan. Ninataka kukuambia kwamba sisi waumini wa Kanisa tunakuidhinisha na kukupenda. [Tuna] bahati kwamba ulikuwa hapa na tulisikia kutoka kwako. Ilikuwa ni siku ya thamani katika maisha ya familia yangu kwamba tulionana na Mtume.”1

Kukutana na Watakatifu kama Kaka Arshad ulikuwa ni uzoefu wa aina yake, kwa kutumia maneno yake, “ni siku ya thamani” kwangu pia.

Mwezi Januari viongozi wa Kanisa walishiriki katika matangazo Ana kwa Ana na vijana, viongozi wao, na wazazi ulimwengu kote. Matangazo yalirushwa moja kwa moja kupitia tovuti kwenda sehemu nyingi katika nchi 146, maeneo mengine yalikuwa na wahudhuriaji wengi kanisani, na wengine walikuwa nyumba moja pekee yenye kijana mmoja aliyehudhuria. Kwa ujumla, mamia na maelfu waliungana nasi.

Picha
Ana kwa Ana na Mzee Rasband, Dada Oscarson, na Ndugu Owen

Katika kuungana na wahudhuriaji, Dada Bonnie Oscarson, rais mkuu wa Wasichana; Kaka Stephen W. Owen, rais mkuu wa Wavulana; na mimi—nikiungwa mkono na vijana wetu waandaalizi, wanamuziki, na wengine—nilijibu maswali kutoka kwa vijana wetu.

Picha
Mada ya Mutuali ya 2016

Lengo letu lilikuwa ni kutambulisha Mada ya Mutuali kwa mwaka 2016, “Songa Mbele kwa Uthabiti katika Kristo” kutoka 2 Nefi ambayo inasema: “Kwa hivyo, lazima msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, mkiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote. Kwa hivyo, kama mtasonga mbele, mkila na kusherekea neno la Kristo, na mvumilie hadi mwisho, tazama, hivi ndivyo asema Baba: Mtapokea uzima wa milele”2.

Kwa kusoma maswali mengi ya vijana wetu, tulijifunza nini? Tulijifunza kwamba vijana wetu wanampenda Bwana, wanawaidhinisha viongozi wao, na wanapenda kuona maswali yao yakijibiwa! Maswali ni ishara ya kutaka kujifunza zaidi, kuongeza kwenye kweli ambazo tayari zipo kwenye shuhuda zetu, na kujiandaa vizuri “kusonga mbele katika Kristo.”

Urejesho wa injili ulianza na kijana, Joseph Smith, akiuliza swali. Mafundisho mengi ya Mwokozi katika utumishi Wake yalianza na swali. Kumbuka swali Lake kwa Petro: “Ninyi mnasema mimi ni nani?”3 Na Petro akajibu: “Wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”4 Tunatakiwa kusaidiana kupata majibu ya Baba wa Mbinguni kupitia mwongozo wa Roho.

Katika matangazo yale, niliwaambia vijana:

“Viongozi wa Kanisa si wageni wa maswala yenu, wasiwasi wenu, na changamoto zenu.

“Tuna watoto. Tuna wajukuu. Mara kwa mara tunakutana na vijana duniani kote. Na tunaomba kwa ajili yenu, tunaongea juu yenu katika maeneo matakatifu, na tunawapenda.”5

Ningependa kushiriki moja ya, mijibizo mingi tuliyoyapata toka kwenye tukio hilo.

Lisa kutoka Grande Prairie, Alberta, Canada aliandika: “Mkutano huu wa Ana kwa Ana ulikuwa wa kupendeza. Ni imarisho jinsi gani kwa ushuhuda wangu na kusadiki injili. Tumebarikiwa sana kuwa na viongozi wazuri ambao wameitwa kuhudumu katika uwezo tofauti.”6

Liz, kutoka Pleasant Grove, Utah, aliandika kwenye chapisho la awali: “Ninashukuru kwa imani yangu binafsi na nafasi ya kumuidhinisha nabii wa Mungu na wanaume na wanawake wanaohudumu pamoja naye.”7

Tumewaidhinisha viongozi leo ambao wana maongozi matakatifu, wameitwa kutufundisha na kutuongoza na ambao wanatuambia tujitahadharishe na hatari tunazokutana nazo kila siku—kutokana na kuitukuza siku ya Sabato kijuujuu, hadi kwenye vitisho kwa familia, shambulio kwa uhuru wa dini, na hata kupingana na ufunuo wa siku za mwisho. Akina kaka na dada, je, tunasikiliza ushauri wao?

Mara nyingi katika mikutano, vipindi vya sakramenti, na Msingi, tumeimba maneno laini, Niongoze, Nionngoze, tembea kando yangu.”8 Maneno hayo yana maana gani kwako? Nani anakuja akilini wakati unapofikiri juu yake? Umehisi msukumo wa viongozi waadilifu, wale wafuasi wa Yesu Kristo ambao hapo kale na kuendelea leo kuyagusa maisha yako, wanaotembea katika njia ya Bwana pamoja nawe? Wanaweza kuwa karibu nyumbani. Wanaweza katika mkusanyiko wa mtaani kwako, au wakiongea toka mimbarini kwenye mkutano mkuu. Wafuasi hawa wanashiriki nasi baraka za kuwa na ushuhuda wa Bwana Yesu Kristo, kiongozi wa Kanisa hili, kiongozi wa nafsi zetu, ambaye ametuahidi, “Changamkeni, na msiogope, kwani mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu nayi.”9

Nakumbuka Rais Thomas S. Monson akishiriki habari ya kualikwa kwenye nyumba ya rais wake wa kigingi kujiandaa kupata Ukuhani wa Melkizedeki. Ni baraka za aina gani kwamba rais wa kigingi, ambaye hakujua kwa wakati ule alikuwa anamfundisha kijana wa Ukuhani wa Haruni ambaye siku moja angekuwa nabii wa Mungu.10

Nimekuwa na wakati wangu mwenyewe wa kujifunza toka kwa nabii wetu mpendwa, Rais Monson. Hakuna hofu katika fikra zangu au kwenye moyo wangu kwamba yeye ni nabii wa Bwana hapa duniani; nimekuwa mpokeaji mnyenyekevu anapopokea ufunuo na kutenda juu yake. Amekuwa akitufundisha kuwafikia wengine, kulindana, kuokoana. Ndivyo ilivyofundishwa kwenye maji ya Mormoni. Wale waliotamani “… kuitwa watu wake” walikuwa wapo radhi “kubeba mizigo ya mmoja na mwingine,” “kuomboleza na wanaoomboleza,” na “kusimama kama mashahidi wa Mungu.”11

Ninasimama leo kama shahidi wa Mungu Baba wa Milele na Mwana Wake, Yesu Kristo. Ninajua Mwokozi wetu yu hai na anatupenda na anawaongoza watumishi Wake, wewe na mimi, ili kutimiza malengo Yake hapa duniani.12

Tunaposonga mbele, tukichagua kufuata mwelekeo na maonyo ya viongozi wetu, tunachagua kumfuata Bwana wakati ulimwengu ukienda upande mwingine. Tunachagua, kushikilia fimbo ya chuma, kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, kuwa upande wa Bwana, na kujazwa “na furaha kubwa.”13

Swali linaloendelea leo lipo wazi: je, unasimama pamoja na viongozi wa Kanisa katika ulimwengu wa giza ili uweze kueneza Nuru ya Kristo?

Mahusiano na viongozi ni muhimu sana. Bila kujali umri wa kiongozi wako, ukaribu na umbali, au ni lini wanaweza kuwa waligusa maisha yetu, ushawishi wao unaakisi maneno ya mshairi Mmarekani Edwin Markham, ambaye alisema:

Kuna kudra ambayo hutufanya sisi kuwa ndugu:

Hakuna yeyote ambaye huenda njia yake pake yake:

Yale yote tunayotuma katika maisha ya wengine

Hurudi tena kwetu wenyewe.14

Shakeel Arshad, rafiki yangu wa Pakistan, alituma uungaji mkono wake kwangu, kaka yake na rafiki yake. Vivyo hivyo wengi wenu. Tunapojitokeza kusaidia mmoja na mwingine, tunathibitisha yale maneno yenye nguvu: “Hakuna yeyote ambaye huenda njia yake peke yake:

Zaidi ya yote, tunamhitaji Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Mojawapo ya maelezo kutoka kwenye andiko ambalo kila mara liliniongoza kiroho ni wakati Yesu Kristo alipotembea kwenye maji kukutana na wanafunzi Wake waliokuwa wakisafiri kwa mashua katika Bahari ya Galilaya. Hawa walikuwa viongozi wapya, walioitwa kama wengi wetu hapa mbele hivi leo. Maelezo yameandikwa katika Mathayo:

“Na wakati huo mashua ilikuwa imeshafika katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu: kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.

“Usiku, karibu na mapambazuko Yesu aliwaendea, akitembea juu ya maji.

“Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, … wakapiga yowe kwa hofu.

“Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo; ni mimi; msiogope.”15

Petro aliusikia wito ule wa kutia moyo toka kwa Bwana.

“Petro akamjibu na akamwambia, Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.

“Na [Yesu] akasema, Njoo.”16

Ujasiri mkubwa. Petro alikuwa mvuvi, na alijua madhara ya bahari. Hata hivyo, alijizatiti kumfuata Yesu—usiku au mchana, iwe kwenye mashua au nchi kavu.

Siwezi kufikiria kwamba Petro aliruka upande wa mashua, bila kusubiri mwaliko wa pili, na akaanza kutembea juu ya maji. Hakika, maandiko yanasema, “Akatembea juu ya maji, kwenda kwa Yesu.”17 Wakati upepo ulipozidi nguvu na mawimbi yakimpiga kwenye miguu, Petro akaanza kuogopa “na akaanza kuzama, akapiga mayowe, akisema, Bwana, niokoe.

Na mara moja Yesu akanyoosha mkono Wake, na akamshika.”18

Hilo ni somo lenye nguvu. Bwana alikuwa pale kwa ajili yake, kama Yeye alivyo hapa kwa ajili yako na mimi. Alinyoosha mkono Wake na kumleta Petro Kwake na kwenye usalama.

Nimemhitaji Mwokozi na mkono Wake wa uokozi mara nyingi. Ninamhitaji sasa kuliko mwanzo, ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Nimehisi ujasiri wakati fulani kuruka upande mwingine wa mashua, kuongea kwa istairi, katika maeneo yasiyo ya kawaida, kuja kugundua kwamba siwezi kufanya hivyo peke yangu.

Tukijadiliana kipindi cha Ana kwa Ana, Bwana mara kwa mara alikuja kwetu kupitia familia zetu na viongozi wetu, akitualika kuja Kwake—kama alivyofanya kumwokoa Petro.

Nanyi pia mtakuwa na nyakati zenu nyingi kujibu mialiko ya mara kwa mara ya “njoo kwa Kristo.”19 Hivi si ndivyo maisha ya duniani yalivyo? Wito unaweza kuwa wa kuja kumwokoa mwana familia; kuja kuhudumu misheni; kurudi kanisani; kuja katika hekalu takatifu; na, kama hivi karibuni nilisikia kutoka kwa vijana wetu katika tukio la Ana kwa Ana, tafadhali njoo unisaidie kujibu swali langu. Kwa wakati muafaka, kila mmoja wetu atasikia wito “Njoo nyumbani.”

Ninaomba tuweze kufikia—kufikia na kuchukua mkono wa Bwana ambao ameunyoosha kwetu, mara nyingi kwa kupitia viongozi Wake walioitwa kitakatifu na wana familia wetu—na kusikiliza wito Wake wa kuja.

Ninajua kwamba Yesu Kristo yu hai; Ninampenda, na ninajua kwa moyo wangu wote kwamba Anampenda kila mmoja wetu. Yeye ni Mfano wetu mkubwa na kiongozi mtakatifu kati ya watoto wote wa Baba. Kwa haya ninatoa ushahidi wangu wa dhati katika jina la Yesu Kristo, amina.