2010–2019
Mafuta ya Uponyaji ya Msamaha
Aprili 2016


Mafuta ya Uponyaji ya Msamaha

Msamaha ni kanuni tukufu, ya uponyaji. Hatuhitaji kuwa waathiriwa mara mbili. Tunaweza kusamehe.

Yale yote ambayo ni ya Mungu hujumuisha upendo, nuru, na ukweli. Na hali sisi binadamu tunaishi katika ulimwengu ulioanguka, wakati mwingine uliojaa giza zito na machafuko. Si ajabu kwamba makosa yatafanyika, udhalimu hutatokea, na dhambi zitatendwa. Matokeo yake, hakuna nafsi iishiyo ambayo haitatenda dhambi wakati mmoja au mwingine, kuwa mwathiriwa wa matendo ya uzembe ya mtu mwingine, mwenendo wa kuumiza, au hata tabia za dhambi. Hicho ni kitu kimoja ambacho sote tunalingana.

Kwa shukrani, Mungu, kwa upendo na huruma Wake kwa watoto Wake, ameandaa njia ya kutusaidia wakati mwingine kupitia matukio ya misukosuko ya maisha. Ameandaa njia ya kuepuka kwa wale wanaoathiriwa na matendo maovu ya wengine. Ametufundisha kwamba tunaweza kusamehe! Ingawa tunaweza kuwa waathiriwa mara moja, hatutakiwi kuwa waathiriwa mara mbili kwa kubeba mzigo wa chuki, uchungu, maumivu, maudhi, au hata kisasi. Tunaweza kusamehe, na tunaweza kuwa huru!

Miaka mingi iliyopita, nikiwa natengeneza ua, kichane kiliingia kwenye kidole changu. Nilifanya jaribio dogo la kuondoa kichane hicho na nikafikiria nimeweza, lakini yamkini sikuwa nimeweza. Muda ukiwa unakwenda, ngozi ikawa inafunika kichane hicho, kukawa na uvimbe kwenye kidole changu. Ilikuwa inanisumbua na wakati mwingine kuuma.

Miaka kadhaa baadaye niliamua kuchukua hatua. Nilichokifanya ilikuwa ni kupaka mafuta kwenye uvimbe na kufunga bandeji. Nilirudia zoezi hili mara kwa mara. Huwezi kuamini wakati siku moja, nilipoondoa bandeji, kipande cha mbao kilitokea kwenye kidole changu.

Mafuta yalikuwa yamelainisha ngozi na kutengeneza njia kwa kile kitu ambacho kinanisababishia maumivu kwa miaka mingi sana. Baada ya kichane kutolewa, kidole kikapona haraka, na hadi leo, hakuna mabaki ya kuonyesha jeraha lolote.

Kwa mfano kama huu, moyo usiosamehe hupenda sana maumivu ya bure. Tunapotumia mafuta ya uponyaji ya Upatanisho wa Mwokozi, Atalainisha mioyo yetu na kutusaidia kubadilika. Anaweza kuponya nafsi iliyojeruhiwa (ona Yakobo 2:8).

Nina uhakika kwamba wengi wetu wanataka kusamehe, lakini inakuwa vigumu kufanya hivyo. Tunapokumbana na udhalimu, kwa haraka tunaweza kusema, “Mtu yule alifanya makosa. Wanastahili adhabu. Haki iko wapi? Kwa makosa tunafikiria kwamba kama tunasamehe, kwa namna fulani haki haitatendeka na adhabu itakwepwa.

Hivi sivyo kamwe. Mungu atatoa adhabu ambayo ni sahihi, kwani rehema haiwezi kuiibia haki (ona Alma 42:25). Mungu kwa upendo ananihakikishia mimi na wewe: “Niachieni hukumu mimi peke yangu, kwani ni yangu nami nitalipa. [Lakini] acha amani na iwe kwenu” (M&M 82:23). Nabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo pia aliahidi kwamba Mungu “atawafariji katika mateso yenu, na atatetea kesi yenu, na kuwateremshia hukumu wale wanaotaka kuwaangamiza”(Yakobo 3:1).

Kama waathiriwa, kama tuna imani, tunaweza kupata ufariji mkubwa kwa kujua kwamba Mungu atatufidia kwa kila la udhalimu tunaopata. Mzee Joseph B. Wirthlin alifundisha: “Bwana huwafidia waaminifu kwa kila hasara. … Kila jonzi leo hatimaye litalipiliziwa mara mia kwa machozi ya furaha na shukrani.”1

Tunapojitahidi kuwasamehe wengine, acheni pia tujaribu kukumbuka kwamba sote tunakua kiroho, lakini wote tupo kwenye ngazi tofauti. Huku ikiwa rahisi kuangalia tofauti na ukuaji wa kimwili, ni vigumu kuona ukuaji katika roho zetu.

Kitu muhimu katika kuwasamehe wengine ni kujaribu kuwaona jinsi Mungu anavyowaona. Kuna wakati, Mungu aweza kufungua pazia na kutubariki na kipawa cha kuona katika moyo, nafsi, na roho ya mtu mwingine ambaye ametuhudhi. Ufahamu huu huweza hata kutuongoza kwenye upendo mkubwa kwa mtu huyo.

Maandiko yanatufundisha kwamba upendo wa Mungu kwa watoto Wake ni kamili. Anajua uwezo wao wa kuwa wema, bila kujali matendo yao ya wakati uliopita. Kwa hali zote, pasingekuwa na adui mkali wa wafuasi wa Yesu Kristo zaidi ya Sauli wa Tarso. Na hali mara Mungu alipomwonyesha Sauli nuru na kweli, kamwe hapakuwa na mfuasi mwingine wa Mwokozi kwa kujitoa, shauku, au mwanafunzi asiyekuwa na woga. Sauli akawa Mtume Paulo. Maisha yake yanatoa mfano kwamba Mungu anawaona watu siyo kama walivyo sasa lakini pia kama wanavyoweza kuwa. Sisi sote tunae, katika maisha yetu wenyewe, mtu kama Sauli mwenye uwezo kama wa Paulo. Unaweza kufikiria jinsi familia zetu, jamii, na ulimwengu kijumla unavyoweza kubadilika kama sisi sote tungejaribu kujiona kama Mungu atuonavyo?

Mara nyingi tunawaangalia wakosaji kama vile tunavyoangalia siwa barafu—tunaona tu ncha na si chini yake. Hatujui yale yote yanayoendelea katika maisha ya mtu. Hatujui mambo yao ya hapo awali, hatujui shida zao, hatujui maumivu waliyonayo. Ndugu na dada, tafadhali msielewe vibaya. Kusamehe siyo kupuuza. Haturazimu tabia mbaya au kuruhusu mtu kututendea mabaya kwa sababu ya shida, maumivu, au mapungufu yao. Lakini tunaweza kupata uelewa mzuri na amani tunapoona kwa mtazamo mpana.

Hakika wale ambao hawajakua kiroho wanaweza kufanya makosa makubwa—hata hivyo hakuna hata mmoja wetu awezaye kuelezea mambo mabaya pekee tuliyowahi kuyafanya. Mungu ni hakimu wa haki. Anaona chini ya uso. Anajua yote na anaona yote (ona 2 Nefi 2:24). Amesema, “Mimi, Bwana, nitamsamehe yule nitakaye, lakini ninyi mnatakiwa kuwasamehe watu wote” (M&M 64:10).

Kristo Mwenyewe, wakati aliposhitakiwa bila haki, ndipo alidhihakiwa, alipigwa, na kuachwa akiteseka msalabani, wakati huo akasema, “Baba, wasamehe, kwani hawajui walitendalo” (Luka 23:34).

Katika upeo wetu mdogo, wakati mwingine tunaweza kuona kuwa ni rahisi kuwachukia wengine wasiotenda au kufikiri kama sisi. Tunaweza kukuza misimamo isiyovumilia inayotokana na vitu finyu kama vile kushabikia timu zinazopingana, kuwa na mtazamo tofauti wa kisiasa au kuwa na imani tofauti ya dini.

Rais Russell M. Nelson alitoa ushauri wa busara aliposema, “Fursa ya kuwasikiliza wale wenye ushawishi tofauti wa kidini au kisiasa kunaweza kukuza uvumilivu na kujifunza.”2

Kitabu cha Mormoni kinasema kuhusu wakati ambao “watu wa kanisa walianza kujiinua kwa kiburi machoni mwao, na … Wakaanza kufanyiana madharau, wao kwa wao, na kuanza kuwatesa wale ambao hawakuamini kulingana na nia yao na mapenzi yao” (Alma 4:8). Acha sote tukumbuke kwamba Mungu hatazami rangi ya jezi au chama cha siasa. Badala yake, kama Amoni alivyosema, “[Mungu] anatazama chini kwa watoto wa watu; na anafahamu mawazo yote na nia zote za moyo” (Alma 18:32). Ndugu na dada, katika mashindano ya maisha, kama tunashinda, acha tushinde kwa neema. Kama tutashindwa, acheni tushindwe kwa neema. Kwani, kama tutaishi kwa neema kwa watu wengine, neema itakuwa ni tuzo letu siku za mwisho.

Kama sote tulivyo waathiriwa wa matendo maovu ya wengine kwa wakati mmoja au mwingine, sisi pia wakati mwingine ni wakosaji. Sote tumepungukiwa na tunahitaji neema, huruma, na msamaha. Lazima tukumbuke kwamba msamaha wa dhambi na makosa yetu wenyewe hutegemea jinsi tunavyowasamehe wengine. Mwokozi alisema:

“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia:

“Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu” (Mathayo 6:14–15).

Kwa mambo yote ambayo Mwokozi angeyasema katika Sala ya Bwana, ambayo ni fupi, inapendeza kwamba Alichagua kujumuisha “Na utusamehe makosa yetu, kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea” (Mathayo 6:12; 3 Nefi 13:11).

Msamaha ndiyo hasa sababu ya Mungu kumtuma Mwanawe, kwa hivyo acha tufurahie katika toleo Lake la kutuponya sisi sote. Upatanisho wa Mwokozi siyo tu kwa wale wanaohitaji kutubu, pia ni kwa wale wanaohitaji kusamehe. Kama unapata shida kumsamehe mtu mwingine, mwombe Mungu akusaidie. Msamaha ni kanuni tukufu, ya uponyaji. Hatuhitaji kuwa waathiriwa mara mbili. Tunaweza kusamehe.

Ninashuhudia upendo na uvumilivu wa Mungu kwa watoto Wake wote na matamanio Yake kwamba tupendane kama Anavyotupenda sisi (ona Yohana 15:9, 12). Tunapofanya hivi, tutapita katika giza la ulimwengu huu kuelekea kwenye utukufu na ukuu wa ufalme Wake wa mbinguni, Tutakuwa huru. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Joseph B. Wirthlin, “Come What May, and Love It,”Liahona, Nov. 2008, 28.

  2. Russell M. Nelson, “Listen to Learn,” Ensign, May 1991, 23.