2010–2019
Gharama ya Uwezo wa Ukuhani
Aprili 2016


Gharama ya Uwezo wa Ukuhani

Je, tuko tayari kuomba, kufunga, kujifunza, kutafuta, kuabudu, na kuhudumu kama wanaume wa Mungu ili tuweze kuwa na uwezo wa ukuhani?

Miezi sita iliyopita katika mkutano mkuu wa Oktoba 2015, nilizungumza na kina dada wa Kanisa kuhusu wajibu wao mtakatifu kama wanawake wa Mungu. Sasa ningependa kuzungumza nanyi ndugu zangu kuhusu jukumu lenu takatifu kama wanaume wa Mungu. Ninaposafiri ulimwenguni, nashangazwa na nguvu na wema kamili wa wanaume na wavulana wa Kanisa hili. Kwa kweli hamna njia ya kuihesabu mioyo mliyoponya na maisha mliyoinua. Asanteni!

Katika ujumbe wangu wa mwisho, nilielezea tukio langu la kutisha miaka mingi iliyopita wakati, mimi kama mpasuaji wa moyo, sikuweza kuokoa maisha ya kina dada wawili wadogo. Kwa ruhusa ya baba yao, ningependa kusema zaidi kuhusu familia hiyo.

Ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao uliwatesa watoto watatu waliozaliwa na Ruth na Jimmy Hatfield. Mwana wao wa kwanza, Jimmy Jr, alikufa bila utambuzi bainifu. Nilipata kujua wakati wazazi walipokuwa wakitafuta msaada kwa mabinti zao wawili, Laurel Ann na dada yake mdogo, Gay Lynn. Nilivunjika moyo wakati wasichana wote wawili walipokufa kufuatia upasuaji wao.1 Hakika, Ruth na Jimmy walipondeka kiroho.

Kwa muda, niligundua kwamba walikuwa na machungu dhidi yangu na Kanisa. Kwa karibu miongo sita, nimekuwa nikisumbuliwa na hali hii na nimehuzunika kwa ajili ya kina Hatfields. Nilijaribu mara kadhaa kuanzisha mawasiliano nao, bila ya mafanikio.

Kisha, usiku moja mnamo Mei iliyopita, niliamshwa na wale wasichana wawili wadogo kutoka upande mwingine wa pazia. Ingawa sikuweza kuwaona au kuwasikia kwa hisia zangu za kimwili, nilihisi uwepo wao. Kiroho, nilisikia kilio chao. Ujumbe wao ulikuwa mfupi na wazi: “Ndugu Nelson, hatukuunganishwa kwa mtu yeyote! Je, unaweza kutusaidia?” Muda mfupi baadaye, niligundua kwamba mama yao alifariki, lakini baba yao na ndugu yao mdogo bado walikuwa hai.

Kwa kutiwa moyo na kilio cha Laural Ann na Gay Lynn, nilijaribu tena kuwasiliana na baba yao, ambaye niligundua kuwa alikuwa akiishi na mwanawe Shawn. Wakati huu walikuwa tayari kukutana na mimi.

Mnamo mwezi wa Juni, kwa hakika nilipiga magoti mbele ya Jimmy, sasa mwenye miaka 88, na tukawa na majadiliano wa karibu pamoja naye. Niliongea kuhusu kilio cha mabinti zake na kumwambia kwamba ingekuwa ni heshima yangu kufanya ibada ya uunganisho kwa familia yake. Pia nilimwelezea kuwa itachukua muda na juhudi nyingi kwa upande wake na Shawn ya kuwa tayari na kustahili kuingia hekaluni, kwa kuwa hakuna yeyote kati yao aliyewahi kubarikiwa hekaluni.

Roho wa Bwana alidhihirika wakati wote wa mkutano huo. Na wakati Jimmy na Shawn walipokubali ombi langu, nilijawa na furaha tele! Walifanya kazi kwa bidii na rais wao wa kigingi, askofu, waalimu wa nyumbani, na kiongozi wa misheni ya kata, vilevile pamoja na wamisionari vijana na wamisionari wanandoa wakongwe. Na kisha, si muda mrefu uliopita, katika Hekalu la Payson Utah, nilikuwa na fursa ya kipekee ya kuwaunganisha Ruth na Jimmy na watoto wao wanne kwao. Wendy na mimi tulilia tuliposhiriki katika tukio hilo la kuvutia. Mioyo mingi iliponywa siku hiyo!

Picha
Mzee na Dada Nelson hekaluni pamoja na familia ya Hatfield

Katika kutafakari, nimeshangazwa na Jimmy na Shawn na kile walichokuwa tayari kufanya. Wamekuwa mashujaa kwangu. Kama ingekuwa ni mapenzi ya moyo wangu, ingekuwa kwamba kila mwanamume na kijana katika Kanisa hili angeonyesha ujasiri, nguvu, na unyenyekevu wa baba huyu na mwanawe. Walikuwa tayari kusamehe na kuacha machungu na tabia ya zamani. Walikuwa tayari kunyenyekea kwa uongozi kutoka kwa viongozi wao wa ukuhani ili Upatanisho wa Yesu Kristo uweze kuwasafisha na kuwakuza. Kila mmoja alikuwa tayari kuwa mtu ambaye anashikilia ukuhani kwa ustahilifu “kwa mfano mtakatifu wa Mungu.” 2

Kushikilia maana yake ni kusaidia uzito wa kile kilichoinuliwa. Ni jukumu takatifu kushikilia ukuhani, ambayo ni uwezo mkuu na mamlaka ya Mungu. Fikiria jambo hili: ukuhani tuliyotunukiwa juu yetu ni nguvu ile ile na mamlaka ambayo kupitia kwayo Mungu aliumba dunia hii na zingine zisizo na hesabu, kusimamia mbingu na ardhi, na kutukuza watoto Wake watiifu.3

Majuzi, Wendy nami tulikuwa katika mkutano ambapo mpiga kinanda alikuwa tayari kucheza wimbo wa ufunguzi. Macho yake yalikuwa kwenye muziki, na vidole vyake vilikuwa juu ya vitufe. Alianza kubonyeza vitufe, lakini hapakuwa na sauti. Nilimnong’onea Wendy, “Hamna umeme.” Nilimaanisha kuwa kitu kilikuwa kimekatiza mtiririko wa nguvu za umeme kwenye kinanda hicho.

Ndugu zangu, vivyo hivyo, nahofia kwamba kuna wanaume wengi ambao wamepewa mamlaka ya ukuhani lakini hawana uwezo wa ukuhani kwa sababu mtiririko wa nguvu umezuiliwa na dhambi kama vile uvivu, kukosa uaminifu, kiburi, ukosefu wa maadili, au kutawaliwa na mambo ya dunia.

Ninahisi kuwa kuna wamiliki wengi mno wa ukuhani ambao wamefanya kidogo au hawajafanya chochote ili kuendeleza uwezo wao wa kupata nguvu za mbinguni. Nina wasiwasi kuhusu wote walio wachafu katika mawazo yao, hisia, au matendo au wanaowadharau wake zao au watoto, na hivyo kutupilia mbali nguvu za ukuhani.

Ninahofia kwamba watu wengi mno kwa masikitiko wamesalimisha wakala wao kwa adui na wanasema kwa mienendo yao, “Ninajali zaidi kuhusu kutosheleza tamaa yangu mwenyewe kuliko kumiliki uwezo wa Mwokozi wa kubariki wengine.”

Ninahofia, ndugu zangu, kwamba baadhi kati yetu siku moja wataamka na kutambua ni uwezo gani ulio katika ukuhani na kuona majuto makuu kwamba walitumia muda mwingi wakitafuta uwezo juu ya wengine au uwezo kazini badala ya kujifunza kutumia kikamilifu uwezo wa Mungu.4 Rais George Albert Smith alifundisha kwamba “hatuko hapa kupitisha masaa ya maisha haya na kisha kupita katika nyanja ya kuadhimishwa; lakini tuko hapa kujihitimisha wenyewe siku baada ya siku kwa ajili ya nafasi ambazo Baba yetu anatutarajia kujaza hapo baadaye.”5

Kwa nini mtu yeyote apoteze siku zake na kukubali chakula cha ndengu cha Esau6 wakati ameaminika na uwezekano wa kupata Baraka zote za Ibrahimu?7

Ninamsihi kwa haraka kila mmoja wetu kuishi kustahili fursa zetu kama wamiliki wa ukuhani. Katika siku zijazo, ni tu wale wanaume ambao wanatumia ukuhani wao kwa makini, kwa kutafuta kwa bidii kufundishwa na Bwana Mwenyewe, wataweza kubariki, kuongoza, kulinda, kuimarisha, na kuponya wengine. Ni yule mtu ambaye amelipia dhamana ya uwezo wa ukuhani ndiye atakayeweza kufanya miujiza kwa wale anaowapenda na kuweka ndoa na familia yake salama, sasa na kwa milele yote.

Inagharimu nini ili kukuza uwezo wa ukuhani kama huo? Mtume mkuu wa Mwokozi, Petro—yule Petro ambaye pamoja na Yakobo na Yohana walitunuku Ukuhani wa Melkizedeki juu ya Joseph Smith na Oliver Cowdery8—walitangaza sifa ambazo tunapaswa kutafuta ili “kuwa washirika wa tabia ya Uungu.”9

Picha
Petro, Yakobo, na Yohana wakitunukia Ukuhani wa Melkizedeki.

Alitaja imani, wema, maarifa, kiasi, saburi, utauwa, upendano wa ndugu, upendo, na bidii.10 Na usisahau unyenyekevu!11 Basi, mimi nauliza, ni vipi wanafamilia wetu, marafiki, na wafanyakazi wenzetu watasema wewe na mimi tunafanya katika kuendeleza karama hizi na zingine za kiroho?12 Kadri tunavyoendeleza sifa hizo, ndivyo uwezo wetu wa ukuhani utakuwa mkubwa.

Ni kwa njia gani tena tunaweza kuongeza uwezo wetu katika ukuhani? Tunahitaji kuomba kutoka mioyoni mwetu. Utongoaji wa upole wa mambo ya zamani na shughuli zijazo, zikiwemo maombi mengine ya baraka, haziwezi kutosheleza aina ya mawasiliano na Mungu ambayo huleta nguvu ya kudumu. Je, uko tayari kuomba kujua jinsi ya kuomba kwa nguvu zaidi? Bwana atawafundisheni.

Je, uko tayari kupekua maandiko na kushiriki maneno ya Kristo13—kujifunza kwa bidii ili kuwa na uwezo zaidi? Kama unataka kuona moyo wa mke wako ukiyeyuka, acha akupate kwenye mtandao ukisoma mafundisho ya Kristo14 au ukisoma maandiko yako!

Je, uko tayari kuabudu katika hekalu kila mara? Bwana anapenda kufanya mafundisho Yake mwenyewe katika nyumba Yake takatifu. Fikiria jinsi Angefurahi kama ungemuuliza Akufundishe kuhusu funguo za ukuhani, mamlaka, na uwezo unaposhiriki maagizo ya Ukuhani wa Melkizedeki katika hekalu takatifu.15 Fikiria wingi wa uwezo wa ukuhani ambao unaweza kuwa wako.

Je, uko tayari kufuata mfano wa Rais Thomas S. Monson wa kuwahudumia wengine? Kwa miongo amechukua njia ndefu wa kurudi nyumbani, kufuatia misukumo ya Roho kuwasili kwenye mlango wa mtu na kisha kusikia maneno kama vile, “Ulijuaje ni maadhimisho ya kifo cha binti yetu?” au “Ulijuaje ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwangu?” Na, kama kweli unataka uwezo zaidi wa ukuhani, utathamini na kuhudumia mke wako, ukimkumbatia yeye na ushauri wake.

Sasa, kama hii yote inaonekana kuzidi, tafadhali fikiria jinsi uhusiano wetu ungekuwa na wake wetu, watoto, na washirika kazini ungekuwa tofauti kama tungekuwa vile tulivyojitahidi kuhusu kupata uwezo wa ukuhani jinsi tulivyo katika kuendelea kazini au kuongeza mabaki katika akaunti ya benki yetu. Kama tutajiwasilisha kwa unyenyekevu mbele za Bwana na kumwomba kutufundisha, atatuonyesha jinsi ya kuongeza ufikiaji wetu kwa uwezo Wake.

Katika siku hizi za mwisho, tunajua kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali mbalimbali.16 Pengine moja ya sehemu hizo mbalimbali zitakuwa katika nyumba zetu wenyewe, ambapo “mitetemeko” ya hisia, fedha, au kiroho zinaweza kutokea. Uwezo wa ukuhani unaweza kutuliza bahari na kuponya majeraha katika nchi. Uwezo wa ukuhani pia hutuliza akili na kuponya majeraha katika mioyo ya wale tunaowapenda.

Je, tuko tayari kuomba, kufunga, kujifunza, kutafuta, kuabudu, na kuhudumu kama wanaume wa Mungu ili tuweze kuwa na aina hiyo ya uwezo wa ukuhani? Kwa sababu wasichana wawili wadogo walikuwa na shauku kubwa ya kufungishwa kwa familia zao, baba yao na ndugu walikuwa tayari kulipa dhamana ya kumiliki Ukuhani mtakatifu wa Melkizedeki.

Ndugu zangu wapendwa, tumepewa jukumu takatifu—mamlaka ya Mungu ya kuwabariki wengine. Acha kila mmoja wetu ainuke kama mwanaume ambaye Mungu alituteua kuwa—tayari kumiliki ukuhani wa Mungu kwa ujasiri, na hamu ya kulipa gharama yoyote inayohitajika ili kuongeza uwezo wake katika ukuhani. Kwa huo uwezo, tunaweza kusaidia kuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Hii ni Kanisa Lake, likiongozwa leo na nabii Wake, Rais Thomas S. Monson, ambaye mimi nampenda na kumwidhinisha. Mimi nashuhudia hivyo kwa jina la Yesu Kristo, amina.