2010–2019
Tutafanya Nini?
Aprili 2016


Tutafanya Nini?

Tunajenga ufalme tunapowalea wengine. Pia tunajenga ufalme wakati tunaponena na kushuhudia ukweli.

Punde baada ya Ufufuko na Kupaa kwa Yesu, Mtume Paulo alifundisha. “Acheni wote … mjue kwa hakika, kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.” Wasikilizaji walikuwa amepigwa katika nyoyo zao na kumwuliza Petro na wengine, ”Ndugu zangu, tufanye nini?” 1 Na wao hatimaye walitii mafundisho ya Petro kwa furaha.

Kesho ni Jumapili ya Pasaka, na natumaini kwamba sisi pia tumepigwa katika mioyo yetu kukiri Mwokozi, kutubu, na kutii kwa kuraha.

Katika mkutano huu mkuu, tutasikia mwongozo mtakatifu ukitolewa na viongozi wa Kanisa, wote wanaume na wanawake. Tukijua kwamba mioyo yetu itaguswa na maneno yao, ninawauliza jioni hii, “Wanawake na akina dada, tutafanya nini sisi?”

Rais mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, Eliza R. Snow alisema kwa akina dada karibu miaka 150 iliyopita, “Bwana ameweka wajibu mkuu juu yetu.”2 Ninashuhudia kwamba tamko lake bado ni kweli hata leo.

Kanisa la Bwana huhitaji wanawake wenye kuongozwa na Roho ambao wanatumia vipaji vyao vya kipekee ili kutunza na pia kunena na kutetea ukweli wa injili. Mwongozo na msukumo ni sehemu muhimu ya kujenga ufalme wa Mungu, ambao kwa kweli inamaanisha kutenda sehemu yetu ili kuleta wokovu kwa watoto wa Mungu.

Kuujenga ufalme kupitia malezi

Tunajenga ufalme tunapowalea wengine. Hata hivyo, mtoto wa kwanza wa Mungu ambaye lazima tumjenge katika injili iliyorejeshwa ni sisi wenyewe. Emma Smith alisema, “Mimi natamani Roho wa Mungu ili nijijue na kujielewa mwenyewe, kwamba niweze kushinda tamaduni zozote au asili ambayo haitasaidia kuinuliwa kwangu.”3 Sisi ni sharti tujenge imani thabiti katika injili ya Mwokozi na kusonga mbele, kwa nguvu za maagano ya hekalu, kuelekea kuinuliwa.

Itakuwaje kama baadhi ya tamaduni zetu hazina nafasi katika injili ya Yesu Kristo iliyorejeshwa? Kuziacha kunaweza kuhitaji msaada wa kimhemko na ulezi wa wengine, kama ilivyofanyika kwangu.

Nilipozaliwa, wazazi wangu walipanda mti wa magnolia kwenye ua la nyuma ili pawepo na maua ya magnolia wakati wa sherehe yangu ya harusi, ikifanyika katika kanisa la Kipentekosti la babu zangu. Nikiwa na mwaka mmoja kanisani kama mwongofu wa Kanisa, nilisafiri kwenda Salt Lake City, Utah, kupokea endaumenti yangu hekaluni na kuunganishwa na David, mchumba wangu.

Nilipoondoka Louisiana na kukaribia Utah, hisia za kunyong’onyea zikanijia. Kabla ya harusi, nilikuwa nikikaa na bibi wa kambo wa David, mwenye upendo aliyejulikana kama Shangazi Carol.

Hapa nilikuwa, mgeni Utah, kwenda kuisha katika nyumba ya mtu nisiyemjua kabla ya kuunganishwa milele katika familia niliyoijua kidogo. (Kitu kizuri nilimpenda na kumwamini mume wangu mtarajiwa na Bwana!)

Wakati mimi nilipokaribia mlango wa mbele wa nyumba ya Shangazi Carol, nilitaka kusita. Mlango ukafunguliwa—nilisimama pale kama sungura mwenye woga—na Shangazi Carol, bila ya neno, akaja na akanichukua kwa mikono yake. Yeye, ambaye hakuwa na watoto wake mwenyewe, alijua—moyo wake wa ulezi ulijua—kwamba nilihitaji sehemu ya kuishi. Ee, ufariji na utamu wa tukio lile! Woga wangu ukatoweka, na pale ikaja kwangu hisia za kutia nanga pahala pa usalama wa kiroho.

Upendo ni kutoa nafasi katika maisha yako kwa ajili ya mtu mwingine, kama Shangazi Carol alivyofanya kwangu.

Akina mama hutoa nafasi katika miili yao kumlea mtoto ambaye hajazaliwa,—na kwa matumaini nafasi katika mioyo wanapowalea—lakini kulea hakuishii katika kuzaa na kuwatunza watoto. Hawa aliitwa “mama” kabla yeye kupata watoto.4 Mimi naamini kwamba “kuwa mama” humaanisha “kuleta uhai.” Fikiria juu ya njia nyingi unaweza kuleta uhai. Hiyo inaweza kuwa kuleta maisha ya mhemko kwa wasio na tumaini au maisha ya kiroho kwa mwenye shaka. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, tunaweza kujenga mahala pa uponyaji kimhemko kwa wale waliobaguliwa, waliokataliwa, na wageni. Katika njia hizi laini lakini zenye nguvu, tunaujenga ufalme wa Mungu. Kina dada, sisi sote tulikuja duniani na vipawa hivi wa kuleta uhai, kulea, umama kwa sababu huo ndiyo mpango wa Mungu.

Kufuatia mpango Wake na kuwa mjenzi wa ufalme kunahitaji dhabihu isiyo na ubinafsi. Mzee Orson F. Whitney aliandika: “Kwa yote tunayoteseka na yote tunayovumilia, hususani tunapovumilia kwa uvumilivu, … hutakasa mioyo yetu … na hutufanya kuwa wapole na wenye hisani, … Ni kwa kupitia … kuhangaika na dhiki, ndipo tunapata elimu … ambayo itatufanya tuwe kama Baba na Mama yetu wa Mbinguni.”5 Haya majaribu ya kutakasa hutuleta Kwake Kristo, ambaye anaweza kutuponya na kutufanya tutumike katika kazi Yake wokovu.

Kuujenga Ufalme kwa njia ya Kunena na Kushuhudia

Pia tunajenga ufalme wakati tunaponena na kushuhudia ukweli. Tunafuatia mpangilio wa Bwana: Yeye husema na hufundisha kwa uwezo na mamlaka ya Mungu. Akina dada sasa, sisi tunaweza pia. Wanawake kwa kawaida wanapenda kuongea na kukusanyika! Tunapofanya kazi kwa mamlaka ya ukuhani tuliyopawa, kuongea na kukusanya kwetu hukua na kuwa mafundisho ya injili na uongozi.

Dada Julie B. Beck, aliyekuwa rais mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, alifundisha: “Uwezo wa kuwa na sifa wa, kupokea na kutenda juu ya ufunuo binafsi ni ujuzi pekee muhimu ambao unaweza kupatikana katika maisha haya. … Unahitaji juhudi za kufahamu.”6

Ufunuo binafsi toka kwa Roho Mtakatifu mara zote utatusukuma kujifunza, kunena, na kutenda juu ya ukweli wa milele—ukweli wa Mwokozi. Kadiri tunavyomfuata Kristo, ndivyo tutakavyohisi upendo na mwongozo Wake, kadiri tunavyohisi upendo Wake na mwongozo Wake ndivyo tutataka zaidi kusema na kufundisha ukweli jinsi Yeye alivyofundisha, hata kama tutakabiliwa na upinzani.

Miaka kadhaa iliyopita, niliomba ili nipate maneno ya kuutetea umama pale nilipopokea simu isiotambulika.

Mpiga simu aliuliza, “Wewe ni Neill Marriott, mama wa familia kubwa?”

Nilijibu kwa furaha, “Ndio!” nikitarajia yeye atasema kitu kama, “Sawa, ni vizuri!”

Lakini hapana! Sitosahau jibu lake wakati sauti yake ikiwa na mikwaruzo kwenye simu: “Nimechukizwa kwamba ungewaleta watoto katika ulimwengu huu uliofurika!

“Ee,” nikabwabwaja, “Naona jinsi unavyojisikia.”

Akasema kwa ghadhabu, “Hapana—hujui!”

Kisha nikanong’ona, “Sawa, huenda sijui.”

Akaanza kujitapa juu ya ujinga wangu wa kuchagua kuwa mama. Akiwa anaendelea, nilianza kuomba kwa ajili ya msaada na mawazo yakanijia: “Ni nini ambacho Bwana angemwambia?” Kisha nikahisi kwamba nilikuwa nimesimama katika ardhi thabiti na nikapata ujasiri wa nikiwa namfikiria Yesu Kristo.

Nilijibu, “Nina furaha kuwa mama, na nina kuahidi nitafanya kila kilicho katika uwezo wangu kuwalea watoto wangu katika hali ambayo wataufanya ulimwengu kuwa sehemu nzuri ya kuishi.”

Alijibu, “Sawa, nategemea utafanya hivyo!” na akakata simu.

Kilikuwa ni kitu kidogo—zaidi ya yote nilikuwa nimesimama salama katika jikoni mwangu mwenyewe! Lakini kwa njia yangu mwenye, niliweza kuongea katika utetezi wa familia, kina mama, na walezi kwa sababu ya vitu viwili: Nilielewa na kuamini mafundisho ya Mungu juu ya familia, na niliomba kwa ajili ya maneno ya kuwasilisha kweli hizi..

Kuwa tofauti na wa kipekee mbali na ulimwengu kutaleta baadhi ya ukosoaji, lakini lazima tutie nanga katika kanuni za milele na kushuhudia juu yake, bila kujali mwitikio wa ulimwengu.

Tunapojiuliza sisi wenyewe, “Tutafanya nini?” acheni tutafakari swali hili: “Ni nini ambacho Mwokozi hufanya mara zote?” Analea. Anatengeneza. Anahamasisha kukua na wema. Wanawake na akina dada, tunaweza kufanya vitu hivi! Wasichana wa Msingi, je, kuna mtu yeyote katika familia yenu ambaye anahitaji upendo na ukarimu wenu? Tunaujenga ufalme kwa kuwalea wengine.

Uumbaji wa Mwokozi wa dunia, chini ya usimamizi wa Baba Yake, lilikuwa tendo zuri la kulea. Alitoa nafasi kwetu ili kukua na kuendeleza imani katika nguvu za upatanisho Wake. Imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake ni nafasi ya uponyaji na tumaini, kukua na malengo. Sisi wote tunahitaji mahala pa kiroho na kimwili pa kuishi. Sisi, akina dada wa umri wote, tunaweza kutengeneza hicho, hata sehemu takatifu.

Jukumu letu la juu ni kuwa wanawake ambao wanamfuata Mwokozi, wanaolea kwa maongozi, kuishi ukweli bila woga. Tunapomuomba Baba aliye Mbinguni atufanye sisi kuwa wajenzi wa ufalme Wake, nguvu Zake zitatiririka ndani yetu na tutajua jinsi ya kulea, hatimaye kuwa kama wazazi wetu wa mbinguni. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Matendo ya Mitume 2:36–37.

  2. Eliza R. Snow, in Daughters in My Kingdom: The History and Work of Relief Society (2011), 42.

  3. Emma Smith, katika Daughters in My Kingdom, 12.

  4. Ona Mwanzo 3:20.

  5. Orson F. Whitney, katika Spencer W. Kimball, Faith Precedes the Miracle (1972), 98.

  6. Julie B. Beck, “And upon the Handmaids in Those Days Will I Pour Out My Spirit,” Liahona, May 2010, 11.