2010–2019
Furaha na Kupona Kiroho
Oktoba 2016


Furaha na Kupona Kiroho

Tunapolenga maisha yetu katika Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au kisichotokea—katika maisha yetu.

Wapendwa kaka na dada, leo ningependa kujadili kanuni ambayo ni msingi kwa kupona kwetu kiroho. Ni kanuni ambayo itakuja kuwa muhimu zaidi wakati majanga na kejeli zikiongezeka.

Hizi ni siku za mwisho, kwa hivyo hakuna yeyote kati yetu anayepaswa kushangaa tunapoona unabii ukitimia. Manabii wengi, akiwemo Isaya, Paulo, Nefi, na Mormoni, waliona kwamba nyakati za dhiki zingekuja,1 kwamba katika siku yetu ulimwengu wote ungekuwa kwenye ghasia,2 kwamba watu wangejipenda wenyewe, … bila upendo wa asili, … wapenda starehe kuliko kumpenda Mungu,”3 na wengi wangekuwa watumishi wa Shetani wanaoinua kazi za adui.4 Hakika, wewe na mimi “tunashindana dhidi ya watawala wa giza wa ulimwengu huu, [na] dhidi ya uovu wa kiroho katika sehemu za juu.”5

Wakati migogoro kati ya mataifa ikiendelea kuzidi, kama magaidi waoga wakiwawinda wasio na hatia, na huku ufisadi katika kila kitu kutoka kwenye biashara hadi serikalini unaongezeka na kuwa kitu cha kawaida, nini kinachoweza kutusaidia? Ni nini kinachoweza kumsaidia kila mmoja wetu na mapambano yetu binafsi na changamoto kali za maisha katika siku hizi za mwisho?

Nabii Lehi alifundisha kanuni ya kupona kiroho. Kwanza, fikiria hali yake: Alikuwa akiteseka kwa ajili ya kufundisha ukweli katika Yerusalemu na aliamriwa na Bwana kuacha mali yake na kukimbia na familia yake kwenda nyikani. Aliishi kwenye hema na aliishi kwa chakula alichoweza kukipata njiani akielekea mahali asipopajua, na alishuhudia watoto wake wawili, Lamani na Lemueli, wakipingana na mafundisho ya Bwana na kuwashambulia wadogo zao Nefi na Samu.

Bila shaka, Lehi alijua upinzani, wasiwasi, maumivu ya moyo, maumivu, kukata tamaa, na huzuni. Hata hivyo, alitangaza kwa ujasiri bila kusita kanuni aliyofunuliwa na Bwana. “Wanadamu wapo, ili wapate shangwe.”6 Fikiria! Katika maneno yote ambayo angeweza kutumia kuelezea asili na malengo ya maisha yetu duniani, alichagua neno shangwe!

Maisha yamejaa michepuko na njia zisizoendelea, majaribu na changamoto za kila aina. Kila mmoja wetu amekuwa na nyakati ambapo mateso, uchungu na kukata tamaa karibu vitumalize. Bado tupo hapa kupata furaha?

Ndio! Jibu ni ndiyo! Lakini hiyo inawezekanaje? Na tunatakiwa tufanye nini kupata furaha ambayo Baba wa Mbinguni ameihifadhi kwa ajili yetu?

Eliza R. Snow, Rais wa pili wa Muungano wa Uasidizi wa Kina Mama, alitoa jibu la kuvutia. Kwa sababu ya amri ya udhalimu, iliyotolewa wakati wa majira ya baridi ya mwaka 1838,7 yeye na Watakatifu wengine walilazimishwa kukimbia jimbo msimu huo huo wa baridi. Jioni moja, familia ya Eliza ililala kwenye kibanda kidogo cha miti kilichotumika na Watakatifu wakimbizi. Zaidi ya nyufa katikati ya gogo zilitolewa na kuchomwa moto na wale waliowatangulia, hivyo pakawa na shimo katikati ya magogo makubwa ya kutosha paka kupitia. Kulikuwa na baridi kali, na vyakula vyao viliganda kabisa.

Usiku ule watu 80 walibanana ndani ya kibanda kile kidogo, futi 20 mraba tu (mita 6.1 mraba). Wengi wao walikaa au kusimama usiku kucha kujaribu kupata joto. Nje, kikundi cha wanaume walitumia usiku ule kuota moto, wengine wakiimba nyimbo na wengine wakichoma viazi vilivyoganda. Eliza alieleza: “Hakuna nung’uniko lililosikika—wote walikuwa na furaha, na ukiangalia kwa nje, wageni wangetuona sisi kuwa ni kikundi cha wenye furaha badala ya kikundi kilicho furushwa na gavana.”

Taarifa ya Eliza ya kuchoka kule, jioni ya baridi hata kwenye-mifupa ilikuwa ya matumaini. Alitangaza: “Ule ulikuwa usiku wa furaha. Hakuna mtu mwingine bali watakatifu wanaweza kuwa na furaha wakiwa kwenye kila hali.”8

Hivyo ndivyo ilivyo! Watakatifu wanaweza kuwa na furaha wakiwa kwenye kila hali. Tunaweza kuwa na furaha hata kama tuna siku mbaya, wiki mbaya, au hata mwaka mbaya!

Wapendwa kaka na dada, furaha tuliyonayo haichangiwi na hali ya maisha yetu na kitu chochote kinachuhusiana na maisha yetu.

Tunapoweka umakini wa maisha yetu ni katika mpango wa wokovu wa Mungu, ambao Rais Thomas S. Monson ametufundisha, na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au kisichotokea—katika maisha yetu. Furaha inakuja kutoka na kwa sababu Yake. Yeye Ndiye kiini cha furaha yote. Tunaihisi wakati wa Krismasi pale tunapoimba, “Shangwe ulimwenguni, Bwana yuwaja.”9 Na tunaweza kuhisi hivyo mwaka mzima. Kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, Yesu Kristo ni furaha!

Hii ndiyo sababu wamisionari wetu huondoka nyumbani kwenda kutangaza injili Yake. Malengo yao siyo kuongeza idadi ya waumini wa Kanisa. Badala yake, wamisionari wetu hufundisha na kubatiza10 ili kuleta furaha kwa watu wa ulimwengu!11

Kama vile Mwokozi anavyotoa amani ambayo “inapita akili yote,”12 Yeye pia anatoa kiwango, kina, upana wa furaha ambayo inapita uelewa wa mwanadamu au uelewa wa kimwili. Kwa mfano, inaonekana haiwezekani kuwa na furaha wakati mtoto wetu anapoumwa na ugonjwa usiotibika, au unapopoteza kazi yako, au mwenza wako anapokusaliti. Hata hivyo hiyo ndiyo furaha anayotoa Mwokozi. Furaha Yake ni ya muda mrefu, ikituhakikishia kwamba “mateso yetu yatakuwa kwa muda”13 na yatatakaswa kwa ajili yetu.14

Ni vipi, tunaweza kupata furaha hivyo? Tunaweza kuanza kwa “kumtegemea Yesu aliye mwanzo na mwisho wa imani yetu”15 “katika kila wazo.”16 Tunaweza kutoa shukrani Kwake katika maombi yetu na kwa kutunza maagano tuliyoyaweka pamoja naye na Baba yetu wa Mbinguni. Kadiri Mwokozi wetu anapokuwa kweli kwetu zaidi na zaidi na tunapoomba furaha Yake ili tupewe, furaha yetu itaongezeka.

Furaha ina nguvu, na malengo ya furaha huleta nguvu ya Mungu katika maisha yetu. Jinsi ilivyo katika vitu vyote, Yesu Kristo ni mfano wetu mzuri, “kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba.”17 Fikiria hilo! Ili Yeye aweze kuvumilia mateso makali ambayo hajawahi kuyavumilia hapa duniani, Mwokozi wetu alilenga furaha!

Na nini ilikuwa furaha ambayo iliwekwa mbele Zake? Hakika inajumuisha furaha ya kusafisha, kuponya, na kutuimarisha; furaha ya kulipia dhambi za wote watakaotubu; furaha ya kutuwezesha wewe na mimi kurudi nyumbani—safi na wema—ili kuishi na wazazi wetu wa mbinguni na familia.

Kama tunalenga katika furaha itakayokuja kwetu, au kwa wale tuwapendao, nini tunachoweza kuvumilia ambacho sasa kinaonekana kushindikana, kichungu, cha kutisha, kisicho haki, au haiwezekani?

Baba mmoja katika hali halisi ya kiroho alilenga furaha ya kuwa safi na haki pamoja na Bwana—furaha ya kuwa huru kutokana na hatia na aibu—na furaha ya kuwa na amani ya akilini. Lengo hilo lilimpa ujasiri kukiri kwa dhati kwa mke wake na askofu kuhusu tatizo lake na picha za ngono na kutokuwa mwaminifu kwake. Sasa anafanya kila kitu anachoshauriwa na askofu wake na anajaribu kwa moyo wake wote kurudisha uaminifu wa mke wake.

Msichana alilenga kwenye furaha ya kuwa msafi kimwili, kumsaidia kuvumilia kejeli za marafiki, alipoondoka kwenye kundi maarufu na la kushawishi, lakini la hatari kiroho.

Mwanaume ambaye mara nyingi hakumheshimu mke wake na kuendekeza hasira kwa watoto wake, alilenga katika furaha ya kuwa mwema ili kupata Roho Mtakatifu kama mwenza wa daima. Lengo hilo linamtia moyo kumwacha mwanadamu wa asili,18 ambaye mara nyingi ameshindwa, na kufanya mabadiliko yanayohitajika.

Rafiki yangu mpendwa hivi karibuni aliniambia majaribu yake makali ya miongo miwili iliyopita. Alisema, “Nimejifunza kuteseka kwa furaha. Mateso yangu yalimenzwa na furaha katika Kristo”19

Je, kati ya wewe na mimi tunaweza kuvumilia, tunapolenga kwenye furaha ambayo “imewekwa mbele” yetu?20 Je, ni toba gani ambayo basi itawezekana? Je, ni udhaifu gani unaweza kuwa ni nguvu?21 Je, ni kujirudi kupi kutakuwa kwa baraka?22 Je, ni kukatishwa tamaa kupi, hata majanga, ambayo yatageuka kuwa uzuri kwetu?23 Na ni huduma gani kwa Bwana yenye changamoto ambayo tunaweza kuitoa?24

Tunapomlenga Mwokozi na kisha kufuata mfano wake wa kulenga furaha, tunahitaji kuepuka mambo ambayo yanaweza kukatiza furaha yetu. Mkumbuke Korihor, mpinga-Kristo? Alieneza uongo kuhusu Mwokozi, Korihori alikwenda sehemu moja hadi nyingine hadi pale alipoletwa mbele ya kuhani mkuu aliyemwuliza: “Kwa nini unazunguka ukiharibu njia za Bwana? Kwa nini unafundisha hawa watu kwamba hakutakuwa na Kristo, kukatiza furaha yao?”25

Chochote ambacho kinapinga Kristo au mafundisho Yake kitakatiza furaha yetu. Hiyo inajumuisha falsafa za mwanadamu, ambazo zipo kwa wingi mitandaoni na kwenye blogi, ambazo zinafanya sawa na kile alichofanya Korihori.26

Kama tunauangalia ulimwengu na kufuata kanuni kwa ajili ya furaha,27 kamwe hatutaijua furaha. Waovu wanaweza kupata idadi yoyote ya mihemko na hisia, lakini kamwe hawawezi kupata furaha!28 Furaha ni zawadi kwa walio wema.29 Ni zawadi ambayo inakuja kwa kutaka kujaribu kuishi maisha ya wema, kama ilivyofundishwa na Yesu Kristo.30

Alitufundisha jinsi ya kupata furaha. Tulipomchagua Baba wa Mbinguni kuwa Mungu wetu31 na tunapoweza kuhisi Upatanisho wa Mwokozi ukifanyakazi katika maisha yetu, tutajazwa na furaha32 Kila wakati tunawastawisha wenza wetu na kuwaongoza watoto wetu, kila wakati tunamsamehe mtu au kuwaomba msamaha, tunaweza kuhisi furaha.

Kila siku ambayo wewe na mimi tunachagua kuishi sheria ya selestia, kila siku ambayo tunatii maagano yetu na kuwasaidia wengine kufanya hivyo, furaha itakuwa yetu.

Yasikie maneno haya ya Mtunga Zaburi: “Nimemweka Bwana mbele yangu daima: kwa sababu yupo upande wangu wa kulia, wala sitatikisika. … Katika uwepo [Wake] ni furaha tele.”33 Wakati kanuni hii inapoingia katika mioyo yetu, kila siku inaweza kuwa siku ya furaha na shangwe.34 Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. 2 Wakorintho 3:1–5.

  2. Ona Mafundisho na Maagano 45:26; 88:91.

  3. 2 Timotheo 3:2–4.

  4. Ona Mafundisho na Maagano 10:5.

  5. Waefeso 6:12.

  6. 2 Nefi 2:25.

  7. Governor Lilburn W. Boggs of Missouri alitoa amri ya kuangamiza Wamormoni mnamo Oktoba 27, 1838 (ona Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 349.

  8. Ona Eliza R. Snow, in Edward W. Tullidge, The Women of Mormondom (1877), 145–46.

  9. “Joy to the World,” Hymns, no. 201.

  10. Wamisionari hufanya vile Bwana alivyoamuru: kuhubiri, kufundisha, na kubatiza katika jina Lake (ona Mathayo 28:19; Marko 16:15; Mormoni 9:22; Mafundisho na Maagano 68:8; 84:62; 112:28). Katika Sala Yake ya Maombezi, Yesu alitangaza uhusiano Wake kwa furaha ya wafuasi Wake. Yeye aliseima, “Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. ” (Yohana 17:13; mkazo umeongezewa).

  11. Ona Alma 13:22.

  12. Wafilipi 4:7.

  13. Mafundisho na Maagano 121:7.

  14. Ona 2 Nefi 2:2.

  15. Waebrania 12:2.

  16. Mafundisho na Maagano 6:36

  17. Waebrania 12:2.

  18. OnaMosia 3:19. Muhtasari: “mtu wa kawaida” siyo adui tu kwa Mungu; ni adui kwa mke na watoto wake.

  19. Ona Alma 31:38.

  20. Waebrania 12:2.

  21. Ona Etheri 12:27.

  22. Ona Alma 12:6.

  23. Ona Mafundisho na Maagano 122:7.

  24. Ona Mathayo 19:26; Marko 10:27.

  25. Alma 30:22. Kitabu cha Mormoni kimejaa mifano ya wanaume na wanawake ambao walipata furaha na shangwe kwa sababu walichagua kumfuata Yesu Kristo. Uchaguzi wowote, kama ilivyokuwa kwa Korihori, uongoza hata kwenye maangamizo.

  26. Uzushi, humaanisha uzingiziaji, inaekezewa kama taarifa za uongo na uovu zinazo kudusiwa kuvunja hadhi ya mtu au kitu. Uzushi ulikuwa ukitokea katika siku za Korihor, na inatokea sasa. Nabii Joseph Smith aliongea juu ya uimara wa Kanisa hata wakati wa uzushi. Alisema: “Kiwango cha Ukweli kimewekwa; hakuna mkono mchafu unaweza kuisimamisha kazi isiendelee; adha inaweza kuongezeka, makundi yaweza kujikusanya, majeshi yaweza kusimama, uzushi unaweza kukashifu, lakini ukweli wa Mungu utasonga mbele kwa ujasiri, uadilifu, na kwa uhuru, hadi itakapoingia kila bara, kutembelea kila tabia, kufagia kila nchi, na kusikika katika kila sikio, hadi pale lengo la Mungu litakapo kamilika, na Yahova Mkuu atakaposema kazi imekwisha” (Teachings: Joseph Smith, 444.

  27. Ulimwengu unafundisha kwamba ununuzi wa Vitu utaleta furaha. Na kama hilo halitoshi, nunua zaidi! Pia unafundisha kwamba unaweza kutenda dhambi ili kupata furaha. Na kama hilo halitoshi, tenda dhambi zaidi! Ahadi ni kwamba katika kila mwisho wa upinde wa maisha ya anasa ni jungu la furaha. Si kweli!

  28. Siyo katika ulimwengu huu au ulimwengu ujao.

  29. Watakatifu Wema “waliovumilia misalaba ya ulimwengu … wataurithi ufalme wa Mungu, … na furaha yao itajaa milele” (2 Nefi 9:18).

  30. Kwa mfano ona2 Nefi 27:30; 3 Nefi 27:16–18.

  31. Ona 1 Nefi 17:40.

  32. Ona Mosia 4:2–3.

  33. Zaburi 16:8, 11.

  34. Isaya 35:10; 2 Nefi 8:3.