2010–2019
Jifunzeni kutoka kwake Alma na Amuleki
Oktoba 2016


Jifunzeni kutoka kwake Alma na Amuleki

Ni tumaini langu kwamba wale ambao wamepotoka kutoka kwenye njia ya uanafunzi wataona na mioyo yao na kujifunza kutoka kwa Alma na Amuleki.

Alma Mdogo

Miongoni mwa wahusika wasiosahaulika katika maandiko ni Alma Mdogo. Ingawaje alikuwa mwana wa nabii mkuu, alipoteza mwelekeo kwa muda na kuwa “mtu mwovu na mwenye kuabudu sanamu.” Kwa sababu ambazo twaweza tu kukisia, alijishughulisha na kumpinga babake na akatafuta kuangamiza Kanisa. Na kwa sababu ya ufasaha wake na uwezo wake wa kushawishi, alifanikiwa sana.1

Lakini maisha yake Alma yalibadilika wakati malaika wa Bwana alijitokeza kwake na kuzungumza naye kwa sauti ya radi. Kwa siku tatu mchana na usiku, Alma “alisononeshwa na uchungu usio na mwisho, … hata na uchungu wa nafsi iliyolaaniwa.” Na kisha, kwa njia fulani, kumbukumbu dhaifu ilirudisha mwangwi katika giza la akili yake—ukweli wa milele, uliofundishwa na babake: kwamba Yesu Kristo angekuja “kulipia dhambi za ulimwengu.” Alma alikuwa ametupilia mbali kitambo sana dhana kama hizi, lakini “akili zake zikafikiria sana wazo hili,” na kwa unyenyekevu, bidii, aliweka imani yake katika nguvu ya Kristo ya upatanisho.2

Wakati ambapo Alma alipokwishapitia tukio hili, alikuwa mtu aliyebadilika. Kutoka wakati huo, alijitolea maisha yake kurekebisha makosa yake. Yeye ni mfano wa nguvu wa toba, msamaha, na uaminifu unaodumu.

Alma hatimaye alichaguliwa kumrithi babake kama kiongozi wa Kanisa la Mungu.

Kila raia wa taifa la Wanefi ni lazima alijua hadithi ya Alma. Twitter, Instagram na Facebook za siku zake zingekuwa zimejazwa na picha na habari kumhusu. Pengine alionekana mara kwa mara kwenye jalada la Zarahemla Weekly na alikuwa mada ya tahariri, matoleo maalum ya mitandao. Kwa kifupi, alikuwa pengine mtu mashuhuri aliyejulikana zaidi siku zake.

Lakini wakati ambapo Alma aliona watu wake walikuwa wanamsahau Mungu na kujiinua kwa kiburi na kuzozana, aliamua kujihuzulu kutoka kazi ya serikali na kujitolea yeye mwenyewe “kabisa kwa ule ukuhani mkuu ulio mpango mtakatifu wa Mungu,”3 akihubiri toba miongoni mwa Wanefi.

Mwanzoni, Alma alifanikiwa mno—hiyo ni, hadi aliposafiri hadi jiji la Amoniha. Watu wa jiji hilo walijua vyema kwamba Alma hakuwa kiongozi wao wa kisiasa, na walikuwa na heshima kidogo kwa mamlaka yake ya ukuhani. Walimkashifu, wakamkejeli, na wakamfurusha nje ya jiji lao.

Akiwa amevunjika moyo, Alma aliupa mgongo mji wa Amoniha.4

Lakini malaika alimwambia arudi.

Ee, fikiria juu ya hili: aliambiwa arudi kwa watu ambao walikuwa wanamchukia na wenye uhasama kwa Kanisa. Ilikuwa hatari, pengine kazi iliyotishia maisha. Lakini Alma hakusita. “Alirudi kwa haraka.”5

Alma alikuwa amefunga kwa muda wa siku nyingi wakati alipoingia jiji lile. Yeye alimuuliza mtu mgeni kabisa kama“angempatia mtumishi mnyenyekevu wa Mungu kitu cha kula.”6

Amuleki

Mwanaume huyu aliitwa Amuleki.

Amuleki alikuwa tajiri, raia aliyejulikana wa Amoniha. Ingawaje alitoka kwenye laini ndefu ya ukoo wa waaminifu, imani yake ilikuwa imekuwa dhaifu. Baadaye alikiri kwamba, “Niliitwa mara nyingi lakini sikusikia; kwa hivyo nilijua kuhusu vitu hivi, lakini nisingeweza kuvifahamu; kwa hivyo nikaendelea kumuasi Mungu.”7

Lakini Mungu alikuwa akimtayarisha Amuleki, na wakati alipokutana na Alma, alimkaribisha mtumishi wa Bwana nyumbani kwake, ambapo Alma alikaa kwa muda siku nyingi.8 Wakati huo, Amuleki alifungua moyo wake kwa ujumbe wa Alma, na mabadiliko ya ajabu yakaja. Kutoka hapo na kuendelea, Amuleki hakuamini tu, bali pia alikuwa mbingwa wa ukweli.

Wakati Alma alirudi kufundisha miongoni mwa watu wa Amoniha, alikuwa na shahidi wa pili pamoja naye, Amuleki, mmoja wao.

Matukio yanayofuata yanachangia mojawapo ya simulizi za huzuni na furaha katika maandiko yote. Unaweza kusoma kuhusu haya katika Alma mlango wa 8–16.

Leo ningependa kuwauliza mzingatie maswali mawili:

Kwanza: “Ni kipi naweza kujifunza kutoka kwake Alma?”

Pili: “Ni namna gani nafanana na Amuleki?”

Ni kipi naweza kujifunza kutoka kwake Alma?

Acha leo nianze kwa kuwauliza viongozi katika Kanisa la Yesu Kristo wa zamani, wa hivi sasa, au wa siku zijazo, “Ni kipi mnaweza kujifunzeni kutoka kwake Alma?”

Alma alikuwa mtu mwenye kipawa cha kipekee na mwenye ujuzi. Inaweza kuwa ilikuwa rahisi kufikiria kwamba hakuhitaji usaidizi wa mtu yeyote. Lakini ni kipi Alma alifanya aliporudi Amoniha?

Alma alimpata Amuleki na kumuomba usaidizi.

Na Alma alipata usaidizi.

Kwa sababu yeyote ile, mara nyingine viongozi husita kutafuta na kuuliza kina Amuleki wetu. Pengine tunafikiria kwamba tunaweza kufanya kazi bora sisi wenyewe, ama tunasita kuwasumbua wengine, au tunadhani kwamba wengine hawangetaka kuchangia. Mara nyingi sisi husita kuwaalika watu kutumia vipaji vyao walivyozawadiwa na Mungu na kuchangia kazi kuu ya wokovu.

Fikiria kuhusu Mwokozi—alianzisha Kanisa Lake peke yake?

La.

Ujumbe wake haukuwa “Songa kando. Nitashughulikia jambo hili.” Badala ilikuwa “Njoo, nifuate.”9 Alitoa maongozi, alialika, akafundisha, kisha akawa na imani katika wafuasi wake “kufanya vitu ambavyo mmeniona nikifanya.”10 Katika njia hii, Yesu Kristo hakujenga tu Kanisa Lake bali pia watumishi Wake.

Katika nafasi yoyote ile unayohudumu—iwe ni kama rais wa akidi ya mashemasi, rais wa kigingi, au Rais wa Eneo—kufanikiwa, ni lazima utafute kina Amuleki wako.

Inaweza kuwa ni mtu ambaye ni mnyenyekevu au hata asiyeonekana katika ushirika wenu. Inaweza kuwa ni mtu ambaye anaonekana asiyetaka au ambaye hawezi kuhudumu. Amuleki wenu waweza kuwa vijana au wazee, wanaume au wanawake, wenye tajriba, wachovu, au wasioshiriki kikamilifu Kanisani. Lakini kile kinachoweza kosa kuonekana mwanzo ni kuwa wana hamu ya kusikia kutoka kwako maneno “Bwana anakuhitaji. Ninakuhitaji!”

Kwa undani kabisa, wengi wanataka kumtumikia Mungu wao. Wanataka kuwa chombo mikononi Mwake. Wanataka kuingiza mundu zao na kujitahidi kwa uwezo wao kutayarisha dunia kwa kurudi kwa Mwokozi. Wanataka kujenga Kanisa Lake. Lakini wanasita kuanza. Mara nyingi wao husubiri kuulizwa.

Ninawaalika mfikirie kuhusu wale katika matawi yenu na kata, katika misheni zenu na vigingi, ambao wanahitaji kusikia mwaliko wa kutenda. Bwana amekuwa akishughulika nao—akiwatayarisha, akilainisha mioyo yao. Watafute kwa kuona na moyo wenu.

Watafuteni. Wafundishe. Watie msukumo. Waombe.

Shiriki nao maneno ya malaika kwake Amuleki—kwamba baraka ya Bwana itakuwa juu yao na nyumba zao.11 Unaweza ukashangaa kugundua mtumishi jasiri wa Bwana ambaye vinginevyo angebaki asijulikane.

Ni Namna Gani Nafanana na Amuleki?

Wakati wengine wetu tunapaswa kuwa tukimtafuta mtu kama Amuleki, kwa wengine swali laweza kuwa “Ni namna gani nafanana na Amuleki?”

Pengine, kwa miaka iliyopita, umekuwa mdhaifu kwa uanafunzi wako. Pengine moto wa ushuhuda wako umefifia. Pengine umejitoa kutoka mwili wa Kristo. Pengine umesikitika au hata kukasirika. Kama wengine wa Kanisa la kale la Efeso, unaweza kuwa umeuacha “upendo wako wa kwanza”12—kweli tukufu, za milele za injili ya Yesu Kristo.

Pengine, kama Amuleki, unajua moyoni mwako kwamba Bwana “alikuita [wewe] mara nyingi” lakini “hausikia.”

Hata hivyo, Bwana anaona ndani yako kile alichokiona ndani ya Amuleki—uwezo wa mtumishi shupavu mwenye kazi muhimu ya kufanya. Kuna watu ambao wanahitaji kusikiliza ushuhuda wako. Kuna huduma ambayo hakuna mwingine anayeweza kuitoa katika njia kama hiyo. Bwana amekukabidhi ukuhani Wake mtakatifu, ambao una uwezo mtakatifu wa kubariki na kuinua wengine. Sikiliza kwa moyo wako na fuata msukumo wa Roho.

Safari ya Muumini Mmoja

Niliguswa na safari ya ndugu mmoja ambaye alijiuliza, “Wakati Bwana ataitana, nitasikia?” Nitamwita ndugu huyu mzuri David.

David alijiunga na Kanisa miaka 30 iliyopita. Alihudumu misheni kisha akajiunga na shule ya sheria. Wakati alipokuwa akisoma na kufanya kazi kukimu familia yake changa, alipata habari fulani kuhusu Kanisa ambayo ilimchanganya. Vile alivyozidi kusoma aina hii ya rasilimali hasi, ndivyo alivyozidi kutokuwa mtulivu. Hatimaye aliuliza jina lake kutolewa kutoka kwenye rekodi za kanisa.

Kutoka wakati huo, kama Alma katika siku zake za uasi, David alitumia muda mrefu sana akijadiliana na waumini wa Kanisa, akichangia mijadala katika intaneti, na kupinga imani yao.

Alikuwa mahiri sana kufanya hivi.

Mmoja wa wauminii aliojadiliana nao nitamwita Jacob. Jacob sikuzote alikuwa mkarimu na alimheshimu David, lakini alikuwa imara katika kulitetea Kanisa.

Kwa muda wa miaka mingi, David na Jacob waliunda heshinma na uarafiki. Kile ambacho David hakufahamu ni kwamba Jacob alianza kumuombea David na alifanya hivyo kwa uaminifu kwa muda wa zaidi ya mwongo mmoja. Aliweka jina la rafiki yake kwa maombi katika mahekalu ya Bwana na kutumaini kwamba moyo wa David ungelainika.

Baada ya muda, pole pole, David alibadilika. Alianza kukumbuka kwa upendo matukio ya kiroho ambayo aliwahi kuwa nayo, na alikumbuka furaha aliyohisi wakati alipokuwa muumini wa Kanisa.

Kama Alma, David hakuwa amesahau kabisa kweli za injili ambazo alikuwa amezikubali kwa wakati fulani. Na kama Amuleki, David alihisi Bwana akimtafuta. David sasa alikuwa mbia katika kampuni ya sheria—kazi ya kifahari iliyompa mapato mazuri. Alikuwa na sifa kama mkosoaji wa Kanisa, na alikuwa na kiburi kupindukia kiasi cha kutouliza kukubaliwa tena.

Hata hivyo, aliendelea kuhisi mvuto wa Mchungaji.

Aliyachukulia moyoni maandiko “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”13 Aliomba, “Mungu mpendwa, nataka kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho tena, lakini niko na maswali yanayohitaji majibu.”

Alianza kusikiliza minong’ono ya Roho na majibu yenye misukumo kutoka kwa marafiki, jinsi alivyokuwa hajawahi awali. Moja baada ya nyingine, shaka zake ziligeuka kuwa imani, hadi alipogundua hatimaye kwamba, angeweza kuhisi ushuhuda wa Yesu Kristo na Kanisa Lake lililorejeshwa.

Katika hatua hiyo, alifahamu kwamba angeweza kushinda na kiburi chake na kufanya kila kilichotakikana ili akubalike tena Kanisani.

Hatimaye, David aliingia katika maji ya ubatizo na akaanza kuhesabu siku hadi wakati angeweza kurejeshewa baraka zake.

Nina furaha kusema kuwa msimu huu wa jua uliopita, baraka za David zilirejeshwa kwake. Yeye pia alianza kushiriki kikamilifu Kanisani na anahudumu kama mwalimu wa Mafundisho ya Injili katika kata yake. Anachukua kila nafasi kuzungumza na wengine kuhusu kubadilika kwake, kuponya uharibifu alioleta, na kushuhudia injili ya Yesu Kristo.

Hitimisho

Ndugu zangu wapendwa na marafiki, natutafuteni, tupate, tutie msukumo, na tutegemee maneno ya Amuleki katika kata zetu na vigingi vyetu. Kuna Amuleki wengi humu Kanisani leo.

Pengine unajua mmoja wao. Pengine wewe ni mmoja wao.

Pengine Bwana amekuwa akikunong’onezea, akikusihi urejelee penzi lako la kwanza, uchangie vipaji vyako, utumie ukuhani wako kwa ustahiki, na uhudumu bega kwa bega na Watakatifu wenzako katika kumkaribia Yesu Kristo na kujenga Ufalme wa Mungu.

Mwokozi wetu Mpendwa anajua mahali ulipo. Anajua moyo wako. Anataka kukuokoa. Atakufikia. Fungua tu moyo wako Kwake. Ni matumaini yangu kwamba wale ambao wamepotea kutoka njia ya uanafunzi—hata kwa hatua chache tu—watatafakari wema na neema ya Mungu, waone kwa mioyo yao, watajifunza kutoka kwake Alma na Amuleki, na kusikia maneno ya Mwokozi yanayobadilisha maisha: “Njoo Unifuate”

Ninawahimiza mtii mwito huu, kwa kweli wale ambao watafanya hivyo watapokea mavuno ya mbinguni. Baraka za Bwana zitakuwa juu yako na na nyumba yako.14

Juu ya haya nashuhudia, ninapowaachia baraka zangu, katika jina la Yesu Kristo, amina.