2010–2019
Usije Ukayasahau
Oktoba 2016


Usije Ukayasahau

Nawahimiza mkumbuke, hususani katika wakati wa upeo wa tatizo, wakati ulipomhisi Roho na ushuhuda wako ulikuwa imara; kumbukeni misingi ya imani mliyoijenga.

Habari za Asubuhi kina kaka na kina dada wapendwa. Tumebarikiwa vipi wakati wa huu mkutano mkuu. Mwaka wangu wa kwanza kama mshiriki wa akidi ya Mitume Kumi na Wawili umekuwa wa kunyenyekeza sana. Umekuwa mwaka wa kutumika sana, na wa ukuaji, na wenye heri, maombi ya haki kila wakati kwa Baba yangu wa Mbinguni. Nimezihisi sala za kuidhinisha za familia, marafiki, na waumini wa Kanisa ulimwenguni kote. Asanteni kwa mawazo yenu na sala zenu.

Nimekuwa pia na nafasi ya kukutana na marafiki wapendwa, baadhi kutoka miaka iliyopita na wengi nimekutana nao hivi majuzi. Ilikuwa baada ya kukutana na rafiki mpendwa ambaye nimemjua na kumpenda kwa miaka mingi kwamba nilijisikia kushawishika kutayarisha mazungumzo yangu leo.

Wakati tulipokutana, rafiki yangu aliniambia kwa siri kwamba amekuwa akipambana. Alihisi alikuwa anapata uzoefu fulani, kwa kutumia maneno yake, “upeo wa tatizo la imani” na akatafuta ushauri wangu. Nilijisikia kuwa na shukrani kwamba angeshiriki hisia zake na wasi wasi wake pamoja nami.

Alionyesha hamu kubwa kwa kile alichokuwa anahisi kiroho hapo mwanzo na kile sasa anafikiri alikuwa anakipoteza. Alipokuwa akizungumza, nilisikiliza kwa makini na kusali kwa dhati kujua nini Bwana atataka mimi niseme.

Rafiki yangu, kama pengine baadhi yenu, aliuliza maswali rahisi yenye nguvu yaliyowekwa kimsemo katika wimbo wa Msingi, “Baba wa Mbinguni, kweli wewe upo?”1 Kwa wale kati yenu watakaokuwa wanauliza swali hili hili, ningependa kushiriki nanyi ushauri ambao ningetoa kwa rafiki yangu na kutumaini kwamba kila mmoja wenu ataweza kuona kuwa imani yenu imeimarishwa na kukusudia kurudia upya kuwa mfuasi mwenye msimamo wa Yesu Kristo.

Ninaanza kwa kukumbusha kwamba wewe ni mwana na binti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na kwamba upendo Wake unabaki imara. Najua kwamba hisia hizi za uhakika za upendo ni ngumu kukumbuka wakati unapokuwa katikati ya mapambano binafsi au majaribu, masikitiko au ndoto zisizovunjika.

Yesu Kristo anajua kuhusu mapambano makali na majaribu. Alitoa maisha Yake kwa ajili Yetu. Saa zake za mwisho zilikuwa za kikatili, zaidi ya kitu chochote tunachokifahamu, lakini dhabihu yake kwa kila mmoja wetu ilikuwa dhihirisho kuu zaidi la upendo Wake safi.

Hakuna makosa, dhambi, au uchaguzi itakaobadili upendo wa Mungu kwa ajili yetu. Hio haimaanishi tabia ya dhambi inakubalika,wala haitoi wajibu wetu wa kutubu wakati dhambi zimefanywa. Lakini msisahau Baba wa Mbinguni anamjua na kumpenda kila mmoja wenu, na siku zote Yeye yu tayari kusaidia.

Wakati nilipotafakari hali ya rafiki yangu, akili yangu iliwaza kuhusu hekima kubwa inayopatikana katika Kitabu cha Mormoni. “Na sasa,wana wangu, kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu; kwamba ibilisi atakapo tuma mbele pepo zake kali, ndio, mishale yake kimbungani,wakati mvua yake ya mawe na dhoruba kali itapiga juu yenu, hautakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake mmejengwa, ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka,”2

Nina shuhudia kwamba “Shimo la taabu na msiba usioisha” ni mahali hakuna yoyote anataka kuwa. Rafiki yangu alijihisi kama alikuwa anakaribia ukingoni.

Wakati nimewashauri watu binafsi, kama vile rafiki yangu, nimetafiti maamuzi yao yaliyofanywa kwa miaka mingi ambayo yaliwasababishia kusahau uzoefu mtakatifu, kudhoofika, na kuwa na shaka. Niliwatia moyo, kama ninavyowatia moyo nyinyi sasa, kukumbukeni hususani katika wakati wa upeo wa tatizo, wakati ulipomhisi Roho na ushuhuda wako ulikuwa imara; kumbukeni misingi ya imani mliyoijenga. Ninaahidi kwamba kama mtafanya hivi, mtaepuka vitu ambavyo havijengi wala kuimarisha ushuhuda wenu au kile kinachodhihaki imani yenu, nyakati hizo za thamani wakati ushuhuda wenu ulistawi utarudi kwenye kumbukumbu zenu kupitia kwa sala ya unyenyekevu na kufunga. Nawahakikishieni kwamba mtahisi mara nyingine tena usalama na joto la injili ya Yesu Kristo.

Kila mmoja wetu lazima kwanza kujiimarisha wenyewe kiroho na kisha kuimarisha wale wanaotuzunguka. Tafakari maandiko kila siku, na kumbuka mawazo na hisia unazopata unapoyasoma . Tafuta vilevile vyanzo vingine vya ukweli, lakini sikiliza ushauri huu kutoka kwenye maandiko: “Lakini kuelimika ni vyema ikiwa watatii mawaidha ya Mungu.”3 Hudhuria mikutano ya Kanisa, hususani mikutano ya sakramenti, na pokea sakramenti na yafanye upya maagano yako, pamoja na ahadi daima kumkumbuka Mwokozi ili Roho Wake apate kuwa pamoja nawe.

Haidhuru makosa gani tumeyafanya au jinsi gani tunajihisi kama hatujakamilika, siku zote tunaweza kuwabariki na kuwainua wengine. Kuwafikia katika huduma ya Kikristo kunaweza kutusaidia kuhisi upendo wa Mungu ndani zaidi katika mioyo yetu.

Ni muhimu kukumbuka ushauri wa nguvu unaopatikana katika Kumbukumbu la Torati: “Lakini, jihadhari nafsi yako, ukalinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.”4

Vizazi vinaathiriwa na chaguzi tunazofanya. Shiriki ushuhuda wako na familia yako, watie moyo kukumbuka jinsi walivyohisi wakati walipomgundua Roho katika maisha yao na kuziandika hisia hizo katika shajara na historia binafsi ili kwamba maneno yao wenyewe yaweze, yanapohitajika, kuleta kumbukumbu zao jinsi Bwana amekuwa mwema kwao.

Mtakumbuka, kwamba Nefi na kaka zake walirudi Yerusalemu kuchukua mabamba ya shaba ambayo yalikuwa na historia iliyoandikwa ya watu wao, katika sehemu, ili kwamba wasije wakasahau maisha yao ya nyuma.

Pia, katika Kitabu cha Mormoni, Helamani aliwaita watoto wake kwa majina ya “baba zao wa mwanzo’ ili wasije wakasahau wema wa Bwana:

“Tazama, wana wangu, nanataka kwamba mtii amri za Mungu. …Tazama, nimewapatia majina ya wazazi wenu wa kwanza ambao walitoka nchi ya Yerusalemu; na nimefanya hivyo ili mnapokumbuka majina yenu mtaweza kuwakumbuka; na mnapowakumbuka mngekumbuka kazi yao; na mkikumbuka kazi zao mgejua vile imesemwa, na pia kuandikwa, kwamba walikuwa wazuri.

“Kwa hiyo, wanangu, ninataka kwamba mfanye yale ambayo ni mazuri, ili izungumzwe juu yenu, na pia iandikwe, hata vile ilivyozungumzwa na kuandikwa juu yao.”5

Wengi siku hizi wana desturi sawa na hizi za kuwaita watoto wao kwa majina ya mashujaa wa maandiko au mababu waaminifu kama njia ya kuwatia moyo kutosahau urithi wao

Nilipozaliwa, nilipewa jina la Ronald A. Rasband Jina langu la mwisho linaheshimu ukoo wa mababu wa baba yangu. Herufi ya katikati A nilipewa kunikumbusha kuheshimu ukoo wa kidenishi wa mama yangu Anderson.

Babu ya babu ya babu yangu Jens Anderson alitokea Denmark Na katika mwaka wa 1861 Bwana aliwaongoza wamisionari wawili wa Mormoni kwenye nyumba ya Jens na Ane Cathrine Anderson, ambako wamisionari waliwatambulishia mwana wao wa miaka 16, Andrew, kwa injili ya urejesho. Hivyo ulianza urithi wa imani ambao familia yangu nami ni wanufaishwa. Ukoo wa Anderson ulisoma Kitabu cha Mormoni na walibatizwa muda mfupi baadaye. Mwaka uliofuata, familia ya Anderson waliitika mwito wa nabii kuvuka Atlantic kujiunga na watakatifu katika Amerika Kaskazini.

Kwa huzuni, Jens alikufa safarini baharini, lakini mkewe na mwanawe waliendelea mpaka Salt lake Valley, wakawasili mnamo Septemba 3, 1862. Licha ya shida zao na huzuni wao mkubwa, imani yao kamwe haikuyumba, na wala imani ya wengi wa vizazi vyao haijayumba.

Picha
Mchoro katika Ofisi ya Mzee Rasband

Katika ofisi yangu umetundikwa mchoro6 ambao kwa umaridadi unaonyesha kiishara makumbusho ya ule mkutano wa kwanza kati ya wahenga wangu na wamisionari waaminifu. Mimi nimeamua kutosahau urithi wangu, kwa sababu ya jina langu milele nitakumbuka hiba ya uaminifu na dhabihu yao.

Kamwe usisahau, ukatilia shaka, au kupuuza uzoefu mtukufu wa kiroho wa kibinafsi. Mpango wa adui ni kutuvuta kutoka kuwa mashahidi wa kiroho, wakati mataminio ya Bwana ni kutuelimisha na kutushirikisha katika kazi Yake

Wacha nishiriki mfano wa kibinafsi wa ukweli huu. Dhahiri nakumbuka wakati nilipopokea hisia katika jibu kwa sala yenye nguvu. Jibu lilikuwa wazi na lenye nguvu Hata hivyo, nilishindwa kutenda mara moja, na baada ya kipindi cha muda, nilianza kushangaa kama kile nilichohisi kilikuwa kweli. Baadhi yenu mnaweza kuwa mmewahi kupatwa na udanganyifu ule wa adui pia.

Siku chache baadaye, niliamka na hii mistari yenye nguvu ya maandiko katika mawazo yangu.

“Amini, amini, ninakuambia, kama unataka ushahidi zaidi, rejesha mawazo yako juu ya usiku ule uliponililia katika moyo wako. …

“Sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili? Ni ushahidi gani mkubwa zaidi unaoweza kupata kuliko kutoka kwa Mungu?7

Ilikuwa kama Bwana alikuwa anasema, “Sasa, Ronald, nilikwisha kukuambia nini ulihitaji kufanya. Sasa kifanye!” Ni jinsi gani nilishukuru kwa masahihisho yale ya upendo na maelekezo! Nilifarijiwa mara moja na msukumo huu na niliweza kusonga mbele, nikijua moyoni mwangu kwamba sala yangu imejibiwa.

Ninashiriki uzoefu huu, kaka na dada zangu wapendwa, ili kuonyesha jinsi kwa haraka akili zetu zinaweza kusahau na jinsi uzoefu wa kiroho unavyotuongoza. Nimejifunza kuthamini nyakati kama hizo, “nisije nikayasahau.”

Kwa rafiki yangu, na kwa wote wanaotaka kushikilia imani yao, ninawapeni ahadi hii: unapoishi kwa uaminifu injili ya Yesu Kristo na kuishi kwa mafundisho yake, ushuhuda wako utalindwa, na utakua. Yaweke maagano uliyoyafanya, bila kujali matendo ya hao wanaokuzunguka. Muwe wazazi wenye bidii, akina kaka na akina dada, mababu mashangazi, wajomba, na marafiki mnaowaimarisha wapendwa wenu na ushuhuda binafsi na mnaoshiriki uzoefu wa kiroho. Bakini waaminifu na thabiti, hata kama dhoruba za shaka zinashambulia maisha yenu kupitia matendo ya wengine. Tafuta kile ambacho kitawaadilisha na kuwaimarisha kiroho. Epuka matoleo ya kughushi ya yanayoitwa ‘kweli” ambayo yanaitwa ya kuenea pote, na kumbuka kuandika hisia zako za “upendo, furaha, amani, ustahimilifu, upole, wema, imani, unyenyekevu, [na] kiasi.”8

Katikati ya dhoruba kali za maisha, usisahau urithi wako wa kiungu kama mwana na binti wa Mungu au majaliwa yako ya milele ya siku moja kurudi kuishi na Yeye, ambayo itapita chochote ulimwengu unaweza kutoa. Kumbuka maneno laini ya Alma: “Tazama, ninawambia, ndugu zangu ikiwa mmepata mabadiliko ya moyo, na ikiwa mmesikia kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi, nigeuliza, mnaweza kuhisi hivyo sasa?”9

Kwa wote wanaohisi kuwa na haja imani yao iimarishwe, ninawasihi, msiahau!: Tafadhali msisahau.

Ninatoa ushahidi kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu. Ninajua alimwona na alizungumza na Mungu Baba na Mwanae, Yesu Kristo, kama alivyoandikwa katika maneno yake mwenyewe. Jinsi gani nilivyo na shukrani kwamba yeye hakusahau kuandika juu ya uzoefu ule, ili tuweze wote kujua juu ya ushuhuda wake.

Ninatoa ushahidi wangu wa dhati wa Bwana Yesu Kristo. Anaishi; najua anaishi na anasimama kwenye kichwa cha Kanisa hili. Vitu hivi najua mwenyewe, huru wa sauti nyingine yoyote au shahidi, na ninaomba kwamba wewe nami kamwe hatutasahau kweli takatifu za milele—kwanza na kwanza kabisa kwamba sisi ni wana na mabinti wa Wazazi wa Mbinguni wanaoishi na wenye upendo, wanaotamani furaha yetu ya milele tu. Juu ya kweli hizi nashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.