2010–2019
Inukeni kwa Nguvu, Kina Dada Mlio Sayuni
Oktoba 2016


Inukeni Kwa Nguvu, Kina Dada Mlio Sayuni

Kuwa washika maagano walioongoka, tunahitaji kujifunza mafundisho muhimu ya injili na tuwe na ushuhuda usiotikisika wa ukweli wake.

Ni furaha iliyoje kukusanyika hapa katika Kituo cha Mikutano pamoja na wasichana na wanawake wa Kanisa. Pia tunafahamu kabisa kwamba kuna maelfu ya makundi mengine ya kina dada waliokusanyika duniani kote wakitazama matukio haya, na nina shukrani kwa nafasi na njia zinazotuwezesha kujiunga kwa pamoja katika umoja na madhumuni jioni hii.

Mnamo Oktoba 2006, Rais Gordon B. Hinckley alitoa hotuba iliyoitwa “Inukeni, Enyi Wanaume wa Mungu,” iliyoitwa kutokana na wimbo wa injili ulioandikwa mwaka 1911.1 Ulikuwa ni mwito wa kutenda kwa wanaume wa Kanisa kuinuka na kuwa bora. Hotuba hiyo imesalia akilini mwangu huku nikisali kujua kile nitakachoshiriki nanyi.

Kina dada tunaishi katika “nyakati hatari.”2 Hali ya siku zetu haifai kuwa ya kushangaza kwetu. Imetabiriwa kwa milenia kama ilani na onyo ili tuweze kuwa tayari. Sura ya 8 ya Mormoni inatoa maelezo halisi ya kutia wasiwasi kuhusu hali ya siku zetu. Katika sura hii, Moroni anasema kwamba ameona siku zetu, na inajumuisha vita na tetesi za vita, uharibifu mkubwa, mauaji, wizi, na watu wanaotuambia kwamba hakuna haki na uwongo mbele ya macho ya Mungu. Anaelezea kuhusu watu waliojawa na kiburi, waliojiweka katika kuvaa mavazi yenye bei ghali, na wanaokejeli dini. Anaonyeshwa watu walioshikilia vitu vya duniani kiasi cha kuwaachilia “wanaohitaji, na walio uchi, na wagonjwa wanaoteseka kupita kando”3 bila ya kuonekana.

Moroni anauliza swali la kuchunguza nafsi zetu—sisi tunaoishi katika nyakati hizi. Alisema, “Kwa nini mnaaibika kujivika jina la Kristo?”4 Agizo hili linaelezea kwa usahihi hali inayozidi kuwa ya kidunia katika ulimwengu wetu.

Joseph Smith—Mathayo inaashiria kwamba katika siku za mwisho hata “wateule … kulingana na agano”5 watadanganywa. Wale wa agano ni pamoja na wasichana wadogo, wasichana wakubwa, na kina dada wa Kanisa waliobatizwa na kufanya maagano na Baba yao wa Mbinguni. Hata sisi tuko hatarini kudanganywa na mafundisho ya uwongo.

Kina dada, siamini kwamba hali zitabadilika tukisonga mbele. Ikiwa mitindo ya sasa ni ishara, tunahitaji kujitayarisha kwa ajili ya tufani zinazokuja. Inaweza kuwa rahisi kwetu kukata tamaa, lakini kama watu wa agano, tusiwahi kata tamaa. Kama vile Mzee Gary E. Stevenson anavyosema, “Fidia karimu ya Baba wa Mbinguni kwa kuishi katika nyakati hatari ni kwamba pia tunaishi katika nyakati timilifu.”6 Ninapenda faraja ya tamko hilo.

Rais Russell M. Nelson alitueleza mwaka mmoja uliopita: “Mashambulizi dhidi ya Kanisa, mafundisho yake, na jinsi tuishivyo yataongezeka. Kwa sababu ya haya, tunahitaji wanawake ambao wanaelewa kwa kina mafundisho ya Kristo na watakaotumia kuelewa huko, kufundisha na kusaidia kulea kizazi kinzani kwa dhambi. Tunahitaji wanawake ambao wanaweza kugundua udanganyifu katika maumbo yake yote. Tunahitaji wanawake ambao wanajua jinsi ya kufikia nguvu ambayo Mungu anafanya ipatikane kwa wale wanaotii maagano na wanaoonyesha imani yao kwa ujasiri na hisani. Tunahitaji wanawake walio na ujasiri na maono ya Mama yetu Hawa.”7

Ujumbe huu unanihakikishia kwamba licha ya hali ya siku zetu, tunazo sababu nyingi za kufurahia na kuwa na matumaini. Ninaamini kwa moyo wangu wote kwamba sisi kina dada tunayo nguvu asili na imani ambayo itatuwezesha kukabiliana na changamoto za kuishi katika siku za mwisho. Dada Sheri Dew aliandika, “Ninaamini kwamba wakati tutakapojifunza kuachilia huru ushawishi mzima wa wanawake walioongoka, wanaotii maagano, ufalme wa Mungu utabadilika mara moja.”8

Itachukua juhudi za pamoja kuongoka na kutii maagano yetu. Kufanya hivyo, tunahitaji kuwa wasichana na wanawake ambao wanasoma mafundisho muhimu ya injili na tuwe na ushuhuda usiotikisika wa ukweli wake. Kuna sehemu tatu ambazo ninaamini ni za msingi kwa ushuhuda wa nguvu na ninazozingatia kuwa muhimu kwa uelewa wetu.

Kwanza, tunahitaji kukubali umuhimu wa Mungu Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo, katika imani yetu na wokovu. Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Tunahitaji kusoma na kuelewa Upatanisho Wake na jinsi ya kuutumia kila siku; toba ni mojawapo ya baraka kubwa zaidi kila mmoja wetu aliyonayo kubakia kwenye njia. Tunahitaji kumtazama Yesu Kristo kama mfano wetu wa msingi wa kuigwa na mfano vile tunapaswa kuwa. Tunahitaji kuendelea kufundisha familia zetu na madarasa yetu kuhusu mpango mkuu wa Baba yetu wa wokovu, ambao unajumuisha mafundisho ya Kristo.

Pili, tunahitaji kuelewa umuhimu wa urejesho wa mafundisho, mpangilio, na funguo za mamlaka katika siku hizi za mwisho. Tunahitaji ushuhuda mtakatifu kwamba Nabii Joseph Smith alichaguliwa na kuteuliwa na Bwana kuleta urejesho huu na kutambua kwamba aliwashirikisha wanawake wa Kanisa kulingana na mpangilio uliokuwa katika Kanisa la Bwana la kale.9

Na tatu, tunahitaji kujifunza na kuelewa amri na maagano ya hekaluni. Hekalu lina sehemu muhimu sana katika imani yetu tukufu, na Bwana anatutaka tushiriki, tutafakari, tujifunze, na tutafute maana na matumizi ya kibinafsi. Tutakuja kuelewa kwamba kupitia maagizo ya hekaluni, nguvu za uchamungu hujidhihirisha maishani mwetu10 na kwa sababu ya maagizo ya hekaluni, tunaweza kujihami na uwezo wa Mungu, jina Lake litakuwa juu yetu, na utukufu Wake utuzingire pande zote, na malaika wake watulinde.11 Ninajiuliza ikiwa tunatumia kikamilifu uwezo wa ahadi hizo.

Kina dada, hata aliye mdogo zaidi katika hadhira hii anaweza kuinuka katika imani na kufanya jukumu muhimu katika kujenga ufalme wa Mungu. Watoto huanza kupata ushuhuda wao kupitia kusoma na kusikiliza maandiko, kuomba kila siku, na kushiriki sakramenti katika njia ya maana zaidi. Watoto wote na wasichana wanaweza kuhimiza mikutano ya jioni ya familia nyumbani na kushiriki kikamilifu. Mnaweza kuwa wa kwanza kupiga magoti wakati familia zenu zinapokuja pamoja katika sala za familia. Hata kama nyumba zenu hazipo jinsi mngependelea, mifano yenu ya kibinafsi ya kuishi injili kwa uaminifu kunaweza kushawishi maisha ya familia na marafiki.

Wasichana wa Kanisa wanahitaji kujitazama kama washirika muhimu katika kazi ya wokovu inayoongozwa na ukuhani na sio tu kama watazamaji au wafuasi. Mko na miito na mmesimikwa na wale wenye funguo za ukuhani mtende kama viongozi wenye nguvu na mamlaka katika kazi hii. Mnapotukuza miito yenu katika urais wa madarasa na kujitayarisha kiroho, mkishauriana pamoja, mkitafuta kuwahudumia washiriki wa darasa lenu, na mkifundisha kila mmoja wenu injili, mnachukua nafasi yenu katika kazi hii na nyinyi pamoja na wenzenu mtabarikiwa.

Wanawake wote wanahitaji kujitazama kama washiriki muhimu katika kazi ya ukuhani. Wanawake katika Kanisa hili ni marais, washauri, walimu, washiriki wa mabaraza, kina dada, na kina mama, na ufalme wa Mungu hauwezi kufanya kazi isipokuwa tuinuke na kutenda majukumu yetu kwa imani. Mara nyingine tunahitaji tu kuwa na ono kubwa la kile kinachowezekana.

Picha
Dada Maldonado akiwa na Dada Oscarson

Hivi karibuni nilikutana na dada kutoka Mexico ambaye anaelewa maana ya kutukuza mwito wake kwa imani. Marffissa Maldonado aliitwa kufundisha Shule ya Jumapili ya vijana miaka mitatu iliyopita. Alikuwa na wanafunzi 7 walioshiriki alipoitwa, lakini sasa yuko na 20 ambao wanashiriki mara kwa mara. Nilimuuliza, kwa mshangao, kile alichokuwa amefanya kuongeza idadi yao. Alisema kwa staha, “Ee, sio mimi tu. Washiriki wote wa darasa walisaidia.” Pamoja, waliona majina ya wasioshiriki kikamilifu kwenye orodha na wakaanza kwenda pamoja na kuwaalika warudi kanisani. Pia wamekuwa na ubatizo kutukana na juhudi zao.

Picha
Darasa la Shule ya Jumapili huko Mexico

Dada Maldonado alifungua tovuti katika mtandao wa kijamii kwa ajili tu ya washiriki wa darasa lake kwa jina “Mimi ni Mtoto wa Mungu,” na yeye hutuma mawazo ya kutia msukumo na maandiko mara kadhaa kwa wiki. Mara kwa mara kupitia ujumbe mfupi yeye huwatumia wanafunzi wake mazoezi na faraja. Anahisi kwamba ni muhimu kuwasiliana nao kupitia njia wanazohusiana nazo vyema zaidi, na inafanya kazi. Aliniambia tu, “Ninawapenda wanafunzi wangu.” Niliweza kuhisi upendo huo aliponieleza kuhusu juhudi zao, na mfano wake ulinikumbusha kuhusu kile ambacho mtu mmoja mwenye imani na vitendo anaweza kutimiza katika kazi yake kwa usaidizi kutoka kwa Bwana.

Vijana wetu wanakabiliana na maswali magumu kila siku, na wengi wetu tuna wanapendwa wale ambao wanahangaika kutafuta majibu. Habari njema ni kwamba kuna majibu kwa maswali yanayoulizwa. Sikiliza jumbe za hivi karibuni kutoka kwa viongozi wetu. Tunahimizwa tusome na tuelewe mpango wa furaha wa Baba yetu wa Mbinguni. Tumekumbushwa kuhusu kanuni zilizoko katika tangazo la familia kwa dunia.12 Tunahimizwa kufundisha na kutumia rasilimali hizi kama vifaa vya kupima ili tusalie katika njia iliyosonga na nyembamba.

Karibu mwaka mmoja uliopita, nilimtembelea mama mwenye watoto wadogo ambaye aliamua kuchukua hatua ya mapema kuwakinga watoto wake dhidi ya ushawishi hasi waliokuwa wanapata katika mtandao na shuleni. Yeye huchagua mada fulani kila wiki, mara nyingi mojawapo ya zilizoibua mijadala katika mtandao, na yeye huanzisha majadiliano ya maana katika wiki wakati ambapo watoto wake wanaweza kuuliza maswali na anaweza kuhakikisha kwamba wanapata mtazamo wa haki kuhusu mara nyingi maswala magumu. Anafanya nyumbani kwake kuwa mahala salama pa kuuliza maswali na kuwa na mafundisho muhimu ya injili.

Nina hofu kwamba tunaishi katika mazingira haya ya kuepuka kuwakosea watu kiasi cha kukosa kabisa kufundisha kanuni sahihi mara nyingine. Tunakosa kuwafundisha wasichana wetu kwamba kujitayarisha kuwa mama ni muhimu zaidi kwa sababu hatutaki kuwakosea wale ambao hawajaolewa, wale wasioweza kupata watoto, au kuonekana kama kwamba tunakandamiza uchaguzi wa baadaye. Kwa upande mwingine, tunaweza kosa kusisitiza umuhimu wa masomo kwa sababu hatutaki kutoa ujumbe kwamba ni muhimu kuliko ndoa. Sisi huepuka kutangaza kwamba Baba yetu wa Mbinguni anafafanua ndoa kuwa baina na mwanaume na mwanamke kwa sababu hatutaki kuwakosea wale wanaovutiwa kimapenzi na watu wa jinsia moja. Na twaweza kupata ni vigumu kuzungumzia maswala ya jinsia au ujinsia bora.

Hakika, kina dada, tunahitaji kutumia unyeti, lakini pia tutumie fikra zetu na kuelewa kwetu kwa mpango wa wokovu kuwa wajasiri na kusema waziwazi tunapowadia kuwafundisha watoto wetu na vijana kanuni muhimu za injili ambazo ni lazima wazielewe ili waweze kusafiri duniani wanamoishi. Ikiwa hatutawafundisha watoto wetu na vijana mafundisho ya kweli—na kuyafundisha wazi—dunia itawafundisha uwongo wa Shetani.

Ninapenda injili ya Yesu Kristo, na nina shukrani milele kwa mwelekeo, nguvu, na usaidizi wa kila siku ninaopata kama binti wa agano wa Mungu. Ninashuhudia ya kwamba Bwana ametubariki, kama wanawake tunaoishi katika hizi nyakati hatari, na nguvu zote, vipaji, na ushupavu unaohitajika ili kusaidia kutayarisha dunia kwa Ujio wa Pili wa Bwana Yesu Kristo. Ninaomba kwamba tuweze kuona uwezo wetu wa kweli na kuinuka ili tuwe wanawake wenye imani na ujasiri ambao Baba yetu wa Mbinguni anahitaji tuwe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.