2010–2019
Kuvuta Nguvu za Yesu Kristo katika Maisha Yetu
Aprili 2017


Kuvuta Nguvu za Yesu Kristo katika Maisha Yetu

Injili ya Yesu Kristo imejaa nguvu Zake, ambazo zinapatikana kwa kila binti au mwana wa Mungu atafutaye kwa bidii.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, tunaishi katika kipindi kigumu sana cha mwongozo wa kiungu. Changamoto, mabishano, na magumu yametuzunguka. Nyakati hizi za ghasia zilitabiriwa na Mwokozi. Yeye mwenyewe alituonya kwamba katika siku zetu adui atachochea hasira katika mioyo ya watu na kuwapotosha.1 Hata hivyo Baba yetu wa Mbinguni katu hakukusudia kwamba tungepambana na mzingile wa matatizo haya binafsi na mambo ya kijamii peke yetu.

“Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee.”2 kuja kutusaidia.3 Mwanawe, Yesu Kristo, alitoa uhai Wake kwa ajili yetu. Yote, ili kwamba tuweze kuzifikia nguvu za uungu—nguvu za kutosha kukabiliana na magumu, vikwazo, na majaribu ya siku zetu.4 Leo ningependa kuongea kuhusu jinsi tunavyoweza kuvuta katika maisha yetu nguvu ya Mwokozi wetu na Bwana, Yesu Kristo.

Tunaanza kwa kujifunza kuhusu Yeye.5 Haiwezakani kwetu [sisi] kuokolewa katika ujinga.”6 Tunapojua zaidi kuhusu huduma na wito wa Mwokozi7—tunaelewa zaidi mafundisho Yake8 na alichofanya kwa ajili yetu—tunajua zaidi kwamba Yeye anaweza kutupa nguvu tunazohitaji kwa ajili ya maisha yetu.

Mapema mwaka huu, niliwaomba vijana wa Kanisa kutenga sehemu ya muda wao kila wiki ili kujifunza kila kitu ambacho Yesu alisema na kutenda kama ilivyoandikwa katika vitabu vitakatifu.9 Niliwaalika kufanya dondoo za maandiko kuhusuYesu Kristo katika Mwongozo wa Mada uwe kiini cha mtaala wao binafsi.10

Nilitoa changamoto hiyo kwa sababu mimi mwenyewe tayari nilikuwa nimeikubali. Nilisoma na kupigia mstari kila mstari uliodondoa kuhusu Yesu Kristo, kama ilivyoorodheshwa chini ya vichwa vidogo 57 vya habari katika Mwongozo wa Mada.11 Nilipomaliza zoezi hilo la kufurahisha, mke wangu aliuliza ilikua na matokeo gani kwangu. Nilimwambia, “sasa mimi ni mtu tofauti!”

Nilihisi moyo mpya wa kujitolea Kwake wakati niliposoma tena katika Kitabu cha Mormoni maelezo ya Mwokozi mwenyewe kuhusu wito Wake hapa duniani. Alitangaza:

“Nilikuja kwenye ulimwengu kufanya mapenzi ya Baba, kwa sababu alinituma.

“Na Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba.”12

Kama Watakatifu wa siku za Mwisho, tunarejea huduma Yake kama Upatanisho wa Yesu Kristo, ambao ulifanya ufufuko kuwa jambo halisi kwa wote na kufanya uzima wa milele uwezekane kwa wote wanaotubu dhambi zao na kupokea na kushika ibada na maagano muhimu.

Kimafundisho haijitoshelezi kuongelea dhabihu ya Bwana ya kulipia dhambi kwa vifungu vya mkato kama vile “Upatanisho” au “ nguvu ya uwezesho ya Upatanisho” au “kutumia Upatanisho” au “kuimarishwa na Upatanisho.” Maelezo haya huwakilisha hatari halisi ya kuipotosha imani kwa kulifanya tukio kana kwambalina uwepo hai na uwezekano wa kujitegemea lenyewe mbali na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanae, Yesu Kristo.

Chini ya mpango mkuu wa milele wa Baba, ni Mwokozi ndiye aliyeteseka. Ni Mwokozi ndiye aliyefungua kamba za mauti. Ni Mwokozi aliyelipa deni la dhambi zetu na uvunjaji wetu wa sheria na kuziondoa kwa masharti ya toba yetu. Ni Mwokozi ndiye anayetukomboa kutokana na kifo cha kimwili na cha kiroho.

Hakuna kitu kisicho na umbo maalum kinachoitwa “Upatanisho” ambacho kwacho tunaomba msaada, uponyaji, msamaha, au nguvu. Yesu Kristo ndiye chanzo. Maneno matakatifu kama vile Upatanisho na Ufufuko huelezea kile ambacho Mwokozi alifanya, kulingana na mpango wa Baba, ili kwamba sisi tuishi na kuwa na tumaini katika maisha haya na kupokea uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Dhabihu upatanisho ya Mwokozi—ni tendo kuu la historia yote ya wanadamu hueleweka vizuri na kushukuriwa wakati tunapouelezea na kwa ufasaha zaidi tunapouunganisha na Yeye.

Umuhimu wa huduma ya Mwokozi ulisisitizwa na Nabii Joseph Smith, aliyetangaza kwa mkazo kwamba “kanuni muhimu za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba alikufa, alizikwa, na kufufuka tena siku ya tatu, na kupaa mbinguni, na mambo mengine yote yahusuyo dini yetu ni viambatisho tu kwa hilo.”13

Ilikuwa ni kauli hii hasa ya Nabii iliyotoa kichocheo kwa manabii 15, waonaji na wafunuzi kutoa na kutia sahihi ushuhuda wao katika kukumbuka maadhimisho ya miaka 2,000 ya kuzaliwa Bwana. Ushuhuda huo wa kihistoria unaitwa “Kristo Aliye Hai.”14 Waumini wengi wamekariri kweli zake. Wengine wanajua kwa kiasi kidogo kuhusu uwepo wake. Unapotafuta kujifunza zaidi kuhusu Yesu Kristo, nakusihi ujifunze “Kristo Aliye Hai.”

Tunapowekeza muda katika kujifunza kuhusu Mwokozi na Upatanisho Wake, tunavutwa kushiriki katika kipengele kingine muhimu cha kuzifikia nguvu Zake: tunachagua kuwa na imani Naye na kumfuata.

Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo wako tayari kusimama, kuongea, na kuwa tofauti na watu wa ulimwengu. Hawana woga, wamejitolea na ni wajasiri. Nilijifunza juu ya wafuasi kama hao wakati wa kazi yangu ya hivi karibuni huko Mexico, ambapo nilikutana na viongozi wa serikali vile vile viongozi wa madhehebu mengine. Kila mmoja alinishukuru kwa ushujaa wa waumini wetu na juhudi za mafanikio katika kulinda na kutunza ndoa na familia imara katika nchi yao.

Hakuna kitu rahisi au kinachokuja chenyewe kuhusu kuwa mfuasi imara. Kuzingatia kwetu lazima kuwe imara katika Mwokozi na injili Yake. Inahitaji ukakamavu wa akili kujitahidi kumwangalia katika kila wazo.15 Lakini tunapofanya hivyo, wasiwasi wetu na woga huondoka.16

Hivi karibuni nimejifunza juu ya Laureli mdogo jasiri. Alialikwa kushiriki katika mashindano ya jimbo kwa niaba ya shule yake ya upili jioni ile alikuwa amehidi kushiriki katika mkutano wa kigingi wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Alipogundua muingiliano huo na kuwaelezea viongozi wa mashindano hayo kwamba angehitaji kuondoka mapema mashindanoni ili kuhudhuria mkutano muhimu, aliambiwa angeondolewa kama angefanya hivyo.

Laureli huyu wa siku za mwisho alifanya nini? Alitunza ahadi yake ya kushiriki mkutano wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama . Kama ilivyoahidiwa, aliondolewa kutoka kwenye mashindano ya jimbo. Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake, alijibu kwa ufupi, “vema, Kanisa ni muhimu zaidi, sivyo?”

Imani katika Yesu Kristo hutusukuma kufanya vitu ambavyo vinginevyo tusingeweza kufanya. Imani inayotusukuma kwenye matendo hutuwezesha kuzifikia zaidi nguvu Zake.

Tunaongeza pia nguvu ya Mwokozi katika maisha yetu tunapofanya maagano matakatifu na kutunza maagano hayo kwa usahihi. Maagano yetu hutuunganisha Naye na kutupatia nguvu ya kiungu. Kama wafuasi waaminifu, tunatubu na kumfuata Yeye kwenye maji ya ubatizo. Tunatembea kwenye njia ya agano na kupokea ibada zingine muhimu.17 Na tunashukuru, kwamba mpango wa Mungu huwezesha baraka hizo kutolewa kwa mababu waliokufa bila nafasi ya kuzipata katika maisha yao duniani.18

Wanaume na wanawake-watunza maagano hutafuta njia za kujilinda na dunia pasipo mawaa hivyo hakutakuwepo na chochote cha kuwazuia kufikia nguvu ya Mwokozi. Mke mmoja na mama muaminifu aliandika hiki hivi karibuni: “Hizi ni nyakati sumbufu na hatari. Jinsi gani tumebarikiwa kuwa na ufahamu mkubwa wa mpango wa wokovu na muongozo wa kiungu kutoka kwa manabii, mitume na viongozi wenye upendo, ili kutusaidia kuvuka salama bahari yenye dhoruba. Tuliacha tabia yetu ya kufungulia redio asubuhi. Badala yake, sasa tunasikiliza mkutano mkuu kwenye simu zetu za mkononi kila asubuhi tunapojiandaa kwa siku mpya.”

Jambo jingine katika kuvuta nguvu ya Mwokozi maishani mwetu ni kumwendea katika imani. Kumwendea huko kunahitaji bidii, na juhudi za msisitizo.

Picha
Mwanamke akigusa upindo wa vazi la Mwokozi

Unaikumbuka hadithi ya Biblia ya mwanamke aliyeteseka kwa miaka 12 kwa tatizo la kudhoofisha?19 Alionyesha imani kubwa kwa Mwokozi, akisema, “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.”20

Mwanamke huyu mwaminifu na mwenye fokasi alihitaji kujinyoosha kwa kadiri alivyoweza ili kufikia nguvu Zake. Kujinyoosha kwake kimwili ni ishara ya kujinyoosha kwake kiroho.

Wengi wetu tumelia kutoka kwenye vina vya mioyo yetu kwa maneno ya kufanana na ya mama huyu: “Kama ningeweza kujinyoosha kiroho vya kutosha kupokea nguvu ya Mwokozi katika maisha yangu, ningejua jinsi ya kushughulikia hali yangu ya kusononesha moyo. Ningejua cha kufanya. Na ningepata nguvu za kukifanya.”

Unapotafuta nguvu ya Mwokozi katika maisha yako kwa ukubwa kama wa mfa maji wakati anapohangaika na kuhangaika kwa ajili ya hewa, nguvu kutoka kwa Yesu Kristo itakuwa yako. Mwokozi anapojua unataka kweli kumfikia—wakati Yeye anapohisi hiyo tamaa kuu ya moyo wako ni kuvuta nguvu yake katika maisha yako—utaongozwa na Roho Mtakatifu kujua vyema kabisa kile unachohitajika kufanya.21

Unapojinyoosha kiroho kuliko chochote ulichowahi kufanya kabla, ndipo nguvu yake itatiririka kuingia kwako.22 Na ndipo utaelewa maana ya kina ya maneno tunayoimba kwenye wimbo “Roho wa Mungu”:

Bwana anapanua uelewa wa Watakatifu. …

Elimu na nguvu za Mungu zapanuka;

Pazia ulimwenguni linaanza kufunguka.23

Injili ya Yesu Kristo imejaa nguvu Zake, ambazo zinapatikana kwa kila binti au mwana wa Mungu atafutaye kwa bidii. Ni ushuhuda wangu kwamba tunapovuta nguvu zake katika maisha yetu, wote Yeye na sisi tutafuraha.24

Kama mmoja wa mashahidi wake maalum, natamka kwamba Mungu yu Hai! Yesu ndiye Kristo! Kanisa Lake limerejeshwa hapa duniani! Nabii wa Mungu duniani leo ni Rais Thomas  S. Monson, ambaye ninamkubali kwa moyo wangu wote. Ninashuhudia hivyo kwa onyesho langu la upendo na baraka kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona 2 Nefi 28:19–30.

  2. OnaYohana 3:16.

  3. Yesu alikuwa Mpakwa mafuta—alipakwa mafuta na Baba wa Mbinguni kuwa mwakilishi wake binafsi katika mambo yote yahusuyo wokovu wa mwanadamu. Yesu alipakwa mafuta kuwa Mwokozi wetu na Mkombozi. Kabla ya ulimwengu kuumbwa, Yesu alipakwa mafuta kufanya kutokufa kuwe halisi na uzima wa milele kuwezekana kwa watoto wote wa Mungu (ona Yohana 17:24; 1 Petro 1:20) Hivyo Yesu alibeba sifa mbili za kipekee: Masiya (Kiebrania) na Kristo (Kigriki)—kila moja likimaanisha mpakwa mafuta.” (Ona kamusi ya Biblia, “Mpakwa mafuta.”)

  4. Tunaweza kujilinda kwa kujua na kuishi kwa neno la Mungu (ona Waefeso 6:17–18; Mafundisho na Maagano 27:18).

  5. Chini ya maelekezo ya Baba yake, Yesu aliumba dunia (ona Yohana 1:2–3) na dunia zingine zisizo na idadi (ona Musa 1:33). Zamani kabla ya kuzaliwa kimwili, Yesu alikuwa Yehova mkuu—Mungu wa Agano la Kale. Alikuwa ni Yehova aliyeongea na Musa juu ya Mlima Sinai. Alikuwa ni Yehova aliefanya agano na Ibrahimu kwamba mataifa yote ya dunia yatabarikiwa kupitia uzao wa Ibrahimu. Na alikuwa Yehova aliyefanya agano na familia ya nyumba ya Israeli. Yesu pia alikuwa Immanueli aliyeahidiwa, kama ilivyotabiriwa na Isaya (ona Isaya 7:14).

  6. Mafundisho na Maagano 131:6

  7. Ona Mafundisho na Maagano 76:40–41.

  8. Ona 2 Nefi 31:2–21.

  9. Biblia Takatifu, Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu.

  10. Ona Mwongozo wa Maandiko, “Yesu Kristo.” Kwa kuongezea maneno yaliyoko chini ya kichwa hicho cha habari, kuna vichwa vidogo vya habari 57 kumhusu. Kwa maandiko yasiyo ya kiingereza, tumia Mwongozo wa Maandiko.

  11. Zaidi ya orodha 2,200 zimeonyeshwa kwenye hizo kurasa 18 za Mwongozo wa Mada.

  12. 3 Nefi 27:13–14.

  13. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 49.

  14. Ona “Kristo Aliye Hai: The Testimony of the Apostles,” Liahona, Apr. 2000, 2.

  15. Ona Helamani 8:15.

  16. Ona Mafundisho na Maagano 6:36.

  17. Yesu Kristo alitufundisha umuhimu wa ibada takatifu, kama vile ubatizo (ona Yohana 3:5), sakramenti (ona Mafundisho na Maagano 59:9) na endaumenti na ibada za hekaluni za kuunganishwa (ona Mafundisho na Maagano124:39–42).

  18. Ona Mafundisho na Maagano 124:29–32.

  19. Ona Musa 8:43–44.

  20. Marko 5:28.

  21. Ona Mafundisho na Maagano 88:63.

  22. Wakati mwanamke mwaminifu alipogusa vazi la Mwokozi, haraka alisema,”naona kwambanguvu [kwa Kigiriki dunamis, ikimaanisha “nguvu”] zimenitoka” (Luka 8:46 msisitizo umeongezwa).

  23. “Roho wa Mungu,” Hymns, no. 2.

  24. Ona 3 Nefi 5:20.