2010–2019
Mchungaji Wetu Mwema
Aprili 2017


Mchungaji Wetu Mwema

Yesu Kristo, Mchungaji wetu Mwema, anapata furaha anapowaona kondoo wake wagonjwa wakiendelea kufikia uponyaji.

Tunapata kuona kidogo tu tabia ya Baba yetu wa Mbinguni huku tukitambua huruma kubwa aliyo nayo kwa wenye dhambi na kuthamini jinsi anavyotofautisha baina ya dhambi na wale wanaotenda dhambi. Kuona huku kidogo tu hutusaidia sisi kuwa na [uelewa] sahihi juu ya tabia yake, ukamilifu Wake, na sifa Yake”1 na ni wa msingi katika kuifanyia kazi imani yetu kwake Yeye na kwa Mwanawe, Yesu Kristo. Huruma ya Mwokozi mbele ya upungufu wetu inatuvuta kwake na inatutia moyo katika mapambano yetu ya mara kwa mara katika kutubu ili tuwe kama Yeye. Tunapozidi kuwa kama Yeye, tunajifunza kuwatendea wengine jinsi afanyavyo, bila ya kujali sifa zo zote za nje au tabia.

Athari ya kutofautisha kati ya sifa za nje za mtu na mtu binafsi mwenyewe ni kiini cha kitabu Les Misérables, cha mwandishi Mfaransa Victor Hugo.2 Kama kitabu kinavyoanza, msimulizi anamtambulisha Bienvenu Myriel, askofu wa Digne, na anazungumzia mtanziko unaomkumba askofu. Je, amtembelee, mwanaume ambaye amekiri kwamba yeye ni mkanamungu na anaye dharauliwa katika jumuia kwa sababu ya tabia zake hapo zamani katika Mapinduzi ya Ufaransa?3

Msimulizi anasema kwamba askofu anaweza kiasilia kuhisi chuki kubwa sana kwa mwanaume huyo. Kisha msimulizi anauliza swali rahisi: “Hata hivyo, je vigaga vya kondoo vinapaswa kumsababisha mchungaji wa kondoo kurudi nyuma?”4 Akijibu kwa niaba ya askofu, msimulizi anatoa jibu la uhakika: “La”— na kisha anaongezea maoni ya ucheshi: “Lakini kondoo wa aina gani!”5

Katika kifungu hiki, Hugo analinganisha “uovu” wa bwana huyu na ugonjwa wa ngozi wa kondoo na analinganisha askofu na mchungaji ambaye hatoroki wakati anapokabiliana na kondoo aliye mgonjwa. Askofu ana huruma na baadaye katika kitabu anaonyesha huruma kama hii kwa mwanaume mwingine, mhusika mkuu katika kitabu, mfungwa aliyewachiliwa hasiyeheshimiwa, Jean Valjean. Huruma na kuelewa kwa askofu kunamtia moyo Jean Valjean kubadilisha mwenendo wa maisha yake.

Kwa vile Mungu hutumia magonjwa kama sitiari ya dhambi kote katika maandiko, kuna busara kuuliza, “Ni namna gani Yesu Kristo anafanya wakati anapokabiliana na magonjwa yetu ya kisitiari—dhambi zetu?” Baada ya yote, Mwokozi alisema ya kwamba “siwezi kuiangalia dhambi na kuivumilia hata kidogo”;6 kwa hivyo ni namna gani anaweza kutuangalia, jinsi tulivyo wapungufu, bila ya kuchukizwa na kuudhika ?

Jibu ni rahisi na wazi. Kama Mchungaji Mwema,7 Yesu Kristo huona ugonjwa katika kondoo wake kama hali ambayo inahitaji matibabu, utunzaji na huruma. Mchungaji huyu, Mchungaji wetu Mwema, anapata furaha katika kuona kondoo wake wagonjwa wakiendelea kufikia uponyaji.

Mwokozi alitabiri ya kwamba “atalilisha kundi lake kama mchungaji,”8 “nitawatafuta waliopotea, … nitawarudisha waliofukuzwa, … nitawafunga waliovunjika, na … nitawatia nguvu wagonjwa.”9 Hata kama Israeli iliyoasi ilionyeshwa kama iliyoharibiwa na “jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha,”10 Mwokozi alihamasisha, akahimiza, na kuahidi uponyaji.11

Huduma ya Mwokozi duniani hakika ilijulikana kwa upendo, huruma, na kuelewa. Hakutembea kwa dharau katika barabara za vumbi za Galilaya na Judea, akishtuka alipowaona wenye dhambi. Hakuwakwepa kwa kuchukizwa mno. La. Alikula pamoja nao.12 Alitoa usaidizi na kuwabariki, akainua na kujenga, akabadilisha hofu na kukata tamaa kwa tumaini na furaha. Kama Mchungaji wa kweli Naye ndiye, Hututafuta na kutupata ili atupe msaada na tumaini.13 Kuelewa huruma na upendo Wake kunatusaidia kuwa na imani Naye—ili tutubu na tuponywe.

Injili ya Yohana inasema uzuri wa Mwokozi wa kumwelewa mtenda dhambi. Waandishi na Mafarisayo walimleta mwanamke kwa Mwokozi aliyepatikana katika kitendo cha uzinzi . Waliomshtaki walidokeza kwamba alistahili kupigwa kwa mawe, katika kutii sheria ya Musa. Yesu, katika kujibu maswali yaliyokuwa mengi, mwishowe aliwaambia, “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.”

Waliomshtaki waliondoka, “na Yesu alibaki peke yake, na mwanamke akiwa amesimama katikati.

“Wakati Yesu … Hakumwona mwingine bali mwanamke peke yake, alimwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliye kuhukumu kuwa una hatia?

“Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu: Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”14

Hakika, Yesu hakuvumilia uzinzi. Lakini pia hakumlaani mwanamke yule. Alimhimize abadili maisha yake. Alihamasika kubadilika kwa sababu ya huruma na rehema yake. Tafsiri ya Joseph Smith ya Bibilia inathibitisha kufuatia kwa uanafunzi wake yule mwanamke. “Na Mwanamke akamsifu Mungu kutoka wakati huo, na akawa na imani katika jina lake.”15

Wakati Mungu anapoonyesha huruma, hatupaswi kuamini kimakosa kwamba anakubali na yuko tayari kukubali dhambi. Hayuko hivyo. Mwokozi alikuja duniani kutuokoa kutokana na dhambi zetu, na muhimu, hatatuokoa katika dhambi zetu.16 Mhojaji mmoja mwenye ujuzi, Zeezromu, wakati fulani alijaribu kumtega Amuleki kwa kumuuliza: “Je itakuwaje [Masiya ajaye] atawaokoa watu wake katika dhambi zao? Na Amuleki akajibu na kumwambia: Nakwambia kwamba hatafanya hivyo, kwani haiwezekani kwake Yeye kukana neno lake. … Hawezi kuwaokoa katika dhambi zao.”17 Amuleki alisema ukweli wa kimsingi kwamba ili tuweze kuokolewa kutoka katika dhambi zetu, ni lazima tutii “masharti ya toba,” ambayo yanaachilia nguvu za Mkombozi za kuokoa roho zetu.18

Huruma,upendo, na rehema ya Mwokozi hutuvuta kwake.19 Kupitia Upatanisho Wake, haturidhiki tena na hali yetu ya dhambi.20 Mungu yuko wazi kuhusu kilicho haki na kinachokubalika Kwake na kile kilicho makosa na dhambi. Hii sio sababu anataka kuwa na wafuasi wasiofikiri, wanaomtii. La, Baba yetu wa Mbinguni anawataka watoto Wake kwa kujua na kwa hiari wachague kuwa kama Yeye21 na wawe na sifa ya kuwa na maisha kama yale anayofurahia.22 Katika kufanya hivyo, watoto Wake wanatimiza hatima yao tukufu na kuwa warithi wa yote aliyonayo.23 Kwa sababu hii, Viongozi wa Kanisa hawawezi kubadili amri au mafundisho ya Mungu kinyume na mapenzi Yake, ili iwe rahisi au maarufu.

Hata hivyo, katika jitihada zetu za maisha ya kumfuata Yesu Kristo, mfano Wake wa ukarimu kwa wale wanaotenda dhambi hapa kuna fundisho. Sisi, ambao ni wenye dhambi, ni lazima, kama Mwokozi, tuwaendee wengine kwa huruma na upendo. Jukumu letu pia ni kusaidia na kubariki, kuinua na kujenga, na kubadili hofu na kukata tamaa kuwa tumaini na furaha.

Mwokozi aliwakemea watu waliowatoroka wengine ambao waliwaona kama wasio wasafi na waliojihesabia wenye haki kwa kuwahukumu wengine kama wenye dhambi kuliko wao.24 Hilo ndilo somo hasa ambalo Mwokozi alielekeza kwa wale “waliojipambanua ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine .” Alisimulia fumbo hili.

“Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Mfarisayo, wa pili mtoza ushuru.

“Yule Mfarisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

“Mimi hufunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.

“Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.”

Kisha Yesu akamalizia, “Nawaambia, huyu [mtoza ushuru] alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule [Mfarisayo]; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”25

Ujumbe huu kwetu u wazi, mtenda dhambi anayetubu anamkaribia Mungu zaidi kuliko mwenye kujihesabu kuwa mwenye haki anayemhukumu mtenda dhambi.

Mwelekeo wa binadamu wa kujihesabia mwenye haki ulikuwepo pia katika siku za Alma. Wakati watu “wakaanza kuimarisha kanisa sana … kanisa walianza kupata kiburi … [na] watu wa kanisa walianza [ku]jivuna kwa macho yao, … walianza kufanyiana madharau, wao kwa wao, na wakaanza kuwatesa wale ambao hawakuamini kulingana na nia yao na mapenzi yao.”26

Mateso haya yalikuwa bayana yamekatazwa: “Sasa kulikuwa na sheria kali miongoni mwa watu wa kanisa, kwamba kusiwe na mtu yeyote, miongoni mwa washiriki wa kanisa, atakayeinuka na kuwatesa wale ambao sio washiriki wa kanisa, na kwamba kusiwe na mateso miongoni mwao.”27 Kanuni inayoongoza Kwa Watakatifu wa Siku-za Mwisho ni sawa. Hatupaswi kuwa na hatia ya kumtesa mtu yeyote ndani au nje ya Kanisa.

Wale ambao wameteswa kwa sababu yoyote wanafahamu jinsi ukosefu wa haki au itikadi kali inavyosikika. Kama kijana nikiishi kule Ulaya miaka ya 1960, nilihisi kwamba nilionewa na kukandamizwa kwa sababu nilikuwa Mmarekani na kwa sababu nilikuwa muumini wa Kanisa. Baadhi ya wanafunzi wenzangu shuleni walinitendea kana kwamba mimi binafsi nilipaswa kuwajibikia kutokana na sera za nchi za nje za Marekani ambazo hazikuwa maarufu. Nilitendewa kama kwamba dini yangu ilikuwa ni kama fedheha kwa mataifa ambamo niliishi kwa sababu ilitofautiana na dini zilizodhaminiwa na taifa hilo. Baadaye, katika mataifa tofauti duniani, nimepata kuona kidogo ubaya wa chuki na ubaguzi wanaopitia wale wanaolengwa kwa sababu ya asli zao au makabila yao.

Mateso huja kupitia njia nyingi: kejeli, kunyanyaswa, kuonewa, kuachwa na kutengwa, au chuki kwa wengine. Ni lazima tujikinge dhidi ya itikadi kali ambayo inainua sauti yake dhidi ya wale walio na maoni tofauti. Itikadi kali zinajitokeza, kwa kiwango fulani, kwa sababu ya kutotaka kuwa na usawa wa kujieleza.28 Kila mtu, ikiwa ni pamoja na watu wa dini, anayo haki ya kueleza maoni yake katika umma. Lakini hakuna aliye na ruhusa ya kuwa na chuki kwa wengine wakati maoni hayo yanapotolewa.

Historia ya Kanisa inatupatia ushahidi wa kutosha kuhusu waumini wetu wakitendewa kwa chuki na itikadi kali. Ingekuwa vibaya na ya kusikitisha kiasi gani ikiwa tungewatendea wengine jinsi tulivyotendewa. Mwokozi alifundisha, “Yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo.”29 Sisi tukitaka kuheshimiwa, ni lazima tuheshimu. Zaidi ya hapo, kuongoka kwetu kwa kweli kunaleta, “unyenyekevu na upole wa moyo,” ambao unamwalika “Roho Mtakatifu [na kutujaza na] upendo kamili,”30 “upendo usio unafiki”31 kwa wengine.

Mchungaji wetu Mwema habadiliki na anajisikia namna hiyo hiyo kuhusu dhambi na watenda dhambi jinsi alivyojisikia wakati alipokuwa duniani. Yeye hachoshwi nasi kwa sababu tunatenda dhambi, hata ikiwa Yeye, mara nyingine, lazima afikirie, “Lakini ni kondoo wa aina gani huyu!” Anatupenda sana kiasi cha kuwa alitayarisha njia ili tuweze kutubu na kuwa wasafi ili tuweze kurudi Kwake na kwa Baba yetu wa Mbinguni.32 Katika kufanya hivyo, Yesu Kristo pia alitupa mfano wa kufuata—kuonyesha heshima kwa wote na kuwa bila chuki kwa yeyote.

Kama wanafunzi Wake, natuige upendo Wake na tupendane wazi wazi na kikamilifu kiasi cha kwamba hakuna anayehisi ameachwa, yu mpweke, au hana matumaini. Ninashuhudia ya kwamba Yesu Kristo ni Mchungaji wetu Mwema, ambaye anatupenda na anatujali. Anatujua na alitoa uhai Wake kwa ajili ya kondoo Wake.33 Pia anaishi kwa ajili yetu na anataka tumjue na tuwe na imani Naye. Ninampenda na ninamuabudu Yeye, na nina shukrani kubwa sana Kwake, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Lectures on Faith (1985), 38.

  2. Kitabu Les Misérables, na Victor Hugo (1802–85), kinasimulia simulizi kumhusu Jean Valjean ambaye alitenda kosa dogo la kuiba mkate ili aweze kuilisha familia ya dada yake. Alihukumiwa kipindi cha miaka 5 gerezani, Valjean alihudumu miaka 19 ya kufanya kazi ngumu kwa sababu ya majaribio mane ya kutoroka gerezani. Alitoka gerezani mwanaume sugu na mwenye uchungu.

    Kwa sababu ya rekodi yake ya uhalifu, Valjean alishindwa kupata kazi, chakula, na makazi. Mchovu na akiwa amevunjika moyo, hatimaye alipewa makazi na askofu wa Digne, ambaye alimuonyesha ukarimu na huruma. Wakati wa usiku, Valjean alishindwa na hisia ya kukata tamaa na akaiba vyombo vya fedha vya askofu kisha akatoroka.

    Valjean alikamatwa na kurudishwa kwa askofu. Kwa njia isiyoelezeka na kinyume na matarajio ya Valjean, askofu aliwaeleza askari kwamba Valjean alikuwa amepewa vyombo hivyo vya fedha na akasisitiza kwamba Valjean achukue vinara viwili vya mishumaa pia. (Ona Hugo, Les Misérables [1987], book 2, sura ya 10–12.)

  3. Ona Hugo, Les Misérables, book 1, sura ya 10.

  4. Msimulizi anauliza, Toutefois, la gale de la brebis doit-elle faire reculer le pasteur? (Hugo, Les Misérables [1985], book 1, sura ya 10, ukurasa wa 67). Gale, katika elimu ya magonjwa ya mifugo, inahusu aina ya maradhi ya ngozi yanayosababishwa na wadudu wadogo wanyonyaji na inayotambulika kwa kupoteza kwa nywele na kutokeza kwa vigaga (“upele wa wanyama” kwa Kiswahili). Maneno haya yametafsiriwa katika njia mbali mbali kwa Kingereza.

  5. Maoni ya ucheshi ya kihariri msimulizi kumhusu mwanadesturi ni Mais quelle brebis! imetafsiriwa mara kadhaa kama “Lakini kondoo mweusi kiasi gani.”

  6. Mafundisho na Maagano 1:31.

  7. Ona Yohana 10:11, 14; Alma 5:38; Mafundisho na Maagano 50:44.

  8. Isaya 40:11.

  9. Ezekieli 34:16.

  10. Isaya 1:6.

  11. Ona Isaya 1:18.

  12. Ona Luka 15:1–2.

  13. Ona Mathayo 18:11.

  14. Ona Yohana 8:3–11.

  15. Tafsiri ya Joseph Smith, Yohana 8:11 (katika Yohana 8:11, tanbihi c).

  16. Ona D. Todd Christofferson, “Abide in My Love,” Liahona, Nov. 2016, 48.

  17. Alma 11:34, 37.

  18. OnaHelamani 5:10–11.

  19. Ona 3 Nefi 27:14–15.

  20. Katika nyakati za kisasa, Mwokozi alifafanua: Kile kivunjacho sheria, na hakiishi kwa sheria, lakini chatafuta chenyewe kuwa sheria, na kiko tayari kuishi katika dhambi, na moja kwa moja kinaishi katika dhambi, hakiwezi kutakaswa kwa sheria, si kwa rehema, haki, wala hukumu. Kwa hiyo, lazima wazidi kuwa wachafu” (Mafundisho na Maagano 88:35).

  21. Ona 2 Nefi 2:26–27.

  22. Ona Mafundisho na Maagano 14:7; 132:19–20, 24, 55.

  23. See Warumi 8:16–17; Mafundisho na Maagano 84:38.

  24. Ona Mathayo 23:13.

  25. Luka 18:9–14.

  26. Alma 4:4, 6, 8.

  27. Alma 1:21.

  28. OnaOxford English Dictionary, “bigotry” and “intolerance,” oed.com.

  29. Mathayo 7:12.

  30. Moroni 8:26

  31. 1 Petro 1:22.

  32. Ona Makala ya Imani 1:3.

  33. Ona Yohana 10:11–15.